Zitto awatangazia vita wabunge 10 wa CCM

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,011
na Martin Malera, Dodoma

SIKU mbili baada ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujenga mtandao mahususi wa hoja za kumwangusha na kumsimamisha kuhudhuria vikao vya Bunge kwa miezi mitano, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto amezindua mkakati mahususi unaowalenga wabunge 10 wa chama hicho tawala walioongoza harakati za kumwadhibu.

Zitto, mbunge maarufu kuliko mwingine yeyote hivi sasa, alitangaza mkakati wake huo mahususi juzi usiku wakati wa hafla maalumu ya kumpongeza iliyoandaliwa na wabunge wenzake wa kambi ya upinzani na kufanyika katika Hoteli ya Dodoma.

Chini ya mkakati huo, mbunge huyo kijana mwenye ushawishi mkubwa, ameandaa ziara ya kuzunguka katika majimbo yote wanayotoka wabunge hao wa CCM kwa lengo la kuwashitaki kwa wapiga kura wao, lengo ikiwa ni kuwaandalia mazingira ya kuwakataa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Katika orodha ya wabunge hao wa CCM, yumo Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, ambaye ndiye aliyekuwa mlengwa mkuu wa Zitto katika hoja yake binafsi aliyoiwasilisha bungeni, Jumanne wiki hii na ikahitimishwa kwa kusimamishwa kwake.

Mbali ya Karamagi, wabunge wengine wa CCM walio katika orodha hiyo ya Zitto ni Ruth Msafiri (Muleba Kaskazini) , Suleiman Kumchanya (Lulindi), Adam Malima (Mkuranga), Siraju Kaboyonga (Tabora Mjini), Mudhihir Mudhihir (Mchinga), Hafidh Ali na Andrew Chenge (Bariadi Magharibi).

Aidha, mbali ya hao, wabunge wengine wawili wa CCM ambao nao wanaingia katika orodha hiyo ya kuundiwa mkakati ni wanaotoka katika majimbo mawili tofauti yaliyo Kigoma anakotoka Zitto mwenyewe.

Wabunge hao ni Manju Msambya (Kigoma Kusini), aliyepata kuwa naibu waziri na mkuu wa wilaya, na mbunge mwingine kijana, Peter Selukamba (Kigoma Mjini).

Mbunge huyo ambaye hivi karibuni aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA alisema mkakati huo mahususi dhidi ya wabunge hao, utaratibiwa na kusimamiwa na chama chake kwa kushirikiana na kambi nzima ya upinzani.

Alisema wakati wa ziara ya kuwakosanisha wabunge hao na wapiga kura wao, watakuwa wakitumia kumbukumbu rasmi za Bunge (Hansard).

“Kazi yetu hapa ni rahisi tu. Tunachukua hansard, tunakwenda nayo kwenye kila jimbo la mbunge aliyechangia, tutawasomea wananchi wake waone kama hiyo ni kazi waliyomtuma,” alisema Zitto kwa kujiamini.

Akizungumza na Tanzania Daima kwa simu jana jioni, Zitto alisema tayari alikuwa ameshakusanya hansard za michango ya wabunge hao wa CCM walipojadili hoja yake na mingine ya siku zilizopita.

Mbunge huyo alisema kuwa harakati hizo zitaanzia katika jimbo la Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, ambaye alidai alilipotosha Bunge kuwa Hansard haiwezi kuwa kitu cha kuamini wakati Karamagi alitumia Hansard ya Bunge katika kujibu baadhi ya hoja zake alizodai ameshindwa kuthibitisha.

Akizungumzia hoja yake iliyosababisha asimamishwe kutokana na pendekezo ambalo lilianza kutolewa na Mudhihir, Zitto alisema maandalizi ya hoja hiyo hayakuwa yake peke yake, bali ya kambi nzima ya upinzani ambayo ndiyo iliyompa yeye dhamana, kuisimamia na kuisemea.

“Hoja hiyo haikuwa yangu, ilikuwa ya kambi nzima ya upinzani. Wazee wakaniamini, wakanipa niendelee nayo na nashukuru kwa ushirikiano mkubwa walioutoa wabunge wa kambi ya upinzani katika kutetea hoja hiyo,” alisema Zitto.

Zitto alisema wakati alipopata nafasi ya kutetea hoja yake na kujibu hoja za wabunge Jumanne jioni, alijikuta akiwa na nguvu za ajabu na hata kujikuta akijibu kwa usafaha maswali yote kiasi cha kuwachang'anya wabunge wa CCM na viongozi wao.

Alisema pamoja na ukweli kwamba wabunge wa CCM walionekana kushikamana kumkandamiza, hakuna hata mmoja aliyeweza kuthibitisha tuhuma yoyote ya uongo dhidi yake.

Kwa upande wake, Kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Hamad Rashid Mohamed (Wawi-CUF), alisema Zitto amekuwa mtu mzito nchini kwani hoja hiyo na uamuzi uliofanywa na Bunge, umempa heshima na umaarufu mkubwa kama kiongozi wa nchi.

