Waraka toka Zambia: Dalili ya Ushindi wa Upinzani Tanzania 2015

John Mnyika

JF-Expert Member
Jun 16, 2006
712
1,240
Waraka toka Zambia: Ushindi wa Sata na PF ni funzo kwa Afrika na dalili njema ya upinzani kushinda Tanzania 2015
Uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani uliofanyika Zambia tarehe 20 Septemba 2011 umetoa mafunzo mengi kwa nchi mbalimbali za Afrika na dunia kwa ujumla.

Aidha; masuala, matukio na matokeo ya uchaguzi huo yametoa dalili njema ya ushindi wa chama mbadala katika uchaguzi mkuu wa Tanzania wa mwaka 2015 ili kuliweka taifa katika mkondo wa mabadiliko ya kweli miaka 50 baada ya Uhuru.


Nimeshuhudia Zambia ikiandika tena historia kama moja ya nchi chache barani Afrika ambapo mabadiliko ya utawala yamefanyika kidemokrasia huku Rais aliye madarakani akikubali kushindwa na kushiriki bega kwa bega katika kuapishwa kwa Rais mpya Michael Sata.

Walau kama ilivyokuwa kwa Ghana na nchi nyingine chache, Afrika imeepushwa na wimbi la aibu la watawala ama kuhujumu uchaguzi au kuchochea vurugu na hatimaye kuendelea kung’ang’ania madarakani kwa kivuli cha serikali za mpito ama umoja wa kitaifa kama ilivyokuwa kwa Zimbabwe, Kenya na kwingineko.

Naandika waraka huu baada ya kutazama hatua kwa hatua kuandikwa kwa historia hiyo kipindi vyama vya nchi hii vikishiriki katika kampeni, wasaa Wazambia walipojitokeza kupiga kura, wakati wa kura kuhesabiwa, muda matokeo yalipotangazwa na hatimaye Rais Mteule alipoapishwa. Tanzania na Afrika kwa ujumla tuna mengi ya kujifunza kutokana na masuala, matukio na matokeo ya uchaguzi wa Zambia.

Kwa Zambia ile methali ya ‘asiyekubali kushindwa si mshindani’ imekuwa ni sehemu ya utamaduni wa kisiasa wa nchi yao toka ilipoingia katika mfumo wa vyama vingi kwa Dr Keneth Kaunda na chama chake cha United National Independence Party (UNIP) kukubali kuondoka madarakani baada ya kushindwa na Fredrick Chiluba wa chama cha Movement for Multi Party Democracy (MMD) mwaka 1991. Miaka 20 baadaye chama cha MMD nacho kimeachia hatamu; kwa maneno ya Rais aliyemaliza muda wake Rupiah Banda wakati wa kuwaaga wananchi akizungumza na vyombo vya habari kwa hisia alisema kukataa kukubali matokeo ni sawa na kusaliti historia ya nchi hiyo.

Wimbi la mabadiliko nchini Zambia pamoja na kuwa halikutabiriwa na wachambuzi wengi wa kimataifa lilikuwa bayana katika taifa hili na ukuu wa nguvu ya umma dhidi ya hujuma za aina mbalimbali umedhihirika.


Kwa wachambuzi wengi, kuvunjika kwa ushirikiano wa vyama vikuu vya upinzani wa Patriotic Front (PF) na United Party for National Development (UPND) mwezi Machi 2011 vilivyosaini mkataba wa ushirikiano mwezi Juni mwaka 2010 pamoja na kazi iliyofanywa na Rupiah Banda kuanzia alipoingia madarakani mwaka 2008 baada ya kifo cha Levy Mwanawasa ni kati ya sababu ambazo zilielezwa kwamba zingehakikisha ushindi kwa chama cha MMD.

Kwenye uchaguzi mkuu wa nchi hiyo wa mwaka 2006 hayati Levy Mwanawasa (MMD) alipata 42.98%, Michael Sata (PF) 29.37% na Hakainde Hichilema (UPND) 25.32%.

Kwenye uchaguzi mdogo wa mwaka 2008 Rupiah Banda (MMD) alipata 40.09 %, Michael Sata (PF) 38.13% na Hakainde Hichilema (UPND) 19.70%; mshindi wa urais akatangazwa kwa tofauti ndogo ya kura 35,209 tu.

Kutokana na nguvu kubwa ya UPND ukanda wa kusini wa Zambia na kuvunjika kwa mkataba wa ushirikiano baina ya chama hicho na PF ilitarajiwa kwamba kura za upinzani zingeendelea kugawanyika lakini Wazambia wametoa funzo kwa nchi nyingine kuwa pamoja na kuwepo wagombea tisa wa upinzani walielekeza nguvu zao kwa mgombea na chama kinachokubalika zaidi. Wachambuzi wa mambo walipaswa kuzingatia kwamba asilimia za kura za urais, na viti vya ubunge vya PF vilikuwa vikiongezeka kila baada ya uchaguzi wakati za vyama vingine vya upinzani na chama tawala vilikuwa vikiporomoka.

Ushindi huu wa hakika ulitangazwa kabla hata ya kumaliza kujumlisha matokeo ya Urais kutoka majimbo yote 150 ya nchi kwa Msimamizi wa Uchaguzi kumtangaza Michael Sata (PF) kuwa Rais Mteule wa Nchi hiyo kwa kupata 43%, akifuatiwa na Rupiah Banda(MMD) 36.1% na Hakainde Hichilema (UPND) 18.5%; tofauti ya kura ikiwa 188,249 bila ya kura za majimbo saba yaliyokuwa yamesalia.

Hakika ushindi huu umetokana pia na shimo ambalo MMD ililichimba katika mchakato wa mabadiliko ya katiba ya nchi hiyo kwa lengo la kufukia upinzani lakini shimo hilo hilo limeifukia yenyewe. Toka mfumo wa vyama vingi uanze Wazambia wamekuwa wakidai katiba mpya ili kuweka uwanja sawa wa ushindani na kuongeza uwajibikaji kwa maendeleo ya nchi yao. Kwa miaka takribani nane iliyopita Zambia imekuwa katika mchakato wa katiba; huku kukiwa na upinzani mkali kuhusu mchakato uliopitishwa hususani muundo wa mkutano wa taifa wa katiba. Mkutano huo wa katiba ulikaa kati ya mwaka 2007 mpaka 2010 na kuandaa mapendekezo ya mabadiliko ya katiba ya nchi hiyo ambayo mengi yaliungwa mkono na wadau mbalimbali. Hata hivyo, serikali ya nchi hiyo ikayaacha baadhi ya mapendekezo katika rasimu iliyopeleka bungeni kwa maelezo kwamba masuala hayo yataamuliwa katika kura ya maoni.

Matokeo yake ni rasimu hiyo kushindwa kupita bungeni tarehe 29 Machi 2011 baada ya serikali kushindwa kufikisha theluthi mbili ya kura zilizohitajika. Wabunge wa chama kikuu cha upinzani cha wakati huo PF, walipiga kura ya hapana isipokuwa wenzao 17 ambao waliungana na chama tawala MMD kupiga kura ya ndio kwa marekebisho hayo. Huku wabunge wa chama kinachofuata cha upinzani cha UPND wakiacha kupiga kura kutokana na kutoridhika na marekebisho hayo.

Hii ni kwa sababu Serikali ya MMD iliingilia mchakato ili kukiahirisha kiufundi kifungu kilichopendekezwa na Mkutano Mkuu wa Taifa wa Katiba chenye kuhitaji mshindi wa urais apate 50%+moja (yaani zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa). Pia, serikali ya MMD ilikiondoa kifungu cha kutaka makamu wa Rais kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi tofauti ya katiba ya sasa ambapo makamu huteuliwa na Rais baada ya kuchaguliwa. Dhamira iliyokuwa imejificha kwa serikali ya MMD kuhusu vifungu hivi ni kupunguza uwezakano wa ushirikiano na ushindi wa upinzani kwa njia za kiufundi. MMD ilijua kwamba kwa historia ya chaguzi za vyama vingi za Zambia chaguzi tatu mfululizo za urais za 2001, 2006 na 2008 hakuna mshindi aliyepata zaidi ya 50%. Hivyo, MMD ilijua kwamba kama kifungu hiki kingeingizwa kwenye katiba basi kungekuwa na marudio ya uchaguzi hali ambayo ingefanya kishindwe hata kama kingeongoza katika hatua ya awali. Kinyume chake kifungu hiki kimetoa fursa kwa Michael Sata wa PF kushinda urais kwa 43% bila kuwa na marudio.

Kwa upande mwingine, MMD ilijua kwamba upinzani ulihitaji mgombea urais kuwa mgombea mwenza kwa mujibu wa katiba ili kuweka mazingira mazuri ya kutekeleza ushirikiano wa vyama vikuu viwili kwa kimoja kuwa na mgombea urais kingine kuwa na mwenza. Suala hili lilikuwa la muhimu kutokana na mazingira ya kutokuaminiana yaliyokuwa yamegubika mkataba wa ushirikiano baina ya PF na UPND, kila kimoja kikiwa na hisia kwamba kama makamu wa Rais atateuliwa baada ya uchaguzi chama kimojawapo kinaweza kukitumia kingine kushinda urais lakini kisizingatie makubaliano katika kuteua makamu wa rais. Shimo hili lilichimbwa na MMD kutumbikiza upinzani, na hatimaye mkataba wa ushirikiano ulikuja kuvunjika kutokana na sababu mbalimbali. Hata hivyo, MMD bado inaweza ikatumbukia katika shimo ambalo imelichimba lenyewe kwa sasa katiba inatoa fursa kwa Michael Sata kutumia uteuzi wa makamu wa Rais kujenga himaya yake ama ndani ya PF yenyewe au miongoni mwa vyama vingine hususani UPND.

Izingatiwe kwamba pamoja na Michael Sata kushinda urais kwa 43% ataongoza nchi yenye bunge lilogawanyika kwa kiwango kikubwa. PF inaongoza bunge kwa kuwa na wabunge 60, ikifuatiwa kwa karibu na MMD yenye wabunge 55, huku UPND ikiwa na wabunge 28, vyama vingine viwili wabunge wawili na wabunge binafsi wako watatu. Ikiwa Sata akitumia nafasi zake nane za uteuzi kuongeza wabunge wa PF na hata kama chama hicho kikishinda kwenye majimbo mawili ambayo chaguzi zake zimesogezwa mbele kutokana na vifo vya wagombea bado kutahitajika ushirikiano katika kupitisha maamuzi ya msingi. Katika muktadha huo Hakainde Hichilema na UPND wataendelea kuwa na nafasi ya pekee katika siasa za Zambia katika awamu hii ya uongozi wa nchi hiyo.

Kukwama kwa katiba mpya na kutoboreshwa kwa mazingira ya kisheria na kitaasisi kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi hakukukatisha tamaa wananchi wa Zambia wala vyama vya upinzani kufanya mabadiliko waliyoyakusudia.

Izingatiwe kwamba wakati wa kampeni za uchaguzi ilionekana chama tawala kikitumia rasilimali za umma hali iliyozua malalamiko miongoni mwa upinzani. Vyombo vya habari vya umma viliegemea kwa uwazi chama tawala huku vikifanya propaganda za hali ya juu dhidi ya Michael Sata na chama chake cha Patriotic Front (PF). Chama tawala kilionekana bayana kuwa na rasilimali nyingi zaidi huku fulana, vitenge na bidhaa nyingine zikitumika kama hongo badala ya kuwa vifaa vya uenezi. Kwenye maeneo yenye njaa, chakula cha msaada kiligawiwa kwa malengo ya kisiasa. Huku miradi ya maendeleo ikifanyika mpaka kipindi cha lala salama kwa lengo la kuwaghibilibu wananchi. Lakini Michael Sata na PF waliendelea na kauli mbiu yao “Don’t Kubeba”, yaani ‘usiseme’. Ni kauli mbiu iliyobeba mantiki yenye elimu ya uraia na kisiasa kwa wananchi kwamba kura ni siri yao , chama tawala kikiwapa chochote kuwaghilibu wapokee lakini mwisho wa siku waonyeshe kwa vitendo kwenye sanduku la kura. Nimeshuhudia umasikini uliokithiri nilipotembelea majimbo ya ukanda wa magharibi ya Sikongo, Kalabo na Mongu kati ardhi ya Barotse hali ambayo ingekuwa mtaji wa chama tawala lakini wananchi wa eneo hilo kama ilivyo kwa maeneo mengine waliona umasikini wao ni sababu tosha ya kuchagua mabadiliko.

Banda na MMD walijikita katika propaganda za kisiasa na kuigeuza kauli mbiu Don’t kubeba) ni ushahidi wa Sata na PF kutokuwa na sera wala miradi ya maendeleo waliyoitekeleza kama chama cha upinzani; ndio maana hawana cha kusema. MMD ikajikita katika kueleza mafanikio ya miaka 20 ya uongozi wake kwenye kuvutia wawekezaji kutoka nje, kukuza uchumi, kuboresha miundombinu na kupanua wigo wa huduma za afya hususani elimu na afya na kuahidi kuongeza kasi katika kutekeleza miradi ya maendeleo. PF kwa upande iliweka kipaumbele masuala ya kushughulikia ufisadi mkubwa, kupunguza ukubwa wa serikali, kufanya mabadiliko ya kimfumo katika utawala na utumishi wa umma na kujenga taifa lenye kutoa fursa afya, elimu na huduma nyingine kwa wote. Aidha, PF iliahidi kuhakikisha wananchi wa Zambia wananufaika na rasilimali za nchi hiyo hususani madini ya shaba kwa kuongeza mapato ya serikali na kuboresha mazingira ya kazi katika migodi pamoja na kupanua wigo wa ajira kwa vijana. PF wakati wote ilieleleza kusikitishwa na umasikini uliokithiri katika taifa, kuongezeka kwa gharama za maisha na tofauti ya pengo baina ya wenye nacho na wasiokuwa nacho. PF iliahidi kuanza kuchukua hatua ikiweko kuhusu mchakato wa katiba ndani ya siku 90 za utawala; muda ambao MMD uliuita ni hadaa.

Kampeni ziliendelea pamoja na malalamiko ya hapa na pale kuhusu maandalizi ya uchaguzi hususani kuhusiana na uteuzi wa tume ya uchaguzi pamoja na uamuzi wa kuchapa karatasi za kura nje ya nchi badala ya kutumia mchapaji wa ndani. Malalamiko yalikuwa makubwa zaidi baada ya kuibuka kwa kashfa ya mmoja ya waliokuwa wafanyakazi wa tume ya uchaguzi kubainika kupewa hongo ya mamilioni na kampuni hiyo. Pamoja na imani ambayo wadau wengi walikuwa nayo kwa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi wa nchi hiyo, bado mashaka yalikuwepo kwa kuwa ni mwenyekiti huyo huyo Jaji Ireen Mambilima ndiye aliyeongoza tume hiyo kwenye uchaguzi wa mwaka 2006 ambao ulielezwa kuwa na kasoro mbalimbali.

