Waraka kutoka Houston, Texas (US)

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,011
WARAKA KUTOKA HOUSTON, MAREKANI

Mama Kilango, maneno matupu hayavunji mfupa

Innocent Mwesiga Julai 30, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

NAMPONGEZA Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela kwa msimamo thabiti na mchango wake wa mawazo bungeni. Kwa mujibu wa Raia Mwema, toleo la wiki iliyopita, Mama Anne Kilango na wabunge wa CCM wa aina yake, hawapigi vita ufisadi tu kama wanavyochukuliwa, bali kila aina ya uozo wakiwa na lengo la kubadilisha mfumo uliopo sasa wa keki ya taifa kuliwa na ‘wajanja' wachache tu.

Ingawa natofautiana kidogo na Mama Anne Kilango kwani nadhani keki ya taifa hailiwi na Watanzania; bali na mabeberu - na wanaoitwa wajanja wachache wanatupiwa makombo. Nakubaliana naye katika suala la kubadili mfumo uliopo. Ili kupata ufumbuzi wa tatizo lolote, hatua ya kwanza kabisa ni kujua chanzo cha tatizo. Naamini tatizo letu ni mifumo mibovu inayowapa wachache mamlaka ya kuwakabidhi mabeberu keki ya taifa.

Mbunge ana kazi kubwa tatu; kutunga sheria, kupitisha sera na kuidhinisha bajeti ya Serikali. Mbunge anaweza kuzungumza kwa mbwembwe, ukali au upole. Wakati akizungumza aweza kurusha mateke na mikono hewani kama ishara ya uthabiti. Matendo yote haya yanageuka kuwa usanii kama mwisho wake ataunga mkono bajeti, sera au sheria mbaya.

Ibara ya 4 (1) na (2) ya Katiba imeweka bayana mgawanyo wa kazi wa mihimili ya dola. Serikali ina mamlaka ya utendaji, Mahakama inatoa haki na Bunge linatunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma. Bunge ndio chombo kikuu chenye madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Katiba.

Katiba haikutamka wazi kwamba nani ndani ya ndoa ya Serikali na Bunge anayepaswa kuanzisha muswada. Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mawaziri na Manaibu wao ndiyo tu hujipendelea kupeleka miswada bungeni. Waliobaki kazi yao ni kuuliza maswali, kukaripia, kupiga makofi, vigelegele na nderemo, kujadili na kupitisha sera, sheria na bajeti.

Ibara ya 97 (5) ya Katiba inaruhusu bunge kumkabidhi mtu yeyote au asasi yoyote ya Serikali madaraka ya kuweka kanuni za nguvu ya kisheria. Serikali huanzisha asasi na kupitisha miswada bungeni ya kuzipa madaraka makubwa. Nao mawaziri hupitisha miswada bungeni inayowapa mamlaka ya kuhodhi nguvu kubwa za kisheria zisizo na mipaka.

Mfano, Aprili 1992, Serikali kupitia bungeni ilibadili sheria ya Mashirika ya Umma ya mwaka 1969, na kuruhusu ushiriki wa makampuni binafsi katika uendeshaji na umiliki. Ndipo Asasi ya Kubinafsisha Mashirika ya Umma (PSRC) ilipoanzishwa. Novemba 1993 kupitia bungeni, Serikali iliiongezea madaraka zaidi (PSRC). Hata hivyo, PSRC haikupewa uwezo wa kufuatilia utendaji wa mashirika iliyoyauza.

Sheria hiyo (Public Corporation Act 1993/1999/2003) iliainisha kwa kinaga ubaga utaratibu mzima wa kuingia mikataba yote ya kuyauza mashirika ya umma. Kwamba uamuzi wa kuliuza shirika unafanywa na Waziri husika. Iliagiza kuundwa timu (Divestiture Technical Team – DTT), iliyojumuisha maofisa kutoka wizara husika, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, PSRC na shirika lililobinafsishwa.

Sheria ilikipa kikao cha Baraza la Mawaziri mamlaka ya mwisho kupitisha au kukataa mapendekezo ya timu (DTT) katika hatua za mwisho za kuuza Shirika. Bunge lilipitisha hiyo sheria bila kuweka sharti lolote linalolilazimisha Baraza la Mawaziri kupeleka bungeni mikataba yote ili ijadiliwe kabla au baada ya kusainiwa.

