Watoto wa mitaani; bomu linalosubiri kulipuka nchini

Saint Ivuga

JF-Expert Member
Aug 21, 2008
54,377
58,384
Watoto wa mitaani; bomu linalosubiri kulipuka nchini
Send to a friend
Thursday, 21 July 2011 20:30
0digg

Na Patricia Kimelemeta
WAKATI nchi za Afrika zilipofanya maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, Juni 16 ikiwa ni njia mojawapo ya kuwakumbuka na kuwaenzi watoto wa Afrika Kusini ambao walifanyanyaswa na kubaguliwa na hata kuuawa wakati wa ubaguzi wa rangi, Tanzania inaelezwa kuwa haina takwimu sahihi za watoto wa mitaani.

Kukosekana kwa takwimu hizo kumeelezwa kuwa kunatokana na sababu mbalimbali ikiwamo kuongezeka siku hadi siku kila sehemu kwa watoto hao, hali ambayo inawafanya watendaji wa Serikali wakose takwimu hizo.Pia, inaelezwa kwamba watoto wengine wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi kwa afya zao, lakini bila kutambuliwa.

Wakiwa mitaani huko, watoto hao wamekuwa wakikumbana na mambo mbalimbali yakiwamo kubakwa, kunyanyaswa, kudhalilishwa kijinsia, vitendo wanavyofanyiwa na watu mbalimbali wakiwamo watoto wenzao na hata watu wazima.

Ugomvi wa wazazi kwenye familia,kutowajibika ipasavyo na umaskini ni sababu mojawapo ya zinazofanya watoto hao kutoroka na kuingia mitaani na kuishi katika mazingira magumu, hali ambayo inaonyesha wazi kuwa, jamii imeshindwa kuwajibika ipasavyo.Watoto hao ambao wanategemewa kuwa viongozi wa baadaye, lakini wanaonekana kuwa na maisha magumu yanayosababisha kukosa elimu, malezi bora jambo ambalo linawafanya waishi katika mazingira hatarishi.

Ili kutatua tatizo hilo, Serikali, jamii na wadau mbalimbali zikiwamo taasisi za kiraia zina wajibu wa kushirikiana kwa pamoja na ili kuhakikisha kuwa, wanatoa elimu kuhusu suala hilo.Mbali na wadau hao, walimu pia wana nafasi kubwa ya kutoa elimu kwa wazazi na wanafunzi kupiga vita suala la kutupwa watoto,unyanyasaji, ubebaji wa mimba bila ya kujiandaa jambo ambalo linaweza kupunguza kama si kumaliza tatizo hilo.

Idd Mohamed, ambaye ni mtoto wa mitaani mwenye umri wa miaka 11,aliyezaliwa Tanga katika kitongoji cha Mabawa.Yeye, ni mtoto wa pekee kwenye familia yake, alianza darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Miembeni, lakini alishindwa kuendelea na masomo baada ya wazazi wake, baba na mama kuachana na hatimaye baba kuoa mke mwingine.

Kutokana na hali hiyo, mtoto huyo anasema alishawishiwa na watoto wenzake kuwa mjini kuna maisha mazuri kuliko kijijini, wakieleza kwamba mtu akitaka fedha anaokota kama karatasi ,hali ambayo ilimshawishi na kuzamia kwenye gari ili aweze kuja.

Baada ya kufika Dar es Salaam anasema alijiunga na watoto wa mtaani katika kituo cha mabasi ya Ubungo na kuanza kuishi maisha hayo, maarufu kama uchokoraa ambayo tayari alipewa taarifa na wenzake, lakini anakiri kuwa amekutana na mambo mbalimbali ikiwemo kupigwa na watoto wenzake tangu afike.

Akizungumza na Mwananchi, Idd anasema kuwa mwaka 2007 ndipo alipotoka nyumbani kwao (Tanga) na baada ya kuishi muda mrefu katika kituo cha Ubungo aliamua kwenda Kariakoo ambako kuna vijiwe mbalimbali vya watoto wa mitaani.Huko alijiunga na kijiwe na ‘Roundabout’ na watoto wenzake bila ya kuwa na uangalizi wa aina yoyote huku akiishi kwa kuomba omba.

“Nilikuwa nakaa katika kijiwe cha’Roundabout’, lakini najitegemea kila kitu, nikiamka naenda kuomba hela kwa watu wanaofika kwenye maeneo hayo, wakinipa naenda kununua chakula, nakula, mpaka sasa,”anasema Idd.

Anaongeza,akiumwa anaomba msaada kwa watu ili waweze kumsaidia kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kumpa dawa ili aweze kunywa au kumeza ili aweze kuendelea na maisha kama kawaida.

Anaongeza kuwa maisha hayo ni mabaya, amechoka na kwamba anatamani kurudi nyumbani kwao, lakini anashindwa kwa sababu hana usafiri wa kumrudisha.“Nimechoka kuishi huku,sasa hivi hawatupi hela kama zamani, tunaishi katika mazingira magumu,nashinda njaa, maisha mabaya natamani kurudi nyumbani ili niweze kuendelea na maisha yangu,”anaongeza.

