Wazanzibari watakiwa kuchangamkia mjadala wa katiba

abdulahsaf

JF-Expert Member
Aug 31, 2010
858
130
Na Jabir Idrissa,
TAASISI nne zisizo za kiserikali zilizosajiliwa Zanzibar zinafanya kazi muhimu kwa sasa ambayo miaka ya nyuma isingekuwa rahisi kuifanya.
Zanzibar Indian Ocean Research Institute (ZIORI), Zanzibar Legal Services Centre (ZLSC), Zanzibar Law Society (ZLS) na Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo (WAHAMAZA) zimejumuika kuandaa mjadala kuhusu mustakbali wa Tanzania kikatiba.
Kinachofanyika kwa wiki ya tatu sasa ni kuongoza mjadala wa wananchi kuhusu hali halisi ya nchi kikatiba pamoja na fursa inayotengenezwa ya kila mmoja kutoa maoni yake.
Taasisi hizo zinawajengea wananchi uwezo wa kutambua nafasi yao ya haki ya kutoa maoni pale itakapokuja fursa ya kueleza wanachokiona kinawafaa katika mabadiliko ya katiba yanayopangwa kufanywa.
Kitu kinachofurahisha katika mjadala huu, ni ile fursa ya elimu inayopatikana kutokana na makongamano yaliyoanza kufanyika kwa kuhusisha mada nzitonzito zilizotolewa na wajuzi wa masuala ya katiba, sheria na haki za binadamu.
Wa kwanza alikuwa Profesa Issa Shivji, gwiji wa yote hayo; mtaalamu aliyebobea na ambaye ameandika sana kuhusu muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa 26 Aprili 1964.
Profesa Shivji aliwachukua wasikilizaji waliokutanishwa ukumbi wa EACROTANAL, mjini Zanzibar , kutoka kusikojulikana hadi alipowaeleza kuwa katiba zote mbili zinazotumika katika jamhuri ya muungano wa Tanzania hazina ridhaa ya wananchi.
Katika mada iliyoitwa na waandaaji wa mjadala kama “Kwanini tunahitaji Katiba mpya Tanzania ,” Profesa Shivji yeye alikuja na alichokiita, “Historia ya utungaji wa katiba za Tanganyika , Zanzibar na Tanzania .”
Alichokilenga, na ambacho alifanikiwa kukielimisha kwa wasikilizaji wakiwemo wananchi wa kawaida, wanasiasa, wasomi vijana na wakongwe katika fani mbalimbali, ilikuwa ni kutafuta uhalali wa kisiasa na ule wa kisheria kuhusu katiba zilizopo.
Uhalali wa kisiasa wa katiba hutokana na katiba yenyewe kukubalika na kuheshimika na umma. Bali kwa uhalali wa kisheria, profesa alisema hupatikana kwa katiba kuandikwa kwa kufuata utaratibu wa kisheria uliowekwa na vyombo husika, hususan makubaliano ya umma.
Katika kuzidi kuzamisha mawazo yake vifuani mwa wananchi, Profesa Shivji alisema uwanja unaotumika kujenga uhalali wa kisiasa si lazima uwe sheria au kwa mujibu wa inavyoelekeza katiba.
Kumbe uwanja waweza kuwa itikadi tu. Na hapa alitoa mfano wa enzi za Mwalimu Nyerere, alipotumia itikadi ya chama kilichokuwepo. Alimaanisha kwamba tangu wakati wa TANU kwa upande wa Tanganyika , mara tu baada ya kupata uhuru kutoka kwa Waingereza.
Lakini Profesa Shivji anaeleza zaidi hili. Katiba ya nchi yoyote inaweza kuwa na uhalali wa kisiasa tu peke yake na ikafanya kazi inayotumainiwa na umma.
Kwa mfano, anasema utungaji wa katiba ya Muungano ya mwaka 1977 kwa kiasi kikubwa ulifuata utaratibu wa kisheria lakini uliokuwa kinyume na dhamira ya kisiasa.
Kwa upande wa katiba ya Zanzibar ya mwaka 1979, akasema ilipata uhalali wa kisiasa bali ikakosa uhalali wa kisheria katika kuitunga. Ile, ilifungua milango ya kujenga demokrasia Zanzibar , anasema.
Mzee Aboud Jumbe Mwinyi, aliyekuwa rais wa Zanzibar wakati huo, aliwasilisha rasimu ya sheria mbele ya Baraza la Mapinduzi. Rasimu hiyo ilikuwa sehemu ya utaratibu wa kutunga katiba ulioanza kwa amri (decree) Na. 5 ya 1964.
