Wenje awasuluhisha CCM, CHADEMA

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
Deus Bugaywa


Mwanza


234_wenje.JPG



Wenje akikabidhi misaada


Wachangia Elimu ya Nyamagana
Joto la uhasama wa Kirumba chini


HARAMBEE ya kuchangia mfuko wa elimu wa Jimbo la Nyamagana hapa, iliyoitishwa na mbunge wa jimbo hilo, Ezekiah Wenje (CHADEMA), imefanya kile ambacho hakikutarajiwa.

Harambee hiyo imepunguza hisia za chuki na uhasama zilizotawala wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wa Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya matukio na uchaguzi wa udiwani wa Kata ya Kirumba.

Ushiriki wa viongozi wa CCM katika harambee hiyo ulionyesha kuwa katika suala la maendeleo wananchi wote wanatakiwa kushikamana na kusahau tofauti zao kisiasa, lakini pia uliwafanya washabiki wa CHADEMA kupunguza munkali uliotokana na kukatwa mapanga kwa wabunge wao, Highness Kiwia na Salvatory Machemli katika vurugu zilizohusishwa na uchaguzi huo wa Diwani kata ya Kirumba.


Wafuasi wa CHADEMA wamekuwa wakiwatuhumu wafuasi wa CCM kuwa ndio waliohusika na huku wa CCM nao wakiwanyooshea kidole wale wa CHADEMA kuwa chanzo cha vurugu zilizosababisha wabunge hao kujeruhiwa.


Katika harambee hiyo mbunge wa Rorya kwa tiketi ya CCM Lameck Airo, kupitia kampuni ya La kairo Investment alichangia kiasi cha shilingi milioni tano, Mbunge wa Bumbuli Januari Makamba alichangia shilingi milioni tatu, Mbunge wa Kibaha Vijijini Abuu Juma (CCM) shilingi milioni moja, mweka hazina wa CCM Mwigulu Nchemba alichangia shilingi laki tano na wabunge wa viongozi wengine wa CCM nao wakachangia.


Wakati wa kampeni za CCM kwenye uchaguzi wa Kata ya Kirumba Mbunge wa Rorya, Airo, kwa kushirkiana na mfanyabiashara maarufu hapa na mjumbe wa NEC ya CCM, Mwita Gachuma, waliahidi kujenga barabara katika kata hiyo na kutoa madawati kwa shule za kata hiyo ikiwa mgombea wa CCM angeshida uchaguzi huo.


Hata hivyo ahadi hizo zilishambuliwa vikali katika majukwaa ya kampeni za CHADEMA kuwa vigogo hao wamekuwepo siku zote na wanayaona matatizo ya Kirumba hawakuwahi kutaka kuwasaidia na kuwaonya wananchi waepukane na ahadi hizo hewa.

“Hatua hii ya Lakairo kuamua kuchagia katika harambee hii kwa ajili ya elimu Nyamagana inaonyesha uzalendo wa kweli uaovuka mipaka ya vyama vya siasa linapokuja suala la maendeleo, na hii imekuwa ni kitu kizuri kwa sababu umeona vijana hawa walivvyoshangilia. Hii ni ishara kuwa wameridhika na hata ule uhasama wao na wana CCM utapungua” alisema mzee Sospeter Mchele mkazi wa Kirumba aliyehudhuria mkutano huo uliofanyika katika viwanja vya Sahara.

Tangu kukatwa mapanga wabunge wa CHADEMA alfajiri ya Aprili Mosi, kuamkia siku ya uchaguzi wa Kata ya Kirumba, kumekuwa na hali tete katika Jiji la Mwanza na hasa katika kata hiyo ambapo wafuasi wa CCM na CHADEMA wamekuwa wakitishana kulipiziana visasi wenyewe, huku pande zote zililaumu Polisi kupendelea upande mmoja.


Hali hiyo ya uhasama na mvutano wa vyama imefanya baadhi ya vijana waliokuwa wakishiriki katika kampeni za vyama hivyo wakiwa mstari wa mbele kuukimbia mji na wengine kuishi kwa kujificha ficha kuhofia kushambuliwa na kundi la wapinzani wao.


Baada ya kuona tatizo hilo linaelekuwa sugu kamati ya ulinzi na usalama Mkoa wa Mwanza imemuelekeza Mkuu wa Wilaya ya Ilemela kuunda kamati ya haki na jinai ili kutafuta suluhu miogoni mwa wanajamii wa Kata ya Kirumba.


