2009 tukiamua na sisi tunaweza | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

2009 tukiamua na sisi tunaweza

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by BAK, Jan 1, 2009.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Jan 1, 2009
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,548
  Likes Received: 81,990
  Trophy Points: 280
  2009 tukiamua na sisi tunaweza

  Lula wa Ndali-Mwananzela Disemba 31, 2008
  Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

  MWAKA 2008 ndiyo huo unatokomea katika kurasa za historia. Ni mwaka ambao katika vipimo vyovyote vile unabakia kuwa wa kihistoria kutokana na matukio mbalimbali ambayo yameacha alama zake katika maisha na mioyo ya wananchi wetu.

  Mwaka huu unaoisha ni mwaka wa kukumbuka kwa mambo mengi, mazuri na mabaya, ya raha na ya karaha, ya kicheko na ya machozi! Ni mwaka ambao kama tungetaka kuurudia tungejikuta tunakabiliwa na utata wa kuchagua kama matamu yaliyotokea yanazidi machungu yaliyotokea.

  Niwape pole wasomaji wetu ambao wao kama mimi mwaka huu tumepoteza watu wa karibu, ndugu, jamaa na marafiki ambao tumekua nao; na wale ambao wamepoteza wenzi wao na watoto wao au wazazi wao. Haya ni machungu ambayo ni sehemu ya maisha yetu kama wanadamu, lakini ni machungu ambayo hayazoeleki wala kutabirika. Ni Mungu mwenyewe ndiye aliye faraja yetu na msimamizi wetu wakati wa mateso. Kwake yeye tunazikabidhi na kuziombea huruma roho za marehemu wote, Amina.

  Pia ninawapa pongezi na mkono wa baraka wote ambao kutokana na nafasi zao walisimama kutekeleza wajibu wao katika utumishi wa nchi yao. Wapo maelfu ya watumishi wa umma ambao bila ya shaka wanamaliza mwaka wakiwa na dhamira safi mbele zao na mbele za Mungu wa imani zao kuwa walifanya kwa uaminifu kile ambacho Taifa lao liliwakabidhi kufanya. Hawa wengi wao majina yao hayatajwi hadharani na yale waliyoyafanya hayaadhimishwi barazani.

  Ni hawa ambao wamelifanya Taifa liende na kufika hapo lilipofika. Ni hawa ambao licha ya hali ngumu ya maisha, licha ya migogoro mbalimbali na matatizo ya maisha yao binafsi wameamka kila asubuhi wakifikiria utumishi kwa nchi yao. Ni hawa ambao majina yao hayatajwi wakati wa shukrani viongozi wanaposimama, na ya kwamba vitabu vya historia vitakapoandikwa hata kuwapo kwao kunaweza kusitajwe.

  Hawa ndugu zangu ndiyo nguvu iliyofichika ambayo ndiyo imekuwa ikisukuma mjadala wa Taifa na kutupa tumaini kuwa na sisi pia tunaweza.

  Kwa hawa tunawashukuru kwa utumishi uliotukuka kwa taifa letu kwa mwaka huu uliopita, pasipo nyinyi bila ya shaka mambo mengi yasingefanyika na vita hii dhidi ya mafisadi na ufisadi nchini isingefikia hapa. Tunawashukuru.

  Pamoja na hao hata hivyo hatuna budi kukiri jukumu la pekee la wale ambao wamelisimamia Taifa na idara mbalimbali wakati huu ambapo mafisadi nusura watawale kama kwa kupenda bila ya kujali matokeo yake (with impunity).

  Tulifika mahali ambapo tulidhania nchini kuna watu hawagusiki, hawazungumziki wala kunyooshewa vidole lakini wapo wale ambao licha ya mapungufu yao binafsi na hata yale mapungufu ya nafasi zao wamejaribu kufanya kile ambacho wamepaswa kufanya!

  Kwa namna ya pekee hatuna budi kukiri jukumu la Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe na wenzake na pia Timu ya Mwanasheria Mkuu Johnson Mwanyika. Timu hizi mbili kwa kiwango kikubwa zimetupa chembe kidogo tu ya fahari ya utumishi wa umma.

  Hatuwezi kusema mengi bila kukiri michango ya wabunge mbalimbali ambao na wao wamesimama kidete kusimamia maslahi ya Taifa na wametuonyesha tofauti ya wabunge tulionao.

  Sasa hivi tunajua ni nani kweli "mtetezi" wa nchi yetu na ni nani hasa "mtetezi" wa ulaji wake na wa marafiki zake! Mwaka huu unaopita umetuchorea mstari ardhini kati ya wawakilishi wa watu na wawakilishi wa vyama! Leo hii hatuna utata tena kati ya nani "mwenzetu" na ni nani "mwenzao".

  Tumefika ukikongoni mwa mwaka huu tukijua wazi kwamba kama kuna sehemu ya Taifa ambayo imekumbana na changamoto kubwa ni idara ya Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa na TAKUKURU. Vyombo hivi vitatu kwa namna ye pekee sana vinawajibika katika kuhakikisha sisi kama Taifa tunaendelea kubakia katika hali ya utulivu, amani na utawala wa kisheria. Vyombo hivi pamoja na Idara ya Mwendesha Mashtaka zinawajibika kwa kiwango kikubwa kuhakikisha kuwa nchi yetu inaendelea kuwa moja, na mahali ambapo kila Mtanzania anajisikia yuko salama.

  Kwa muda mrefu tumeandika jinsi gani taasisi hizi zimekuwa zikituangusha na kutufanya tuhoji kama zina uwezo kweli wa kutimiza majukumu yao. Ni kweli tumeshuhudia changamoto nyingi ambazo tunaamini kama vyombo hivi vingekuwa vinafanya kazi yake sawasawa huko, nyuma tusingefika hapa.

  Ni hilo ndilo lilikuwa msingi mkubwa wa ukosoaji wetu hasa kwa upande wa Usalama wa Taifa. Tunaamini kuwa mahali popote ambapo idara za aina hii ni dhaifu basi utawala wa kifisadi unashamiri. Tumeyaona sehemu mbalimbali duniani na hapa kwetu sasa ni mfano.

  Pamoja na ukosoaji wetu huo jambo moja ambalo tumekuwa tukilitambua ni nafasi ya pekee ya vyombo hivi na hivyo kutokana na mazingira yaliyopo, unyeti wa majukumu yao hatuna budi kuwashukuru na kuwatambua kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha leo hii mapambano ya ufisadi. IGP said Mwema, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa Rashid Othman, Dk. Edward Hosea wa TAKUKURU na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mwanyika wamefanya kazi katika mazingira magumu na yenye changamoto kubwa. Idara zao zinabeba jukumu kubwa mno la kuhakikisha kuwa mafisadi na uzao wao hawafanikiwi!

  Licha ya ukweli kwamba wao wenyewe wanakabiliwa na maswali kadha wa kadha ambayo bado yanahitaji majibu hatuna budi kukiri na kukubali juhudi zao ambazo zimeonyesha matunda kwa kiasi cha kutamanika.

  Bado wanajukumu kubwa la kufanikisha vita dhidi ya ufisadi, mauaji ya albino, ujambazi, na mengineyo. Vyovyote vile ilivyo, mchango wao kwa mwaka huu hatuna budi kuutambua na kuukubali.

  Hatuna budi pia kukiri kwa kiwango kikubwa mchango wa pekee wa Rais wa Jamhuri, Jakaya Kikwete na chini yake uongozi wote wa juu wa nchi kwa jinsi ambavyo licha ya matukio mbalimbali ambayo yangeweza kutikisa nchi kama Zimbabwe, kwetu yameweza kusimamiwa kwa umakini, uthabiti, na uthubutu mkubwa.

  Ni wazi, pasipo shaka, kuwa ni kutokana na mtindo wake wa uongozi ambao kwa wengi wetu bado ni mgeni tunaweza kuona mambo mbalimbali ambayo wengine tuliamini hayatatokea.

  Kwa mtindo huu tunaamini mwaka unaoanza, 2009, tutawaona watu wengine mashuhuri wakisimamishwa kizimbani. Yote hayo ni muunganiko wa kihistoria kati ya matamanio ya watawaliwa na ujasiri wa uongozi wa watawala.

  Katika yote ambayo yametokea mwaka huu ambayo yametufanya tuone fahari na kuanza kwa mbali kuturudishia heshima ya utu wetu, hatuna budi kukiri kuwa na sisi "tunaweza".

  Matukio yote haya na mengine mengi na kutokana na michango ya watu mbalimbali kwenye utumishi wa Serikali na nje ya Taifa, hatuna budi kukiri tena vichwa vyetu vikiwa vimeinuliwa juu kwa kujiamini kuwa na sisi tunaweza.

  Tunaweza kutawala vizuri! Tunaweza kuwajibishana, tunaweza kusimamia raslimali zetu, tunaweza kubuni mikakati mizuri ambayo tunaweza kuitekeleza; na ya kuwa na sisi tunaweza kujenga katika ardhi ya wazazi wetu Taifa la kisasa.

  Ni moyo huu wa kujiamini ndio ambao hatuna budi kuujenga ndani ya watu wetu. Tusiwe wepesi kukimbilia nje kutafuta suluhu ya matatizo yetu. Suala la ATCL, kwa mfano, ni suala ambalo liko ndani ya uwezo wetu kulishughulikia kama vile masuala ya nishati na miundo mbinu mingine kuwa yako ndani ya uwezo wetu.

  Mwaka huu unaokuja naamini kabisa ya kuwa jukumu letu kubwa ni kujenga moyo wa kujiamini na kujitoa katika utumishi wa Taifa. Ninaamini ya kuwa ndani ya vijana wetu, watoto wetu na watu wazima, ile fikra kujiona duni na kutoweza itapigwa vita kwa vitendo.

  Tutajipa changamoto wenyewe kufanya yale ambayo tunaweza kuyafanya. Naamini asilimia zaidi ya 90 ya matatizo yetu yako ndani ya uwezo wa vichwa vyetu kuweza kuyatatua endapo tu tutakubali, kukiri na kusema kuwa na "sisi tunaweza".

  Tunapouingia mwaka huu mpya, badala ya kubadilisha magari, nyumba, au kupeana pongezi tu za heri ya kuuona mwaka mpya, tuamue kweli kulibadili Taifa na tuanze kulijenga upya. Ni lazima mwaka huu turudi tena kwenye yale ya msingi ambayo ni ujenzi wa Taifa.

  Hilo, hata hivyo, halitafika popote isipokuwa lazima litanguliwe na mabadiliko ya kifikra. Kwamba, ni lazima tujiamini kuwa na sisi tunaweza! Si kuweza kukosoa tu, si kuweza kulalamika tu, si kuweza kukebehi na kukejeli, si kuweza kuandika kwa umahiri, si kuweza kukashfiana na kutafutana; bali kuweza kweli kujenga nchi ya kisasa ambapo ni taifa kweli la watu "walio huru na sawa"! Taifa ambalo ni kitovu cha mafanikio ya watu wengi na fahari ya raia wake!

  NA SISI TUNAWEZA!

  Karibu 2009!

  Barua-pepe: lulawanzela@yahoo.co.uk
   
Loading...