Wanzibar na Muungano; Mwaweza Kuishi bila Itikadi lakini hamwezi Kuepuka Mwelekeo!

KAMBOTA

Senior Member
Mar 21, 2011
176
103
Na Nova Kambota,

Kwa takribani miaka 50 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar kuunda Jamuhuri yaw Muungano wa Tanzania imekuwa ni nadra au mara chache sana kwa mtanganyika kuwashauri wazanzibar juu ya maswala yahusuyo muungano, nitangulie kusema kuwa makala hii (ikieleweka vema) hakunashaka yoyote kuwa itakuwa msaada mkubwa kwa wazanzibar hasa wa aina ya Dr Harith Ghassany wanaopigania kile wanachoita “hadhi ya nchi yao Zanzibar”. Hivyo basi pasipo kuniweka kwenye mizani ya utanganyika wangu ni imani yangu kuwa wazanzibar watafaidika na maandiko haya, lakini pasipo kumung’unya maneno niseme wazi kuwa atakayeona yafaa kunijibu ruksa isipokuwa akumbuke kuwa makala yangu hii imepangwa kwa mtiririko wa hoja zenye mantiki hivyo naye atalazimika kunijibu kwa mtiririko huohuo;



Harakati za Wazanzibar
Labda neno harakati laweza kuwa na maana zaidi ya moja lakini kwa wazanzibar ni kama linapotoshwa au limeanza kupoteza maana yake sanifu, kama umesoma mawazo ya wazanzibar au kuwasikia wakizungumza utabaini neno harakati kwao halimaanishi kingine zaidi ya malalamiko yao dhidi ya ndugu zao watanganyika.



Kila wanapotaja harakati lazima utawasikia wakijumuisha na neno muungano. Kwa mantiki hiyo ina maana kuwa siku ambayo wazanzibar watashikana mikono na kusema “harakati zimefanikiwa” ama la itakuwa siku muungano utakapovunjika(kama baadhi yao wanavyotaka hata Nyerere aliliona hili) au siku “madai yao” yatakaposikilizwa(kwa maana wanadai hawasikilizwi na watanganyika).

Ingawaje watajitokeza wazanzibar wachache (kwa unafiki wao) watapinga hiki nachokisema lakini bado haitaondoa ukweli huu wa harakati za wazanzibar, na kwa vile huu ndiyo ukweli wenyewe basi hakuna ubishi kuwa hili ni tatizo namba moja katika siasa za Zanzibar na uhai wa Muungano wa Tanzania.

Mmeng’enyo wa ndani kwa ndani?
Kwa nje Zanzibar yaweza kuwa moja ikiundwa na visiwa viwili ambavyo ni Unguja na Pemba lakini kwa ndani ni kama vile hakuna kabisa kitu kinachoitwa Zanzibar . Wapo watakaosema kuwa najaribu kutonesha kidonda cha uhasama miongoni mwa wapemba na waunguja la hasha! Sina maana hiyo na labda awali ya yote nikiri wazi Serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar angalau imetuliza hali ya mambo visiwani humo lakini hii haitoshi kabisa kuhitimisha maelezo ya ufasaha kuhusu siasa za Zanzibar. Kwanini nasema hivi? Nitaeleza;



Ukiacha Uzanzibar wao, Wazanzibar wamegawanyika katika makundi kadha wa kadha kwa vigezo vikuu viwili ambavyo ni “mitazamo” na “viongozi”. Kwa kuzingatia mitazamo , kuna Wazanzibar wanaoitazama Zanzibar kama nchi huru inayostahili kuwa na kiti Umoja wa Mataifa, kuwa mwanachama wa FIFA, na hata ikiwezekana kusiwepo na kitu kiitwacho Tanzania, pia kundi lingine ni lile linaloamini kuwa watanganyika ni ndugu zao hivyo bado wanawahitaji cha muhimu ni kuamua aina nzuri ya muungano(kwa maana hawaitaki ya sasa) ama uwe wa serikali tatu au moja. Lakini pia kuna kundi la tatu ambao hawa ni wale wanaoamini mfumo wa sasa wa serikali mbili ni mzuri kabisa hivyo hawaoni sababu ya kupinga kile kilichoasisiwa na Julius Nyerere na Mzee Abeid Karume.

