Watuhumiwa EPA warushiana mpira kuhusu mgao wa mabilioni

Ochu

JF-Expert Member
May 13, 2008
975
47
Watuhumiwa EPA warushiana mpira kuhusu mgao wa mabilioni
Na Nora Damian

WASHITAKIWA wa kesi ya wizi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Farijala Hussein na Rajabu Maranda wamerushiana mpira katika maelezo yao waliyoyaandika kwenye tume.

Katika maelezo ya Maranda yaliyosomwa mahakamani jana, mshitakiwa huyo alisema fedha zote zilizoingia katika akaunti yao kutoka BoT zilichukuliwa na mshitakiwa mwenzake Farijala.

Maelezo ya mshitakiwa Farijala yaliyosomwa wiki iliyopita na kupokelewa mahakamani kama ushahidi, Farijala alisema pesa zote zilichukuliwa na Maranda.

Maelezo hayo yalisomwa na shahidi wa sita katika kesi hiyo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Salum Kisai ambaye ndiye aliyeandika maelezo ya Maranda na Farijala.

Kisai alisema aliandika maelezo ya Maranda Oktoba 6 na 7, mwaka jana katika ofisi za Tume ya kuchunguza sakata la EPA zilizoko Mikocheni kwa madai kwamba, wakati anaandika maelezo hayo mtuhumiwa alimueleza kuwa anaumwa.

Kwa mujibu wa maelezo hayo, Maranda ameeleza kuwa alikuja jijini Dar es Salaam mwaka 1994 na kwamba, tangu wakati huo amekuwa akijishughulisha na biashara ya mitumba na uuzaji wa mafuta ya dizeli na ya taa.

Maranda ameeleza kuwa analifahamu jina la biashara la Kiloloma & Brothers ambalo linadaiwa kutumika kuiba Sh1.8 bilioni kutoka BoT na kwamba, mmiliki wake ni Charles Isaack Kissa.

“Farijala aliniambia kuwa Kissa ni rafiki yake na ni mjomba wa aliyekuwa Gavana wa BoT, Daudi Balali,”alisema Maranda.

Shahidi wa kwanza katika kesi hiyo Esteriano Mahingira ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Majina ya Biashara na Makampuni (Brela), alidai mahakamani hapo kuwa Charles Isaack Kissa ndiye mmiliki wa jina la biashara la Kiloloma & Bros Enterprises.

Mahingira alidai mahakamani hapo kuwa jina la Kiloloma & Brothers ambalo wamiliki wake ni Maranda na Farijala halitambui na kwamba lilighushiwa.

Maranda ameeleza katika maelezo yake kwamba, Farijala ndiye anayejua alikozipata nyaraka mbalimbali za usajili wa jina la Kiloloma & Brothers ikiwemo hati ya usajili wa jina hilo.

Ameeleza kuwa alimkopesha Kissa Sh 150,000 na kwamba alikuja kwake na kumuomba afungue akaunti na baada ya kufungua alimtaarifu kuwa wameingiziwa fedha kutoka BoT Sh 1.8 bilioni.

“Baada ya pesa kuingia mimi nilichukua hela yangu Sh 150,000 na pesa zingine ziliendelea kutolewa benki kwa maelekezo ya Kissa,” alisema Maranda.

Maranda alisema anaifahamu kampuni ya BC Cars ya nchini India na kwamba, Oktoba 24, 2005 alituma Sh308 milioni kwenda nchini Uingereza.

Alisema pia alichukua Sh400 milioni na kumpa Jay Somani ambaye ni rafiki yake na Kissa pia

Jay Somani ni mmoja wa washitakiwa katika kesi za EPA ambaye anashitakiwa pamoja na Ajay Somani kwa kuiibia BoT Sh 5.9 bilioni baada ya kudanganya kuwa kampuni yao ya Liquidity Services imepewa deni na kampuni ya Society Asacienne De Construction De Machines Textiles.

Naye Coplo Beatus Alex ambaye ni mlinzi katika ofisi za Tume ya kuchunguza sakata la EPA zilizoko Mikocheni, alidai mahakamani hapo kuwa anamfahamu Maranda kwasababu alikwenda katika ofisi hizo kati ya Oktoba 6 na 7, mwaka jana.

Baada ya kusikiliza hoja zote kiongozi wa jopo la mahakimu watatu wanaosikiliza kesi hiyo, Cypriana William aliahirisha kesi hiyo hadi leo ambapo upande wa utetezi utaleta ushahidi ili kuthibitisha kama Maranda alikuwa mgonjwa wakati akiandika maelezo yake.

Katika hatua nyingine, shahidi Hassan Kilule ambaye upande wa mahakama uliomba akamatwe kwa kushindwa kufika mahakamani kutoa ushahidi, jana alifika na kutakiwa kufika leo kwa ajili ya kutoa ushahidi wake.

Farijala Hussein na Rajabu Maranda wanadaiwa kuwa kati ya Aprili mosi na Septemba 2 mwaka 2005 mkoa wa Dar es Salaam, waliiba kutoka BOT Sh 1,864,949,294.45 baada ya kudanganya kuwa kampuni ya Kiloloma & Brothers imepewa deni na kampuni ya BC Cars Export ya Mumbai India.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom