Watanzania tutatoka vipi ndani ya chupa?

Wateule

JF-Expert Member
Sep 17, 2010
390
368
CHUPA.jpg

Kama tujuavyo "Msema Pweke Hakosi", labda tu kwa faida ya wasomaji wetu, ni wakati muafaka kutumia fursa hii kuwekana sawa. Hii methali ina maanisha kwamba yeyote yule anayesema na nafsi yake huwa hakosei, kwa maana kwamba yale usemayo kwenye nafsi yako ndio yatokeayo. Hivyo basi, cha msingi tunapozungumza na nafsi zetu tuzungumze yaliyo chanya, ili kupata matokeo chanya. Tunajua dhahiri kwamba nchi yetu ipo katika vuguvugu zito la mabadiliko, na kama Watanzania tunao wajibu wa kutumia vichwa vyetu ipasavyo ili kufanya maamuzi sahihi, ambayo yatatuletea mabadiliko yenye faida kwa wote.

Jamii kubwa ya Watanzania leo hii wanateseka ndani ya nchi yao. Yaani wala usitake nianze kusema matatizo ya Umeme, Mabomu, Umaskini na huduma mbovu za afya. Wengi wetu tunajihisi kama hicho kikaragosi ndani ya chupa! Yaani tumefungiwa ndani ya Kachupa, bila kufahamu tutatoka vipi na lini! Mchora kikaragosi (Katuni) ndugu GebiNtoni ameuliza swali "Jamani, ina maana kunitoa humu ndo imeshindikana?" Hili ni swali zuri na la msingi sana……..lakini kwa faida yetu kama WaTanzania tulitakiwa tujiulize swali hili kama ifuatavyo "Jamani, ina maana kujitoa humu ndo tumeshindwa?" Tutakapo jiuliza swali sahihi, ni dhahiri tutapata jibu sahihi tu. Baada ya kuweka swali letu sawa, tunagundua kwamba jukumu la kujikwamua kutoka ndani ya chupa hilo, ni letu sote kama Watanzania.

Hatutoshindwa kujitoa kwenye chupa hilo endapo tutatumia fursa zinazojitokeza sasa katika nchi yetu. Kwa mara ya kwanza serikali ya CCM imekubali kwa shingo upande suala la katiba mpya lijadiliwe, na hapa haswa ndio tutakapo anzia safari yetu yakutoka ndani ya Chupa hilo. Najua kuna baadhi ya mijadala kama ya "White Paper" ili wahi kufanyika huko siku za nyuma, ambayo ukiichunguza ilikuwa ni kama geresha tu. Kwa mtazamo wangu, huu wa sasa una muamko na ushiriki mkubwa wa wananchi. Katiba yetu imepitwa na wakati kwa muda mrefu sasa na kwa bahati mbaya serikali zilizotangulia kabla hii ya Mh. Jakaya Kikwete (JK) zimekuwa zinalifumbia macho suala hili. Kutokana na hali halisi ya upepo wa kisiasa, serikali ya CCM haina budi, bali kukubali kwamba huu ni wakati muafaka wa kuitazama katiba yetu upya. CCM na serikali yake wanajua wazi kwamba katiba yenye kuendeana na mfumo wa sasa wa vyama vingi itawapa Watanzania fursa ya kuchagua nani wa kuongoza nchi yao. Katika uchaguzi huo, ni dhahiri kwamba chama chochote chenye sera muafaka za kumtoa Mtanzania kwenye chupa ndicho kitakacho pewa usukani, hivyo basi suala la mjadala wa katiba mpya ni muhimu sana, na Watanzania wote popote tulipo hatuna budi kuliwekea mkazo kwa nguvu zote.

Sote tunatakiwa tushiriki katika mijadala inayoendelea sasa, na inapolazimika kujitokeza katika maandamano ya amani yenye lengo la kuishinikiza serikali kusikiliza mapendekezo ya mabadiliko ya vipengele kandamizi katika katiba ya sasa. Sitotumia muda mwingi hapa kuvichambua vipengele hivyo kwa ibara na mistari, isipokuwa nitavitaja kwa uchache tu.