Kigezo cha pili kinachowagawa Wazanzibar ni viongozi , hapa ndipo ngondo ilipo kama si kizungumkuti kabisa kwa maana amini usiamini msomaji wangu mwamko wa kisiasa Zanzibar ni mkubwa kuliko Tanganyika tena viongozi wa Wazanzibar hawajawahi kukemea makundi(bilashaka wanayafurahia), Zanzibar hakuna CUF wala CCM, hivi vyama jina tu, vyama halisi vya Zanzibar ni Amani Karume, Seif Sharif Hamad, Dr Gharib Mohamed Bilal, Mohamed Seif Khatibu, Ismail Jussa, Hamad Rashid, Hamid Yusuf Mansoor, Juma Shamhuna na Dr Ally Mohamed Shein. Sasa Zanzibar ambayo ina vijizanzibar lukuki vya aina hii ndani yake ni tatizo la pili kwa Zanzibar yenyewe na kwa uhai wa Muungano wa Tanzania.

Ujasiri wa Viongozi wa Zanzibar uko wapi?
Yawezekana swali hili lisieleweke kwenye masikio ya wazanzibar, lakini ili nieleweke vema sina budi kuliuliza pasipo kigugumizi, kwa maana mpaka leo hii kwa kuiangalia Zanzibar ni vigumu kufahamu Wazanzibar wanapima vipi ujasiri wa viongozi wao? Hivi katika mgawanyiko huu wa kimtazamo kama nilivyoeleza hapo juu , je nini itikadi ya Zanzibar? Je katika ufuasi wa wazanzibar kwa viongozi wao nini itikadi ya watu wa visiwa hivi?

Hakika ni swali gumu kulijibu , ugumu wa kujibika swali hili unafanya nijadili tatizo la tatu la Zanzibar ambalo ni kukosa itikadi hatua inayowafanya wananchi wa visiwa hivi kuyumbishwa kushoto na kulia, hii tisa kumi ni jinsi ushabiki wa kisiasa ulivyoingia kwenye mirija ya damu ya wazanzibar kiasi cha kuwapofusha, eti kuna kiongozi mmoja yeye anapendwa kwa sababu ya uconservative wake( kutotaka mabadiliko ya mwafaka na wapemba) yeye yungali anaimba kiitikio cha “Mapinduzi daima” huku akiamini kuwa mapinduzi yaliletwa na waunguja si wapemba, watani wa huyu kule kisiwandui wanamcheka kwasababu amekwisha makali yake sasa yuko Tanganyika(kwa matakwa ya chama chake).



Mwingine yeye anasifiwa kwa uwezo wake wa kuongea pasipo uwoga, mtiririko huu unaenda hivyo mpaka mwisho, ni sifa za namna hiyo kwayo “utukufu” wa viongozi hao unachotwa, come sun, come rain uimara wa viongozi wa Zanzibar kwa wazanzibar ni jinsi wanavyoweza kuwasilisha malalamiko ya wazanzibar dhidi ya watanganyika na si vinginevyo, ndiyo maana binafsi sikushangaa pale kiongozi mmoja kijana wa chama cha siasa Zanzibar alivyovikwa ushujaa visiwani humo kwa ufundi mkubwa aliotumia “kuparuana” na waziri wa ardhi, nyumba na makazi wa Tanzania Prof Anna Tibaijuka.