Alisema kambi ya upinzani imeandaa maandamano makubwa kesho Jumamosi ya kumpokea Zitto kwa ushajaa na pia kuunga mkono suala la muafaka ili ufikiwe mapema na kuwataka wabunge wote wa upinzani kuhudhuria mandamano hayo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Karatu, Dk. Willibrod Slaa, alisema kambi ya upinzani inajivunia kuwa na Zitto na kuahidi kwamba, kuanzia sasa hoja binafsi ni ajenda mama kwa wabunge wa kambi ya upinzani.

Alisema kuwa kambi yake itakuwa inafanyia kazi tuhuma nzito za ubadhirifu wa mali za umma na kuwasilisha hoja binafsi kama alivyofanya Zitto.

Katika hatua nyingine, Spika wa Bunge, Samuel Sitta, hadi jana alishindwa kueleza endapo hoja binafsi ya Dk. Willibrod Slaa itawasilishwa leo, ambayo ni siku ya mwisho kwa kikao cha Bunge la Bajeti.

Kutokana na ukimya huo wa Spika, Dk. Willibrod Slaa, jana alitangaza rasmi kuiondoa hoja hiyo baada ya kile alichokieleza kuwa kukosekana kwa dhamaira ya kweli kutoka kwa Spika.

Katika barua aliyomwandikia Spika jana na kutoa nakala kwa vyombo vya habari, Dk. Slaa alisema kuwa ameamua kuondoa hoja hiyo kwa madai ya kile alichokielezea kuwa ni kupigwa danadana kwa hoja hiyo.

Alisema kuwa baada ya kuwasilisha hoja hiyo, Spika Sitta alimtaka kuwasilisha vielelezo vya hoja hiyo, naye alifanya hivyo, lakini hadi jana saa sita alikuwa hajapewa jibu endapo hoja hiyo itapangwa kusikilizwa na kujadiliwa katika kikao hicho cha Bunge.

“Hoja yangu imewasilishwa kwa mujibu wa Kanuni ya 104 (1) na (2) za kanuni za Bunge, toleo la 2004. Kwa mujibu wa kanuni hiyo, sikutakiwa kuwasilisha maelezo ya hoja yangu pamoja na vielelezo vyovyote. Hata hivyo mimi nilitekeleza hilo kwa kumwonyesha Spika ili imsaidie katika kuielewa vizuri hoja yangu. Na hata baada ya kunitaka niwasilishe vielelezo husika nilifanya hivyo na kuwasilisha kwake Vol 1-1V ya vielelezo hivyo,” alisema Dk. Slaa.

Alisema kwa vile tuhuma alizozitoa ni muhimu sana kwa taifa na nzito kwani zinahusu taasisi nyeti, alitarajia Bunge lingesikiliza kwa uharaka hoja hiyo.

“Kwa vile Bunge linafikia muda wake na hakuna dalili yoyote kuwa hoja hiyo imepangiwa muda maalumu katika shughuli za Bunge, nimeona nitafute njia nyingine za haraka zaidi katika kulishughulikia suala hili hasa ikizingatiwa kuwa tuhuma hizi zinahusu matumizi mabaya ya fedha za taifa letu, ucheleweshaji wowote unaweza pia kutoa mwanya kuvuruga ushahidi wowote katika hatua ya baadaye,” alisema Dk. Slaa.

Alibainisha kuwa ametafakari na kubaini kuwa kwa muundo na mfumo wa Bunge ulivyo, masuala mazito hayataweza kufanyiwa kazi kama inavyotakiwa.

Hata hivyo, alisema kambi ya upinzani imeamua kukata rufaa juu ya hoja hiyo kwa wananchi na kupeleka taarifa zake katika vyombo vya fedha vya kimataifa vinavyoipa misaada Tanzania, vya Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF).

Awali, hoja ya Dk. Slaa ilipangwa kusikilizwa siku moja baada ya hoja ya Zitto juzi, kabla ya Spika Sitta kutangaza kuizuia, kwa maelezo kuwa alikuwa akihitaji kuipitia ili ajiridhishe kabla ya kuileta bungeni.
 
Duh, Aluta kontinua!! Sio kwenye majimbo ya hao waliochangia kumuaondoa, hata majimbo mengine ile Watanzania watambue PUMBA na MCHELE
 
yani inasikitisha sana kuona hali ya namna hii inatokea na sisi kama wanataifa la tanzania tukiendelea kukaa kimya!hii haivumiliki hatakidogo. huu ni muda wa kutoka mbele ya computer zetu na kwenda kuunga mkono maandamano na jitihada zingine za kupinga ufedhuli wa aina hii katika nnchi yetu
 
Dah Chenge again? Kati ya hao wabunge 10 naona kamshindwa Chenge maana kwenye kashfa ya Escorow Zitto alikubali kufuata muongozo wa Chenge

Chenge sijui analoga na nini
 
Back
Top Bottom