Hadi kufikia Juni 2005 zaidi ya makampuni ya umma 319 yalikwisha kubinafsishwa. Makampuni 177 kwa Watanzania, 27 kwa wageni na yaliyobakia kwa ubia kati ya Watanzania na wageni. Kwamba mashirika yaliyobinafsishwa yalikuwa yanalipa kodi. Mfano, TBL, NBC, TCC, CRDB, DAHACO, Kilomero, na Mtibwa Sugar, Tanga na Mbeya Cement, Mponde Tea Factory, Tanzania Portland Cement na Canvas Mill.

Desemba 2006, Rais Benjamin Mkapa, mjasiriamali na kinara wa sera ya ubinafishaji, alitoa changamoto kwa waliopinga sera hiyo, kuangalia aliyouita mfano bora wa mafanikio ya mradi wa Kiwanda cha Usindikaji wa Vyakula vya Kilimo na Mifugo cha Sumbawanga (SAAFI), unaomilikiwa na mzalendo, Mbunge wa Kwela, Chrisant Mzindakaya.

Mradi huo ulimiliki ardhi ya heka 17,000, Ng'ombe 3,000 na ungeleta ajira 300.

Kumbe Aprili 2005, Mzindakaya alipata mkopo wa kuendesha mradi huo kutoka Benki ya Standard Chartered kwa dhamana ya Serikali, ambayo baadae ilihamishiwa katika Benki ya Rasilimali (TIB). Dhamana hiyo ilitokana na mpango wa Serikali wa kudhamini miradi ya wananchi ili kuongeza ajira, kukuza uchumi na kukuza uwezo wa Tanzania wa kuuza bidhaa nje.

Binafsi sioni kama mazingira yanayozunguka mradi wa Mzindakaya ni mfano bora wa sera ya ubinafsishaji. Kama Benki zilizoingia nchini kwa sera za uwekezaji na ubinafsishaji haziwezi kumkopesha Mbunge maarufu Kama Mzindakaya mpaka adhaminiwe na Serikali, zinaweza kumkopesha Mtanzania wa kawaida? Je ni watanzania wangapi na wa aina gani wanaoweza kupata dhamana ya Serikali?

Desemba 1999, Benki ya Dunia ilitangaza Mkopo wa dola milioni 45.9 kwa Tanzania kwa ajili ya kubinafsisha mashirika ya umma. Wananchi wanalazimika kudhamini mkopo wa kuuza mashirika na mkopo wa aliyenunua shirika mojawapo. Akishindwa kulipa watalazimika kulipa mikopo yote miwili na riba. Wananchi wanapata faida gani?

Wakati huo, Rais Benjamini Mkapa na baadhi ya mawaziri wake wana hisa au wanamiliki baadhi ya mashirika yaliyobinafsishwa, kama vile mradi wa Kiwira. Sheria ya kubinafsisha mashirika inakipa kikao cha Baraza la Mawaziri mamlaka ya mwisho ya kuridhia uuzwaji wa Shirika. Ibara ya 54 (2) ya katiba inasema, Rais ndiye anaongoza vikao vyote ya Baraza la Mawaziri.

Kama Rais, ambaye anaongoza kikao kinachoridhia uuzaji wa Shirika la Umma, ni miongoni mwa washindani wanaotaka kulinunua, atawatendea haki wengine bila upendeleo? Je maslahi ya wamiliki wa shirika ambao ni wananchi, yanasimamiwa na nani katika kikao cha kuridhia mauzo, kama Mwenyekiti au wajumbe wa kikao ndiyo waridhiaji, wauzaji na wanunuzi? Je wamiliki hawapaswi kuona kilichoandikwa wakati wa mauzo?

Aprili 2007, akichangia Muswada wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Mbunge wa Kyela, Dkt. Harrison Mwakyembe, alisikitishwa kuona kamati za bunge zinanyimwa ripoti za mikataba kutoka Serikalini. Julai 2007, aliyekuwa Waziri wa Sheria na Katiba, Mary Nagu, alisema bunge halipaswi kufanya kazi ya kupitia mikataba kabla ya kutiwa saini. Kwamba mikataba inafanywa siri kwa lengo la kulinda maslahi ya biashara.

