We need more Viulas

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,011
Mkapa asilipwe mafao - Kiula

2008-02-27 08:54:20
Na Joseph Mwendapole


Waziri wa zamani wa Ujenzi wa Serikali ya Awamu ya Pili, Bw. Nalaila Kiula, ameishauri serikali kusitisha mafao na marupurupu ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa, kwa madai kuwa alikiuka maadili ya uongozi kwa kufanya biashara akiwa Ikulu.

Pia amemtuhumu kiongozi huyo kuwa alichokifanya wakati wa utawala wake, ni uroho wa mali na kwamba hakuwa na sababu ya kufanya hivyo.

Aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu ufisadi na rushwa serikalini.

Alisema hakuna sababu ya kuendelea kumpa mafao kiongozi ambaye hakuwa mwadilifu na aliyekiuka maadili ya dhamana aliyopewa.

Bw. Kiula ambaye alikuwa Waziri wakati wa awamu ya Rais Ali Hassan Mwinyi, alisema anamwonea huruma Bw. Mkapa kutokana na tuhuma nyingi anazokabiliwa nazo wakati wa uongozi wake.

``Hata Ibara ya 17 ya Katiba ya CCM inasema kiongozi atosheke na asiwe na tamaa ya mali,`` alikumbusha Bw. Kiula ambaye alikuwa Mbunge wa Iramba Singida kwa miaka 20.

Alisema anashangaa kuona rais huyo anafanya biashara akiwa madarakani wakati analipiwa kila kitu na kupewa huku akihudumiwa na serikali hadi mwisho wa maisha yake.

Bw. Kiula ambaye alikuwa Waziri wa Ujenzi kati ya mwaka 1991 hadi 1995, alisema: ``(Mkapa) aliingia kwa mbwembwe kuwa hatakuwa na suluhu na rushwa lakini akaishia kuwa mfanyabiashara? Rais ana mafao mengi lakini inashangaza kuona mtu kama Rais anakuwa na tamaa,`` alidai.

Bw. Kiula aliwaambia waandishi wa habari kuwa kuna haja kwa Bw. Mkapa kutoa maelezo dhidi ya tuhuma zinazoelekezwa kwake badala ya kusingizia kuwa anapumzika na amestaafu.

Waziri huyo wa zamani alisema ana uhakika tuhuma kuwa Rais mstaafu alikopa Dola 500,000 za Marekani ili afanyie biashara ni za kweli.

Aidha, alisema inashangaza kuona yeye (Kiula) alipokopa Sh. milioni 12 ikawa nongwa na kufunguliwa mashitaka ya rushwa.

``Mimi nilikopa Sh. milioni 12 nikapatwa na msukosuko mkubwa sana lakini huyo aliyekopa dola 500,000 hakuguswa,`` alihoji.

Alisema Bw. Mkapa alifanya hivyo kwa kuwa hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere hakuwepo wakati huo na kwamba angekuwa hai asingethubutu.

Akizungumzia kesi ya tuhuma za rushwa dhidi yake, alidai ilipandikizwa kwa chuki binafsi za Rais Mkapa kutokana na umaarufu aliokuwa nao wakati huo.

``Wakati Mzee Mwinyi ananiteua kuwa Waziri wa Ujenzi alinisifu sana kuwa ni kijana mchapakazi na mwadilifu na alikuwa akinisifu mara kwa mara sasa naona hapo ikawa nongwa na gere,`` alidai Bw. Kiula ambaye mpaka mwaka 2000 alikuwa Mbunge wa Iramba.

Aliongeza kuwa hata Mzee Rashid Kawawa alikuwa akimsifu kwa utendaji wake na kwamba hali hiyo huenda ndiyo ilimfanya achukiwe.

Waziri huyo wa zamani pamoja na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. George Mlingwa, walikuwa watuhumiwa wa kwanza kufikishwa mahakamani kwa rushwa.

Kesi yao ilifuatia ripoti ya kamati ya Jaji Warioba ya kuchunguza na kubainisha mianya ya rushwa iliyotolewa mwaka 1996.

Katika kesi hiyo, Bw. Kiula alionekana hana hatia lakini mahakama ilimuona Bw. Mlingwa akiwa na hatia. Mlingwa alikata rufaa.

