Waziri Mkulo jifunze kwa mtangulizi wako

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,314
33,108
mustafamkulo.jpg Mzee Mramba Abdallah Bakari THAMANI ya Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani inazidi kushuka, huku mfumuko wa bei ukipanda na kufikia hivi karibuni asilimia 18, hivyo kuchangia ongezeko la kasi ya ugumu wa maisha kwa Watanzania. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo shilingi imeporomoka na kufikia wastani wa kati ya sh.

1700 hadi 1900 kwa dola, wakati mfumuko wa bei umepindukia asilimi 18, kiwango ambacho ni kikubwa mno ukilinganisha na enzi ya utawala wa serikali ya awamu ya Tatu iliyoongozwa na Benjamin Mkapa. Kumbukumbu zinaonesha kuwa katika utawala wa awamu ya tatu, mfumuko wa bei ulishuka na kufikia asilimia 4.5 wakati thamani ya sarafu ya Marekani ilikuwa sawa na Sh1,000. Maisha yalikuwa nafuu kiasi japo wananchi wailalamikia pia hali hiyo. Waziri wa fedha wa wakati huo, Basil Mramba, bila shaka yeye ndiye aliyemsaidia kwa karibu sana rais Benjamin Mkapa kuhakikisha kuwa thamani ya sarafu inatengamaa ili kupunguza makali ya maisha ya watanzania.

Serikali ya awamu ya nne chini ya rais Jakaya Kikwete ilipoingia madarakani iliingia na yake na mara hali ikaanza kubadilika kufuatia thamani ya shillingi yetu kuendelea kuporomoka kila uchao na taratibu mfumuko wa bei ukaanza kuongezeka kutoka tarakimu moja hadi sasa ziko mbili. Waziri wa fedha na Benki Kuu ya Tanzania wana dhima ya kuhakikisha kuwa thamani ya sarafu yeti inatengemaa. Tunaamini kuna kuna mahali fulani mambo hayaendi vyema. Kuna ulegevu na watanzania hawaambiwi ukweli kwani maisha yanazidi kupanda. Waziri Mustafa Mkulo kauli za matumaini zimechusha masikioni.

Kama Mramba aliweza kuiimarisha sarafu ya Tanzania, ukizingatia kuwa serikali ya Mkapa iliingia madarakani wakati hali ya uchumi ilikuwa mbaya zaidi na ilimaliza awamu yake uchumi ukiwa haujambo sana tu. Tunajiuliza kulikoni Mkulo na watu wake wanashindwa kuurejesha uchumi wetu kwenye reli kwa kudhibiti thamani ya sarafu yetu na kulinda mfumo wa bei. Kwa hali iliyofikia ni dhahiri kuwa upeo wa Waziri Mkulo na wasaidizi wake katika kunusuru uchumi umefika kikomo, ndiyo mwisho wa fikra zao, kunahitajika msaada kutoka kwa wengine ili tulijenge taifa lenye uchumi imara. Inaaminika kuwa kila binadamu ana mwisho wa upeo wake wa kufikiri na kutenda.

Hivyo ili kuongeza upeo ni lazima kuingizwa watu wapya, na kama suala ni la kitaaluma basi ni vema kuwaona na kuwatumia wanataaluma waliosheheni vyuo vyetu vikuu ambao kwa sasa wanajishughulisha na ufugaji wa kuku na warsha kwa kuwa hawana la kufanya. Nasema hivyo kwa sababu tunayo hazina kuwa ya watu waliofanya vizuri katika kada hiyo, ni Watanzania wenzetu, ambayo bila shaka wapo tayari kulitumikia taifa lao .

Bila shaka Mkulo anatambua kuwa yeye si wa kwanza kushika wadhifa huo, pili kuwapo kwa viongozi waliofanya vizuri katika kada hiyo ni fursa kwake ya kukimbilia kupata ushauri pale mambo yanapomuelea. Miongoni mwa viongozi hao ni Basili Mramba, ambaye kwa upeo wangu wa kufikiri aliimarisha uchumi wa Tanzania kwa kiasi kikubwa kuliko hali ya sasa, huyu kama hayupo kule Rombo, mkoani Kilimanjaro basi atakuwa Dar es Salaam na kama huko kote hayupo basi mawasiliano yake yanaweza kuwakutanisha.

Ndiye aliyewezesha serikali kuanza kutekeleza miradi mikubwa kwa fedha za ndani, rejea mradi wa maji kutoka ziwa Viktoria kwenda mikoa ya Shinyanga, mradi ambao uliwashinda wakoloni, ujenzi wa daraja la Mkapa, ujenzi wa barabara kuu za lami nchini na mengine mengi. Hii iliashiria kuwa Taifa lilianza kujitegema na kupunguza utegemezi wa misaada kutoka nje ambayo imekuwa na masharti magumu. Ni mipango ya kiuchumi iliyosababisha nchi tajiri duniani kuzifutia madeni nchi masikini, Tanzania ikiwemo. Kaondoka Mkapa na Mramba, uthubutu pia umeondoka.

Ni sera madhubuti za uchumi na zinazosimamiwa kwa utahbiti ndizo huzaa taifa lenye uchumi imara, kwa hali ilivyo ni wazi kuwa uchumi wetu utaendelea kuporomoka hadi pale nchi misingi ya uchumi mpana itakaposimamiwa vyema. Aidha, kutokana na usimamizi mbaya wa uchumi, wafanyabiashara wamekuwa wanaitisha serikali iliyowapatia leseni ya kufanya biashara zinazowavimbisha kichwa. Mgomo wa waauzaji wa petroli wa hivi karibuni ni ushuhuda wa serikali kushindwa kusimamia uchumi.

Tabia ya wafanyabiashara ya kuipuuza serikali ya kutouza bidhaa na huduma kwa kutumia fedha za kigeni itaendelea kuichimbia kaburi sarafu ya Tanzania. Serikali imetangaza mara kadhaa kupiga marufuku kulipia huduma kwa pesa za kigeni lakini hata viduka vya uchochoroni vinapokea fedha za kigeni. Serikali haijui fedha za kigeni zilizoko kwenye mzunguko.

Mkakati wowote wa kudhibiti kuanguka kwa shillingi hautashinda katika mazingira hayo. Kwa mtazamo wangu, Mkulo anastahili kubeba lawama zote. Tunasema hivi kwa sasa yeye ndiye mwenye dhamana katyika kuhakikisha kuwa uchumi wa nchi unakua na kutengemaa wakati wote. Anapaswa kuwa mbunifu na kuhakikisha kuwa uchumi unaimarika na mfumuko wa wa bei unakuwa ule utakaoyafanya masiaha ya wananchi kuwa na nafuu.

Ni ushari wangu kuwa Mkulo akajifunze kwa Mramba namna ya kuimairisha uchumi wa nchi. Si kwako tu Mkulo hata huku kwetu mambo yakituzidi huwa tunakwenda kwa wazee kutafuta busara na uzoefu wa namna ya kukabiliana, nakutakia safari njema ya mafunzo kwa Mramba. Mwandishi 0787104785/0715104785

Chanzo: Waziri Mkulo jifunze kwa mtangulizi wako
 
Back
Top Bottom