Watawala wasioheshimu utawala wa sheria, wanatawalaje?

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,007
Watawala wasioheshimu utawala wa sheria, wanatawalaje?

Mwandishi Wetu Aprili 29, 2009

Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

KUNA kila dalili kuwa watawala wetu wana tatizo la kuheshimu utawala wa sheria.

Kuheshimu huko kunaonyeshwa kwa njia moja tu nayo ni kuifuata sheria na kutekeleza kile sheria inataka kwa namna yoyote ile.

Matukio kadhaa ya hivi karibuni yanazidi kunifanya niamini kuwa watawala wetu wanataka kutawala kwa hisia, vionjo na mitazamo yao binafsi, wakiamini kuwa vitu hivyo kwa namna moja au nyingine vina uhusiano wowote ule na sheria.

Sasa, kama mtu anayeonyesha kutokujali sheria ni mtu wa ngazi ya chini, ambaye hana madaraka makubwa, tunaweza kusema kuwa anahitaji kupelekwa semina au mafunzo fulani au kupewa maelekezo ya nini cha kufanya.

Lakini inapotokea kuwa mtu anayeonyesha kutokufuata sheria na kuheshimu utawala wa sheria ni waziri au kiongozi wa ngazi za juu serikalini, basi kiwango cha matatizo kinakuwa kimeongezwa kwa kasi ya ajabu.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi) Hawa Ghasia wiki iliyopita alisema kitu bungeni ambacho kilinikumbusha alichosema Waziri Mkuu miezi michache iliyopita pale alipohalalisha uvunjaji wa sheria tena kwa machozi.

Wote wawili japo kwa namna mbalimbali wameendelea kuthibitisha kila ambacho wengi tunakijua, tumekishuhudia na kwa muda mrefu tumekivumilia yaani, sheria inafuatwa pale wanapojisikia, na pale wanapotakiwa kuifuata wanajizuia kwa kusingizia kujisikia.

Kwa Waziri Mkuu alipozungumzia lile suala la mauaji ya albino tulipiga kelele na kwa machozi yake akatutuliza. Lakini baadaye akaenda Iringa ambako huko nako akasema maneno fulani ambayo japo hayakupata mbiu kubwa kwenye vyombo vya habari lakini kimsingi yalikuwa yanaingilia utendaji kazi wa Mahakama kuhusiana na viongozi wa serikali kumfungulia mashtaka kiongozi mmoja wa CCM.

Lakini kilichonishtua zaidi ni haya ya mama Ghasia. Wengi walioandika juu ya kauli yake walikwazwa zaidi na suala la nyaraka kuwa ni za siri na wanaovujisha watachukuliwa hatua. Binafsi kilichonikwaza zaidi ya hicho ni madai kuwa kwenye Bunge letu kuna wezi!

Yaani Waziri wa Utumishi akitoa msimamo wa Serikali anatambua kuwa kuna wizi unafanyika tena wa nyaraka za siri na wezi hao wamo bungeni. Si yeye tu mwenye mawazo ya namna hiyo bali pia wapo wabunge wanaoshikilia nadharia hiyo hiyo kuwa kati yao wapo wezi wa nyaraka za “siri” za Serikali. Kwamba, Waziri na kundi la wabunge kadhaa wanajua wezi na hakuna mwenye ujasiri wa kwenda mahakamani!

“Tunawajua” alitangaza Waziri Ghasia. Akishangaliwa na wenzake ambao nao kama kawaida yao walikuwa wanafuata mkumbo tu. Yaani, Waziri anatangaza hadharani kuwa kuna wezi kwenye Bunge, wezi ambao Serikali inawafahamu na wezi ambao wanajulikana wameiba nini lakini zaidi anachotaka ni kuwa “wajirekebishe” na kuacha wizi wao!

Je, utawala wa sheria una maana gani basi? Kwa mujibu wa watawala wetu inaonekana utawala wa sheria kwao una maana ya pale ambapo wanapojisikia kufuata sheria. Dhana hii haina msingi.

