Wasomi wapinga anasa katika matumizi ya serikali

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,299
33,080
MATUMIZI ya Sh10 trilioni kwa mwaka yamewashtua wasomi na wachumi nchini wakisema yanaashiria hatari kwa uchumi na kuitaka serikali ipunguze matumizi ya anasa, hasa ununuzi wa magari ya kifahari na safari zisizo muhimu.
Mwananchi iliongea na wasomi hao baada ya serikali kutoa taarifa ya mwenendo wa uchumi inayoonyesha kuwa Sh10 trilioni zinatumiwa na serikali wakati mapato yake ni Sh5 trilioni tu. Bajeti ya matumizi ya serikali ya mwaka 2009/10 ni Sh9.5, wakati mapato ni Sh5 trilioni tu.
Taarifa hiyo pia inaonyesha kuwa ukusanyaji wa mapato umeshuka na hivyo kuiweka serikali katika hali ngumu, kw amujibu wa ripoti iliyotolewa juzi na katibu mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Ramadhani Kijja ambaye alisema nakisi hiyo ya Sh5 bilioni huzibwa na misaada kutoka nchi wafadhili pamoja mikopo.
Wakizungumza na gazeti hili jana kwa nyakati tofauti, Dk Honest Ngowi na Profesa Delfin Rwegasira walisema kutegemea pesa za misaada na mikopo ni hatari kwa ukuaji wa uchumi nchini na kwamba hali hiyo inaashiria kuwa maisha ya Watanzania yatazidi kuwa mabaya zaidi.
Dk Ngowi, ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, alisema pengo la pesa hizo linatokana na matumizi yasiyo ya lazima yanayofanywa serikalini.
¡°Imefika wakati kwa serikali kubana matumizi na kuondokana na matumizi ya anasa yaani ya kutumia magari ya kifahari, safari zisizo na ulazima pamoja na kupunguza semina,alisema Dk Ngowi.
¡°Haya mambo ndio yanaisababishia serikali kuwa na matumizi makubwa wakati hayana umuhimu wowote.
Serikali ilishahidi kuachana na ununuzi wa magari ya kifahari, maarufu kama mashangingi na pia kutangaza kuwa semina zote zitalazimika kupata kibali cha ofisi ya Waziri Mkuu, lakini imekuwa kimya kuhusu safari zisizo na umuhimu.
Dk Ngowi alisema kuwa kuendelea kutegemea misaada na mikopo kutoka nchi wahisani katika wakati huu ambao uchumi wa dunia umekumbwa na misukosuko, ni hatari na kwamba nchi inaweza kukosa misaada hiyo na hivyo kusababisha mipango ya maendeleo iharibike.
Dk Ngowi pia aliishauri serikali akisema: ¡°Ili tuondokane na utegemezi, serikali iongeze nguvu na ikusanye mapato kwa umakini sana maana wapo Watanzania wengi ambao hawalipi kodi kama inavyostahili.
Naye Profesa Delfin Rwegasira wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) aliitaka serikali ifanye kila liwezekanalo ili matumizi yalingane na mapato yake na kwamba utegemezi Sh5 triioni ni hatari katika ukuaji wa uchumi.
¡°Ni kawaida kwa nchi zinazoendelea kusaidiwa lakini kiwango hiki ni kikubwa na mara nyingi pesa zenyewe haziji katika wakati muafaka.
¡°Hivyo ili nchi isiyumbe kiuchumi ni lazima serikali ifanye kila linalowezekana ili matumizi yake yaendane na kipato cha nchi, zaidi ya hapo hali ya maisha ya Watanzania itazidi kuwa mbaya tofauti na ilivyo sasa,¡± alisema Profesa Rwegasira
Kijja alisema katika kipindi cha miaka mine mapato ya serikali yamepanda kwa mwezi kutoka Sh150 bilioni mwaka 2005/6 hadi Sh400 bilioni hivi sasa.
Hata hivyo, alisema mbali ya matumizi hayo, serikali bado inakabiliwa na deni la taifa ambalo hadi mwezi Juni mwaka 2009 lilikuwa Dola za Kimarekani 8.25 bilioni ambapo kati ya hizo Dola 5.69 bilioni ni deni la nje na Dola 2.60 bilioni deni la ndani.
Alisema sababu zilizochangia kuongezeka kwa deni hilo ni mikopo mipya kutoka ndani na mikopo yenye masharti nafuu kutoka nje, kushuka kwa thamani ya shilingi, malimbikizo ya riba hasa katika nchi zisizo wanachama wa Paris Club na mikopo ya kibiashara.
Pia Kijja alisema pato la Mtanzania kwa mwaka limeongezeka kutoka Sh 548,388 mwaka 2007 hadi kufikia Sh 628,259 mwaka 2008 na kwamba pato hilo limekuwa likiongezeka kwa kipindi chote cha awamu ya nne.
Alisema umaskini wa kipato pia umepungua kutoka asilimia 35.7 mwaka 2001 hadi kufikia asilimia 33.3 mwaka 2007 huku uchumi ukikua kwa asilimia 7.2.
Alisema pia katika kipindi cha miaka minne kasi ya ongezeko la bei imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka ambapo hadi mwezi Desemba mwaka jana ulifikia asilimia 12.2 lakini kwasasa umeanza kurudi chini na kufikia asilimia 10.9 mwezi Januari mwaka huu.


http://www.mwananchi.co.tz/newsrids.asp?id=18343
 
Back
Top Bottom