Aidha, kulikuwa na mashaka zaidi kuhusiana na uteuzi wa baadhi ya makamishna wa tume hiyo. Pamoja na malalamiko hayo na kasoro za kikatiba na kisheria, bado tume ya uchaguzi ya Zambia ni huru zaidi ukilinganisha na nchi nyingi za kusini mwa Afrika ikiwemo Tanzania; tunaweza kusema tume hii inahitaji kuboreshwa zaidi ili ifikie viwango nchi kama Afrika Kusini, Ghana na nchi nyingine chache Afrika zilifikia viwango vya kimataifa.

Zambia uteuzi wa Rais wa makamishna wa tume ya uchaguzi lazima uidhinishwe na bunge. Pia, Zambia pamoja na kuwatumia watendaji wa serikali na watumishi wa umma kwenye ngazi za chini katika kusimamia uchaguzi; umma hushirikishwa katika uteuzi wao na pia sehemu kubwa ya waombaji hufanyiwa mtihani kabla ya kuteuliwa kuwa wasimamizi ikiwemo katika vituo vya kura. Kwa upande wa Urais, pamoja na kuwepo na mwenyekiti wa tume pamoja na makamishna wenzake; msimamizi wa uchaguzi ni Jaji Mkuu wa nchi hiyo

Asasi za kiraia pamoja na taasisi za dini za Zambia zilichukua nafasi muhimu katika uchaguzi. Pamoja na kutoa elimu ya uraia, asasi na taasisi hizo zilikwenda mbele zaidi katika kuhakikisha haki inalindwa katika uchaguzi. Tofauti na chaguzi nyingi za bara la Afrika katika siku ya kupiga kura na kutangaza matokeo asasi na taasisi hizi hazikuwa na wafuatiliaji wachache wanaozunguka maeneo mbalimbali, zilikuwa na watendaji wake ndani ya vituo vya kupigia kura sambamba na mawakala wa vyama vya siasa. Asasi na taasisi hizi zilikuwa na mfumo wake wa kufuatilia idadi na uhalali wa wapiga kura wanaingia vituoni na pia kuhakiki zoezi la kuhesabu kura vituoni na kujumlisha matokeo toka vituo mbalimbali sambamba na mfumo wa tume ya uchaguzi (parallel voters tabulation system). Suala hili lilizua mvutano kati ya tume na wadau mbalimbali huku tume ikitaka zoezi hilo kufanywa na tume pekee. Hatimaye makubaliano yakawa tume ibaki na haki yake ya kisheria ya kutangaza matokeo pekee bali wadau wote waendelee kuwa na haki yao ya kisheria ya kuhakiki na kujumlisha matokeo.

Kwa vyovyote vile, ilikuwa vigumu kwa tume hiyo kutangaza matokeo tofauti hata kama ingekuwa na dhamira hiyo kwa hofu kwamba wadau wengine tayari walikuwa wanayafahamu matokeo ya uchaguzi huo bila kuitegemea tume yenyewe. Kutokana na hali hiyo, kuchelewa kutangazwa kwa matokeo hususani ya urais kutokana na matatizo ya kimiundombinu kwa baadhi ya majimbo na pia udhaifu katika matumizi ya mfumo wa kujumlisha matokeo kwa kutumia kompyuta (electronic results management system) katika majimbo kadhaa; vilichangia kuzua tafrani katika maeneo ya Lusaka, Kitwe na kwingineko kwa wananchi kuanza kuunganisha nguvu ya umma kushinikiza matokeo kutangazwa. Mazingira haya yalichangiwa pia na kumbukumbu za matokeo ya uchaguzi ya mwaka 2008 na uvumi mwingi uliokuwa ukienea katika uchaguzi wa mwaka 2011 kwa nyakati mbalimbali.

