Wanasiasa ndiyo tatizo, si viongozi wa dini - Jaji Warioba

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
50,956
22,148
Wanasiasa ndiyo tatizo, si viongozi wa dini - Jaji Warioba




SEPTEMBA 29, 2009, Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais (mstaafu), Jaji Joseph Warioba, alizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala kadhaa ya kitaifa na pia kutoa ushauri kwa viongozi waliopo madarakani. Mwandishi Wetu, GODFREY DILUNGA, aliyehudhuria mazungumzo hayo, anarejea yale ambayo Jaji Warioba aliyasema katika mkutano huo na waandishi wa habari.



“TANZANIA bado ni nchi ya amani na utulivu na tunaendelea na jitihada za kuleta maendeleo. Ni miaka 10 tangu Mwalimu atutoke na hayo mnayosema kama angekuwapo, hili lisingefanyika na hili lingefanyika.



Jaji Joseph Warioba
Mimi nadhani katika kipindi hiki tangu atutoke, bado kazi yetu ni kubwa sana lakini tumepiga hatua. Nadhani bahati mbaya wakati mwingine hatutathmini maendeleo yetu, tunaona mapungufu zaidi. Nina uhakika kama angekuwapo angesema tumejitahidi katika maeneo fulani fulani.

Katika kipindi hiki, tangu atutoke 1999 tumefanya jitihada kubwa sana kwenye huduma za jamii elimu, afya, maji, kumekuwa na maendeleo katika miundombinu kuna jitihada kubwa sana imefanywa kuendeleza barabara, madaraja. Kipindi kile, Magufuli (aliyekuwa Waziri wa Ujenzi) alifanya kazi nzuri kusimamia ujenzi wa miundombinu.

Tunayo matatizo sehemu fulani fulani, kama kilimo eneo ambalo ni kubwa sana kwenye maendeleo yetu. Tuna matatizo katika huduma za kiuchumi, hasa utilities mambo ya nishati, usafiri na usafirishaji, ndege, reli, bandari tunayo matatizo lakini jitihada zinafanywa.

Vurugu zilizotokea za uchumi duniani zimetuathiri kama nchi nyingine, lakini hali si mbaya sana tunaweza ku-recover isipokuwa sasa hivi inflation (mfumuko wa bei) imepanda sana imefika zaidi ya 12. Kwa hiyo, siyo kwamba hakuna jitihada zilizofanywa.

Lakini ni kweli pia katika kipindi hiki, tumepata matatizo mengi na hali hairidhishi. Nitazungumzia masuala mawili kwa ujumla. Moja, umoja wetu kama nchi, nimeanzia kwa kusema Tanzania ni nchi ya amani na utulivu, mambo ambayo msingi wake ni umoja wetu kama taifa.”

Umoja wa Taifa

“Kwa sasa hivi, kuna dalili kwamba umoja wetu unaanza kusambaratishwa. Tulikuwa ni nchi ambayo wananchi wake walishikamana sana. Hapakuwa na ubaguzi wa aina yoyote, tulikuwa tunaitana ndugu, lakini sasa tumeanza kugawanyika katika vikundi.

Kwanza sasa tuna matabaka katika nchi, kuna tabaka la matajiri na masikini. Hii iko wazi kabisa, na tofauti kimapato ni kubwa sana kati ya makundi haya mawili-matajiri na masikini. Na hata katika utumishi wa umma unaona kama kuna mgawanyiko wa namna hiyo.

Kuna wanaopata kipato kikubwa na wale wanaopata kipato kidogo, huko nyuma kama nchi tulijitahidi kupunguza pengo kati ya wale wa kipato cha juu na cha chini. Nadhani ilifika mahali ilikuwa uwiano wa 1:9 sasa hivi hilo pengo ni kubwa sana, nadhani kima cha chini ni 100,000 lakini kuna watu wanapata kima cha juu hadi milioni 5 na hata zaidi, kwa hiyo unaweza kuona uwiano ule ni 1:50 ukiingiza marupurupu mengine wanayopata wakubwa kama posho ya vikao, hili pengo ni kubwa sana.