“Hili sasa ni tatizo la kijamii, hii kamata kamata inaweza isisadie sana kulimaliza, kwa hiyo tumeamua kuunda kamati ya haki na jinai itakayoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela. Hii itahusisha watu wa vyama vyote, viongozi wa dini, wanaharakati na hata ninyi waandishi mnaweza kuwemo ili kuzungumza na kuambiana ukweli,” Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, aliwaambia waandishi wa habari wiki jana baada kumaliza kikao cha kamati ya ulinzi na usalama.


CHADEMA wamekuwa wakihamasisha wafuasi wao kuwashughulikia watuhumiwa ambao wanahisi ndio waliohusika kwa namna moja ama nyingine kujeruhi wabunge wao na CCM nao wamekuwa wakifanya hivyo hivyo kwa watu wanaodhani waliwanyima ushindi.

CHADEMA pia kimekuwa kikitaka Polisi kuwakamata baadhi ya viongozi wa CCM wanaodaiwa waliohusika katika tukio la kukatwa mapanga kwa wabunge wao na kuwahoji baadhi ya vigogo wa CCM ambao magari yao yalionekana eneo la tukio.

Akihutubia mkutano wa kuwashukuru wananchi wa Kata ya Kirumba kwa ushindi waliopata katika uwanja wa Magomeni Mbunge wa Nyamagana Wenje alisema Polisi wanajua watu waliokuwapo eneo la tukio kwa sababu baadhi ya viongozi wa CHADEMA waliokuwapo eneo hilo wamehojiwa na kuwataja wote waliokuwapo na magari yaliyoonekana eneola tukio.


Katika mkutano huo pia Wenje alimtaja Diwani wa Kata ya Mkolani, Stanslaus Mabula, kuwa alihusika katika tukio la kumpiga risasi mama mmoja eneo la Ibanda Ziwani, ambaye alikuwa mmoja wa akina mama waliokuwa wamekusanywa usiku huo nyumbani kwa Balozi wa CCM Jenga Mtera, eneo la Ibanda Ziwani na kumtaka Kamanda wa polisi kuchukua hatua.


“Barlow (Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza) aeleze ukweli kuna kitu gani anataka kuficha. Wametuita Polisi tumetoa maelezo na kuwaeleza kulikuwa na magari ya viongozi wa CCM yalionekana eneo la tukio. Nasikia anasema wabunge walipigwa na wananchi wenye hasira. Wananchi hao walitoka wapi usiku huo na waliingia vipi kwenye magari ya CCM?”, alihoji Wenje.


Siku tatu baada ya tukio hilo Kamanda Barlow aliwaambia waadishi wa habari kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa wabunge waliojeruhiwa walipigwa na wananchi wenye hasira kali. Kauli hiyo ya Kamanda, hata hivyo, ilitofautiana na kauli aliyotoa siku ya tukio hilo kuwa wabunge hao walishambuliwa na washabiki wa CCM, hali ambayo ilizidi kuwachanganya wananchi na hasa wafuasi wa CHADEMA.


Hata hivyo, Diwani Mabula amekanusha kuhusishwa na tukio hilo, na aliliambia Raia Mwema kuwa Wenje ni mzushi na akawataka wananchi wasiendelee kuamini maneno hayo ya uchochezi.


“Nimesikia amenitaja kwenye mkutano huo. Mimi sijawahi kumiliki silaha na hata Ibanda Ziwani sijawahi kufika na sipajui. Ninawaomba wananchi wa Kata ya Mkolani waendelee kuniamini. Sijahusika na tukio hilo, ” alisema Mabula.


Alieleza pia kuwa ana mipango ya kumchukulia hatua za kisheria Wenje kwa kumtuhumu katika tukio ambalo hahusiki.


Chama cha Mapinduzi kwa upande mwingine kimekuwa kikilia na jeshi la polisi kwa kuwaachia vijana wa CHADEMA kuwakamata wafuasi wao na kuwafanyia vurugu hatua ambayo ilimfanya katibu wa chama hicho, Wilaya ya Ilemela, Shaibu Akwilombe, kulionya jeshi hilo lisipochukua hatua kuwadhibiti wao wataelekeza vijana wao pia wajibu mapigo.


Hata hivyo, Kamanda Barlow aliwaonya viongozi hao wa vyama kuacha kauli za kuhasimiana kwa kuwa kufanya hivyo ni kuendelea kuchochea vurugu katika hali ambayo tayari ni tete.