Ni maslahi ya biashara gani ambayo wananchi waliomiliki mashirika au wabunge wanaowawakilisha, hawaruhusiwi kuyaona? Kusimamia ni kuwa mwangalizi wa jambo, shughuli fulani, au kukabidhiwa dhamana ya kuangalia kwamba kazi zinatendeka kama ipasavyo (Kamusi ya Kiswahili -1981). Je bunge linaweza kusimamia jambo lisilolijua: yaani mikataba ya siri isiyoonekana?

Akifungua semina ya kuboresha Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) Januari 2008, Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, Dkt. Juma Ngasongwa, alikiri kuwa Serikali ilifanya makosa katika zoezi la kubinafsisha mali za nchi, hali iliyowafanya wageni kumiliki zaidi uchumi.

Mwaka 1998 Serikali ililiomba bunge kupitisha Sheria ya Madini (Mining act 1998), ambayo ibara ya 10 fasili ya (1) na (2), vifungu vidogo (a), (b) na (c), vinampa Waziri wa Madini bila kushauriana na bunge, uwezo wa kusamehe au kuahirisha kodi. Hata hivyo, ibara ya 99 fasili ya (1) na (2) (a) kifungu kidogo (i), inalipiga marufuku bunge kutunga sheria za kutoza au kubadili kodi kwa namna nyingine yoyote isipokuwa kupunguza.

Sheria ya Madini inaweka mazingira ya rushwa kwa kumtia majaribuni Waziri aliyepewa nguvu kubwa za misamaha ya kodi. Wazaire husema, katika nchi ya mbilikimo hata mrefu wao ni mbilikimo. Ufukara wa Watanzania unawafanya baadhi ya mawaziri waonekane ni matajiri. Lakini utajiri wao haufui dafu mbele ya mitaji mikubwa ya mabeberu. Waziri mmoja anaweza kughilibiwa na "vijisenti" ambavyo ni chembe tu ya hiyo mitaji.

Katika ripoti; A Golden Opportunity? Mark Curtis na Tundu Lissu wanaandika kuwa kipindi cha miaka sita (2000-2006), malipo ya kodi zote ya Kampuni ya Anglo Gold Ashanti (AGA), kwa Serikali yalikuwa dola milioni 96.8. Ndani ya kipindi hicho ilipata aunsi milioni tatu za dhahabu, zenye thamani ya dola bilioni 1.43. Hivyo, malipo ya kodi zote ya AGA kwa Serikali ni sawa na asilimia 6.1 tu ya dhahabu iliyosafirishwa nje na kampuni hiyo.

Makampuni yanayochimba dhahabu hayalipi kodi stahiki na wabunge hawajawahi kuiona mikataba yote isipokuwa wa Buzwagi uliovuja katika vyombo vya habari. Serikali haijaweka wazi makubaliano yaliyosainiwa mwaka 2007 na kampuni ya Anglo Gold Ashanti.

Jambo la kushangaza ni kwamba Mei 9, 2006 Benki ya Dunia ilitoa habari namba 2006/400/AFR, ya kuipatia Tanzania mkopo wa dola milioni 40 kwa ajili ya uwajibikaji, uwazi na uadilifu.

Je Serikali itazirudishaje hizi fedha? Tangia lini uadilifu na uwazi ikawa miradi inayozalisha fedha? Mbona Serikali inasita kuiweka mikataba wazi? Serikali inakopa fedha ili iwajibike au iwe wazi? Wako wapi Wabunge waliotumwa na wanaolipwa na wananchi kuiwajibisha Serikali? Kwa nini wananchi wanabebeshwa msalaba wa madeni, na nchi inawekwa rehani kwa mambo yasiyohitaji fedha kutekelezeka?

Hii ni mojawapo ya mifano tele inayodhihirisha udhaifu wa katiba na sheria zinazopitishwa na bunge, ambazo zinawarundikia madaraka ‘wajanja' wachache, na wanayatumia vibaya kwa faida ya mabeberu, huku wao wakiramba masazo.

