Zitto, Nape wamvaa Maghembe

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,005
Zitto, Nape wamvaa Maghembe

na Edward Kinabo
Tanzania Daima~Sauti ya Watu

WAKATI walimu wakitarajia kuanza mgomo wao leo, huku baadhi ya vyuo vikuu vikiwa vimefungwa kutokana na migomo, kada machachari wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye amemtaka Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jumanne Maghembe, kuacha kutumia ubabe na badala yake kuwakalisha wadau wa elimu ili kupata ufumbuzi wa hatma ya elimu nchini.

Nape alisema hali hiyo ikiachwa iendelee, inaweza kuiweka pabaya CCM hasa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Nape alitoa kauli hiyo jana wakati akitoa maoni yake kuhusu mgomo wa walimu uliotarajiwa kuanza leo pamoja na kufungwa kwa vyuo vikuu kadhaa nchini kutokana na madai ya kupinga sera ya uchagiaji elimu ya juu.

Nape alisema anashangazwa na ubabe wa serikali katika kutatua tatizo hilo kwani kinachotakiwa ni waziri mwenye dhamana kutumia busara ya kukaa na wadau wa elimu ili kurekebisha kasoro iliyopo, vinginevyo CCM na Serikali yake inazidi kujiweka kwenye wakati mgumu zaidi.

“Kinacholalamikiwa hapa ni sera ya uchagiaji elimu juu ambayo lengo lake ni kuwasaidia Watanzania, sasa kama wenyewe wanalalamika maana yake kuna tatizo katika sera ya uchangiaji na ili kuiondoa kasoro hiyo waziri anapaswa kukaa na wadau wa elimu badala ya kutumia ubabe au kikimbilia mahakamani,” alisema Nape.

Mwanasiasa huyo ambaye siku za hivi karibuni alijikuta kwenye mzozo mzito na Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM), alisema anakerwa na tabia ya ubabe ya Maghembe na wizara yake ambayo alisema si dawa ya kukabiliana na migomo.

Kuhusu mgomo wa walimu, Nape alisema ni aibu kwa Serikali kukimbilia mahakamani kusaka suluhu kwani madai ya walimu ni ya muda mrefu na njia sahihi ni kuyalipa.

“Ni vizuri Waziri Maghembe akaangalia namna ya kuondoa tatizo hilo. Serikali kukimbilia mahakamani ni aibu na hata Serikakali ikipata haki, haina maana kwani walimu wataendelea kufanyakazi kwa shingo upande.

Nape alisisitiza kuwa hali hiyo ikiachwa iendelee, itakuwa mbaya kwa CCM kwani wanaolalamikia kutotendewa wengi ni wanachama CCM na ndio wapiga kura wao.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Zitto Kabwe alisema kitendo cha serikali, kushindwa kutatua migogoro ya wanafunzi na walimu ni kielelezo kuwa CCM imechoka na haina uwezo tena wa kuwaongoza Watanzania.

Zitto alisema hayo juzi wakati akitoa mada kuhusu hali ya uchumi nchini katika kongamano la wanafunzi wa vyuo vya elimu juu vya Mkoa wa Iringa, lililofanyika katika Ukumbi wa Jumba la Maendeleo, mjini Iringa.

Mbele ya maelfu ya wanafunzi waliofurika katika kongamano hilo, Zitto alisema CCM imechoka kufikiri ndio maana kwa muda mrefu sasa imekuwa ikishughulikia matatizo ya migomo ya wanafunzi kwa kufunga vyuo na kuwatisha, njia ambazo hazitaweza kumaliza matatizo yaliyopo.

“Tunaiambia serikali, huwezi kutatua matatizo ya uchangiaji wa elimu ya juu kwa kufunga vyuo. Huwezi kutatua migogoro ya elimu ya juu kwa kutishia wanafunzi. Matatizo ya elimu ya juu yatatuliwe kwa njia ya majadiliano na si mazungumzo kati ya serikali na wanafunzi pekee, yanapaswa kuwa mazungumzo yatakayoshirikisha jamii nzima….jamii nzima ikae na iamue jinsi gani ya kugharamia elimu ya juu,” alisema Zitto.

Zitto alitumia fursa hiyo kujibu tuhuma zinazotolewa na viongozi wa serikali na wa CCM kwamba CHADEMA imekuwa ikitumia viongozi na makada wake, kuchochea migomo katika vyuo hivyo.

Alisema CHADEMA haijawachochea wanafunzi wagome na haiwezi kufanya hivyo lakini inaunga mkono juhudi zote za kundi lolote linapodai haki zao, kama walimu na wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu wanavyodai haki zao.

Alisema chama chake kinatetea zote haki za wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini kwani kimejengwa na kuimarishwa na vuguvugu la wasomi wa vyuo vikuu na wanaharakati mbalimbali nchini, akiwemo yeye mwenyewe na viongozi wengine.

