Wasahau mwili wa marehemu, wazika jeneza tupu

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
KATIKA hali isiyo ya kawaida na ya kusikitisha, familia moja jijini hapa imejikuta ikizika jeneza tupu bila mwili wa marehemu, hali ambayo imeibua taharuki na hofu kubwa.

Tukio hilo la aina yake tangu kuanza kwa mwaka huu wa 2011 lililoibua hisia tofauti miongoni mwa wakazi wa jiji hili na viunga vyake, lilitokea juzi katika Mtaa wa Makunguru, Kata ya Manga, ambapo familia ya Mashaka Mwasubila, ilijikuta ikifanya maziko ya mtoto wao wa miezi sita mara mbili, baada ya awali kuzika jeneza tupu kufuatia kuusahau mwili wa kichanga hicho chumbani.

Taarifa kutoka kwa majirani wa familia hiyo na baadaye kuthibitishwa na baba mzazi wa marehemu, zilieleza kuwa Januari 11 walijikuta kwenye taharuki kubwa iliyosababisha baadhi ya watu waliokuwa nyumbani hapo akiwamo mama mzazi wa marehemu kuanguka na kupoteza fahamu baada ya mwili wa marehemu waliyeamini kuwa wamemzika muda mfupi uliopita kuukuta ukiwa umelala kitandani chumbani kwa wazazi wake.

Akisimulia zaidi tukio hilo, mmoja wa majirani hao aliyeomba jina lake lihifadhiwe alisema baada ya kufika nyumbani kwa familia ya marehemu, siku hiyo ya Januari 11 majira ya saa nane mchana alikuta umati wa watu wakifanya ibada ya kuaga mwili wa marehemu na baadaye jeneza lake kubebwa kuelekea sehemu ya maziko.

“Tulibeba jeneza kutoka Makunguru hadi Ilomba kwa James ambapo mchungaji alifanya sala fupi ya maziko makaburini hapo, na hatimaye tulizika na wote tulirudi nyumbani kwa wazazi wa marehemu ili kumalizia shughuli za msiba,” alisema.

Aliongeza kuwa muda mfupi baada ya kufika nyumbani kwa wazazi wa marehemu huyo, walishangaa kuibuka kwa mayowe ya vilio na punde kupewa taarifa na mmoja wa wanafamilia hao kuwa wamekuta mwili wa marehemu ukiwa kitandani.

Alisema baada ya taarifa hiyo kutolewa kila mtu katika eneo hilo alijikuta katika wasiwasi na taharuki huku baadhi yao wakitimua mbio na wengine kuanguka hovyo kwa kile walichoamini kuwa tukio hilo la kukutwa mwili wa kichanga hicho limetokana na vitendo vya ushirikina.

Tanzania Daima iliwasiliana na baba wa marehemu, ambaye alikiri kutokea kwa tukio hilo na kumtaja mwanae huyo kwa jina la Ephraim Mashaka, miezi 6, ambapo alisema kifo chake kilikuwa cha kawaida.

Akifafanua zaidi kuhusu tukio hilo alisema hali hiyo ilijitokeza baada ya kuwepo uzembe kati ya watu wawili waliopewa jukumu la kushughulikia usafi wa mwili wa marehemu.

“Inasikitisha lakini unajua kazi ya usafi wa mwanangu ilikuwa mikononi mwa watu wawili na baada ya kutokea hali hii tulipowabana kila mmoja alisema kuwa eti alidhani mwenzake alifanya kazi ya kuutumbukiza mwili wa marehemu kwenye jeneza baada ya kumaliza usafi,” alisema Mwasubila.

Hata hivyo mama wa marehemu huyo hakuweza kuzungumza kwa kile kinachodaiwa kupata mshtuko baada ya kukuta mwili wa marehemu ukiwa chumbani baada ya kuamini kuwa tayari walikuwa wameshamzika.

Lakini mmoja wa vijana waliobeba jeneza hilo kulitoa chumbani kwenda mazikoni, aliyejitambulisha kwa jina la Peter Mwandezi, alisema baada ya kuingia chumbani wao walibeba jeneza bila kulifungua wakiamini kuwa kulikuwa na mwili wa marehemu, huku pembeni kukiwa na blankeni likiwa limeviringwa ambalo ndilo lilibainika baadaye kuwa ndiko alikowekwa marehemu baada ya kufanyiwa usafi na si ndani ya jeneza.

Hata hivyo ilibainika kuwa mchungaji wa Kanisa la Pentekoste Hollness Mission (PHM), Layton Mwasaga, ambaye alipewa jukumu la kuendesha sala ya mazishi ndiye alichangia kutokea kwa hali hiyo, baada ya kuzuia mwili huo usiagwe kwa madai kuwa hali ya hewa ya mvua ingeweza kusababisha kukwamisha maziko na kuamuru mwili huo ufanyiwe sala bila ndugu, jamaa na majirani kuaga.
 
Back
Top Bottom