Wapinzani waikosoa CCM; hao ni viongozi wa vyama vya TLP, UPDP, NCCR-Mageuzi na DP

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
Tuesday, 12 April 2011 20:31
Fidelis Butahe

BAADHI ya viongozi wa vyama vya upinzani nchini, wameponda mabadiliko ya uongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa madai kuwa tatizo la chama hicho ni mfumo na si sura za watu.Kauli hiyo imetokana na hatua ya Halmashauri Kuu ya chama hicho (NEC-CCM) kutangaza safu mpya ya uongozi wa juu wa chama hicho huku baadhi ya vigogo wakiwekwa kando, na kutoa siku 90 kwa watuhumiwa wa ufisadi kujiondoa wenyewe NEC ya chama hicho.


Wakizungumza na gazeti kwa nyakati tofauti, viongozi hao wa chama cha TLP, UPDP, NCCR-Mageuzi, DP wamesema CCM bado ina kazi nzito huku Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila akienda mbali zaidi na kudai tatizo la CCM ni Mwenyekiti wake, Jakaya Kikwete.

Mtikila alisema mabadiliko ya CCM si lolote kwa kuwa yamelenga kubadili sura tu ila mfumo ni ule ule.“CCM sio chama cha wanachama, hakuna demokrasia pale, Katibu Mkuu wa sasa wa chama ni wazi kuwa amechaguliwa na Mwenyekiti wa CCM, hata hiyo kamati kuu nayo imechaguliwa na mtu mmoja tu,” alisema Mtikila.

Mtikila alisema kuwa uozo ndani ya CCM unasababishwa na mtu mmoja na kusisitiza kuwa hata hao waliochaguliwa hawataweza kubadilisha kitu kwa kuwa watafuata maelekezo ya mtu huyo.“Sasa kama mtu kakuchagua unafikiri utashindwa kumfuata vile anavyotaka, akikanyaga mguu wa kulia na wewe utakanyaga hapo hapo,” alisema Mtikila.

Katibu mkuu wa NCCR, Samwel Ruhuza alisema: “Gamba si anabaki nyoka, tatizo la CCM ni mfumo bwana sio sura za viongozi wa sasa na wa zamani,”.Alisema kuondoka kwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusuf Makamba na nafasi yake kuchukuliwa na Wilson Mkama hakuwezi kukinufaisha chama hicho.“Siwaombei mabaya kwa kuwa wakivurunda nchi nayo itayumba, sisi wote ni Watanzania, tatizo la CCM hawafuati miiko ya uongozi, Mkama anaweza kuwa kiongozi mzuri ila anaweza kushindwa kufanya kazi kwa sababu ya mfumo wa uongozi wa CCM ulivyo,” alisema Ruhuza.

Mwenyekiti wa Chama cha TLP, Augustine Mrema licha ya kukipongeza CCM kwa hatua hiyo alionya kuwa kisijaribu kuua upinzani kwa madai kuwa hakitafika mbali.“Sawa wamefanya uchaguzi nawapongeza, lakini kamwe wasijaribu kuua upinzani wataishia pabaya sana, watizame maslahi ya taifa na kuacha ubinafsi,” alisema Mrema.

Mrema alisema mabadiliko hayo hayawezi kumfanya arudi CCM na kusisitiza kwamba mafisadi wawekwe pembeni.Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa alisema mabadiliko ndani ya CCM huenda yakawafanya wapinzani kuanza upya harakati za kuking’oa chama hicho madarakani.“Unajua uongozi wa CCM uliopita chini ya Makamba ulikuwa ahueni kwa wapinzani, Makamba alikuwa rahisi sana kupambana naye,” alisema Dovutwa.
 
Back
Top Bottom