Zanzibar, jana leo na Kesho
Kwa wanahistoria wao hudai kuwa maisha ya Jamii fulani na maendeleo yake yanaongozwa na nguzo tatu ambazo, ni kuijua jana, kukabili changamoto ili kuishi leo na hatimaye kutabiri na hata kuandaa kuishi kesho, naam! Ndivyo hali ilivyo visiwani Zanzibar, iwe isiwe huu ni ukweli ambao sharti usemwe pasipo kumung’unya maneno. Come what may , nasema hivi “licha ya uislamu wao mzuri imefika wakati wazanzibar wamle nguruwe aliyenona”. Binafsi sioni mantiki ya wazanzibar “kuogopa kifo ilihali wanaitaka pepo?’’. Imefika wakati wazanzibar waikubali historia yao, ya jana , leo na kesho pia, vinginevyo wataendelea kupigana na adui asiyeonekana(invisible enemy);

Awali ya yote wazanzibar wanapaswa kujiuliza, wanapodai wanaitaka Zanzibar yao, je ni Zanzibar ipi wanaitaka?
-Wanaitaka Zanzibar ya sultani iliyojumuisha mpaka Kilwa na Mombasa?
-Zanzibar ipi? Ile iliyoongozwa na sultani yenye soko kuu la watumwa?
-Ama ile iliyokuwa “protectorate” ya Uingereza ikikandamizwa na ukoloni wa waarabu?
-Wanaitaka Zanzibar ipi? Ile ya mapinduzi yaliyoongozwa na mganda John Okello?
-Ama ile ya Mzee Abeid Karume ambao baadhi wanadai alikuwa na asili ya Malawi?
-Zanzibar ipi wanaitaka? Au ya “Komandoo” Dk Salmin Amour?
-Wanaitaka Zanzibar ipi? Ama ile ya Amani Karume na Seif Sharif ya Januari 27 mwaka 2001?

Pili Wazanzibar wangejitendea haki kama wangejihoji? Nini maana ya kuungana? Au je muungano wa Tanganyika na Zanzibar upo wapi? Kwenye makaratasi au mioyoni mwa wananchi? Je ni serikali inayoshurutisha watu wa nchi hizi kuoana? Ama nani kasema ni lazima wazanzibar wakaishi Tanganyika na kinyume chake? Kukosa kuelewa maswali haya na majibu yake kunaitumbukiza Zanzibar kwenye “mgogoro hewa” na Tanganyika kwa hoja dhaifu za kero za muungano. Je swali ni ama tutatue kero na tuvunje muungano? Au tuvunje muungano ili kutatua kero? Yote haya ni maswali yasiyojibika kwa maana ukweli ni kuwa yawezekana kuvunja muungano wa Tanganyika na Zanzibar lakini haiwezekani kuvunja muungano wa Watanganyika na Wazanzibar, na je nini maana ya Tanganyika pasipo Watanganyika? Au nini maana ya Zanzibar bila Wazanzibar wenyewe? Wazanzibar wasipotaka kuliona hili narudia tena “wataendelea kupigana na adui hewa” kwa miaka mingi ijayo.

Mwishowe nitoe angalizo kuwa Wazanzibar wanaweza kuishi pasipo itikadi lakini ni lazima wawe na mwelekeo. Nayasema haya kwasababu hakuna ubishi wowote kuwa hali hii ya kuishi pasipo itikadi ikiendelea hivi basi tusishangae huko mbele lile kundi la Wazanzibar wasiotaka muungano likapata “Kiongozi” rasmi halikadhalika na kundi la Watanganyika wanaoitaka “Tanganyika yao” likapata kiongozi, hapo ndipo kinachoonekana sasa ni mgogoro hewa kitakapogeuka kuwa “mhimili wa jehanamu” na kuwavutia wanahistoria wengi kutoka kila pembe ya dunia kuja kushuhudia “The Kosovo” of East Africa, tuombe tusifike huko. Naomba nimalizie makala yangu kwa beti mbili za shairi ili kuweka msisitizo;
Kuwafunza waso mboni, ni kazi si lelemama
Kusema pasipo soni, si sawa na kusimama
Mioyo ya visiwani, ukweli siyo salama
Harakati za Wazenji, Mtanange wa hisia.

Zanzibar wanaitaka, Tanganyika kadhalika
Vinywa vinapapatika, Kujibu yaso hakika
Busara yahitajika, pasipo la damu zaka
Mzalendo.net, harakati za wazenji.Nova Tzdream

 
Back
Top Bottom