Ya Kanali Fabian Massawe niliyoyatabiri yametimia -- Sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera!!!

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
Kona ya Karugendo

karugendo_0.jpg


Privatus Karugendo
28 Sep 2011
Toleo na 205




  • Amepewa u-RC kuua kabisa Upinzani Kagera
UCHAGUZI Mkuu wa 2005, jimbo la Mtwara Mjini lilikuwa na upinzani mkubwa. Kulikuwa na upinzani mkali ndani ya CCM kumpata mgombea wake. Ilikuwa ni kazi ngumu kweli; fedha, ubabe na kujuana vilitumika kumpata mgombea.

Yule aliyeshinda kura za maoni, jina lake lilitupwa kule Dodoma na kujenga makundi mawili yanayopingana ndani ya CCM jimbo la Mtwara Mjini. Baadaye kulikuwa na upinzani wa vyama vya siasa na NCCR Mageuzi kikaonyesha nguvu kubwa ya kupambana na CCM.

Hata hivyo, nguvu kubwa na fedha nyingi zilitumika kuhakikisha jimbo la Mtwara Mjini halianguki mikononi mwa wapinzani. Aliyekuwa mkuu wa wilaya, alisimama imara na alifanya kazi ya ziada kuhakikisha ushindi unakuwa wa CCM.


Baada ya uchaguzi, mkuu huyo wa wilaya aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa mkuu wa Mkoa wa Lindi, na sasa amehamishiwa Dar es Salaam.


Katika uchaguzi huo wa 2005, mimi nilikuwa mwangalizi wa uchaguzi huo wa TEMCO, na katika ripoti yangu, pamoja na mambo mengine mengi ya uchaguzi huo katika Mkoa wa Mtwara, niliweka bayana kwamba Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, alipandishwa cheo kuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi kama "zawadi" ya kuhakikisha jimbo la Mtwara Mjini linabaki mikononi mwa CCM.


Ni wazi baada ya tukio hilo la mkuu wa wilaya kupandishwa cheo kama zawadi, yametokea matukio mengine mengi ya vyeo mbalimbali kutolewa kama zawadi au shukrani ya kukilinda na kukitetea Chama cha Mapinduzi.


Ni dhahiri sasa kwamba wakuu wa wilaya wanaohakikisha majimbo kwenye wilaya zao hayachukuliwi na upinzani wanapandishwa kuwa wakuu wa mikoa au vyeo vingine vya juu zaidi.


Kadhalika wakuu wa mikoa wanaohakikisha majimbo yote kwenye mikoa yao hayaendi upinzani wanapandishwa kuwa mawaziri au vyeo vingine vya juu zaidi. Wanaofanya kinyume wanatoswa na kuwekwa pembeni.


Baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2010, niliandika makala juu ya vurugu zilizotokea Karagwe, na hatimaye Tume ya Uchaguzi kumtangaza mgombea wa CCM mshindi kinyume kabisa na matarajio ya wapiga kura wa jimbo la Karagwe.


Kwa faida ya wale ambao pengine hawakupata kuisoma makala hiyo, na kwa vile yale niliyoyatabiri ya mkuu wa wilaya kuzawadia ukuu wa mkoa kwa kuhakikisha majimbo yote ya Wilaya ya Karagwe yanabaki CCM yametokea, narudia sehemu ya makala hiyo. Niliandika hivi:


"Naandika makala hii kama wito kwa wapenda amani, demokrasia, na watu wenye busara na hekima kushirikiana pamoja kulaani kitendo kilichotokea kule Karagwe cha jeshi la polisi kuwapiga mabomu na risasi za moto wananchi waliokusanyika kwenye ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Karagwe kusubiri majibu ya kura za mbunge wao. Watu waliumizwa, walitishwa na wengine wamelazwa hospitali.


Mbaya zaidi matokeo ya uchaguzi mkuu yalitangazwa chini ya ulinzi mkali wa polisi. Haiwezekani mwakilishi wa wananchi kutangazwa chini ya ulinzi mkali wa polisi. Hili ni jambo la kulaani na kuonya kwamba hili halivumiliki.


Watu wamepigwa mabomu na risasi za moto na wengine hadi leo hii wako hospitali. Serikali imetumia Jeshi la Polisi kushinikiza Tume ya Uchaguzi katika Jimbo la Karagwe kumtangaza mshindi wa CCM, Gosbert Blandes.


Wananchi waliopiga kura walikusanyika kwenye ofisi ya Mkurugenzi wa Wilaya ya Karagwe baada ya kuitwa kusikiliza matokeo. Na kufuatana na watu walivyopiga kura, walikuwa na imani ya kutangazwa mgombea wa upinzani.