“CHADEMA ni chaguo la watu makini, ni chaguo la wanaharakati. Aliyewahi kuwa rais wa Serikali ya wanafunzi katika chuo kikuu cha Dar-es-Salaam (Daruso) mwaka 1998/1999, Kitila Mkumbo, ni mwanachama wetu hai. Aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Daruso mwaka 2005/2006, John Mrema, ndiye Mkurugenzi wetu wa sasa wa Bunge na Halmashauri. Aliyewahi kuwa Rais wa serikali ya wanafunzi chuo cha teknolojia Dar-es-Salaam, Msafiri Mtemelwa, ndiye Mkurugenzi wetu wa kampeni na uchaguzi. Aliyewahi kuwa Rais wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania, Dadi Igogo, ndiye afisa mwandamizi wa kurugenzi ya mafunzo.

Wapo wengi sana …..mimi mwenyewe pia nilikuwa Katibu Mkuu wa Daruso. Ndiyo maana serikali inaweweseka,” alisema Zitto na kushangiliwa.

Alisema baada ya vyuo kufungwa, serikali inaweza kuwarudisha baadhi tu ya wanafunzi waliogoma huku wengine wakitolewa mhanga kwa kufukuzwa kabisa na kuwataka wanafunzi hao kutokubali kuwagawanyika na waendelee kupigania haki yao kwa pamoja.

“Msisikitike chuo kufungwa, msisikitike kurudi nyumbani…….nendeni mkawaelimishe watu kuhusu kile mnachokisimamia. Wala msijali kwamba mnachokipigania hakitatokea sasa……mnachokipigania kama si ninyi basi kitakuja kuwanufaisha wadogo zenu. Kina Nyerere na Bibi Titi wasingepigania uhuru mapema tusingeupata mapema…..tungepata uhuru hata kama Nyerere na Bibi Titi wasingepigania, lakini tungechelewa,” alisema Zitto.

Alisema iwapo serikali itapanga mambo yake vema, inaweza kumudu kutoa mikopo ya asilimia 100 kwa wanafunzi wote wa elimu ya juu nchini kutokana na kasi nzuri ya ukuaji wa uchumi.

“Huko nyuma wakati wa Nyerere, serikali iliweza kuwalipa walimu na kugharamia gharama zote masomo. Iliwasomesha watu bure kuanzia elimu ya msingi hadi elimu ya juu wakati ambapo ukuaji wa uchumi ulikuwa chini sana . Leo wakati kasi ya ukuaji uchumi ni nzuri serikali inasema haina fedha.

Akizungumzia hali ya uchumi nchini, Zitto alisema unakua kwa wastani wa asilimia 5.6 ambacho ni kiwango kikubwa kabisa kwa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara, na inatarajiwa mwaka huu utakuwa kwa asilimia 7.2.

Hata hivyo alisema ukuaji huo umeshindwa kuwaondolea watu umaskini kwa sababu unachangiwa sana na ukuaji wa sekta ya madini, mawasiliano na ujenzi, ambazo hazina uhusiano wa moja kwa moja na uborekaji wa maisha ya watu.

Akitoa mfano katika sekta ya mawasiliano, alisema wakati makampuni ya simu ya vodacom, zain na tigo yanajiingizia mabilioni ya fedha kwa siku, hakuna kampuni ya simu hata moja nchini inayolipa kodi ya mapato kwa serikali.

“Chukua mfano wa Zain yenye wateja karibu milioni 3. Kwa huduma yao ya xtreme tu inajiingizia bilioni 3 kila siku. Tigo yenye wateja milioni 2, pigia hesabu wateja milioni moja tu, kwa huduma yake ya ‘xtreme’, kwa siku inajiingizia bilioni 1. Vodacom yenye wateja wengi, ina wateja milioni 5, kwa huduma yake ya chizika, kwa siku inajiingizia bilioni 4. Piga kwa mwezi, kwa mwaka ni sh ngapi…… Lakini hakuna kampuni hata moja ya simu inayolipa kodi ya mapato. Serikali ingekusanya kodi ya mapato kwenye kampuni hizi…..isingeshindwa kuwapa mikopo ya asilimia 100,” alisema Zitto.

Akigusia sekta ya madini, alisema serikali haikufikiria vema katika kunufaika na uwekezaji unaofanyika kwenye sekta hiyo kwani ililenga kupata pesa kutokana na mrabaha tu ilhali kuna njia nyingine ambazo serikali ingeweza kujipatia mapato kutokana na madini, ikiwemo kutoza kodi kwa makampuni ya uchimbaji, kuingia ubia na makampuni hayo na kuhakikisha kuwa kunakuwa na uhusiano kati ya ukuaji wa sekta moja na nyingine.

“Wakati serikali imekuwa ikitegemea kutoza mrabaha wa asilimia 3 ambao hata ukipandishwa hauwezi kuzidi asilimia 12, kwa kipindi cha miaka 10, imekuwa pia ikitoa misamaha ya kodi kwa makampuni ya madini ili yaweze kujiagizia mafuta kwa ajili ya kuzalisha umeme kwenye machimbo yao, ” alisema Zitto.