SOURCE: Nipashe
 
Richmond yamuibua Kiula

na Amana Nyembo
Tanzania daima~Sauti ya Watu

KASHFA ya Richmond iliyomlazimisha aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa na mawaziri wengine wawili kujiuzulu na hatimaye Baraza la Mawaziri kuvunjwa takriban wiki mbili zilizopita, inazidi kuchukua sura mpya kila kukicha.
Sakata hilo la Richmond jana lilimuibua kutoka mafichoni, waziri wa zamani wa Ujenzi na aliyepata kuwa mbunge wa Iramba, Nalaila Kiula, ambaye miaka 11 iliyopita Tume ya Rais ya Kuchunguza Mianya ya Rushwa iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba, ilimtuhumu kuhusika na rushwa, hatua iliyosababisha ashitakiwe na kutiwa mahabusu kwa siku tatu.

Akizungumza na wanahabari katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Dar es Salaam jana, Kiula alieleza kushangazwa na ukimya wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa ambaye vyombo kadhaa vya habari vimemhusisha na taarifa za kukiuka maadili ya uongozi wakati akiwa madarakani.

Aidha, mbali ya hilo, Kiula alieleza kushangazwa kwake na kauli aliyoitoa hivi karibuni Jaji Warioba ya kupinga sababu za kutomhoji Lowassa kulikofanywa na Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza utata katika mkataba wa kuzalisha umeme wa dharura kati ya Richmond Development Company LLC na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe (CCM).

Akifafanua, Kiula aliwaambia waandishi wa habari kuwa anashangaa kuona mtu yuleyule (Warioba) aliyeandaa ripoti ndefu ya tume yake mwaka 1996, akimtuhumu kwa kufuja fedha za umma wakati akiwa waziri wa Ujenzi na kufikia hatua ya kutaka hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake bila ya kumpa fursa ya msingi ya kumsikiliza.

“Naamini tume ya Warioba ingeniita na kunihoji ile ripoti yao isingekuwa vile ilivyokuwa. Nimeshasamehe na Warioba atalipwa kwa mabaya aliyofanya juu yangu na mimi nitalipwa kwa mazuri yangu. Ni bahati kwamba nilishinda kesi Mahakama ya Kisutu na baadaye Mahakama Kuu nikashinda pia,” alisema Kiula.

Alisema hatua hiyo ya Tume ya Warioba ambayo aliilalamikia hata ndani ya Bunge na kufikia hatua ya kusema ana hakika Mungu ndiye atakayemlipia, ilisababisha akamatwe na akalazwa rumande siku tatu akiwa amevuliwa nguo zote na baadaye akafikishwa mahakamani.

“Warioba ameilaumu kamati ya (Dk. Harrison) Mwakyembe (aliyekuwa mwenyekiti), eti haijampa Lowassa nafasi ya kujitetea, je, yeye sasa alaumiwe na nani kwa haya anayoyafanya yasiyokuwa na msimamo, ninasema hivi kwa sababu hii ni nchi yangu.

“Niliposoma gazeti na kukuta Warioba aliyeninyima mimi fursa ya kusikilizwa akihoji sababu za Kamati Teule ya Bunge kutomhoji Lowassa, sikuamini, kwani mtu huyo ndiye yule yule ambaye mwaka 1996 aliandaa ripoti nzito dhidi yangu na akatoa mapendekezo ya mimi kuchukuliwa hatua za kisheria pasipo kunihoji. Hilo ndilo lililonileta leo hii hapa kuzungumza nanyi wana habari,” alisema Kiula.

Akifafanua huku akifunua kwa nyakati tofauti kurasa kadhaa za Ripoti ya Tume ya Warioba, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 1995, lundo la magazeti ambavyo vyote alikwenda navyo katika mkutano huo wa jana, Nalaila alimgeukia Mkapa aliyekuwa rais wakati huo na mtu aliyeunda tume hiyo na akamtuhumu kwa kukiuka maadili ya uongozi wakati akiwa madarakani.

Alisema ni jambo la ajabu kwamba, wakati akiwa madarakani, Mkapa, kiongozi ambaye wakati akikabidhiwa urais wa nchi aliahidi kuwa hatakuwa na simile na mla rushwa yeyote, yeye mwenyewe alipokuwa kiongozi alijikopesha shilingi milioni 500 benki pasipo kuwa na dhamana.

