Wasomi: Serikali isithubutu kutuingilia

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
WANATAALUMA wa vyuo vikuu wameeleza kusikitishwa kwao na hatua ya serikali kutaka kuingilia uhuru wao, jambo ambalo linaweza kusababisha mvurugano.

Wakizungumza na Tanzania Daima wanataaluma hao walisema kuwa wao si walimu wa vyuo vikuu pekee bali ni wa dunia nzima, ndiyo maana wana uwezo wa kutoa mawazo yao bila kuingiliwa na chombo chochote.

Akichangia zaidi, Mhadhiri wa Chuo Kikuu sehemu ya Mlimani jijini Dar es Salaam, Sengondo Mvungi, alisema kuwa ni kitendo cha ajabu iwapo serikali itaingia madarasani na kusikiliza kile ambacho tunakifundisha.

Alisema kitendo hicho kinaweza kusababisha kutoelewana na hata kuvifanya vyuo vikuu kuwa kama shule za msingi kama wataingilia uhuru wa wanataaluma hao.

Mvungi alisema kuwa wahadhiri wanapofundisha hawapangiwi wafundishe kitu gani na hata ikitokea wanafunzi wakauliza swali wanapaswa wapewe majibu ya kutosheleza.

“Leo mwanafunzi ananiuliza swali hata kama linahusiana na Chama Cha NCCR- Mageuzi ninapaswa kuwajibu yale ambayo yanajitosheleza bila kumung’unya kitu chochote na majibu yawe yana maana,” alisema.

Alisema serikali isijaribu wala kuthubutu kuingia wakati anafundisha kwani kitendo hicho ni kinyume cha sheria na inaweza kumfanya akachukua hatua isiyofaa.

Naye Profesa Joseph Mbele katika maoni yake alisema kuwa aliiona taarifa hiyo ya serikali hivyo alitumia wadhifa wake kama mwanataaluma na mzoefu wa kufundisha au kutoa mihadhara vyuo vikuu sehemu mbalimbali za dunia kuchangia hoja hiyo.

Alisema si kazi ya serikali kuingia darasani chuo kikuu ili kuchunguza mwalimu anafundisha nini au anafundishaje.

Hii ni kazi ya wanataaluma na wahadhiri, kufuatana na taratibu zinazotambulika katika jumuia ya wanataaluma.

Taratibu hizo ni za kulinda, kutathmini, kuratibu na kuboresha viwango vya utafiti, ufundishaji na taaluma kwa ujumla.

Profesa Mbele alisema serikali inapaswa kutambua kuwa dhana ya chuo kikuu duniani pote, inaendana na haitengeki na uhuru wa kitaaluma. Walimu wa vyuo vikuu si tu wana wajibu, bali uhuru wa kufukuzia taaluma bila vipingamizi, kwa mujibu wa vigezo vya taaluma hizo vinavyotambulika miongoni mwa wanataaluma kimataifa.

“Kama kuna walakini katika utendaji kazi wa mwalimu wa chuo kikuu, kama vile kutofundisha somo inavyotegemewa, wanaowajibika kuchunguza ni wanataaluma wenzake, si serikali,” alisema.

Aliongeza kuwa serikali haitegemewi wala kuruhusiwa kuingilia uhuru wa walimu na watafiti chuo kikuu katika kufanya utafiti, ufundishaji, uandishi na kwa misingi na viwango vinavyotambuliwa kitaaluma.

Alieleza jambo jingine la msingi kuwa chuo kikuu ni mahala pa tafakari na malumbano kuhusu masuala mbali mbali, kwa kiwango cha juu kabisa. Ni sehemu ambapo fikra za kila aina na hoja za kila aina zinapaswa kusikika na kuchambuliwa.

“Chuo kikuu cha kweli, chenye hadhi ya chuo kikuu, ni maskani ya wachochezi wa fikra na hoja, katika taaluma mbali mbali, ikiwemo siasa. Huwezi kumwambia mtafiti au mhadhiri asiiponde serikali iliyoko madarakani iwapo utafiti na tafakari yake inampeleka huko,” alifafanua.

Alisema dhana ya kwamba kuna wanaoeneza siasa za chuki miongoni mwa wanafunzi wa chuo kikuu ni dhana ya kusikitisha.

Inamaanisha kuwa hao wanafunzi ni wajinga au ni wavivu ambao hawana uwezo au dhamira ya kujibidisha katika kusoma na kutafakari mambo ili waweze kugundua mapungufu ya hoja wanazosikia, na kupambana kwa hoja.

Alieleza kuwa inamaanisha hao ni wanafunzi mbumbumbu, wasio na akili au wasiotumia akili. Kitendawili ni je, walifikaje hapo chuoni, kama si kwa njia za panya?

Profesa Mbele alisema wanafunzi wa chuo kikuu wanawajibika kuwa tayari na makini katika kupambana kwa hoja na wanafunzi wenzao na pia na walimu wao. Ni fedheha iwapo wanafunzi hao kiwango chao ni duni kiasi cha kuweza kupotoshwa na walimu wao.

Alisema hao hawastahili kuitwa wanafunzi wa chuo kikuu, na hicho chuo chenyewe hakistahili kuitwa chuo kikuu. Na ni fedheha kama tumefikia mahali ambapo serikali inaona ije darasani kuwanusuru hao wanafunzi feki.

Mwishoni mwa wiki iliyopita serikali kupitia Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, alisema kuwa inawachunguza wahadhiri wa vyuo vikuu nchini wanaotumia muda mrefu madarasani kuzungumzia siasa badala ya kufanya kazi zinazohusu taaluma.

“Tunaendelea na uchunguzi wa kuwabaini baadhi ya wahadhiri wanaojihusisha na siasa kwa kuingia madarasani na kuzungumzia siasa kwa dakika kumi kabla ya kuanza kufundisha,” alisema Mulugo.

Alisema lengo la wahadhiri hao ni kuwafanya wanafunzi kuchochea migomo na maandamano na kupandikiza chuki baina ya serikali na wanafunzi.

Wasomi: Serikali isithubutu kutuingilia
 
Back
Top Bottom