Alivyokusudia rais, angeitisha mkutano wa kikatiba wa wananchi kwa ajili ya kutunga katiba ya Zanzibar . Kisha akataja wajumbe wa mkutano huo ingawa rais hakuwahi kueleza aliwapataje.
Baraza la Mapinduzi lilifanya marekebisho na kupitisha katiba ya Zanzibar . Mabadiliko makubwa yalihusu uchaguzi wa rais. Rasimu ya Mzee Jumbe, iliweka utaratibu wa kupata jina moja litakalopelekwa Halmashauri Kuu (NEC) ya chama kuidhinishwa.
Jina hilo lingeidhinishwa na kupelekwa Baraza la Wawakilishi ambalo ndilo lingemchagua rais. Baraza la Mapinduzi lilibadilisha kwa kuweka taratibu kuwa baada ya jina kutoka NEC, litapelekwa moja kwa moja kwa wananchi kwa uchaguzi.
Kamati Kuu ya Chama ilifanya marekebisho kidogo kwa kuweka majina mawili ya kupendekezwa kwa Halmashauri Kuu na kurudishwa jina moja kwa wananchi kwa ajili ya kuchagua.
Bali utungaji wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, iliyopo sasa na ambayo imeshafanyiwa marekebisho mara 11, ulikuwa kupitia sheria ya kurekebisha katiba kwa mujibu wa kifungu cha 42(1).
Hitimisho la Profesa Shivji linashawishi wazi kuwa utaratibu mzima wa utungaji wa katiba zote mbili haukushirikisha wananchi, kote Tanzania Bara na Zanzibar .
Katiba ya Muungano ya 1977, akasema ilikuwa ni muafaka wa NEC ya chama. Siyo wananchi. Hapana. Taratibu za kisheria zilifuatwa kwa kiasi fulani, ila, mantiki ya kisiasa yalipindwa.
Hata hivyo, anakiri kuwa viongozi wa Zanzibar wa wakati ule, walishiriki katika utaratibu na walikuwa takriban nusu ya Tume (iliyoshughulikia utungaji) na nusu ya NEC. Isipokuwa walikuwa chini ya theluthi moja ya wajumbe wa Bunge Maalum.
Katiba ya Zanzibar ya 1984 ilitungwa na baraza lisilochaguliwa na wananchi. Hivyo, ilikosa uhalali wa kisiasa.
Utaratibu wa kisheria haukufuatwa kwani ilipitishwa chini ya mamlaka ya kubadili masharti ya katiba. Ndio kusema haikupata uhalali hasa wa kisheria.
Profesa Shivji akasema kitu kingine kilichoamsha mchemko kwa wasikilizaji. Kwamba kwa kuwa katiba zote mbili zimeegemea mfumo wa muungano wa serikali mbili, na kwa vile hazina uhalali wa kutosha – kama alivyobainisha – basi muungano wenyewe unakosa uhalali unaotokana na muafaka wa wananchi wa pande zote mbili za muungano huo.
Ama hili lilichangamsha wahudhuriaji. Ni kama vile profesa alifungua mlango wa hisia kali katika mjadala. Wakati alisema huu hasa ndio wakati wa kurudisha taifa katika muafaka wa kupatikana kwa katiba mpya ya wananchi, alieleza wazi hofu yake kwamba utaratibu wa mjadala usije kutekwa na wanasiasa.
Katiba ya wananchi ni ile tu ambayo wananchi wenyewe watakuwa wamekubaliana kuipanga, kuijadili na hayo iwe kwa kupitia wawakilishi waliowachagua kwa hiari zao, juu ya mifumo ya kuendesha uchumi, utawala, siasa na muundo wa Muungano.
Kwa Profesa Shivji, kilicho muhimu kuliko yote, kabla ya kupatikana katiba, ni mijadala ya wananchi; ushirikishwaji wao kwa kila hatua; chombo mahsusi cha kujenga muafaka – Mkutano wa Katiba; chombo mahsusi walichochagua – Bunge la Katiba; na uidhinishaji wa katiba kupitia kura ya maoni.
Funzo muhimu: Kwamba wakati Wazanzibari wanatafakari fursa iliyokuja kwa Jamhuri ya Muungano, wanapaswa pia kufikiria iwapo wanataka kuishi na katiba wasiyoiridhia ya Zanzibar .
Mjadala wa kujenga uwezo wa wananchi kutambua wajibu wao wa kushiriki na kushirikishwa katika kutunga katiba yao , unaendelea. Kwa Zanzibar, waandaaji wameahidi kuufikisha kwenye maeneo ya wananchi wa kawaida.
 
Back
Top Bottom