Kiula alikielezea kitendo hicho cha Mkapa kuwa ni cha ukiukwaji wa maadili ya uongozi, ambacho iwapo wanasheria watakitumia kinaweza kusababisha rais huyo mstaafu asitishiwe malipo ya marupurupu anayolipwa hivi sasa.

Alisema ni jambo la ajabu kwamba wakati Mkapa akikiuka maadili, yeye alifikishwa mahakamani akituhumiwa kujipatia sh milioni 12 tu isivyo halali, wakati ikijulikana bayana kwamba alikopa fedha hizo benki akiweka dhamana kitabu chake cha akiba ya benki kilichokuwa na sh milioni sita na kile cha marehemu mkewe kilichokuwa na sh milioni tano.

“Kama hiyo haitoshi, nilishitakiwa kwa kosa la kukopa sh milioni 12 benki ili ninunue daladala wakati ushahidi wa mkopo huo ninao na umekwenda kwa haki, lakini nilipelekwa sero wakati Mkapa aliyekuwa madarakani kwa wakati huo alikopa NBC dola 5,000,000 bila ya kuwa na dhamana yoyote. Mtu anayefanya hivi ndiye yule yule aliyesema hatakuwa na simile na wala rushwa,” alisema Kiula kwa mshangao.

Kiula alisema ni jambo baya kwa rais ambaye anapostaafu anapewa mamilioni ya fedha kuwa mdokozi, jambo alilosema anaamini iko siku tsunami itashuka na itamlazimisha Mkapa ambaye amegoma kujibu tuhuma hizi kuzijibu.

“Hivi ni kitu gani kinachokufanya wewe kama rais ambaye unapostaafu unatunzwa hadi ufe, uwe mdokozi, tena katika maeneo tofauti, EPA, Richmond, Buzwagi na IPTL? Lakini ipo siku tsunami itashuka atalazimika kujibu,” alihoji Kiula ambaye alikanusha kutumwa na mtu yeyote.

Kutokana na hilo, aliwataka wananchi kumpa Rais Jakaya Kikwete ‘gloves’ kama zile alizopewa wiki mbili zilizopita na Bunge kupitia Kamati ya Mwakyembe ili aweze kuchukua hatua za kukabiliana na watu waliokiuka maadili ya uongozi kama Mkapa.

Kiula aliyeonekana kuwa na dukuduku na Mkapa na Warioba, alisema anaamini kwamba yeye alipelekwa mahakamani na akadhalilishwa si na serikali bali watu wachache ndani ya serikali waliokuwa na malengo yao binafsi.

Alisema Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 iliitaja sekta ya ujenzi aliyoisimamia wakati akiwa waziri kuwa ni moja ya maeneo ya mfano, yaliyoonyesha mwelekeo wa mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka 10 cha kati ya mwaka 1985 na 1995.

Mbali ya hilo, alisema anaamini kuwa Bunge likifikia maamuzi kama yale ya kuitaka serikali irudishe nyumba zote za wananchi walizouziwa baadhi ya watumishi wa umma, Rais Kikwete atatekeleza maamuzi hayo mara moja bila kujali iwapo yeye (rais) naye amenunua nyumba.

Akizungumzia Ripoti ya Kamati Teule ya Mwakyembe, Kiula alimtaka Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Edward Hosea na naibu wake kuachia madaraka yao kama ilivyopendekezwa na kamati hiyo ya Bunge.

Kiula alisema bado ana nguvu na moyo wa kurudi katika siasa na tayari mwaka 2006 alikutana na Rais Kikwete na katika maongezi yao walikubaliana amtumie katika kazi zake, lakini si kumuweka katika uwaziri au ubalozi.

Aliwataka wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais Kikwete ili aendelee na kazi yake ya kusafisha wale wote wasiokuwa makini katika kazi.

Kwa upande mwingine, aliwaasa wabunge kuukataa muswada wa kuruhusu uraia wa nchi mbili utakapoletwa bungeni kujadiliwa, akisema iwapo utapitishwa kuwa sheria, wezi wanaoiba fedha kupitia mambo kama ya EPA au Richmond watapata fursa ya kuficha fedha nje ili kujijengea mazingira ya kwenda kuishi huko.

Alisema kuwa yeye anapinga sheria hiyo kwa sababu tayari baadhi ya watu wameshaanza kupeleka mabilioni ya pesa nje ya nchi ili waende kuishi huko pindi mambo yao yatakapowaharibikia hapa nchini.




 
Back
Top Bottom