Huko nyuma hawa tunaowaita wadogo walikuwa na sauti katika kuendesha nchi, sasa hivi matajiri ambao ni wachache ndiyo wenye sauti katika kuendesha nchi. Uongozi uko karibu zaidi na matajiri kuliko watu wa kawaida. Sasa matokeo yake mnaanza kuyaona.

Zamani unafanya kazi katika serikali ilikuwa wajibu wako kutunza siri za serikali. Siku hizi zinavuja kwa urahisi sana kwa sababu humo kuna watu hawaridhiki wanaona tofauti hii. Unaona watu wameanza kuchukua hatua kutetea maslahi yao, migomo inaanza kuwa mingi ya walimu, wanafunzi, wafanyakazi hata maandamano ya wananchi.

Wanaanza kutumia nguvu ya umma badala ya kufuata utaratibu wa kawaida wa utawala. Mimi nilishangaa kuona wananchi wa Ngorongoro, wametoka Ngorongoro hadi Dar es Salaam mbele ya Ikulu, ndiyo tunawastukia hapo. Lakini huko walikotoka, wametoka kwenye eneo ambalo lina viongozi.

Maana uongozi wetu unaanzia nyumba 10, kuna madiwani, wabunge, ma-DC, maofisa tawala, viongozi wa vyama vya siasa, wametokana huko hakuna kiongozi aliyejua? Inakuwaje? Maana unategemea kama wanakuja kumwona Rais, wangekuwa wamekwenda kwa viongozi hao kuomba wafanyiwe mipango ili wakutane na Rais, lakini wameamua wenyewe tu.

Nikasoma kuna mahali wananchi wamekwenda wakavamia ardhi ya serikali na wamegawana. Nikasema hawa wananchi wametokea wapi? Hawa wananchi si wanauongozi, imekuwaje waache viongozi, wajipange wenyewe na kuchukua uamuzi.

Unaona inafika mahali hawa wadogo wanaona ni bora wafanye mambo kwa utaratibu wao. Tusipoangalia tunaweza kuwa na utawala wa nchi, lakini wananchi wengi wanaendesha mambo yao wenyewe kwa kufuata utaratibu mwingine. Ile imani ambayo wananchi walikuwa nayo kuhusu serikali, viongozi unaona kama inapungua hivi, wanafanya mambo yao kwa mtindo wao. Kwa hiyo hili ni moja limetugawa, linatugawa katika matabata.”

Ukabila, udini na u-rangi

“Zamani ukabila ilikuwa ni utani, mtu akisema wewe mnyamwezi, muhaya, mpare ilikuwa utani, lakini siku hizi ina maana yake, hata rangi. Tumeanza kujigawa katika kanda, kanda ya ziwa, nyanda za juu kusini. Tunaanza kujigawa inapofika mahali mnafanya kitu mnatazama kwa kanda, siyo kitaifa.

Dini imeingia sasa. Kuna waraka na mwongozo. Mimi suala la udini sianzi kulitazama kwa waraka au mwongozo, nimeanza kuliona mapema kwa ngazi ya viongozi. Tuchukue suala la OIC, OIC ilipojitokeza kulikuwa na mgawanyiko wa kidini na hiyo ilinishangaza mimi.

Unashangaa udini unajitokeza vipi kwenye suala la OIC kwa sababu sio mara ya kwanza kutokea. OIC ndiyo ilikuwa chimbuko la G55, mwaka 1993, wakati ule Zanzibar ilijiunga na OIC, ikajitokeza kukawa na mjadala mkali, msingi wake haukuwa wa udini, bali utaifa.

Kilichojitokeza ni je, Zanzibar ilikuwa na capacity ya kuwa mwanachama wa OIC, na tuliizungumza hivyo na kwa jazba ile ndiyo wakajitokeza vijana katika Bunge, wakasema kama ndiyo hivi basi Tanganyika nayo ipate serikali yake, ndiyo msingi wa G55.

