Wazazi wasiosomea watoto wao vitabu; ni wazazi wazuri?

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,474
39,987
OKTOBA 5, 2012 SIKU YA KUWASOMEA WATOTO KITAIFA

Hakuna zawadi kubwa ambayo mzazi anaweza kumpatia mtoto wake na ikayabadilisha kabisa maisha ya mtoto huyo sasa na hata akiwa mtu mzima kama mapenzi ya vitabu (love of the books). Ni katika kutambua ukweli wa hili baadhi ya wazazi nchini wameamua kufanya Ijumaa hii ya tarehe 5 Oktoba kuwa siku ya kuwasomea watoto vitabu.

Ni kweli kwamba watoto wetu wanafurahia zawadi mbalimbali za kuwafurahisha hisia zao na vionjo vyao. Vitu kama pili, midoli ya kuchezea, magari ya kuchezea na vitu vingi vya kuchezea vyaweza kabisa kumfanya mtoto aone furaha na kukuona mzazi wake kweli unamjali na unapenda kumfurahisha. Na kwa kweli hakuna ubaya wowote wa mzazi au mlezi kumpatia mtoto vitu vya kuchezea kwani kucheza ni haki yake. Lakini hivi vitu vyote cha kuchezea vya utotoni vinaishia utotoni; kusoma kunaenda naye hadi uzee! Ukimkuta mtu mzima anacheza kidali po, kioo kioo au ameshika tairi anakimbia nalo lazima ushangae. Lakini ukimkuta anasoma utajua tu kuwa ana hekima ya aina fulani; kusoma kulivyo kuzuri; Oh zawadi nzuri kiasi gani!!

Nilipoandika riwaya yangu ya “Majeruhi wa Mapenzi” ambayo tumeanza kwenda uchapishaji wa pili lengo kubwa la kwanza kabisa lilikuwa ni kuchochea watu kusoma masimulizi ya Kiswahili. Nilitaka nianze kuwarudisha watu kupenda kushika kitabu kusoma. Sikujua kuwa changamoto moja ambayo nilikutana nayo ni watoto wa kaka yangu ambao wako sekondari na wadogo walipolalamika kuwa wamezuiwa kusoma kitabu changu na kakangu kwa sababu kina maudhui ya watu wazima. Ndipo nilipotambua mara moja kuwa ipo haja ya kuangalia watoto wanasoma vitabu vya saizi yao na wanaburudika navyo.

Ndio sababu kwa wiki kadhaa sasa mimi na Watanzania wengine walioko kwenye mitandao ya kijamii tumeanza kampeni ya kuanza kuleta mabadiliko ya kijamii sisi wenyewe. Kuna mambo mengi ambayo tutayafanya kama mtu mmoja mmoja na kwa pamoja. La kwanza ambalo tumeamua kulifanya na tunakualika na wewe – kama unaamini katika nguvu ya mtu mmoja – ni kuhamasishana kuwasomea watoto wetu vitabu kwa siku hii. Tumegundua jambo moja kuwa hakuna wanasiasa ambao wameonesha hata nia ya kuheshimu vitabu zaidi ya wao wenyewe kujisomea. Hawahamasishi kujisomea, hawaonekani kwenye madarasa wakisoma na watoto, na kwa hakika ukiangalia zawadi zinazotolewa na wanasiasa kwenye maeneo mbalimbali vitabu ni zawadi pekee ambayo haitolewi! Watatoa mabati, watatoa matofali, watoto vingine vyote isipokuwa vitabu! Sitaki kukisia ni kwanini wanaogopa wananchi kujisomea na watoto kujua kusoma zaidi!

Hata hivyo labda unaweza kusema kuna faida gani kuwasomea watoto namna hii mbona ni kama kupoteza muda? Unaweza ukaniuliza “MM lakini mbona mwanangu anajua kusoma yeye mwenyewe”? Unaweza hata ukitaka kuuliza “kwani huko shuleni kwao walimu hawawasomei vitabu”? Naomba nijibu maswali haya kwanza kwa kuhoji kitu ambacho labda watu wetu wengi hawajakaa chini kukifikiria: Ilikuwaje watoto ambao hawajui kusoma na kuandika wakafaulu na kuchaguliwa kwenda kidato cha kwanza?
Wanafunzi 21 huko Iramba waligundulika kuwa wamepangiwa shule za sekondari wakati hawajui kusoma na kuandika. Shule ya Mawezi huko Moshi nayo ilipofanya utafiti kujua kama wanafunzi wake wanajua kusoma na kuandika ikajikuta ina wanafunzi 6 kidato cha kwanza wasiojua kusoma na kuandika; wanafunzi sita kidato cha pili, wanafunzi 3 kidato cha tatu na wanafunzi 2 kwenye kidato cha nne! Sasa msiniulize mtu anafikaje kidato cha nne na hajui kusoma na kuandika!

