Watumishi hospitali wadaiwa kusababisha vifo

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
HOSPITALI ya Wilaya ya Kahama imenyooshewa vidole na madiwani kuwa imekumbwa na vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa maadili ya kazi kwa watumishi wake na hivyo kuwa chanzo cha vifo vya wajawazito na watoto wachanga.

Madiwani walitoa malalamiko hayo katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kahama kilichopitia taarifa mbalimbali za utekelezaji kuanzia Januari na Machi mwaka huu.

Wakati wakipitia taarifa ya Idara ya Afya, iliibuka hoja juu ya uadilifu wa wauguzi, waganga na wakunga katika hospitali ya wilaya.

Diwani wa Kata ya Kahama Mjini, Aoko Nyangusu alisema rushwa imekithiri katika hospitalini hapo kiasi cha watumishi kutotekeleza majukumu yao kama ambavyo kanuni na maadili yanavyowaelekeza.

Kuhusu vifo vya wajawazito na watoto, Diwani wa Viti Maalumu, Josephina Balanoga alisema baadhi ya wanawake wamekuwa wakipoteza maisha pamoja na watoto wanaozaliwa kutokana na wakunga wazoefu kutojishughulisha kikamilifu na huduma hiyo.

Balanoga alisema wazoefu wamekuwa wakiwaachia wanafunzi wa Chuo cha Uuguzi kujifunza kwa vitendo masuala ya ukunga wakati wao wakibakia kupiga soga.

“Hali hii nimeishuhudia kwa mjukuu wangu mwenyewe niliyempeleka kujifungua hospitalini hapo, na kutopatiwa huduma inayostahili kutoka kwa wakunga wazoefu,” alisema Balanoga.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Dk. Leonard Subi alipinga wodi hiyo na nyingine kuwa na wauguzi wanafunzi. Alisema elimu na utaalamu walio nao ndiyo huwafanya wapewe majukumu na siyo umri.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kahama, Duncan Thebas aliahidi kukaa na watumishi wa Afya ili kubaini kiini cha tatizo na kulipatia ufumbuzi.

“Haiwezekani mtu mzima kama Mheshimiwa Balanoga atoe kilio hicho, hapo lazima kuna tatizo pasipo DMO (Mganga Mkuu wa Wilaya) kujua, nitakaa na watumishi wake ili kuiondoa kero na tatizo hilo,” alisema Thebas.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Kahama Alfred Mhanganya alimwagiza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, kulishughulikia kwa ufanisi kuhakikisha kero za namna hiyo zinatatuliwa kuanzia pia kwenye zahanati na vituo vya afya.
 
Back
Top Bottom