Uamuzi wa busara wa Tume ya Uchaguzi kutumia kifungu 74 (3) (b) cha Sheria ya Uchaguzi ya Zambia namba 12 ya mwaka 2006 kutangaza matokeo ya Urais bila kusubiri majimbo saba yaliyobaki ulinusuru nchi hiyo kuingia katika vurugu kubwa za kiuchaguzi ambazo zingeweza kutokea. Vuguvugu la mabadiliko katika uchaguzi wa Zambia pamoja kuendelezwa na kujijenga awamu kwa awamu kwa Michael Sata na chama chake cha PF, kuongezeka kwa ugumu wa maisha miongoni mwa Wazambia huku takribani 70% wakiwa na masikini wa chini ya dola mbili kwa siku na matatizo ya kiutawala katika serikali ya MMD kulichangiwa pia na wimbi la vijana kutaka mabadiliko.

Katika uchaguzi wa Zambia ambao ulikuwa na jumla ya wapiga kura 5,167,174 kati yao takribani 1.2 walikuwa ni wapiga kura wapya walioandikishwa baada ya uchaguzi uliopita katika nchi hiyo. Kati ya wapiga kura wote wa Zambia, 54% ni vijana kati ya umri wa miaka 18 mpaka 35 ambao kwa sehemu kubwa waliunga mkono mabadiliko kupitia PF. Uzee wa Sata wa miaka 74, uzamani wake kutokana na ushiriki wake katika mfumo wa utawala toka wakati wa chama kimoja cha UNIP kilichotawala nchi hiyo toka uhuru, na serikali ya mwanzo ya MMD haukuwazuia kumchagua kwa kuwa yeye na chama chake walisimamie mabadiliko kwa msingi wa nguvu ya umma na waliwaweka mstari wa mbele vijana.

Pamoja na tofauti za mazingira ya kisiasa za hapa na pale, ukichambua siasa za Tanzania katika chaguzi kuu za mwaka 2005 na 2010 pamoja na uchaguzi mdogo unaoendelea hivi sasa Igunga mwaka 2011 na ushiriki wa vyama vikuu vya siasa vya CCM, CHADEMA na CUF kwa kurejea yaliyojiri Zambia kuna mengi ambayo wadau wasiasa wanaweza kujifunza. Jambo lililowazi,ni kwamba masuala, matukio na matokeo ya Zambia ni dalili njema kwa upinzani nchini Tanzania kuelekea ushindi wa mwaka 2015. Nilikuwepo Igunga kwenye uzinduzi wa kampeni tarehe 8 na 9 Septemba 2011 na nitarejea kushiriki siku za mwisho za kampeni; ni rai yangu kwamba uchaguzi huo wa marudio uendeleze safari hiyo ya mabadiliko ya kweli kwa nguvu ya umma.

Wenu katika demokrasia na maendeleo,

John Mnyika (Mb)
Ziarani Zambia - 25/09/2011
 
Imetulia.....ikiwezekana itume kama makala kwenye baadhi ya magezeti.
 
Ndg mh, inatia moyo kuona wenzetu walivyochukua maamuzi magumu katika kuamua mustakabali wao katika miaka mi-5 ijayo! Ila kwa kwetu sie; bado tuna safari ndefu sana kufikia huko ukizingati chama tawala kilipokubali vyama vingi hakikukubali kwa nia dhabiti (Mapendekezo ya Nyalali yaliwekwa pembeni)! Kwanini nasema haya? Kwanza katiba yetu unaimpa Rais nguvu kubwa sana yaani nearly to an imperial!

Hebu tujaribu kuangalia vitu kama uteuzi wa Jaji Mkuu, Mwanasheria Mkuu, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Mkuu wa Majeshi, Mkuu wa Polisi na Msajili wa Chama cha Uchaguzi vinafanywa vyoote na Rais bila hata ya kuhitaji kupitishwa na Bunge! Ukiachilia Mbali Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanaoteuliwa na Rais, Ni Waziri Mkuu tu hupitishwa Bungeni!! Sasa nini maana ya hili?

