Zitto alipua ufisadi wa bil. 20/- za madini

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
Na Grace Michael, Dodoma

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe, jana aliibua kashfa nyingine dhidi ya serikali ya upotevu wa sh. bilioni 20 zinazolipwa na kampuni za madini.

Kutokana na kashfa hiyo, mbunge huyo ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, alipendekeza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukakaguzi.

Mbali na hilo, mbunge huyo pia alielekeza lawama zake kwa Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda na Waziri wa Fedha, Bw. Mustafa Mukulo kwa kutoa misamaha wa kodi kwa kampuni zinazokuja nchini kwa utafiti wa mafuta na gesi.

Alisema kuwa misamaha hiyo haina tija kwa taifa kwa kuwa inasababisha upotevu wa mabilioni ya fedha za Watanzania.

"Nimekuhusisha Waziri Mkuu kwa kuwa ulikwenda kufungua mkutano wa wawekezaji ambao kupitia wewe walipata fursa ya kutoa ombi lao kwako, na hii ndio maana ya kurubuniwa...ifike mahali tutunge sheria itakayozuia kurubuni lakini halikuwa jambo jema kumchukua Waziri Mkuu kwenda kufungua mkutano huo," alisema Bw. Kabwe.

Bw. Kabwe aliyasema jana bungeni wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Waziri Mkuu, ambapo alisema kuwa ni hatari kuona upotevu wa sh. bilioni 20 kwa mwaka mmoja tu.

"Kuna sheria ya madini ambayo tuliipitisha hapa bungeni na serikali iliingia katika mpango wa uwazi katika sekta ya madini (EITI) na baada ya wakaguzi wa mpango huo kupita katika makampuni ya madini kuchunguza fedha wanazotoa serikalini kwa kuonesha risiti na upande wa serikali kwa maana ya kilichopokewa, ilibainika upungufu wa sh. bilioni 20," alisema Bw. Kabwe ambaye pia ni Naibu Katibu Mtendaji wa CHADEMA.

Alisema kuwa ukaguzi huo ulifanyika katika mwaka wa fedha wa 2008/2009 ambapo upotevu wa fedha hizo ulipobainika na akasema kuwa wizara husika ilipobanwa kuhusiana na suala hilo ilieleza kuwa nyaraka zinazohusiana na fedha hizo zimeshateketezwa.

"Inashangaza kuona nyaraka za serikali tena zenye umuhimu kama huo zinachomwa moto kwa muda wa mwaka mmoja...tunaomba CAG achunguze suala hilo tena kwa muda wa miaka 10 iliyopita kwa kuwa inaonesha kuna kundi fulani linanufaika na fedha hizi," alisema Bw. Kabwe.

Akizungumzia suala la misamaha ya kodi kwa kampuni za utafiti wa mafuta, alisema kuwa haikuwa na sababu yoyote kutolewa kwa kuwa baada ya kipindi kifupi Tanzania itakuwa ni nchi pekee ambayo haina mshindani katika mafuta na gesi.

"Hatuna sababu yoyote ya kuendelea kutoa vivutio kwa wawekezaji katika sekta hizi, na ninashangaa kuona Wizara ya Fedha kushikilia msimamo wa kutoa misamaha hiyo tena kwa muda mrefu huku suala hili likiwa limekataliwa na Kamati ya Fedha na Uchumi...hivi kwa mazingira haya tukisema mmehongwa mtakataa?" alisema Bw. Kabwe.

Akizungumzia suala la kupandishwa kwa kodi ya mafuta ya taa, alipendekeza fedha hizo zielekezwe katika mradi wa usambazaji umeme vijijini (REA) ili wananchi wapate umeme na hatimaye kupunguza gharama za maisha.

"Ili wananchi wetu waone tunawapa unafuu ni lazima sasa fedha hizi zielekezwe kwenye umeme ili matumizi ya mafuta ya taa yapungue na hapo watapunguza gharama kwani suala hili limefanyika kwa nia njema ya kupambana na tatizo la uchakachuaji wa mafuta," alisema Bw. Zitto.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Bi. Suzan Kiwanga (CHADEMA), alisema kuwa ili nchi hii iendelee ni lazima serikali iachane na starehe inazoendekeza kama za kutenga sh. milioni 1,900 kwa ajili ya chai ya ikulu.

Alisema kuwa inashangaza kuona mwaka jana fungu hilo lilitengewa sh. milioni 300 ambayo kwa mwaka huu imepanda na kufikia sh. milioni 1,900.

"Wakati uchumi ukikua taratibu matumizi yanakuwa mengi, serikali iache haya mambo ya chai ili fedha hizi ziende kwenye maendeleo, hatuwezi kuendelea kwa starehe hizi," alisema Bi. Kiwanga.

Alishauri kuwa ili mambo yaweze kutekelezeka ni lazima serikali ijielekeze katika jambo moja ambalo litazaa matunda na sio kuwa na vitu vingi ambavyo havitekelezeki.
 
Back
Top Bottom