Mojawapo ya alama inayotambulikana ulimwenguni ya haki isiyo na upandeleo ni alama ya mwanamke aliyeshika mizani mkono mmoja na mkono wa pili kashika sime. Bila ya shaka alama hii ipo hata Kisutu na katika mahakama mbalimbali nchini.

Kitu kimoja ambacho watu wengi yawezekana hawajakiangalia kwa karibu ni kuwa mwanamke huyo ambaye anajulikana kama “lady justice” yaani “mama haki” amefungwa macho yake kwa kitambaa. Yaani, haruhusiwi kuangalia anayempima kwenye mizani ni nani, na anayetakiwa kumuadhibu ni nani.

Hapa ndipo wazo la haki sawa kwa wote linapokuja. Kwamba haki haiangalii mtu, cheo, hadhi, ukumbi au jina la mtu. Wote mbele ya sheria wana haki sawa.

Katika Kiswahili msemo unaoendana na wazo hilo ni pale tunaposema kuwa “sheria ni msumeno”, yaani unakata unapokwenda mbele au kurudi nyuma; unatoa haki sawa.

Katika nchi zenye kuheshimu kweli utawala wa sheria wazo hili limeinuliwa juu zaidi na kufikia kuitwa kile kinachoitwa ni “udikteta wa sheria” (the dictactorship of the law).

Kwenye nchi ambayo kweli inaheshimu utawala wa sheria basi neno la mwisho si la Waziri, si la Rais na si la hisia za mtu, bali sheria. Kwamba kile ambacho sheria inataka ndicho sheria inapata.

Kwa maneno mengine, kama kuna wizi umetokea na Serikali inajua kuwa wizi upo basi uchaguzi wa kushitaki au kutokushitaki haupo bali ni kufuata kwamba mtuhumiwa wa wizi lazima afikishwe mahakamani. Kama Serikali haitaki kesi iendelee kuna taratibu za kisheria za kufuta kesi.

Udikteta huu wa sheria kama watawala wetu wangeuelewa, basi tungekuwa mbali kwani tungejikuta tunafungwa na sheria. Leo hii, tunachukulia sheria kama suala la uchaguzi tu (optional). Kwamba ama tufuate au tusifuate.

Mfano mzuri wa kuelewa jinsi gani somo hili limetupiga chenga ni pale dereva anapofika mahali ambapo kuna alama barabarani inayoonyesha “Simama”. Alama hii haisemi ‘endesha pole pole, punguza mwenzo, angaza macho n.k”. Inasema “Simama”.

Maana ya kusimama ni kukomesha au kusitisha mwendo. Sasa dereva anatakiwa kisheria anapoona alama hiyo lazima asimame kwanza kabla ya kuendelea. Ni wangapi wanasimama kwenye alama hiyo? Kwao, alama hiyo ni kama pendekezo la aina fulani!

Ni sawa na watu wengine ambao wanakutana mahali kwenye maagizo yanayosema “Usitupe takataka hapa kwa amri ya Halmashauri”. Kwa watu wengine wanachokisoma ni kuwa “Takataka kubwa zisitupwe hapa; tupa vichungi vya sigara na maganda ya machungwa!” Neno “Usitupe takataka” kwao ni kama pendekezo tu, si “amri” ya kufuata.

Mfano mzuri wa hili ni katika kusimamia fedha za umma. Ukiangalia ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali hasa ya miaka miwili iliyopita utaona kuwa kwenye wizara, idara na wakala mbalimbali wa Serikali, sheria ya manunuzi ni kama mapendekezo ya aina fulani hivi.

Mapendekezo ambayo yanaweza kufuatwa au kutokufuatwa bila ya matokeo yoyote yale ya adhabu. Matokeo yake watu wamenunua vitu wasivyokuwa na bajeti navyo, wamenunua vitu bila risiti, na wakati mwingine wamehamisha fedha kutoka sehemu moja kwenda nyingine kinyume cha sheria na watu hao wako madarakani!

