Wenye simu za mkononi kubanwa

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,007
Wenye simu za mkononi kubanwa
Basil Msongo
Daily News; Wednesday,January 28, 2009 @21:15​

Kuanzia Machi mosi mwaka huu watumiaji wote wa simu za mkononi nchini, hawataruhusiwa kuficha namba zao za simu wanapowapigia watumiaji wengine wa huduma hiyo ya mawasiliano.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeziagiza kampuni zote za simu za mkononi, kwamba kuanzia Machi mosi mwaka huu, zihakikishe zinaingiza mfumo utakaowezesha kutambulisha namba (CLI) ili kudhibiti matumizi ya 'private'.

Taarifa ya TCRA kwa umma ilieleza jana kuwa lengo la uamuzi huo ni kukomesha vitendo vya watumiaji wachache wa simu za mkononi wasio wastaarabu, kutumia huduma hiyo visivyo.

“Pamoja na ukweli kuwa watumiaji wengi ni waaminifu, wanaheshimu sheria na ni wastaarabu, kuna wachache ambao wanatumia huduma hii visivyo,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya Mkurugenzi Mkuu wa TCRA. Kulingana na taarifa hiyo, mchakato wa kutungwa sheria itakayowalazimisha wote wanaotumia simu za mkononi wasajili, unaendelea.

Kampuni ziliagizwa kutekeleza utaratibu wa kuruhusu namba zote zilizoko kwenye mitandao ya wateja wao kutambulika kwa mpokeaji wa simu na kwamba uamuzi huo si hiyari. TCRA pia imeziagiza kampuni za simu za mkononi, kuanzia Julai mosi mwaka huu kusajili wateja wote wapya wa huduma ya malipo kabla, ndipo ziwauzie laini za simu za mkononi.

“Wateja wengine wote ambao laini zao hazijasajiliwa, wanapaswa kusajiliwa na kampuni ya simu husika wanakopata huduma kuanzia Julai mosi mwaka huu,” ilisema taarifa hiyo. Kwa mujibu wa TCRA, wateja wa huduma za M-Pesa, E-Fulusi, Mobipawa na M-Commerce wataendelea kusajiliwa kwa utaratibu ambao tayari unatumika pamoja na unaofanywa kwa wateja wanaolipa baada ya huduma.
 
Back
Top Bottom