Kwa kuogopa hilo, Serikali iliagiza polisi kutoka Bukoba mjini kuja Kayanga kuwatisha na kuwatawanya wananchi waliokuwa wakisubiri matokeo. Na mbaya zaidi ni kwamba baada ya kuwatawanya wananchi hao, jeshi la polisi lilivuka mipaka na kuingia sokoni Kayanga na kuwapiga mabomu ya machozi watu waliokuwa sokoni wakijifanyia shughuli zao.


Habari tulizozipata kutoka Karagwe ni kwamba baada ya kuwatawanya watu, kesho yake jeshi la polisi lilizingira Ofisi ya Mkurugenzi na matokeo ya uchaguzi kutangazwa chini ya ulinzi mkali.


Baada ya matokeo, mshindi aliyetangazwa, Gosbert Blandes alisindikizwa kwa ulinzi mkali kupanda ndege kuondoka Karagwe, na baada ya siku moja alionekana Karagwe akisindikizwa na polisi kuelekea kijijini kwao. Kwa nini mwakilishi wa wananchi asindikizwe kwa ulinzi wa polisi?


Kuingilia uhuru wa watu kumchagua mwakilishi wanayempenda ni kitu kisichovumilika. Kama wanavyosema watu wa Karagwe, kuingilia uhuru wa uchaguzi wao ni sawa na kuibaka demokrasia. Wananchi hawa wameporwa haki yao na jambo hili ni la kupigia kelele. Ni jambo la kulaani.


Kuna uvumi tunaousikia kwamba wakuu wa wilaya wamepewa ahadi ya kupandishwa kuwa wakuu wa mikoa kama watahakikisha majimbo katika wilaya zao hayachukuliwi na wapinzani. Hivyo ni kazi yao kufanya wawezavyo ili CCM ipate ushindi hata kama kura zinasema vinginevyo.


Hili likitokea kwa Karagwe; kwamba watu wameporwa haki yao ya kumchagua mwakilishi wanayempenda, wamepigwa mabomu na kuumizwa ili mkuu wa wilaya apate ukuu wa mkoa; laana hii itamwandama huyu Mkuu wa Wilaya ya Karagwe hadi vizazi vijavyo"


Hivyo ndivyo nilivyoandika wakati ule. Wakati nikiandika makala hiyo, sote tulifikiria ni uzushi au uvumi tu; maana rais wa nchi anayewapenda watu wake, hawezi kukubali kuzima uhuru wao wa kuchagua kwa kumpandisha mtu cheo.


Kumbe haukuwa uzushi wala uvumi. Ni ukweli; maana sote tumeshuhudia aliyekuwa mkuu wa wilaya wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2010, Kanali Fabian Massawe, ameteuliwa kuwa mkuu wa mkoa, na kama kejeli vile kwa watu wa Karagwe, ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera ili ahakikishe anaua upinzani mkoa wa Kagera!


Hapa sizungumzii utendaji kazi wa Kanali Fabian Massawe; bali nazungumzia yeye kupandishwa cheo kuwa mkuu wa mkoa baada ya uvurundaji ule wa uchaguzi jimbo la Karagwe.


Kuna ushahidi wa kutosha kwamba Kanali Massawe amesimamia usafi wa mji wa Kayanga. Atakumbukwa kwa jambo hilo. Pia ni kwamba alipambana vilivyo na wale waliokuwa wakivusha kahawa kwa magendo na kuziuza nchi jirani ya Uganda.


Tumesikia pia alivyoshughulikia tatizo sugu la mimba mashuleni, na hivyo si kwamba naandika bila kutambua mazuri ambayo Kanali Massawe ameyafanya kule Karagwe.


Ninachopinga ni utamaduni huu wa CCM wa "kuwazawadia" watu vyeo baada ya kuhakikisha ushindi unapatikana; hata kama ushindi huo umepatikana kwa njia ambazo si za haki.


Hapana shaka kwamba wananchi wa Karagwe watakuwa wameliona hili; kwamba Kanali Massawe "amewatumia" kupanda cheo. Aliuzika uhuru wao wa kujichagulia mtu wanayemtaka ili yeye afufuke akiwa na cheo kikubwa na labda baada ya kuhakikisha ameua kabisa upinzani mkoani Kagera apande zaidi ya hapo.


Ni wakati wa wananchi wa Karagwe kusema hapana! Wasimame pamoja na kusema: Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumeibiwa kura zetu kiasi cha kutosha, tumeporwa ushindi wetu kiasi cha kutosha, sasa tunataka mabadiliko!

 
Pengine haya yaliyoandikwa yanakaukweli. Lakini kwa nini japo kidogo tusijaribu kufikiria kuwa Kuufanya mji wa Kayanga safi, kudhibiti magendo ya kahawa, kuwabana mafataki...zisiwe sifa zilizompa mkoa na badala yake tuangalie tu kudhibiti wapinzani? Hebu tupeni sababu za kwa nini tuamini anavyoamini mwandishi aliyejichanganya badala ya the other side of the coin!
 
Back
Top Bottom