Sasa kwenye taifa lenye viongozi na watendaji wa namna hii tunashangaa tunapoona mambo ya Richmond na Dowans? Tunashangaa tunapoona mikataba mibovu isiyo na kichwa wala miguu? Wengine wanaweza kushangaa, lakini ukweli ni kuwa hii ndiyo nchi yetu na hawa ndio watawala wetu.

Hakuna mtu ambaye yuko tayari kuona sheria inafuatwa. Ninaowaonea huruma kwa kweli ni watu wa Mahakama ambao naamini wakati mwingine wanaweza kuchanganyikiwa kwani wao wanaweza kufanya kazi yao pale tu ambapo kesi zinaletwa mahakamani. Hawawezi kwenda kuleta mashtaka wao wenyewe hata kama wanajua makosa yamefanyika.

Swali ambalo sina jibu lake ni kuwa endapo wavunjaji wa sheria wapo hadi bungeni (si wezi tu bali pia mafisadi na wala rushwa – kumbuka Richmond na Dowans?) na watu hao wote wanajulikana hadi kwa Waziri (ina maana Serikali inawajua) ni kwanini basi tuamini kuwa nchi yetu ina utawala wa sheria?

Je, utawala wa sheria kwetu sisi ni suala la hisia za Waziri na wabunge? Je, utawala wa sheria kwetu ni pendekezo tu la kufuatwa au kutokufuatwa? Je, ni kwa kiasi gani tutafuata sheria hata kama inatuumiza? Je, tuko tayari kukinywa kikombe cha sumu kama alivyofanya yule mwanafalsafa Socrates alipohukumiwa kifo na mahakama ya nchi yake japo alijua walifanya hivyo kwa makosa lakini aliheshimu sheria na kwa ujasiri alikunywa sumu kama alivyotakiwa?

Je, leo hii ni nani kati ya watawala wetu mwenye ujasiri wa kuhakikisha kuwa sheria inafuatwa hata kama kwa kufanya hivyo kuna ndugu, rafiki, wapambe, washirikia au jamaa watakaodhurika?

Je, kuna mtu kweli katika Tanzania ambaye yuko tayari kuona sheria kweli inafanya kazi yake bila kuangalia usoni kama isemwavyo kwa simulizi za Kusini kuwa ni “kumkoma nyani giledi mchana kweupe”?

Ni mpaka lini wanaotaka kuua nyani hadi wamuangalie usoni na mwisho wake wanatafuta kila kisingizio cha kutofanya hivyo licha ya kujua kuwa nyani huyo analeta madhara shambani? Tukiwauliza wanasema ati kwa vile “anatia huruma”! Ni nchi gani hii ambayo tunaijenga kwa kusimamia sheria kwa kujisikia?

Nilichotaka kusema baada ya maneno hayo mengi ni kuwa kama mama Ghasia anajua kuna wabunge wezi bungeni, wabunge walioiba nyaraka za siri za Serikali na kuvunja sheria kadhaa alizonukuu kinachotakiwa kufanya ni Mwendesha Mashitaka atangaze mara moja kuwa amepata ushahidi toka kwa Ghasia na mashitaka yanaletwa dhidi ya wabunge hao, na kama hilo halifanyiki au Ghasia hana ushahidi basi yeye mwenyewe atakiwe kubanwa na wabunge wa chama chake kwa kulidanganya Bunge na kulikashfu na ikibi atakiwe kujiuzulu!

Vinginevyo, kama hawataki kusimamia sheria watuambie tu ili kila mtu ajue kufanya mambo kivyake vyake! Vinginevyo kama Bunge lina wezi, mafisadi, na wavunjaji sheria wengine tunajuaje sheria wanazotunga haziendani na maslahi ya aina fulani binafsi ya wahusika?

Ni kitu gani kinaweza kutufanya tuamini kuwa sheria wanazotunga zimeangaliwa kwa ukaribu na zina maslahi kwa taifa?
 
Back
Top Bottom