WITO KUSHIRIKI KWENYE MJADALA WA WAZI WA MUSWADA WA KATIBA KESHO KARMJEE HALL .
Wito unatolewa kwa kila mpenda maendeleo na mpenda Nchi yetu kesho tarehe 07/04/2011 ahakikishe kuwa anawezaa kutenga muda wake na kushiriki katika mjadala wa wazi (public hjearing) utakaofanywa na kamati ya Bunge ya katiba na sheria katika ukumbi wa Karimjee kwa DSM na ukumbi wa Msekwa kule Dodoma .Kwa upande wa Zanzibar bado haijajulikana ukumbi utakuwa wapi ila sehemu ya kamati ya bunge wajumbe wake wataenda Zanzibar .
Ni muhimu sana kushiriki zoezi hili na tuache kulalamika kwenye maandishi yetu kwani ikumbukwe kuwa sheria zote mbaya za Nchi hii zilipitishwa kwa hati ya dharura kuwasilishwa bungeni , najata baadhi ya sheria hizo;
1. Sheria ya hati za Muungano
2. Sheria ya kuweka watu kizuizini
3. Sheria ya wahujumu uchumi
4. Mabadiliko ya katiba ya mwaka 1977
5. Sheria ya gharama za uchaguzi.
Ukiangalia mifano ya hizo sheria utaona wazi kuwa kama serikali inataka kuficha ama kuweka jambo ambalo halina manufaa kwa wananchi ila kwa watawala utaona wazi kuwa wanawasilisha sheria chini ya hati ya dharura.
Kushiriki kwako kesho utaweza kusaidia kuifanya serikali ikasikiliza kwani wingi wa watu utawafanya wajue kuwa wananchi wako serious kwenye jambo hilo, na ikizingatiwa kuwa kesho ni sikukuu hakuna haja ya hata mmoja wetu kukosa fursa hii adimu kwani ni muhimu kwa nchi yetu sote.
Wito wangu kama uko DSM na Dodoma hebu tenga muda wako kesho kuanzia saa tatu asubuhi ukashiriki kuelezea hisia zako na hata kama hutasema ni bora tukawepo wengi ili kulilazimisha Bunge na Serikali kuongeza muda wa kutusikiliza.
Bunge na wabunge lazima wajue kuwa wao ni wawakilishi wa wananchi , hivyo jambo kubwa kama hili wanapaswa kuwashirikisha kwanza wananchi , waende majimboni wakawaulize waliowatuma wanataka mchakato uwe wa aina gani, na sio kutuburuza.
Hivyo , nawaomba wale wote kesho tukutane kwenye kutoa maoni yetu ili nsiku zijazo tusiishie kusema kuwa hatukushiriki wakati fursa ndio hii.
Msimamo wangu ni kuwa hakuna haja ya kujadiliwa kwa dharura sheria muhimu kama hii, tuna muda, wabunge waje wakatusikilize ndipo wapeleke maoni yetu ndani ya Bunge na sio mawazo yao kama wanavyotaka kufanya sasa.
Ewe mwana JF hii ni fursa ya wewe kuchangia katika kuleta mabadiliko unayotaka kuyaona , tuache kulalamika na muda wa kuchukua hatua ni sasa.
Mungu ibariki Tanzania.