Watu wengi waliangalia moja kwa moja matatizo ya walimu na shule kama sababu. Ni wachache walifikiria labda wazazi wanahusika moja kwa moja na matokeo hayo. Tatizo hili si dogo hivyo hata kwa watoto wanaotoka katika familia zenye unafuu wa maisha kusoma na kuandika bado ni shida. Hivi ni wangapi wamewahi kukaa na kuwasikiliza watoto wetu wakisoma kwa sauti na kusikia uwezo wao wa kusoma uko vipi?

Lakini upande mwingine, je tunawaonesha watoto uwezo wetu wenyewe wa kusoma na kuandika? Au tumeacha kazi hii ya kusoma na kuandika kuwa ni kazi ya walimu na viongozi wa umma huku wazazi na walezi kazi yao ikiwa ni kulipa ada, kununua sera na hela ya matumizi huku wanahesabu miezi tu ya mtoto kuhitimu? Hili ni lazima libadilike na hatuwezi kuwategemea wanasiasa hasa ambao mawazo yao yote yako katika kupata madaraka zaidi. Hatuwezi kuwategemea wanasiasa kuweza kuinua watoto wetu kielimu.

Ndugu zangu, kwa wale wafugaji ng’ombe wanajua jambo moja dhahiri sana. Kuna wakati ng’ombe unamvuta kwa kamba aje. Lakini anapogoma kabisa inabidi umshike mapembe. Wapo watu ambao wana nguvu ya kumshika ng’ombe mapemba na kumsalimisha amri. Katika suala hili la mabadiliko wakati umefika wa sisi wenyewe kama raia, kama wananchi bila kujali itikadi zetu, mirengo ya kisiasa au mwelekeo wetu wa kiimani kuanza kutenda na kujiletea wenyewe mabadiliko.

Ndugu zangu, mabadiliko siyo tunayoyangojea. Mabadiliko siyo yale ambayo tunayaombea na wala siyo yale tuliyoahidiwa. Mabadiliko ni yale tu ambayo tunaweza kujiletea. Fikiria hivi: kama kuna tatizo kuvuka mto, watu wanaweza kungojea daraja lijengwe, na wengine wakiombea atokee mfadhili ili atoe fedha za daraja kujengwa na wapo ambao watakuwa wanaendelea kuogelea kuvuka mtu wakisubiri aje mtu na wazo la kujenga daraja. Lakini, anaweza akatokea mtu na kusema wajenge daraja la mbao na watu wakajenga likawavusha. Sasa mabadiliko ni lile daraja la mbao walilojijengea siyo daraja la chuma ambalo wanalingojea au ambalo wameahidiwa.

Sijajua tutafanya nini hasa na tutafanikiwa vipi lakini kusubiri zaidi siyo jambo lililopo tena. Tutaanza kwa kujifunza na kuboresha kwa kadiri tunavyozidi kusonga mbele. Tutahamasisha wananchi wetu kila kona ya taifa letu kwa kutumia mitandao ya kijamii na njia za kisasa kuanza kufanya kitu. Yawezekana tukaanzisha kitu cha kudumu (kama taasisi); hatujui itakuwaje lakini tunauhakika haitakuwaje. Haitakuwa ya kisiasa, kidini na kwa hakika haitatafuta misaada yoyote kutoka nje. Wakati umefika kwa Watanzania kwa kutumia uwezo wa kiakili, vipaji vyao, elimu yao na raslimali zao kuanza kujiletea maendeleo. Na hakuna eneo muhimu sana kama hili la elimu.

Kabla sijakualika kuwa na wewe upange kuwasomea watoto Ijumaa hii naomba nianishe kwa haraka tu faida za kuwasomea watoto (haijalishi umri) kwa sauti. Zipo nyingi hizi chache zatosha kuzitaja:


  1. Kumsomea mtoto kunaonesha unamjali na kuwa uko tayari kutumia muda wako kwake. Mara nyingi tunatingwa na mambo mengi mno kiasi kwamba ule muda wa kukaa na mtoto anaachiwa msaidizi wa nyumba au mzazi mmoja. Hivyo, mzazi mwenyewe kutenga muda hata usiozidi saa moja kukaa na mtoto na kusoma naye kunamfanya mtoto aelewe kuwa mzazi wake anamthamini na kumjali kiasi cha kuacha mambo yake mengine yote na kukaa naye kusoma hadithi!!
  2. Inamsaidia mtoto kufahamu na kumudu lugha. Mara nyingi zaidi tumeacha watoto wetu wapate maneno mapya kwa kusikiliza tu mitaani au wanavyozungumzishwa na hivyo kuweka kikwazo kikubwa cha watoto kujifunza lugha mapema zaidi. Hakuna njia ya haraka ya kumsaidia mtoto kujifunza lugha (iwe Kiingereza au Kiswahili) kama kumsomea kwa lugha hiyo. Atajifunza maneno mapya, kauli mpya, misemo, tamethali za usemi n.k Ukimuacha mtoto ajifunze lugha za kwenye luninga tu ndivyo naye atakavyokuwa anazungumza.
  3. Kumsomea mtoto kunamsaidia kujenga uwezo wa kiakili unaohusiana na ubunifu na udadisi. Mtoto anaposikiliza hadithi au simulizi lenye kumfanya afikirie zaidi na kujaribu kujiona ndani ya simulizi hilo uwezo wake wa kubuni na kufikiria nao unazidi. Na masimulizi ambayo yana utata yanamsaidia mtoto kuwa mdadisi wa nini kilitokea au nini kinaweza kutokea na hivyo anazidi kufunguka kifikra.
  4. Inafundisha mojawapo ya nyenzo nzuri sana maishani; kusikiliza. Kwa kumtuliza mtoto na kumfanya akusikilize unavyosimulia na kuweka chumvi na kachumbari katika simulizi kunateka fikra na mawazo ya mtoto. Huu ujuzi wa kusikiliza ni kitu ambacho kwa kadiri anavyokua atajikluta anakitumia zaidi na zaidi.
  5. Mtoto anapozoeshwa kusomewa na kusikiliza inamsaidia katika kujenga uwezo wa kiakili wa kupokea mafunzo katika maisha yake yote. Usije kushangaa kuwa watu wengi ambao leo wanaonekana wamefanikiwa sana watakuambia kuwa ni kwa sababu walikuwa wanasomewa sana au kupewa nafasi ya kusoma vitabu tangu wakiwa wadogo au wao wenyewe walijizoesha kusoma vitabu.
  6. Insamsaidia katika kumudu kujieleza na kuzungumza. Mojawapo ya shida ambayo nimekuwa nikiona ninapojadiliana na watu kwa muda mrefu sasa ni jinsi gani kwa baadhi ya watu ni vigumu sana kuweza kujieleza. Mara nyingi utasikia mtu anasema kuwa anajua anachotaka kusema lakini hawezi kukiweka vizuri kwa maneno kama mtu mwingine. Ukweli ni kuwa kuna shida ya kuweza kujieleza na kuzungumza na hii yawezekana ni kwa sababu ya kukosa msingi mzuri wa kuzungumza tangu utoto.
  7. Kumfundisha mtoto mantiki tangu akiwa mdogo sana. Mantiki ni mojawapo ya masomo ambayo kukosekana kwake kunatusumbua sana. Leo hii ukisikiliza viongozi wanapozungumza (iwe Bungeni au nje) na wakati mwingine hata watendaji wengine unashangaa wanajengaje hoja. Mtiririko wa hoja zao hauendani kabisa na kanuni za msingi za somo la mantiki. Kwa kuanza kumsomea mtoto hadithi mbalimbali unamsaidia kuanza kuelewa mwelekeo wa kawaida wa mantiki.
  8. Kumsomea mtoto mapema kabla hata hajaanza shule kunamuandaa mtoto vizuri na kujifunza na kupenda kusoma na hasa kupenda elimu. Inapandikiza kiu ya kutaka kujua zaidi. Na mtoto huyo akija kuweza kusoma yeye mwenyewe na akiwekewa vitabu utakuta anapenda kuvishika kusoma. Binafsi kwa upande wangu mapenzi ya vitabu yalipandikizwa mapema sana; sikuwa nakosa kwenda maktaba kila Jumamosi na nilipofika sekondari wakati naingia kidato cha pili nililikuwa nimesoma vitabu zaidi ya 1000 ambavyo vilikuwa sehemu ya mpango wa serikali ya Marekani kuleta vitabu vya Kiingereza mashuleni. Nililikuwa nimesoma kina Oliver Twist, 20,000 League Under the Sea, The Sky is the Limit na Supernatural Powers. Hapa sijaweka vitabu vya Kiswahili vya kina Hamie Rajab, Ben R. Mtobwa, Elvis Musiba, Kajubi Mukajanga n.k Leo watu wanaponisoma wanaweza kufikirai labda nina kipaji cha aina fulani cha kuandika; ukweli ni kuwa ninavuna tu matunda ambayo yamepandwa na waandishi wengi na kupaliliwa na wazazi wangu! Acha kuleta magazeti ya udaku nyumbani; lete vitabu!
  9. Mzazi naye anafaidika na kumsomea mtoto; anajenga ukaribu naye (bonding) anapata furaha ya kumsaidia mtoto au watoto wake.
  10. Kusoma ni furaha! Hadithi nzuri inafurahisha; inajaza tabasamu na kwa hakika kabisa inaburudisha.

