Watanzania wamkumbuka Mwalimu Nyerere leo

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,011
Watanzania wamkumbuka Mwalimu Nyerere leo
Angela Semaya
HabariLeo; Sunday,October 14, 2007 @00:05

WATANZANIA leo wanaadhimisha kumbukumbu ya miaka minane ya kifo cha Rais wa Kwanza na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere huku wengi wakiwa bado wakikumbuka na kuthamini mchango wake katika ujenzi wa taifa.

Licha ya kuwa na mitazamo tofauti wengi miongoni mwa waliohojiwa na HabariLeo Jumapili ikiwa sehemu ya kuadhimisha kumbukumbu ya Mwalimu wamesema wanaamini alikuwa kiongozi wa kweli aliyejitoa na kutetea maslahi ya Watanzania bila kubagua.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Habarileo Jumapili baadhi yao walisema aliweza kujenga amani, utulivu na mshikamano.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Azaveli Lwaitama alisema anamkumbuka Nyerere kama mwanasiasa aliyejitoa mhanga kwa kujitumbukiza katika masuala ya siasa kwa lengo la kuondoa dhuluma na kutetea maslahi ya Watanzania.

“Mwalimu aliibuka katika siasa kutokana na imani yake, alisononeshwa na utawala wa kikoloni, alijitoa mhanga yeye mwenyewe kwa kujielimisha na kuhakikisha anatumia uwezo wake wote kuondoa hali hiyo ya ubaguzi,” alisema.

Dk. Lwaitama alisema Nyerere kwake siasa ilikuwa kuondoa dhuluma na kwamba akiwa mtoto anayetoka katika ukoo wa uchifu alikuwa na fursa nyingine kama watoto wa machifu wengine lakini yeye aliamua kujibana na kujitoa mhanga kuwakomboa Watanzania.

Alisema Mwalimu Nyerere angerudi leo angeshangaa kuona sampuli ya watu wanaoingia katika siasa na serikalini kwani wapo wanaoingia kwa ajili ya kujinufaisha wenyewe.

Dk. Lweitama alisema Nyerere pia angeshangaa kuona tofauti kubwa kati ya viongozi na watu wanaowaongoza.

“Hivi sasa watu wanajiingiza katika masuala ya siasa ni matajiri ambao unajiuliza kama kweli wana uchungu na wananchi wao…huenda wanaingia kwa nia nzuri, lakini ni wachache wanafahamu mazingira hasa waliyonayo wananchi wa kawaida,” alisema.

Dk. Lweitama alisema mfumo wa kutafuta uongozi kwa watu wenye fedha nyingi ni hatari maana miaka ijayo watu wanaweza kushangaa mshikamano, amani na utulivu uliokuwa enzi za Nyerere umetoweka.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP)Augustine Mrema alisema Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi aliyeweka misingi mizuri ya kujenga taifa.

Kwa mujibu wa Mrema, Nyerere alijenga amani, upendo, undugu na alihifadhi rasilimali za nchi tofauti na viongozi waliopo sasa.

“Tunamkumbuka Nyerere wetu, kwani tumebaki na viongozi wa ajabu, hawajali maslahi ya watu…kama Nyerere anaweza kurudi, basi arudi haraka maana tunamhitaji,” alisema.

Ibada maalumu pia inafanyika leo katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Cecilia mkoani Arusha ambayo itahudhuriwa na Rais Jakaya Kikwete, viongozi na wananchi.

Maadhimisho hayo pia yataambatana na kilele cha mbio za Mwenge na Wiki ya Vijana na Rais atalihutubia taifa katika Uwanja wa Sheikh Abeid Aman Karume.

Oktoba 14 ya kila mwaka Watanzania hukumbuka siku ya kifo cha Baba wa Taifa , Mwalimu Nyerere ambaye alikuwa Rais wa Kwanza wa Tanzania, aliyefariki dunia Oktoba 14, 1999 katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas jijini London, Uingereza kwa ugonjwa wa kansa ya damu.


Copyright @TSN 2006 All Rights Reserved
 
Back
Top Bottom