Wizara tatu kufanya kazi kwa ushirikiano

Jul 24, 2012
81
6
jumaa, Agosti 24, 2012 05:48 Benjamin Masese na Adelina Rutale, Dar es Salaam WIZARA tatu, zimesaini mkataba wa pamoja wa ushirikiano ujulikanao kama ‘participation agreement’, ili kukabiliana na tatizo sugu la uchafu na ukosefu wa maji shuleni na vijijini.

Wizara hizo ni Wizara ya Maji, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, baada ya kusaini mkataba huo, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Bashiri Mrindoko, alisema lengo la ushirikiano huo ni kuongeza ufanisi wa kutekeleza programu ya usafi wa mazingira na upatikanaji wa maji safi na salama.

“Utekelezaji wa mpango huu ndani ya miaka minne, umelenga kushawishi kaya 1,300,000 kujenga na kutumia vyoo vilivyo bora.

“Chini ya utaratibu huu, shule zaidi ya 700 zenye hali mbaya kiusafi na ambazo hazina maji, zitanufaika kwa kuboreshewa miundombinu ya maji na vyoo.

“Fedha za utekelezaji wa usafi wa mazingira vijijini kwa muda wa miaka minne, zimekadiriwa kuwa Dola za Marekani milioni 20, sawa na Sh bilioni 30 za Tanzania, kati ya fedha hizo, Sh bilioni 7.1, tayari zimeshatolewa katika mwaka wa fedha 2012/2013.

“Hivyo basi, kutokana na ushirikiano huo, tumegawana majukumu ambapo Wizara ya Maji, itabaki na jukumu la kutafuta fedha na kufanya uratibu wa utekelezaji, Wizara ya Elimu na TAMISEMI, zitakuwa na jukumu la kuhakikisha maji katika shule zote yanapatikana kuanzia ngazi ya wilaya hadi mkoa.

“Wizara ya Afya, itakuwa na jukumu la kushirikiana na TAMISEMI kuhakikisha malengo ya mkataba wa Participation Agreement, yanafanikiwa kusimamia matumizi ya fedha na kuandaa taarifa za matumizi hayo na kuziingiza kwenye mtandao wa kompyuta (MIS),” alisema.

Alisema programu hiyo, inafadhiliwa na Serikali na washirika wa maendeleo na unatekelezwa katika halmashauri 132 na kwamba, programu hiyo ilianza kutekelezwa mwaka 2006, chini ya Wizara ya Maji.

Alisema kuwa dhumuni kuu la usafi wa mazingira vijijini ni kuboresha usafi wa majumbani na shuleni kupitia mbinu mbalimbali za uhamasishaji jamii.

Naye mwakilishi kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Elias Shinamo, alisema zaidi ya asilimia 70 ya magonjwa ya Watanzania, yanatokana na uchafu wa mazingira na kunywa maji yasiyo salama.

Alisema programu hiyo, itasaidia kupunguza idadi ya vifo vya Watanzania wanaokufa kutokana na maradhi yatokanayo na uchafu wa mazingira na maji, wakiwamo watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
 
Back
Top Bottom