Watanzania wamelogwa na nani kutafuta viungo vya wenzao?

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,316
33,125
SIKU chache zilizopita nilipokuwa nikifungua baadhi ya magazeti tandu ili kusoma mambo mbalimbali, katika funguafungua yangu nilikutana na habari moja ya kusikitisha ya mtoto wa miezi mitano kukatwa viganja vyote vya mikono yake na mtu asiyefahamika katika kijiji cha Bwai, wilayani Musoma Vijijini katika Mkoa wa Mara.

Habari hiyo ilieleza tukio la mtoto Simula Magati kukatwa viganja vya mikono yake yote na alikutwa katika hali hiyo baada ya bibi yake Nyapamba Magati aliyekuwa ametoka kurudi.

Kwa vyovyote vile lazima bibi huyo alipatwa na mshtuko usiokuwa wa kawaida kwa maana dakika chache tu alitoka na alivyorudi alikuta mjukuu wake akiwa amefanyiwa ukatili huo.

Baada ya kusoma habari hiyo, jambo la kwanza lililopita kichwani na kwenye fikra zangu, lilikuwa ni namna gani mwanadamu anakuwa mkatili kiasi hiki, bila huruma kuamua kumuumiza mtoto mdogo asiyekuwa na hatia.

Tukio hili halina tofauti na matukio wanayofanyiwa watu wenye ulemavu wa ngozi ambao nao wamekuwa wakiuawa na kukatwa viungo vyao na kusababishiwa ulemavu na maumivu na watu wasiokuwa na huruma wala kuthamini maisha ya wenzao.

Chanzo kikubwa cha matukio haya ni imani za kishirikina ambapo watu wamekuwa wakidanganywa na kuliwa fedha zao na waganga ambao ni matapeli tu.

Hivi kweli viganja vya mtoto mdogo vinaweza kukupatia utajiri wowote, kama ndiyo hivyo mbona unapokwenda kwa baadhi ya waganga hao matapeli wanaishi katika nyumba mbavu za mbwa, kama kweli wanaweza kufanya wengine kuwa matajiri mbona wao wanaishi kimasikini.

Lazima ujiulize kabla hujachukua hatua ya kujeruhi na kuumiza watu wengine wasiokuwa na hatia.

Kwa nini Watanzania tunakubali kufanywa wajinga na baadhi ya watu wajanja wanaojipatia fedha kwa kukatili maisha ya watu wasiokuwa na hatia? Unyama huu utaendelea mpaka lini jamani?

Hii ni aibu kwa taifa hili linalosifika kwa amani, upendo na mshikamano, lakini kwa mtindo huu wa ukatili sidhani kama sifa hii itaendelea kuonekana maana kuna doa tena doa baya! Ifike wakati sasa kwa jamii kukubali kubadilika na kuachana na imani hizi potofu! Ama sivyo tutaendelea kujikuta tukiumizana na kuuana kwa sababu ya imani ambazo kimsingi hazina manufaa zaidi ya kusababishiana majonzi na maumivu.

Naamini sio waganga wote ambao ni matapeli, wako waganga wengine wanaagua watu kwa kutumia dawa za asili, lakini kutokana na vitendo hivi watu wengi wanakosa imani na waganga hao na hivyo kundi la matapeli wachache linachafua sifa yenu maana kuna msemo kwamba, samaki mmoja akioza ni wote.

Kwa mtazamo wangu waganga wa jadi wenyewe mnalo jukumu la kuchunguzana na kufuatiliana ili kuwabaini wale wachache wanaotumia fani yenu kujinufaisha kwa kudanganya watu na kupelekea wengine kufanya vitendo vya kutisha vya kujeruhi na kukatisha maisha ya watu wengine.

Jamii nayo inapaswa kubadilika na kuachana na imani hizi za kishirikina, utajiri, vyeo, mafanikio kamwe hayawezi kuja kwa kuua ama kuchukua viungo vya mtu mwingine, huu ni uongo mtupu!

Pia serikali haiwezi kuwekea kila mtu ulinzi, lakini inao wajibu wa kuhakikisha inadhibiti matukio hayo yasiendelee kutokea kwa kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua kali za kisheria wale watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo vya ukatili.

http://www.habarileo.co.tz/safu/?n=3907
 
Back
Top Bottom