G55 haikuwa na sura ya kidini hata kidogo, nakumbuka baadhi ya waliokuwa katika G55, kulikuwa na Njelu Kasaka, Mateo Qaresi, hawa ni Wakristo Jenerali Ulimwengu na Athman Mhina hawa ni Waislamu, wanalitazama lile suala kitaifa, ilikuwa ni mchanganyiko wa watu wa imani mbalimbali wanalitazama kitaifa, mwisho tukakubaliana kwamba Zanzibar haikuwa na nafasi ya kujiunga OIC.

Lakini Zanzibar ikasema sawa, lakini shirika hili lina manufaa, kama Zanzibar haina nafasi ya kuwa mwanachama, kwa nini Tanzania isiwe mwanachama, tukasema sawa. Tukaanza kuangalia uwezekano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujiunga OIC.

Tulipotazama uwezekano huo tukakuta kwenye Katiba ya OIC kulikuwa na vipengele ambavyo vilikuwa vinazuia Tanzania isijiunge na OIC, tulitazama suala hili kitaifa, tukaomba kwamba OIC itazame Katiba yake kama itaweza kufanya mabadiliko ya Katiba yake ambayo yatatuwezesha kujiunga, wote tunazungumza kwa msingi wa kitaifa, ndipo tulipoliachia hapo.

Juzi juzi, nimemsikia Waziri wa Mambo ya Nje (Bernard Membe) kwenye Bunge akisema kwamba kweli OIC inaangalia Katiba yake, lakini suala hili lilipokwenda bungeni safari hii halikuja na sura ya kitaifa. Ilikuwa akisimama mkristo anapinga, akisimama mwislamu anaunga mkono, kwa hiyo limekuwa suala la kidini, nikashangaa hivi sisi tulikuwa wapi na hawa wanatokea wapi? Suala lile lile tuliloshughulikia kwa misingi ya utaifa, sasa linageuzwa la kidini.”

Mahakama ya Kadhi

“Mahakama ya Kadhi, ina historia ndefu, tumekuwa tukiizungumza tangu 1971, siyo kwa msingi wa kidini, ni kwa msingi wa kitaifa. Labda turudi nyuma, tulipopata uhuru tulikuwa na mikondo tofauti ya Mahakama. Kulikuwa na Mahakama za kawaida, inatoka Mahakama hii unakata rufaa Mahakama ya juu, lakini pia ilikuwapo Mahakama ya natives unatoka kwenye baraza la chifu, unakwenda kwa DC, PC unakwenda kwa Gavana.

Sisi tulipopata uhuru tukasema hapana, lazima tuwe na mfumo mmoja wa Mahakama. Kwa hiyo mwaka 1963 ilipitishwa sheria ya Mahakama - Magistrate Court Act, ndiyo ilianzisha mfumo mmoja waMahakama tukasema Mtanzania kama anatafuta haki anatumia utaratibu ule ule.

Baada ya hapo tukaanza kuona sheria fulani fulani zinabagua, tuzibadili, tukaendelea. Ilipofika mwaka 1971 kuna sheria moja ambayo tulitaka tuitengeneze kwa ajili ya Watanzania wote, Sheria ya Ndoa. Serikali ilikuwa inakuja na sheria, basically ambayo inatambua ndoa ya mke mmoja.

Ilipata upinzani mkubwa sana, mkubwa sana, Mnanka (Kiongozi wa kitaifa enzi hizo kutoka Musoma) alikuwa mmoja wa viongozi waliopinga kwa nguvu sana. Kwa hiyo, sheria hiyo ilipata upinzani kutoka kwa sheria za kimila na kiislamu. Waislamu wakasema kwa imani yao wanaweza kuoa mpaka wanawake wanne, wa mila wakasema idadi inategemea na uwezo wako.

Kwa sababu ya upinzani ule, serikali ikaona kweli hapa hatuwezi kuleta sheria moja ambayo ni lazima ibane kila mmoja, ikasema basi, Serikali itakuwa na sheria yake, na hiyo inapokwenda kufunga ndoa kwenye ofisi ya serikali unaweza kutamka pale kama hiyo ndoa ni ya mke mmoja au zaidi ya mmoja, kwa hiyo sheria ikatambua jamii nzima.

Lakini pia serikali ikasema tutatambua ndoa zote ambazo zinafungwa kihalali, iwe ya kimila, kikristo, kiislamu, kihindu, ya bahai, ikasema tunazitambua, ikifungwa ndoa kwa utaratibu huo ni halali nchini, tunachojitaji tu ni kwamba, baada ya kufunga ndoa hiyo njoo usajili, kwa hiyo suala la kusajili likawa la wote, na hakuna pingamizi, na talaka ikawa hivyo hivyo.

Nakumbuka Wakristo, na hasa Wakatoliki hawakukubaliana na hili la talaka, kwamba umeoa, mmefunga ndoa kanisani mnaishi…kisha hampatani unakwenda mahakamani kuvunja ndoa hiyo. Wakristo wakasema haiwezekani, kama umefunga ndoa kikristo kuivunja ni kwa utaratibu wa kikristo, serikali ikasema hapana kwa sababu walitaka kwenye sheria iseme ndoa ya kikristo haiwezi kuvunjwa mahakamani.

Serikali ikasema hapana, tunatengeneza sheria ambayo itatumiwa na kila mtu hatuwezi kusema hivyo, lakini hatuwazuii kuendelea na sheria zenu huko, kwa hiyo kama mtu ameoa kanisani kisha baadaye amekwenda akapata talaka mahakamani ninyi bado mna uwezo wenu wa kumwadhibu kwa sheria zenu huko na mpaka leo hii.

Mkatoliki, ukifunga ndoa katoliki kisha ukaivunja mahakamani kanisa halitambui na litakuadhibu na kwa muumini hili si dogo, kuna watu ambao wamefunga ndoa na wametoa talaka, kanisa halikutambua wakataka kuoa tena ikabidi wafuate utaratibu wa dini kupata kibali.

Lakini tulikubaliana kwa hilo. Baada tu ya sheria ya ndoa, tukataka tulete sheria ya mirathi lakini hii ndiyo haikuwezekana kabisa kwa sababu hizo hizo. Sheria ya mila wakapinga wakasema sisi tuna utaratibu wetu wa mirathi, Waislamu wakapinga tuna taratibu zetu, nadhani mara tatu Serikali ikajaribu.

Mara ya kwanza, ilikuwa chini ya Mzee Kawawa, wakati ule 1971, masuala ya sheria yalikuwa chini ya Ofisi ya Makamu, haikuwa Wizara kamili. Kwa hiyo, Mzee Kawawa ndiye aliyepeleka pendekezo la kwanza, likakataliwa.

Akaja Waziri Manning, mimi nikiwa Mwanasheria Mkuu wake, tukateua consultant (Mshauri mwelekezi) Profesa Weston, atufanyie utafiti alete mapendekezo tunawezaje kuwa na sheria ya mirathi, akatuletea tukapeleka ikakataliwa.

Baadaye mimi nikawa Waziri wa Sheria nikasema ngoja nijaribu kuifufua tena, nikaenda kupata mawaidha kwa Mzee Kawawa, akaniambia Joseph hili utaliweza?...mimi nilishindwa, Waziri Manning akashindwa. Akasema haya mambo ambayo msingi wake ni imani na utamaduni si mambo ya kuharakisha, lazima itoke ridhaa kwa jamii yenyewe serikali iache.