Suala la Tume huru ya uchaguzi ni moja ya vipengele muhimu katika katiba yetu mpya. Suala la Tume huru ya uchaguzi ndio suala litakalo tuletea uchaguzi huru na wa haki. Uchaguzi ambao Watanzania wote watapiga kura na kuridhika kuwa hamna uchakachuaji wa aina yeyote utakao fanyika kwa lengo la kupora maamuzi yao.

Suala jingine ni uwezo wa vyama shiriki kuwa na uwezo wa kisheria kuhoji matokeo ya Urais mahakamani endapo wana ushahidi kuwa uchakachuaji umefanyika. Tumeshuhudia uchaguzi wa mwaka 2010 ulivyokuwa na matatizo ya hapa na pale (ikiwemo hili la tuhuma nzito za uchakachuaji wa kura)….. lakini je nani wa kumvika Paka kengele?

Jingine nyeti hapa ni lile la mawaziri kuwa wabunge. Ndugu zangu hapa tunawekeana usiku katika suala zima la kujiletea maendeleo. Hapa ningependa tuzingatie mfumo wa Marekani, ambao ndugu zetu Wakenya pia wameutumia katika kupitisha mabadiliko ya katiba yao mpya tarehe 4 Agosti 2010. Wakenya kama Wamarekani walikubaliana kuwa Mawaziri hawatateuliwa na Rais kutoka bungeni, badala yake watakuwa ni wataalam kutoka sekta mbali mbali. Hili ni muhimu sana ndugu zangu katika kuhakikisha kwamba Wabunge wanafanya kazi yao kama Wabunge na Mawaziri wanafanya kazi yao kama Mawaziri, na yeyote miongoni mwao akivurunda inakuwa ni rahisi kuwajibishwa ipasavyo. Kwa sasa wabunge wetu, haswa wale wa chama tawala wanashindwa kufanya kazi yao ipasavyo kutokana na mgongano wa kimaslahi.

Wabunge wetu, ambao wamepewa Uwaziri wanaotakiwa watetee na kupigania maslahi ya wananchi waliowachagua majimboni mwao wanajikuta wana kibarua kingine cha kutetea maslahi ya serikali. Kizungumkuti hiki kinapelekea Wabunge hao kushindwa kutetea wananchi kwa kuhofia kuwa kibarua cha Uwaziri kinaweza kikaota nyasi. Kama wahenga walivyosema "Huwezi kutumikia mabwana wawili" na hili ndio haswa linalowakumba viongozi wetu hawa. Ili kusonga mbele tunatakiwa tuumalize mfumo huu, ili iwe rahisi kwa Wabunge kuibana Serikali kupitia Mawaziri wake wateule bila uwoga wowote. Kumfanya Mbunge kuwa Waziri kwa wakati mmoja ni kwenda kinyume na ule usemi wa "Kinyozi hajinyoi".

Muundo wa Mawaziri na Wabunge huru ndio muundo muafaka katika kufanikisha safari yetu nje ya Chupa. Baada ya vyama vya upinzani kufanikiwa kuongeza idadi ya wabunge kwa asilimia kubwa kupitia uchaguzi wa Octoba 2010, nafikiri mtakubaliana na mimi kwamba Bunge letu limechangamka sasa na hata serikali imekuwa makini zaidi katika utendaji wake. Tunataka muamko huu uendelee, na muamko utaendelea endapo tu tutawapa Wabunge wetu uhuru zaidi.
Tumeshuhudia jinsi muundo huu unavyofanya kazi ipasavyo Marekani, na muda si mrefu utaanza kuzaa matunda Kenya na endapo Watanzania tutaupitisha mfumo huo ni dhahiri kwamba safari yetu ya kutoka ndani ya Chupa itarahisishwa pia! Najua kwamba tuna matatizo mengi kwenye katiba yetu zaidi ya hayo niliyoyataja, lakini endapo tutadai mabadiliko, bila kubadilisha hayo, basi tutakuwa bado tunafurukuta ndani ya Chupa. Wewe unasemaje?
Msema Pweke Hakosi! Ponda Kichwa…….

By Rungwe Jr.
rungwe@thehabari.com
www.thehabari.com
 
Back
Top Bottom