Kwa kweli uamuzi na uwezo uko mikononi mwako. Unaweza kukaa pembeni na kulalamika kuwa watoto wetu hawajui kusoma na kuandika au unaweza kufanya kitu. Unaweza kufunga barabara kutaka mkuu wa idara fulani ya elimu aondolewe kwa sababu wanafunzi wanafanya vibaya au unaweza kufanya kitu; unaweza kucheka na kukebehi kwa sababu watoto wako wanasoma vizuri lakini wengi wa watoto wa nchi yako hawana nafasi hiyo. Yote yamo mikononi mwako.

Ukitaka kuwa sehemu ya mwamko wa mabadiliko ambao umeanza na wananchi bila kujali siasa, dini, itikadi au kabila nitafute kwenye mtandao wa Facebook. Kwani kuanzia wiki hii tutakuwa tuna mambo ambayo tutakuwa tunafanya mmoja mmoja hadi mwisho wa mwezi huu na kutoka hapo tutakuwa katika mazingira ya kujua hasa tunataka kufanya nini nje ya mfumo wa sasa; mfumo ambao umeshindwa na ambao hauwezi kubadilishwa hivi karibuni. Tutajua nini cha kufanya kama Watanzania kubadilisha kile ambacho tumekiona ni cha kawaida. Bila kutegemea wajomba zetu Ulaya!

Usisahau Oktoba 5, 2012; siku ya kuwasomea watoto wetu.

Jiunge nasi: Mimi Mwanakijiji | Facebook
Niandikie: mwanakijiji@jamiiforums.com
 
Napenda kusomea mtoto vitabu, yeye akiwa kama hadhira yangu anasikiliza mara anauliza utasikia hiyo unaandikaje au ina maana gani kama hajaelewa neno ili nimfafanulie zaidi. Muda mwingine yeye anasoma na mimi namsikiliza.
Napenda nimuendeleze hivi, kikubwa kilichosaidia ni kuwa shule aliyoanza kusoma kuanzia pre-school walikuwa wanapewa kitabu kipya kila wiki kusoma na mzazi/wazazi wakitakiwa kuhusika kuwasaidia.
 
ni kweli kuna faida sana, tena kuna wakati kunasaidia kujenga interest za mtoto hata akikua.
 
yah kuna faida nakumbuka nilipokuwa kid uncle zangu walikuwa wananisomea vitabu vya kiingereza na kunitafsiria stories hyo imenijenga kupenda kusoma til now
 
Faida ya kuwasomea watoto vitabu ninauhakika ipo tena kubwa, nakumbuka mama yetu alikuwa anatusomea sana vitabu vya kiingereza na kututafsiria, basi tulikuwa tunafurahi sana na sisi tulikuwa tunaenda kuwasimulia marafiki zetu zile hadithi za picha kwenye vitabu. I can't wait kupata watoto na kuwasomea vitabu.
 
Nakumbuka vitabu ambavyo nilisomewa nikiwa mdogo:

Tintin

250px-TinTin_Congo.jpg

The Beezer Book
beezer_1982.jpg


Halafu comic za Andy Cap

andy_capp.jpg
 
wasomeeni watoto wenu vitabu kama SAMAKI MDOGO MWEUSI ili wawe na mapenzi ya dhati kwa wananchi wenzao na uchungu na nchi yao
 
Kitu cha ajabu sana, mimi ndo nilikuwa na kazi ya kumsomea baba vitabu. Na ilikuwa marufuku kutumia dictionery. Utasoma neno and figure it out yourself. Utaulizwa maana yake, utajaribu ku-make sense akikuongoza hadi utajua maana yake. That way nikajenga msamiati vizuri.
It was a task i hated but nilikuja kuelewa umuhimu wake baadae.
Siku hizi watoto wanataka birthday gift ya play station. Inshaallah, wanangu watasoma vitabu kama vichaa.
 
Mzee Mwanakijiji, tintin na andy cap was my favourites. Nilikuwa nikiona gazeti nakimbilia katuni kwanza. Bogy benda nae alikuwa na kitabu i guess.
 
Last edited by a moderator:
nawaza hii hoja na kumkumbuka mzee wetu kule makiungu anahangaika na maji, umeme, pori halilimiki, maisha magumu nk. kisha naaangalia vitabu vya mkuu wangu......... kweli gap ilianza siku nyingi
 
Back
Top Bottom