Lakini, wakati wote huo tuliendesha mambo haya kwa sura ya kitaifa ya umoja, hakukuwa kwamba wakati tunazungumza, waislamu wanasema hivi na wakristo wanasema hivi. Na wakati wote, Waislamu walikuwa wanasema sisi masuala ya mirathi yanaongozwa na Quran, na wanasema chombo kinachohusika ni Mahakama ya Kadhi, hawa wa mila wanasema taratibu zao, kwa hiyo tuliyatazama haya kwa msingi wa utaifa, miaka yote hiyo, hapakuwapo na mkwaruzano kwa misingi ya dini.

Juzi juzi hapa, nimeangalia majadiliano ndani ya Bunge, akisimama mkristo anapinga Mahakama ya Kadhi, akisimama mwislamu anaunga mkono. Limekuwa ni suala la kidini, badala ya kuangalia katika mfumo wetu wa kitaifa unashughulikia masuala hayo kwa njia zipi. Sasa baada ya hapo imekuja waraka na mwongozo.”

Waraka wa Katoliki

“Mimi kwa kweli lazima nikiri, sijui msingi wa tatizo ni wapi kuhusu waraka huo. Maana tunazungumza msingi wake wa tatizo sijauona hata kidogo. Nyaraka hizi zimekuwa zikitoka kila unapokuja uchaguzi, mimi nimekuwa nazisoma.

Nadhani mwaka 1994, kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, waraka ulitoka, 1999 kabla ya uchaguzi wa 2000 waraka ulitoka, 2004 ulitoka. Na mambo yanayozungumzwa humo ni yale yale isipokuwa msisitizo unabadilika kulingana na wakati.

Na mengine ni kila waraka unayo mambo yake. Ni elimu ya kawaida hiyo, mimi siyo mkatoliki, lakini nilikuwa nasoma waraka huo kama ambavyo mimi siyo mtu wa CUF wala CHADEMA lakini nasoma ilani zao, pamoja na kusoma ya CCM, kwa sababu ni elimu kwa mpiga kura.

Sasa imekuja inazuka wanasema nchi hii inaweza kuwa kama Lebanon, nikasema inatokea wapi? Ukisoma waraka ule hata zilizopita kuna mambo mengi mno ambayo kila siku hawa viongozi wa dini wanayahubiri kwenye makanisa na misikiti yao. Wanahimiza tufuate maadili wakati wote, wanalaani rushwa, wanasisitiza umuhimu wa mambo fulani fulani kama elimu, afya na wanashiriki katika kuendeleza huduma hizo.

Ni mambo ambayo wanayasema. Sasa leo wameyaweka kwenye waraka unasema wasiyaseme hivi tunataka kufika mahali tuwaambie hata wakienda makanisani kama wanataka kulaani rushwa ni lazima tushauriane nao? Mimi ninavyoliona jambo hili pamoja na mengine niliyosema ya tabaka, kabila, rangi, kanda, imefika mahali Watanzania tumejigawa katika makundi na tunayatazama mambo kufuatana na kundi gani umo.

Kwa hiyo kama imekuja ni OIC, aah! hili ni shirika la kiislamu sisi sio waislamu, kwa hiyo wewe mkristo moja kwa moja unalipinga, huendi ukaangalia umuhimu wa shirika hilo kwa nchi, ulitazame ki-nchi kwa kuwa tu wewe ni mkristo lazima ulipinge.

Mahakama ya Kadhi, aah! Hiyo ni ya Waislamu unapinga. Aah! huu waraka ni wa Wakristo unapinga. Mimi naona ni katika mfumo huu, kwamba tumeingia katika makundi. Unajua tunazungumzia kipindi hiki cha miaka 10 baada ya Mwalimu Julius Nyerere kututoka.

Unajua, Mwalimu Nyerere alikuwa ni mcha Mungu sana. Kila siku asubuhi saa 12 alikuwa anakwenda kanisani na Kanisa lake akiwa Dar es Salaam lilikuwa ni Saint Peter, kila siku asubuhi saa 12 alikuwa yuko pale kanisani, akitoka ndiyo anakwenda kunywa chai na kwenda kazini, miaka yote hiyo akiwa kiongozi.

