Wasindika samaki wa Tanga wafungiwa

lifeofmshaba

JF-Expert Member
Feb 19, 2011
867
219
MAMLAKA ya Udhibiti wa Chakula na Dawa (TFDA), imekifungia Kiwanda cha Kusindika Samaki cha Sea Product cha jijini Tanga kwa kosa la kuingiza shehena ya samaki kutoka nje ya nchi bila kibali cha mamlaka hiyo.

Uamuzi wa TFDA kukifungia kiwanda hicho umefikiwa baada ya kufanyika kwa ukaguzi katika kiwanda na kujumuisha maofisa kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Chakula na Dawa, Idara ya Afya ya Jiji la Tanga pamoja na Tume ya Taifa ya Nguvu za Atomiki.

Ukaguzi huo umetokana na kuwepo kwa taarifa ya kuingizwa kwa samaki wa aina mbalimbali kutoka nchini Msumbiji ambao inadaiwa kuwa wameathiriwa na mionzi.

Kaimu Meneja wa TFDA Kanda ya Kaskazini, Bukuku Juma aliwaambia waandishi wa habari kuwa kiwanda hicho kimefungiwa kwa kukiuka sheria inayosimamia uingizwaji wa dawa na chakula.

Naye Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Eric Allard ambaye awali aliwagomea wakaguzi hao kuingia katika kampuni yake alikiri baadaye kuingiza shehena ya samaki aina ya kamba kutoka nje ya nchi.

Pamoja na jopo hilo kutumia muda kumuelimisha kuhusu uhalali wa TFDA katika utekelezaji wa shughuli zake hizo, alidai hatambui umuhimu wa mamlaka hiyo kwa kuwa muda wote amekuwa akifanya kazi kwa kushirikiana na Idara ya Udhibiti wa Ubora ya Wizara ya Maendelo ya Mifugo na Uvuvi tangu mwaka 1996.

“Mimi kwa kweli nimechoshwa na sheria nyingi zinazowekwa kwenye nchi hii, unafanya kazi ukifuata sheria fulani kesho unafuatwa na kuambiwa umekosea kutokana na sheria nyingine,” alisema Allard.

“Kwa hiyo mimi nimechoka maana zinajichanganya kila siku ni bora nifunge hiki kiwanda na hawa wafanyakazi niwakusanye wote muwachukue ninyi TFDA mkawaajiri.”

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, hatua ya kufungwa kwa kiwanda hicho itaathiri zaidi ya wafanyakazi 150 pamoja na wavuvi 3,000 waliopo katika Halmashauri ya Jiji la Tanga wanaouza samaki hapo.

Taarifa ya kuwepo kwa samaki walioathiriwa na mionzi iliibuka hivi karibuni na kuzua hofu kubwa miongoni mwa watumiaji wa kitoweo hicho baada ya kudaiwa kuingizwa kinyemela nchini hasa kutoka Japan.
 
Back
Top Bottom