Baada ya harambee hiyo mtazamo wa vijana wengi hasa wa CHADEMA ulionekana kubadilika, vijana hao walionekana katika makundi makundi wakijadiliana na kuelezana kwa huo walionyesha wana CCM ndiyo siasa na wanatakiwa wawe hivyo siku zote na wasiendekeze chuki.


“Kaka siku za karibuni tulikuwa hatuendi Kirumba ukionekana huko vijana wa CCM wanakwenda kuripoti kwa wakubwa wao kuwa kuna vijana mamluki wamekuja, na wanaanza kukufuatilia nyendo zako” anasema Juma Msafiri kijana machinga anayeishi Mtaa wa Igogo.


Harambee hiyo pamoja na kusaidia kupunguza mvutano wa wafuasi wa vyama hivyo, imechukuliwa na wengi kama ni njia muafaka ya kuwashirikisha wananchi katika harakati za kujiletea maendeleo badala ya kushiriki kuchangia shughuli za kijamii tu kama harusi.


“Mimi nimesoma zamani, na sisi tumesoma vizuri. Leo mimi sina hata shilingi moja, lakini nimeamua kutoa kitoweo hiki (kuku) ambacho wangekula wanangu Pasaka ili auzwe kwa mnada kuchagia elimu ya watoto wetu” alisema Mzee Carol Kagwisage, aliyetoa kuku ambaye alinadiwa kwa shilingi 206,000.


Mgeni rasmi katika harambee hiyo Katibu wa Waziri Mkuu wa Kenya, Carol Omondi ambaye pamoja na kuchangia shilingi za Kitanzania milioni 12, kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu wa Kenya, aliwaasa Watanzania kuwa na moyo wa kujenga nchi badala ya kutegemea wafadhili.


“Sisi Waafrika lazima tuchukue jukumu la kujenga nchi zetu, si kutegema Wazungu. Hizi juhudi za mbunge wenu zimenifurashisha kwa sababu nimeona watu wa aina mbalimbali, matajiri na masikini kila mtu anachangia bila ubaguzi,” alisema katibu huyo.


Akizungumzia harambee hiyo, Mbunge Wenje alisema kuwa aliamua kubuni utaratibu huo tokea mwaka jana ili kusadia sekta ya elimu katika jimbo hilo kusadia pale juhudi za serikali zinapoishia.


Mwaka jana ilifanyika harambee ya ndani ambayo iliwezesha jimbo hilo kununua madawati 500 kwa ajili ya shule za msingi na sekondari katika jimbo hilo.


“Nimeanzisha taasisi ya Nyamagana Education Fund ili kusaidia matatizo yote ya elimu jimboni. Mwaka huu tunatarajia kumaliza au kupunguza sana matatizo ya madawati. Baada ya hapo tuelekeze nguvu kwenye ujenzi wa maabara, vyoo na vyumba vya madarasa,” alisema Wenje.


Alisema tofauti na mwaka jana mwaka huu ameamua kuweka harambee ya hadharani ili kuwashirikisha wananchi wote kwa ujumla wao kama njia ya kuwafanya wawe na uchungu na mali zao zinapoharibiwa.


“Hii inasaidia kwanza kuwashirikisha ili wajue kuwa maendeleo lazima yatokane na wao, lakini pia wanakuwa na umiliki wa mali hizi, hawataachia ziharibiwe huku wanaona kwa kuwa wanajua jasho lao ndilo lilinunua,” alifafanua.


Katika harambee hiyo jumla ya shilingi 50, 685, 000 zilipatikana ambapo shilingi milioni tano kati ya hizo zilitokana na michango ya wananchi wa kawaida walizochangia katika mkutano huo wa harambee.
 
Hivyo ndivyo inavyotakiwa kwenye Siasa, Henje umefanya Vizuri; lakini kama ni Chama tawala Ufitina ungeendelea na nakumbuka CCM wakati wa Nyerere kilikuwa ni chama cha Upendo hakuna fitna
 
Hao wachangiaji wanaccm walikuwa na baraka za viongozi wa ccm, hasa Katibu Mkuu Mzee Mukama? Kama sivyo sitashangaa kusikia wamelimwa barua za onyo kwa kukihujumu chama chao. Tukumbuke Katibu mkuu wao ndio kiranja mkuu wa mambo yote. Si mlicheki Katibu Mkuu Yusuf Makamba alivyowapiga ban wagombea kushiriki midahalo ya "Mchakato Majimboni" hadi kibarua cha Mhando pale Tbc aka tbccm kikaota nyasi kwa "kuhujumu chama na kukipunguzia kura" baada ya uwezo wa watu wao kuanikwa!
 
Back
Top Bottom