Lakini hakuna hata siku moja ambapo Mwalimu alichanganya shughuli za dini na nchi, alitenganisha kabisa, alitenganisha completely. Mambo ya dini yalikuwa yake binafsi, hakuyaingiza katika shughuli za kitaifa, ni sisi (viongozi wa kisiasa) tumekuja kubadilisha utaratibu huu.

Siku hizi ni kawaida wakati wa Pasaka, mtu anatengeneza tafrija akialika watu si kwa msingi wa imani ni msingi wa kisiasa. Wakati wa Krismasi, watu wanaandaa shughuli za Krismasi si kwa msingi wa imani ni kwa msingi wa kisiasa. Siku hizi wakati wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, au sikukuu ya Iddi, watu ambao si Waislamu wanaandaa tafrija au futari si kwa msingi wa imani bali ni kwa msingi wa siasa.”

Viongozi kuingiza siasa kwenye dini

“Sisi viongozi ndiyo tunaingiza dini ndani ya siasa, na hili tulielewe sisi Watanzania, pamoja na haya mambo mengine yote, tujue kuendelea hivi kwa kweli tunasambaratisha umoja wetu, tumefikia hapo tusitafute mchawi.

Mchawi ni sisi wenyewe tumejifikisha hapo. Kwa hiyo nasema kwa kweli suala langu muhimu sana ni umoja wetu kwa sababu haya mambo ya maendeleo tutahangaika yatakuwapo, lakini tunaweza kupiga hatua kubwa kama tuna umoja na mshikamano, lakini sasa hivi kwa haya niliyosema naanza kuwa na wasiwasi tunakokwenda.

Maadili yetu kama wananchi kwa ujumla yameporomoka. Kutowajibika, lawama nyingi bila wajibu ni mambo ya maadili ambayo yameporomoka. Masuala ya ufisadi ni maadili kuporomoka, sijui tufanye nini lakini tutambue kuwa kuporomoka kwa maadili kumetuletea matatizo.

Sina solution lakini kama tukielewa kwamba imefika mahali unaonekana ni mtu mwelewa kama unaweza kuwa-articulate lawama zaidi unaonekana muelewa kabisa, badala ya kuangalia upande wa wajibu, hii imetuletea matatizo yote haya.”

Kesi za ufisadi kortini

“Hizi kesi zipo mahakamani kwa hiyo si rahisi kuzizungumzia kwa undani, lakini naweza kusema labda inatia matumaini kwenye vita dhidi ya maovu, rushwa, ubadhirifu, wizi, matumizi mabaya ya madaraka kwamba sasa angalau kuna watu wazito wamefikishwa mahakamani, hiyo inatia matumaini, sijui tuna kesi ngapi mahakamani sasa nadhani hakuna wakati wowote tumekuwa na kesi nyingi kiasi hiki, hiyo inatia matumaini.

Lakini tuwe na tahadhari na hili nalisema kwa dhati kabisa, kesi nyingi hizi zimetokana na msukumo wa kisiasa na kesi zinazotokana na msukumo wa kisiasa huwa kuna hatari zake baadaye. Nitumie uzoefu tu, mwaka 1979 tulikuwa na operesheni mitumba.

Kulikuwa na kamati za chama zikachunguza watu na kupendekeza wapelekwe mahakamani hatukufanikiwa sana baadaye lakini ilikuwa very popular kama sasa, wakati ule operesheni mitumba ilikuwa very popular. Lakini tumeisahau, tumeisahau kwa kuwa haikuwa na mafanikio makubwa sana.

Mwaka 1983 tukaja na operesheni ya wahujumu uchumi, hii sheria inayotumika sasa ya uhujumu uchumi ilitungwa kwa mara ya kwanza mwaka 1983, Aprili. Ndiyo sheria ya kwanza ya wahujumu uchumi ilitungwa na ikatumika na operesheni ile ilikuwa na msukumo mkubwa sana wa kisiasa, watu wengi sana walikamatwa na wakawekwa ndani, wengine wakafikishwa mahakamani lakini mafanikio yake hayakuwa makubwa sana, nadhani madhara yake yalikuwa makubwa zaidi.

