Wapinzani waibua ufisadi mwingine

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,005
Wapinzani waibua ufisadi mwingine

na Lucy Ngowi
Tanzania Daima

UMOJA wa Vyama vya Upinzani nchini, kwa mara nyingine jana walianika hadharani tuhuma nyingine ya mabilioni yaliyoibiwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu uliopita, mwaka 2005.
Tuhuma hizo zilitolewa katika mkutano maalumu na umoja huo ambao unavishirikisha vyama vya Tanzania Labour (TLP), NCCR – Mageuzi, Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), uliowashirikisha wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na waandishi wa habari, uliofanyika jana katika Ukumbi wa Urafiki.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willbrod Slaa na Mwanasheria mashuhuri, Tindu Lissu, walisema kuwa, kuna taarifa zinazoonyesha kuwepo kwa ufisadi na wizi wa mabilioni mengine ya fedha za umma, uliofanyika wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa 2005.

Kwa mujibu wa wapinzani hao, wizi huo ulifanywa na kampuni moja hewa, ikishirikiana na Benki Kuu kwa upande mmoja na kampuni nyingine kadhaa ambazo utendaji wake unaleta shaka.

"Nyaraka mbalimbali ambazo tumezipata hivi karibuni zinaonyesha kwamba makampuni hewa yalianzishwa katika vipindi tofauti kabla ya Uchaguzi Mkuu kwa lengo mahususi la kupitishia fedha zilizoibiwa BoT. Nyaraka hizo pia zinaonyesha jinsi ambavyo fedha hizo ziliibiwa na kwa wakati gani," alidai Dk. Slaa.

Alidai kuwa Machi 18, 2004 ilianzishwa Kampuni (jina linahifadhiwa) kwa nia ya kufanya biashara kama 'mabepari' na wakopeshaji fedha. Kwa mujibu wa jalada la kampuni hiyo lililokuwa katika ofisi za Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), kampuni hiyo ilikuwa inamilikiwa na wageni ambao walikuwa wakiishi Afrika Kusini. Hata hivyo, jalada la kampuni hiyo inasemekana limetoweka Brela.

Katika hali ya kushangaza, kwa mujibu wa taarifa za kibenki ambazo wapinzani hao walidai wanazo, kampuni hiyo ilifungua akaunti katika Benki ya NBC Mei mosi 2004, siku ambayo ilikuwa ni ya mapumziko kwa ajili ya sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani.

"Kitu cha pili cha kushangaza ni kuwa kampuni hii iliruhusiwa kufungua akaunti hiyo bila ya kuingiza wala kutoa fedha yoyote kwa zaidi ya mwaka mmoja kuanzia Mei 1 2004 hadi Julai 31 2005," alidai Dk Slaa.

Hata hivyo, mambo yalibadilika kuanzia Agosti 2005 ambaapo katika kipindi kifupi cha miezi minne, akaunti hiyo iliyokuwa mfu, ilipokea jumla ya sh 10,484, 005.39 kutoka Wizara ya Fedha na BoT.

Dk. Slaa alitoa mchanganuo wa malipo hayo yaliyoonyesha kuwa kila mara akaunti hiyo ilipokuwa ikipokea mabilioni hayo aidha kutoka Wizara ya Fedha au BoT, fedha hizo zilichukuliwa haraka na haijulikani zilielekea wapi.

"Kutokana na taarifa za Brela, wanahisa wa awali wa kampuni hiyo walikuwa ni mawakili wawili wa hapa nchini (majina tunayahifadhi), Aprili 15, 2005 mawakili hao walihamisha hisa zao katika kampuni hiyo, pia ni mawakili wa kampuni (jina linahifadhiwa), ambayo imehusishwa na ufisadi tuliouelezea katika orodha ya mafisadi," alisema Dk. Slaa.

Dk. Slaa alieleza jambo jingine la kushangaza, pamoja na jina la kampuni hiyo kuashiria kuwa ni taasisi ya kifedha, orodha ya taasisi za kifedha iliyotolewa na BoT, Agosti 21 2007 haionyeshi kwamba kampuni hiyo imewahi kusajiliwa na BoT kama taasisi ya kifedha.

"Hiki kilikuwa ni kipindi cha mchakato na kampeni za Uchaguzi Mkuu uliofanyika Desemba 4, 2005. Pia kuanzia Desemba 11, 2005 hakuna fedha yoyote iliyoingizwa katika akaunti hiyo hadi Februari 27 mwaka huu kampuni hiyo ilipovunjwa kwa hiari ya wanahisa wake.

"Ni muhimu kurudia kwamba, kwa ushahidi huu wa nyaraka za kibenki, kampuni hii haikuwa na hata senti moja kabla ya Agosti mosi, 2005 na wala haikupokea hata thumni mara baada ya Desemba 10, 2005 na mara baada ya Uchaguzi Mkuu," alisema Dk. Slaa.

Naye Lissu alisema kuwa, kuna utata mkubwa zaidi ambao umeigubika Kampuni (jina linahifadhiwa). Licha ya nyaraka kuonyesha kwamba kampuni hiyo ilipewa hati ya kutimiza masharti ya Tanzania, Februari 20, 2006, nyaraka za kibenki walizonazo zinaonyesha kuwa kampuni hiyo ilifungua akaunti ya shilingi katika tawi moja la benki hapa nchini, Januari mosi, 2003.

Alisema kama ilivyokuwa kwa kampuni iliyotangulia, siku kampuni hiyo nyingine ilipofungua akaunti yake, ilikuwa ni siku ya mwaka mpya na siku ya mapumziko kote nchini. Pia taratibu za kibenki za ufunguaji wa akaunti za makampuni zinalazimu kampuni husika kuwasilisha benki nakala ya usajili wa kampuni, katiba yake, leseni ya biashara na hati ya mlipa kodi ya TRA, kabla ya kuruhusiwa kufungua akaunti.

"Swali la kujibiwa na benki pamoja na serikali ni je, kampuni hiyo iliruhusiwa kufungua na kuendesha akaunti ya benki kabla hata haijaandikishwa nchini Mauritius, achilia mbali kupata hati ya kutimiza masharti ya Tanzania?.

"Pili, Kampuni hiyo iliendesha akaunti hiyo bila kuweka au kutoa fedha yoyote ile kati ya Januari mosi 2003 hadi Agosti mosi, 2005, ilipoanza kunyeshewa mvua ya neema ya mabilioni ya fedha za walipa kodi wa Tanzania kutoka BoT," alidai Lissu.

Alisema baada ya kipindi hicho, kampuni hiyo haikupokea wala kuingiza fedha zozote kwenye akaunti yake hadi Juni 6, 2006 ilipohamisha shilingi za Tanzania 220,980,370 kwenda Idara ya Usalama wa Taifa.

"Tangu tarehe hiyo hadi leo hii kampuni hiyo haijaweka wala kutoa fedha nyingine yoyote katika akaunti hiyo, kwa maana hiyo katika kipindi cha miezi minne kampuni hiyo iliingiziwa na BoT sh 4,742,982,627 na ilifanya malipo kwa kampuni mbili ya jumla ya shilingi za Tanzania 3,363,531,259," alisema Lissu.

Dk. Slaa alisema maswali muhimu ya kujiuliza kuhusiana na kampuni hiyo ni kwamba ilikuwaje kampuni ambayo haikuwa hata imeandikishwa kisheria nchini, ikalipwa mabilioni ya fedha za walipa kodi, bila hata maelezo yoyote?

Moja kati ya 'biashara' ambazo kampuni hiyo ilifanya, alidai, ni Oktoba 12, 2005 ilipohamisha sh 39,761, 397.98 kwenda kwenye akaunti ya kampuni nyingine na siku hiyo hiyo kulipa sh 1,690,500,000.00.

Aidha, alihoji ilikuwaje serikali, kupitia Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, itoe taarifa ya uongo bungeni kwamba kampuni mpya (jina linahifadhiwa) imeanzishwa, ili kurithi mali na madeni ya kampuni (jina linahifadhiwa), wakati makampuni yote mawili yalikuwa yakipeana mabilioni ya fedha za umma wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu katika mazingira ya kutatanisha?

Wapinzani hao walihoji pia ni kwa nini malipo ya mabilioni hayo kwa makampuni hayo yalikoma mara baada ya uchaguzi mkuu na iwapo (Jina linalifadhiwa) ni kampuni inayomilikiwa na serikali kama inavyopelezwa, ni vema ziliko ofisi zake na majina ya watendaji wake wakuu yakabainishwa.

Kwa mujibu wa Slaa, hivi karibuni baadhi ya wanachama wa CCM wameanza kuhoji matumizi makubwa ya fedha wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita.

Alisema: "Hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, ametoa hadharani barua aliyomwandikia mwenyekiti wa CCM aliyepita, Benjamin Mkapa, akidai kuwepo kwa ushahidi kuwa 'fedha nyingi zinatumiwa katika Uchaguzi Mkuu'. Kama alivyohoji kuwa fedha hizo zinatoka wapi na ni za nani? Wananchi wa Tanzania waidai serikali iwaeleze mabilioni haya ya fedha za umma yalilipwa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2005 kwa ajili gani?"

Alisema ili kupata majibu sahihi ya maswali yote haya, serikali haina budi kuridhia kuundwa kwa tume huru ya uchunguzi wa tuhuma zote hizi na zile zilizotolewa katika orodha ya mafisadi.

"Ni tume huru pekee itakayoweza kuchunguza ufisadi huu bila woga, upendeleo au hila. Na ni ripoti ya tume huru pekee ndiyo itakayotumika kuwawajibisha wale wote watakaobainika kushiriki kulisababishia taifa letu hasara kubwa namna hii," alisema.

Alimalizia kwa kusema kuwa, kutokana na uzito wa masuala hayo, iwapo serikali itashindwa kuridhia kuundwa kwa tume huru ya kuchunguza tuhuma hizo hadi Novemba 25 mwaka huu, vyama hivyo vitatoa maelekezo kwa wanachama na wananchi juu ya hatua za kuchukuliwa ili kuondokana na kile walichokiita ufisadi, wizi au ubadhirifu wa mali ya wananchi.

Kwa upande mwingine, wapinzani hao walieleza wazi kutokubaliana na ripoti ya ukaguzi uliofanywa na Ernst Young LLP, ikikagua akaunti ya malipo ya nje inayoendeshwa na BoT, kama majibu ya serikali kwa tuhuma zao kwa sababu kilichokaguliwa ni tofauti na tuhuma ambazo wao wanazitoa.

Aidha, wapinzani hao walisema wanakusudia kutoa hadharani mkataba wa uzalishaji umeme ulioihusisha Kampuni ya Richmond Development, ambao serikali ilisema kuwa ni wa siri, na watautolea maelezo hapo baadaye. Baadhi ya wananchi na waandishi wa habari waliokuwepo katika mkutano huo walipata nakala za mkataba huo.

Naye Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema, alisema kuwa, serikali imekamatwa pabaya kwa kuwa tuhuma za mafisadi zilizotolewa katika mkutano wa Mwembeyanga pamoja na viongozi mbalimbali kutishia kwenda mahakamani, hawajafanya hivyo mpaka jana.

"Tunajivunia vyama vyetu vimepata vijana mahiri, mbwa wakali, ili mbwa asonge mbele lazima na wewe mwenye mbwa uwe sambamba naye," alisema Mrema.

Wapinzani hao walisema kuwa wameamua kutangaza mgogoro na serikali kwa kuongea na wananchi badala ya kwenda mahakamani kwa kuwa utaratibu wa kimahakama ni mrefu.
 
I thank God kuwa viongozo wa upinzania wana umoja kiasi hicho. Data walizo nazo basi kiwe ni kichocheo cha wananchi kuanza maandalizi ya uchaguzi 2010. Lakini hiyo Haitoshi majaji na watu wa PCB wako wapi? Polisi wako wapi. Nawashauri viongozi wa vyama vya upinzani kuepeleka ripoti hizo katika vyombo kadhaa vy dola and see watafanya nini. Ili siku wana wanchi wakiingia madarakani basi wajue ni nani wa kuondoa.
 
Back
Top Bottom