Tunaona watu wanateuliwa kwa kutofuata vigezo stahili yaani (merits) tunaona sasa kumezuka utaratibu wa kuwa ni zamu ya watu fulani fulani hata kama yupo mwenye uwezo, ujuzi na Uadilifu zaidi! Nathani hapa uteuzi wa CJ, Army Chief, IGP unaweza ukadhibitisha! Mbali ya haya hata katika mchakato mzima wa NEC tunaona wananchi wanatengwa sana katika shughuli ile muhimu!

Yaani wasimamizi mara nyingi huajiriwa toka cycle fulani ambayo iko kimaslahi kwa chama tawala! Mbali ya udhaifu huu pia kile kipengele cha kutoweza kupinga matokeo ya Urais Mahakamani ndicho huniondoa matumaini kabisa maana mbali ya kusimamia Uchaguzi Mwenyekiti huyohuyo (mmoja na si panel) ana mamlaka ya kuamua ni nani ameshinda Urais! Tunaweza kuona ni rahisi kiasi gani anaweza kusukumwa kutoa matokeo batili!

Sasa kwa mwenendo huu nadhani unaweza kufahamu mtu kama Kiravu anaweza fanya nini katika hili ukizingatia hata moral integrity hana kama ukilinganisha na mtu ambaye yuko katika organs za sheria miaka yoote kama chief Justices! Tukiacha hayo mbali na asasi za kijamii kama LHRC, TAMWA na nyinginezo!

Asasi za kidini zimekosa mshiko, angalau za Kikriso hujaribu kuelimisha integrity ila za hawa ndugu zetu wengine wa Majungu! NI Mwinyazi anajua mpaka lini wataendelea kuturudisha nyuma katika safari yetu ya kutaka mabadiliko! Ila tusikate tamaa vijana wengi wanachipukia na wana moyo wa kujaribu bila kuogopa! Yaani watu kama Masheikh uchwara na Wachungaji hawatafua dafu kutumia nyumba za ibada kupandikiza chuki!

Peoples ....!
 
Ziara yako nchini Zambia kushuhudia uchambuzi ilikuwa ni ya tija na ulikuwa husinzii kama magamba-wassira. Jinsi ulivyochambua binafsi nimekukubali na umezihirisha kuwa wewe ni kamanda, hujatuangusha CDM. Njoo Igunga ushuhudie CCM wanavyoshindwa. Wako hoi, nakuomba uje uongeze nguvu ili mlevi huyu tumsukume kiulaini.
 
nimesoma makala yako leo kwenye mwanahalisi. umefanya analysis nzuri, lkn ccm wataidharau maana wamefumbwa macho na ufisadi.
 
Walau kama ilivyokuwa kwa Ghana na nchi nyingine chache, Afrika imeepushwa na wimbi la aibu la watawala ama kuhujumu uchaguzi au kuchochea vurugu na hatimaye kuendelea kung'ang'ania madarakani kwa kivuli cha serikali za mpito ama umoja wa kitaifa kama ilivyokuwa kwa Zimbabwe, Kenya na kwingineko.
Hiyo kwingineko nafikiri ilitakiwa iwe na Zanzibar ili watu wasipate shida ya kufikiri.
 
Kamanda, aminia babake!!!!!!!!!

Mpaka kieleweke waambie na makamanda wengine wa ukweli Zitto Kabwe, Kihwelu, Mdee, Mwita Maranya, Mzee Mwanakijiji, Dokta wa ukweli, Kamanda Jeshi la Anga CDM - Aikaeli, Ndesa, Msigwa, Lema kwamba baraghumu tayari imelia kule kwa Mzee wa hanjifu jeupe - Baba Kaunda.

Walazwahoi kote nchini sote tujue ya kwamba ukombozi wa taifa letu toka kwa mafisadi iko karibu leo mara mia kuliko hapo jana.

People's pawaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaa!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!
 
Mhe. Mnyika, Hongera Sana Sana kwa aumahili wa hii article yako. Kwa mtanzania yeyote aipendaye nchi yake, bila kujali itikadi ya Chama, ujumbe huu utamnufaisha.
 
Back
Top Bottom