Kwa sababu ya msukumo ule wa kisiasa kuna makosa mengi yalifanywa kuna raia wengi walionewa na baadaye tulipokuja kufanya tathmini ilibidi serikali ikubali kuwalipa wale raia walioonewa. Na moja ya matatizo tuliyopata katika operesheni hizo na hasa mahakamani, unapoandaa kesi kwenda mahakamani kuna utaratibu wake wa kisheria.

Kutumia utaratibu wa tume huna uhakika wa kupata mafanikio, sasa hizi kesi nyingi zimetokana na tume. Sina hakika na hizi tume kumekuwa na msukumo mkubwa wa kisiasa, sina hakika kama maandalizi yake yalifanywa kwa utaratibu wa kisheria au kwa msukumo wa kisiasa, kisha huko baadaye tuje kupata matatizo.

Nimesoma hukumu ya Jaji Masati, nilishangaa kidogo, kwa kesi kama ile ni wazi kweli kuna wananchi wameuawa kinyume cha sheria, hakuna doubt hata kidogo, lakini maandalizi ya kesi ile uamuzi umetokana na tume, kisha hawa ambao wapelelezi wanapewa muda, katika kipindi fulani uwe umekamilisha upelelezi kesi iende mahakamani, imekwenda mahakamani.

Mimi ni mwanasheria, nilisoma ile nikaona kuna gaps nyingi mle, nashangaa watu wanapora kwenye benki vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya juu chini vinawapata, vinawafikisha mbele ya sheria lakini mtu amemiminia watu wanne risasi ameauwa hapatikani, sasa mimi sijui ile kesi matatizo yake ilikuwa ni kwa sababu ya msukumo wa kisiasa kwa hiyo wamepeleka harakaharaka hivi au ilikuwa uzembe au ni makusudi.”

Vyombo vya habari na kesi

“Nasema hivi kwa sababu kwa msukumo wa kisiasa hivi na ninyi watu wa habari mnaandika sana mambo ya kesi hizi, lakini yanavyoandikwa ninyi ndiyo mnaowashitaki na kuwahukumu. Kwa sababu mtu aliyefuatiua kesi ya akina Zombe atashangaa kwa nini wameachiwa, kwa sababu magazeti yalikwishaeleza kuwa wanamakosa.

Wajibu wenu (waandishi wa habari) ni mkubwa kwa sababu msipofanya hivyo mtaifikisha jamii mahala wakaichukia Mahakama bila msingi, kwa sababu ninyi (waandishi) mtakuwa mmewaambia hawa wana makosa maana naona hata wakienda mahakamani kwenye ile tunayosema preliminary hearing ni kusilikiza tu lakini utakuta inaandikwa na kuliambia taifa kuwa huyu amekiri kosa, wakati hata hatua ya kuangalia hilo kosa bado. Nasema press lazima muwe waangalifu sana.

Na ndiyo naziona nyingine hizi tunazozisukuma kisiasa na naogopa, naogopa sana wanapomhusisha Rais, si vyema kumhusisha Rais katika hatua za mwanzo, Rais anakuja mwisho.

Kwa mfano tume za EPA inapeleka ripoti kwa Rais ambaye ndiye anayetangaza hatua inayofuata, siyo mahala pake Rais. Kwa hiyo wamemshauri kwanza fedha hizi zirudi hilo peke yake lina matatizo yake, naamini bila shaka kuna msingi kwa sababu watu waliomshauri ni top officials lakini wamemshauri rudisha fedha wamerudisha, wamemshauri kufuata taratibu fedha zimefikishwa kwenye Bunge, fedha zile zimepangiwa matumizi kesi bado zinaendelea.

