‘Watendaji waliosimamishwa kwa kashfa watafikishwa kortini’

OSOKONI

JF-Expert Member
Oct 20, 2011
10,965
5,336
IKULU imesema watendaji wakuu wa taasisi za Serikali wanaochunguzwa kwa tuhuma za kuhusika na kashfa mbalimbali, hawataishia katika hatua hiyo tu na badala yake, watafikishwa pia mahakamani ikibainika kuwa wana kesi za kujibu.

Imesema uchunguzi huo unafanywa kwa lengo la kupata ushahidi wa kutosha ili Serikali iweze kuutumia mahakamani katika kesi zitakazowakabili na kuhakikishia pia kuwa wanatendewa haki. Hayo yalisemwa jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alipokuwa akizungumza na Mwananchi baada ya hafla fupi ya kuwaaga wanafunzi 160 wa Kitanzania, wanaokwenda Uholanzi kwa masomo ya kozi mbalimbali.

Balozi Sefue alitoa ufafanuzi huo baada ya kutakiwa kuzungumzia hatua zilizochukuliwa na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, Waziri wa Malisili na Utalii, Balozi Hamisi Kagasheki na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda za kuwasimamisha kazi watendaji mbalimbali wa taasisi zilizoko chini ya wizara hizo, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili.

Agosti 23 mwaka huu, Dk Mwakyembe aliwasimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Ephraim Mgawe, wasaidizi wake wawili, Julius Mfuko na Hamadi Koshuma pamoja na Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Cassian Ng'amilo, ili kupisha uchunguzi wa wizi wa vitu mbalimbali yakiwamo makontena ya vitenge, katika Bandari ya Dar es Salaam.

Waziri huyo pia aliwasimamisha kazi Meneja wa Kituo cha Mafuta ya Ndege Kurasini, Emanuel Mataro, Meneja wa Kituo cha Mafuta cha Jet, Kapteni Joseph Bwakabale na mhandisi wa mafuta wa kituo hicho, Kapteni Tumaini Masaro, baada ya kubainika kuwapo kwa wizi wa mafuta. Mei 17 mwaka huu, Dk Kigoda aliiagiza Bodi ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), kumsimamisha kazi Mkurugenzi wake Mkuu, Charles Ekelege.
Alisema Mkurugenzi huyo wa TBS anapaswa kusimamishwa kazi, ili kupisha taratibu za kisheria ikiwa ni pamoja na uchunguzi dhidi yake.

TBS chini ya Ekelege ilidaiwa kuwa na vituo feki vya kukagulia magari mjini Hong Kong, China na Singapore. Agosti 13 mwaka huu, Waziri Kagasheki, alitangaza kuwatimua kazi vigogo watatu wa wizara yake akiwamo Mkurugenzi wa Wanyamapori, baada ya uchunguzi kubaini kuwa walihusika katika kashfa ya utoroshaji wanyamapori hai kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwenda nje.

Jana, Balozi Sefue alisema ni jambo la muhimu kwa mtu yeyote anayekuwa katika nafasi ya uongozi, kuwajibika pale mambo yanapokwenda vibaya. “Uwajibikaji kwa kiongozi ni jambo zuri na siku zote kiongozi anaposhindwa kuwajibika, viongozi wenye mamlaka ya kinidhamu juu yake, lazima wachukue hatua,” alisema Balozi Sefue.

Alisema kiongozi yeyote anayetuhumiwa kujihusisha na mambo yaliyo kinyume na maadili ya kazi yake, anapaswa kuwajibishwa bila kuonewa na kwamba ndio sababu ya kufanyika kwa uchunguzi kabla ya kuchukuliwa hatua. “Viongozi waliochukua hatua za kuwasimamisha kazi watendaji mbalimbali wa taasisi zilizo chini ya wizara zao, walifanya hivyo baada ya kuona mambo hayaendi,” alisema Balozi Sefue na kuongeza; “Ni jambo ambalo lazima tu lizoeleke, aliyesimamishwa kazi lazima uchunguzi ufanyike na hatua zichukuliwe ila kwa haki na si vinginevyo,” alisisitiza.

Huku akizungumza kwa umakini alisema, “Tunafanya uchunguzi ili hata tukienda mahakamani tusishindwe.” Akizungumzia uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili mawaziri waliowajibishwa baada ya kukumbwa na kashfa mbalimbali alisema “uchunguzi huo bado unafanyika, siwezi kulisema hilo kwa sababu unafanywa na mamlaka husika, ila wakikamilisha watatuletea.” Kauli ya Rais Kikwete

Wakati akitangaza Baraza Jipya la Mawaziri, Rais Jakaya Kikwete alizungumzia azma ya Serikali kuchukua hatua kwa watendaji wengine wa Serikali na taasisi zake ambao alisema ni chanzo cha mabadiliko hayo.

Rais Kikwete alisema mawaziri wamekuwa wakijiuzulu hata kwa makosa ambayo si yao na kwamba Serikali itaanza kuchukua hatua kwa watendaji wakiwamo makatibu wakuu, wakurugenzi wa wizara, watendaji wakuu wa mashirika na taasisi za umma pamoja na bodi za mashirika husika.
 
Back
Top Bottom