Alisema matokeo ya kufanya hivyo ni serikali kujikuta imesamehe jumla ya dola milioni 32 kwa makampuni hayo, huku yenyewe ikipata dola milioni 25 tu kutokana na kutoza mrabaha huo wa asilimia 3, wakati ingeweza kuepuka hasara hiyo kwa kuhakikisha kwamba shirika la Umeme (TANESCO) linasambaza umeme katika migodi yote nchini.

Aliongeza kuwa kama serikali isingesamehe kodi kwa makampuni ya uchimbaji wa mafuta pekee kwa mwaka 2006 tu, basi ingeweza kulipa deni la bilioni 16 inalodaiwa na walimu ikiwa ni malimbikizo ya mafao yao .

Alisema chanzo cha serikali kushindwa kuwalipa walimu ni kuyanufaisha makampuni hayo ya madini ambayo ni ya matajiri kwa kuyasemehe kodi, ambayo kama ingekusanywa ingeweza kuepusha mgomo unatarajiwa kuanza kesho Jumatatu.

Alisisitiza kwamba serikali ya CCM imechoka na haiwezi tena kuwaondolea Watanzania umaskini kwani imesahau kujenga uchumi wa vijijini kwa kushindwa kukuza sekta ya kilimo na kujenga miundo mbinu vijijini, hali iliyosababisha kujengeka kwa mataifa mawili ndani ya taifa moja, moja likiwa la matajiri waliyopo mijini na jingine taifa la maskini ambao wapo vijijini.

Katika kongamano hilo, ambalo pia lilijadili rasimu sifuri ya sera ya vijana ya CHADEMA, iliyowasilishwa na Dadi Igogo na Danda Juju, zaidi ya washiriki 200 walijiunga na CHADEMA, huku wawili kati yao wakiwa wamerejesha kadi za CCM.

Kongamano hilo lilikuwa sehemu ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wanafunzi duniani ambapo mwaka jana chama hicho kilifanya maadhimisho kama hayo katika ukumbi wa DDC jijini Dar-es-Salaam.
 
Kazi nzuri Mheshmiwa Zitto. Ila upinzani mna kazi sana ndugu yangu, wachache tunaona mnafanya kazi nzuri ila wengi wenu ni waganga njaa!. Ndio tatizo la upinzani Tanzania.
 
Nawakubali Zitto na hata Nauye, ila tu mabadiliko ya kweli Tanzania yenye nia yakuleta upinzani wa dhati yatakuja tu pale ambapo watanzania walio wengi watapewa elimu kuhusu, kujitambua pamoja na kujua haki zao za msingi!
 
kabla ya kujadili elimu ya Zitto tungeanza kuchambua elimu ya bosi wake ZITTO

AIBU

halafu weye Mwalimu JK Nyerere elimu yake ilikwa ya darasa la ngapi la enzi hizo uliona jinsi alivyoweza kuchambua mambo lakini?? kafa ila maneno yake yanaishi.. Msomi Benja umeona mambo yake ni ku invest tu mara kiwira mara flats na kupanga deal za kuyeyusha mihela ya EPA! huyu wa sasa hivi ona anavyochanganyikiwa anaamini hawezi kuongoza bila kwenda kuona ulaya wanaishije, na kuongeza wife wa pili kupunguza stress hivi nchi na wake wawili na tunavyojua ndoa zilivyo headeche si ndo maana yanamshinda...
angalia wasomi wanavyochemka Karamagi, Maghembe, Mkuchika, Msolwa nk wamefanya nini... mijisomi ikiongoza nchi ni tabu tupu ilikuwa ina ng'ang'ania vitabu tu unafikiri wanaweza kutatua matatizo ya wananchi we need leadership skills sio ujuzi wa kwenye vitabu ati......
ona sasa mafisadi wanaelimu gani mbona wanawashinda wenye elimu hata hosea analijua hilo........................
 
kabla ya kujadili elimu ya Zitto tungeanza kuchambua elimu ya bosi wake ZITTO

AIBU

Kwa nini mnataka kujadili elimu za watu? Jadilini contents za character zao sio elimu! Mkifanya hivyo, baadaye mkimaliza mtaingia kwenye rangi, kabila, dini etc
 
Analysis ya Zitto imetulia sana hata kama ana elimu ya Ngumbaru au PhD. Tena ukweli ni kwamba CHADEMA wana think tankers wazuri kuliko vyama vyote vya siasa (including CCM) hata kama ndani yao wamo wajanja na mafisadi.

Ukweli unabaki hivyo kwa kuwa ndani ya Chama Tawala chenye Wasomi Wabobevu na Wazamivu kwa miaka 47 bado hawajawahi kufikiri critically kama Zitto na Slaa (assume kuwa ni wao tu ndani ya CHADEMA) Vs Wasomi mamia Wazamivu na Wabobevu ndani ya CCM.
 
Back
Top Bottom