Mfumo wa utunzi wa sheria inabidi ufumuliwe na tuanze upya ili kulinusuru taifa letu. Ibara ya 89 (1) ya katiba imelipa bunge mamlaka ya kujiamulia utaratibu wa kutekeleza shughuli zake. Kanuni ya 68 (1) ya Bunge inasema Mbunge yeyote ambaye si waziri aweza kuwasilisha bungeni muswada wa mbunge. Kwa nini hakuna mbunge anayetumia kanuni hii kuwasilisha muswada wa kufanyia marekebisho sheria ya madini, ubinafsishaji na uwekezaji?

Kwa nini hakuna anayewasilisha muswada wa kuilazimisha Serikali kuleta mikataba yote bungeni ambayo imekwisha kusainiwa ili ijadiliwe? Maneno ni muhimu ili wananchi waelimike. Lakini matendo ya wabunge ni muhimu kuliko maneno wakati wa kuunga mkono sheria nzuri na kuzikwamisha mbaya. Kumbuka: maneno matupu hayavunji mfupa.
 

WARAKA KUTOKA HOUSTON, MAREKANI

Innocent Mwesiga Julai 30, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo


...Kwa nini hakuna anayewasilisha muswada wa kuilazimisha Serikali kuleta mikataba yote bungeni ambayo imekwisha kusainiwa ili ijadiliwe? Maneno ni muhimu ili wananchi waelimike. Lakini matendo ya wabunge ni muhimu kuliko maneno wakati wa kuunga mkono sheria nzuri na kuzikwamisha mbaya. Kumbuka: maneno matupu hayavunji mfupa.

Ningeomba Zitto (Mb) atusaidie kwa hilo swali.

Zitto (Mb) aliandika muswada kuhusu kurekebisha sheria ya Maadili. Muswada huo umekuwa ukikusanya vumbi zaidi ya mwaka na nusu sasa. Siku ulipofika mbele, Waziri wa Sera na Uratibu wa Bunge, Marmo (Mb.) akamwambia kwamba Serikali nayo ina muswada wake pia unakuja, hivyo atulie. Halafu ishu ikafa kafa kifo cha mende. Zitto (Mb.) akaingolea hapa, akisikitishwa na jinsi ya alivyotulizwa na huu mchezo aliouita "politics made in Tanzania."

Lakini, siku Mkullo (Mb.) alipoleta bajeti ya mwaka huu, Zitto (Mb.) alisema Bungeni, Juni 16, kwamba anashangaa Mkulo haijafuta sheria za kuwapa wachimba madini unafuu wa kodi. Akaulizwa hapa, ni kwa nini yeye kama Mbunge anasubiri Hazina ndio iandike sheria bora ya mapato ya Serikali. Hatukupata jibu.

Kitu kile kile ambacho Zitto (Mb.) hakukipenda kutoka kwa Marmo (Mb.) ndio hicho hicho akakiomba kwa Mkulo (Mb.)

Zitto (Mb.) tunaomba maelezo tafadhali.
 
Nadhani ni ya kiufundi kidogo, kama sio sana, kuweza kueleweka kwenye vipeperushi vijijini. Inahitaji watu wa kui break down majukwaani.
 
Mkuu Innocent,

Heshima mbele bro, nimekusikia sana kwa washikaji kutoka huko Texas, ninasema siku zote kuwa maneno kama yako ni adimu sana hapa JF, ingawa kuna wachache huwa wanajaribu, wengi huishia kurusha matusi ya nguoni tu,

ninakuahidi kuwa in the next 10 minutes ninaifikisha hii kama ilivyo, Bravo mkuu na mkuu Bubu ubarikiwe pia kwa kuileta hapa
 
Makala safi sana, ipeperushwe vijijini ili wananchi waone wanavyoibiwa hazina yao.

Mkuu Rev Kishoka,

Kila mara ninaposoma makala nzuri kama hizi, huwa nawafikiria wale wa kule vijijini, Je wanapata fursa ya kusoma makala kama hizi? Au ni magazeti ya Uhuru na Mzalendo tu!
 
Well written..cha kusikitisha ni kuwa hakuna jipya katika makala hii. Ukweli na Tatizo hasa ni kuwa wabunge wetu wengi hawako bungeni kuwakilisha wananchi.
 
Back
Top Bottom