Naye mtoto mwingine,Yusuph Mohamed (13) maarufu kama ‘Panya Road’ ni mkazi wa Kigamboni, lakini wazazi wake wanashindwa kuwajibika ipasavyo, jambo ambalo linawafanya waishi katika mazingira magumu
Anasema,wazazi wake wanamtuma kuomba mitaani huku wakishindwa kumpeleka shule kwa ajili ya kupata elimu, jambo ambalo mpaka sasa linamfanya aishi katika mazingira hatarishi.

“Mimi wazazi wangu wapo kule Kigamboni na kwamba wanajua kama naomba, lakini hawajawahi kunikataza, badala yake wanachukua hela zangu ambazo zimepewa na wasamaria wema,”anasema Mohamed.Anasema hajawahi kupelekwa shule tangu azaliwe na kwamba wazazi wake hawaoni umhimu wa kusoma badala yake wanamtuma kuomba mitaani.

“Sijawahi kupelekwa shule na mama yangu anajua kama naomba lakini hajawahi kunikataza, tena anachukua hela zangu, anasema Panya Road.Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo,Jinsia na Watoto, Tukae Njiku anasema kuwa baadhi ya watoto wamekuwa na tabia ya kutoroka majumbani kwao na kuja mjini kutokana na vishawishi mbalimbali kutoka kwa wenzao, hali ambayo inachangia Serikali kutokuwa na takwimu sahihi za watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Anasema watoto hao wamekuwa wakitoroka majumbani kwao kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya migogoro ya kifamilia, wazazi kushindwa kuwajibika au kuwahudumia ipasavyo, jambo ambalo limechangia kukimbia.“Matatizo ya kifamilia katika maisha ni sababu mojawapo ya watoto hao kuwaikimbiza nyumbani, jambo ambalo limechangia kuongezeka kwa idadi ya watoto mitaani, kutokana na hali hiyo wazazi wanapaswa kuwajibika ipasavyo,”anasema Njiku.

Anaongeza kuwa mwaka 2009 Bunge ilipitisha Sheria ya Watoto, lengo ni kuwataka wazazi wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao kuchukuliwa hatua za kisheria ili waweze kubadilika.
“Sheria zipo, lakini mpaka sasa bado kuna baadhi ya watu wanashindwa kujua kuwa mtoto ni wa Serikali na si wa kwao peke yao, jambo ambalo linawafanya washindwe kuwajibika ipasavyo,kutokana na hali hiyo,wazazi hao wanapaswa kuwa makini ili waweze kuwapatia watoto wao malezi bora na ya kisasa,”anaongeza katibu mkuu huyo.

Anabainisha kuwa mbali na Serikali pia,walimu wanapaswa kuwaelimisha wanafunzi juu ya kuhudhuria mabaraza ya wanafunzi yanayofanyika katika shule zao ambayo yanasaidia kutoa fursa kwao kujifunza mambo mbalimbali yakiwemo haki zao za msingi na na jinsi ya kuzitetea, jambo ambalo wanaamini kuwa wanafunzi wanaweza kupata uelewa zaidi.

Anasema kuwa wanafunzi nao wanapaswa kujiheshimu na kuachana na makundi ambayo wanaona yanaweza kuwaharibia maisha jambo ambalo linaweza kuongeza idadi ya watoto mitaani.

Anaongeza kuwa kutokana na hali hiyo jukumu la kulea watoto si Serikali pekee, bali ni kila mmoja kwenye nafasi yake ana wajibu wa kuhakikisha kuwa analinda haki za watoto ili wasiweze kuingia kwenye makundi yasiyofaa.

Naye mwanasheria kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Felista Mauya anasema kuwa kituo hicho kinatoa msaada wa kisheria kwa watoto wanaofika na kutoa malalamiko yao juu ya unyanyasaji na matendo mengine ambayo yanavunja haki za binadamu.“Tunatoa msaada wa kisheria kwa watoto wanaofanyiwa vitendo vya ajabu, ikiwa ni pamoja na kuwasaidia ili waweze kufika kwenye vyombo ya sheria ili waweze kupatiwa haki zao,”anasema Mauya.

Anaongeza kuwa mpaka sasa kuna idadi kubwa ya watoto waliofanyiwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia ikiwa ni pamoja na kubakwa, kudhalilishwa, kunyanyaswa na mambo mengine ambayo na yenyewe yanachangia kiasi kikubwa cha unyanyasaji wamewasaidia, na kwamba juhudi bado zinaendelea na kupambana na hali hiyo.

“Tunashirikiana na wadau mbalimbali nchini ili kuhakikisha kuwa, tunapunguza kama si kumaliza kabisa suala la unyanyasaji wa jinsia hasa kwa watoto wa mitaani,jamboambalo linawafanya waishi katika mazingira magumu na hatarishi kwa maisha yao,”anaongeza.

Anabainisha kuwa wazazi wana jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa, wanawalea watoto wao katika mazingira ya kisasa, lengo ni kusaidia na wadau hao kuondoa tatizo la watoto wa mitaani.

Anasema, kutokana na hali hiyo,baadhi ya wazazi wanaowatelekeza watoto kwa ajili ya maslahi yao binafsi wanachukuliwa hatua za kisheria, ikiwa ni pamoja na kuwafikisha kwenye mamlaka husika ili waweze kushughulikiwa.

0755 037199 au partthybenny1@yahoo.com



 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom