Waraka wa Pascal Mayalla - Asanteni Sana!

Pole sana Paschal, na ni jambo jema kumshukuru Mungu kwa uhai aliokuachia. Ni vema kama hujatoa shukrani basi ukatoe kanisani na familia yako. Na umwombe Mungu aendelee kuupatia mkono wako nguvu uweze kurejea full katika shughuli zako za kushika kamera.
 
Wana Forum,
Salaam.

Naombeni kutoa waraka wangu huu wa Shukrani kupitia Jamii Forums kwa Sababu ni Jamii furum hii ndio iliowajulisha wengi kuhusiana na ajali yangu ndipo namimi nilipoijua hivyo nishukuru sana jamiiforums na natoa shukrani zangu mbalimbali.

Leo 3/08/09 umetimia mwaka mmoja tangu nilipopata ajali mkoani Dodoma.
Sasa nimepona japo mkono wa Kushoto bado haujapona. Leo nimerejea Dodoma kuzuru eneo la ajali, ndipo nilipotulia na kutafakari, nikajikuta ninawiwa kushukuru kwa yote, ndio maana nimetoa waraka huu wa shukrani.

Kwanza kabisa namshukuru Mungu, kuniruhusu kuendelea kuishi, kiukweli ni kama nilishakufa, Mungu Baba akanihurumia kunirudishia uhai ili niendelee kuishi. Hii ni privilage tuu kwa sababu sikustahili. Nasema asante sana Mungu kuniweka hai.

Pili naishukuru sana familia zangu za pande zote nikianzia kwa Familia ya Kasanga, Mayalla, Ukoo wa Kundi wa Kirua Vunjo Moshi, Ukoo wa Mmari wa Sanya Juu, Ukoo wa Mwingira wa Ndumbi Songea, mke wangu na watoto wangu wote 5 kwa yote waliyoyavumilia katika kipindi chote tangu ajali mpaka sasa. Asanteni Sana.

Namshukuru dereva wa Lori la Mafuta la Gapco aliyekuwa na ujasiri wa ajabu wa kuupekua mwili wa mtu aliyedhaniwa kufa, kutoa simu mfukoni na kupiga namba za mwisho zilizopelekea Timu ya PPR iliyokuwa Dodoma ikiongozwa na Adam Njakachai, kuja eneo la tukio na kunipatia msaada wa haraka mpaka hospitali ya mkoa wa Dodoma. Asanteni sana.

Nawashukuru madaktari na manesi wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma tangu mganga mkuu, manesi wa zamu na daktari bingwa aliyelazimika kukatiza mapumziko yake ya jumapili na kuja kukesha usiku kucha na mimi hospitali mpaka nilipopata fahamu. Asanteni sana.

Nawashukuru sana wanahabari wenzangu waliokuweko Dodoma, ambao walisambaza taarifa zangu na hatimaye wateja wa PPR kwenye Maonyesho ya 88 na marafiki zangu wa Dodoma walikuja kwa haraka hospitalini sambamba na michango iliyowezesha kupata kila huduma iliyohitajika mpaka nilipohamishiwa Moi, Asanteni Sana.

Navishukuru vyombo vya habari na jumuiya ya wanablog mbalimbali kwa kuutangazia ulimwengu kuhusu ajali yangu kulikopelekea ndugu jamaa na marafiki waliotapakaa kote ulimwenguni kupata taarifa, hivyo waliniombea uponyaji wa haraka na weghine kutoa support ya hali na mali.

Namshukuru Mdogo wangu Isaack kwa kukubali kugharimia ndege ya kukodisha kuniairlift toka Dodoma mpaka Dar baada ya taarifa ya awali kuwa nimevunjika spinal, pia namshukuru dereva wake aliyekuja Dodoma na strecher vehicle kunifuata na support team. Asanteni Sana.

Nawashukuru sana Madaktari na manesi wa kitengo cha mifupa MOI wakiongozwa na Dr. Kahamba na Daktari wangu Dr. Mareale kwa jinsi walivyohangaika na mimi kwa mwezi mzima niliolazwa hapo Moi mpaka kupata nafuu na kuruhusiwa na kusubiri matibabu zaidi nje ya nchi. Asanteni sana.

Nawashukuru Ndugu, Jamaa,marafiki na majirani waliokuja kunitembelea pale Moi kwa michango yao na zawadi mbalimbali. Sikuwahi kulazwa hospitalini maishani mwangu, na sikuwa na utamaduni wa kutembelea wagonjwa mahospitalini, mpaka niliposhuhudia jinsi nilivyotembelewa nikagundua thamani ya kuwafariji wagonjwa na kuthibitisha ni kiasi gani unathaminiwa. Asanteni Sana.

Pia nawashukuru wale wate ambao hatakufahamiana kabla, sio ndugu, sio jamaa na wala sio marafiki, ni watu tuu wa kawaida lakini waliguswa wakaja hospitalini kunijulia hali na kunifariji, wengine wakija kuangalia wagonjwa wao lakini na mimi nikawa sehemu ya ndugu zao. Asanteni Sana.

Nawashukuru wanahabari waliokuja kunifariji muhimbili akiwemo Athumani Hamisi wa Daily News ambaye naye hatimaye alipatwa na ajali mbaya ya gari bado angaliko Afrika Kusini na Heri Makange wa Channel Ten (RIP) ambaye tulizungumzia pikipiki, nikiwa hospitalini nchini India nikapata taarifa ya kifo chake kwa ajali ya Pikipiki. Mungu apatie Athumani Hamisi uponaji wa haraka na amrehemu Heri Makange apumzike kwa amani.
Kitendo cha mimi niliyekuwa kitandani sasa nimesimama Athumani bado hospitalini na Heri katangulia mbele ya haki, najiona bado mimi ni mwenye bahati sana. Asanteni sana.

Nawashukuru viongozi mbalimbali wa dini, wa kiroho, vikundi vya wanamaombi, wachungaji wa wokovu, walokole na watu wa Jumuiya yangu ya Mtakatifu Gabrieli, Mbezi Beach kwa kuja na kuniendeshea maombi mbalimbali. Asanteni Sana.

Nawashukuru sana majirani,ndugu, jamaa na marafiki wote wa Tanzania, Marekani, Canada na UK kwa kuitikia mwito wa mchango kugharimia sehemu ya gharama za Matibabu zaidi nchini India na nchini Afrika Kusini na kuniwezesha kufikia hapa nilipofikia. Asanteni Sana.

Nawashukuru wateja wa PPR kwa kunivumilia, kwani walishalipia matangazo ya 88, kufuatia ajali hiyo, matangazo yao yaliathirika, huku fedha zao zimekwenda bila kunidai au kutakiwa kurudisha on the spot. na wengine tulishaandikishana mikataba ya malipo na bado wakaendelea kulipa bila huduma za papo kwa papo. Asanteni Sana.

Navishukuru vituo vya Redio na Televisheni, vikiongozwa na TBC, ITV, Star TV na Channel Ten kwa kurusha program za PPR kabla ya ajali yangu zikitarajia kulipwa lakini zikalazimika kukaa mwaka mzima bila kulipwa na mpaka sasa vingine bado havijalipwa. Samahani sana kwa usumbufu uliojitokeza na Asanteni sana,

Naishukuru sana Serikali kupitia Wizara ya Afya, Madakitari wa kitengo cha rufaa za nje pale wizarani nchi kwa kuniwezesha kwenda hospitali ya Apollo nchini India kwa matibabu zaidi na kugharimia matibabu ya msingi. Asanteni Sana.

Namshukuru Balozi wa Tanzania nchini India, Balozi Eng. John Kijazi na timu yake yote ya ubalozini na familia zao wakiongozwa na Makongoro na Yahya kwa kugeuka ndio ndugu, jamaa na marafiki wa wagonjwa watanzania wote wanaolazwa nchini India, hadi kujikuta namna ya kusherekea sikuuu kama Krismasi na Mwaka mpya ni kuwatembelea wagonjwa ambao ki ukweli sio ndugu zao kinasaba bali tumekuwa ndugu Kiutanzania. Asanteni Sana.

Nawashukuru wagonjwa wenzangu ambao tulilazwa wote Appolo Hospital, wenye nafuu kidogo tulitembeleana kufarijiana, huku waangalizi wao wakiwa ndio ndugu wa wote kwa kusaidia kuhudumia bila kujali nani ni nani ikiwemo juhudi za akinamama waangalizi kupika vyakula vya Kitanzania mara kwa mara wakishirikiana na wake za maofisa ubalozini na kutufanya waTanzania kujisikia tuko nyumbani, Asanteni Sana.

Nawashukuru madaktari wangu wa Apollo wakiongozwa na Dr. Prasaad na Dr. Karbinder, manesi, kwa huduma zao za kitabibu na vifaa vya kisasa vinavyoniacha na maswali bila majibu hivi ni kweli Tanzania hatuwezi?!. Nawashukuru sana.

Pia nawashukuru wahudumu wasio wa tiba wakiitwa Bayer kwa kutoa huduma nyinginezo kama hotelini na mgojwa kunyenyekewa kama mfalme, kitu ambacho katika hospitali zetu, bado. Nawashukuru sana.

Nawashukuru viongozi na Watanzania waliotembelea India kwa ziara za kikazi, kutembelea wagojwa na kuwafariji hufanywa ni sehemu ya ziara zao.Hebu fikiria wewe ni mwananchi tuu wa kawaida umelazwa hospitalini ughaibuni, huna ndugu, unakuja kutembelewa mara na mawaziri, mara wakurugenzi, mara balozi, japo unaumwa, lakini unapata faraja fulani kwa kumbe na wewe ni mtu muhimu na unathamani fulani!..
Asanteni Sana.

Nilipata ajali nikikabiliwa na deni fulani Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo nilijaribu LL.B. Nawashukuru sana wanafunzi wenzangu, wafanyakazi na walimu in particular Dean Prof. Mchome, Prof. Kabudi na mwalimu kijana Kitta, kuniwezesha kulilipa hilo deni nikiwa kitandani tangu Muhimbili. Sasa ni mimi ni mwandishi wa habari, mtangazaji na mtayarishaji wa vipindi vya televisheni huku nikimiliki LL.B ya UDSM tena siyo PASS!. Thanks to them. Asanteni Sana.

Sasa ni mwaka mmoja umepita tangu ajali hiyo ilipotokea. Mimi nimerejea rasmi nyumbani, nimepona japo mkono mmoja bado. Kinachoendelea ni kukusanya tena nguvu, kurejea nchini India kwa matibabu ya mwisho. Hivyo ndugu zangu, jamaa na marafiki, msishangae nitakapo wapigia hodi hodi mara muda muafaka ukiwadia.Natanguliza shukrani. Asanteni Sana.

Kutokana na mkono mmoja bado haujapona, ni bahati mbaya sana siwezi tena kushika camera, wala kazi za kuchakarika na mahangaiko ya upiganaji kama zamani. Hivyo kwa sasa, nimelazimika kujishikiza mahali nikifanya kazi za kiofisi.Naishukuru Jamiiforums kwa kuliweka tangazo la kazi yangu ya sasa kwenye ubao wa wa jf wa nafasi za kazi. Niliapply on line nikiwa nje ya nchi, nikaitwa na nikapata kazi. Namshukuru sana mwajiri wangu wa sasa kwa kunikubali hivi nilivyo.

Naishukuru timu mzima ya PPR ikiongozwa na Adam Njakachai kwa upande wa Production, Mohammed Namkape upande wa Still Photos, na Nelly Mwingira kwenye office management, ofisi ya PPR Mkwepu, WDC Mkwepu na vijana wote wa Mkwepu kwa kunilinda na kuhakikisha kazi za PPR zikifana kawa kawaida.Hata hivyo, bado ninafanya part-time PPR siku za Jumamosi na Jumapili. Hivyo nawashukuru sana wateja wa PPR ambao bado wamesimama na mimi katika hali nilio nayo na wanaendelea kunitumia. Asanteni Sana.

Nawashukuru na watu wengine wote wenye mapenzi mema, nawashukuru wale ambao walitaka kuniona hawakujua wanione wapi. Nawashukuru hata wale tunaokutana mara kwa mara wengine wakishtuka kuniona hivi nilivyo, wengine kwa kutoamini macho yao na wengine hata wakitokwa machozi. Asanteni Sana,

Namalizia kwa kuwaomba mzidi kuniombea nipate uponyaji wa kamili, cha muhimu ni mimi nimeikubali hii hali nilionayo kwa sasa kuwa hivi nilivyo ndio sasa niko hivi, at the same time, nothing is imposible under the sun hivyo bado nina matumaini ya uponyaji zaidi.Natanguliza Shukrani.

Ni vigumu kumshukuru kila mmoja wenu ambaye ajali yangu imemgusa kwa namna moja au nyingine. Natamani sana kuataja wote, sitaweza kuwamaliza ila nawashukuru sana Wote nasema ASANTENI SANA.

Pascal Mayalla
0784 270403
pascomayalla@gmail.com
Hili andiko lina mengi sana ya kutufundisha katika maisha yetu ya hapa duniani.
 
Back
Top Bottom