Nasema naogopa, je, ikitokea mtu amerudisha fedha maana sijui kwa msingi gani kisha amekwenda mahakamani ameshinda, unafanyaje? Ndiyo nasema hapo yataanza maswali zilikwendaje, na kwa hiyo hawa hawa wanaomshauri Rais watamgeuka na kusema ilikuwa amri ya Rais.

Maana hata kumtaka aseme kesi gani zinakwenda mahakamani siyo sahihi. Mimi ilinishtua kidogo, wakati Rais anajibu maswali ya wananchi kwenye tv, akasema najua hivi karibuni kuna kesi tatu zitapelekwa mahakamani, wasimhusishe Rais.

Kwa sababu ukifanya hivyo ikija kutokea matatizo na ambaye ametamka hivyo kwa mara ya kwanza ni Rais watasema ni Rais alikuwa anahusika haikuwa sisi. Ningeomba wamlinde Rais akae mbali kwa mfano, hizi za EPA naona makala nyingi tu katika jamii zinazunguka kulikuwa na makampuni 22 yaliyofanya makosa haya, lakini wanaopelekwa mahakamani ni watu wa aina fulani fulani, wengine wanalindwa.

Kwa jamii sasa hivi wanaamini kwamba kuna upendeleo, kulindana. Sasa wangekuwa wamefanya kimya kimya, wakaja wakasema tumefanya kazi tuliowapata na makosa ni hawa hapa wakawapeleka mahakamani, lakini wanasema hawa wamerudisha na kati ya hawa waliorudisha baadhi wamekwenda mahakamani, sasa ukirudisha si umekubali kosa sasa kwa nini wasipelekwe wote mahakamani?

Hizi ni taarifa zilizoifikia jamii, kunakuwa na credibility gap kwa sababu mambo haya huwa yanaandaliwa kisha yanakuwa transparent yakiwa mahakamani, yafanywe kwanza ili yawe transparent mahakamani, kutumia taratibu nyingine hizi kunaleta matatizo.

Sasa ukija kupiga vita ufisadi kisiasa, mimi naamini kwamba kuna umuhimu na kwa kuwa tumeanza hivi kuna umuhimu wa kuendelea kupambana na maovu, sipendi sana neno ufisadi maana kuna rushwa bado tena kubwa kila mahali, tuna wizi mkubwa, ubadhirifu mkubwa tuna matumizi mabaya ya madaraka ni lazima tupambane nayo na mimi nilifarijika sana kuona viongozi wamejitokeza kupambana na hayo.

Sasa hapa katikati ndiyo hii inatuchanganya viongozi kupishana kauli, kabla ya mkutano wa NEC-CCM kulikuwa na maneno yanasemwa kwamba hawa kikundi hiki kinasema kinapiga vita ufisadi kuna wengine wanasema hapana hawa wanajitafutia umaarufu.

Imekwenda kwenye NEC taarifa za mwanzo tulizopata ni hizo kwamba hawa wanaojidai kupiga vita ufisadi wanajitafutia umaarufu tukasikia Spika amepata wakati mgumu na matamko, taarifa za mwanzo zikawa hivyo tukaambiwa kamati imeteuliwa ifanye kazi, kukawa na lugha pale…sasa naanza kuona kauli kwamba hali si hivyo hatuna ugomvi na huyu, mambo ni safi tu,.

Mimi hapa nilichoona there’s a credibility gap kubwa tu, kwa sababu mimi sasa sijui niamini kipi. Lakini kinachoonekana waziwazi kuna viongozi ambao wanataka kupiga vita ufisadi, na kuna viongozi ambao wanawaambia punguza speed, maana hilo linaonekana wazi kwa watu. Mimi ningependa kuona badala ya kusema kwamba hawa wanajitafutia umaarufu ningependa kuona viongozi wengi zaidi wanaingia katika kundi hili la kupiga vita ufisadi.

Kwa sababu ninalolisema hili ndani ya jamii kuna mambo mengi sana ambayo yangefaa kuchunguzwa maana mmekazania sana Richmond, EPA lakini yapo mengi zaidi. Nimeona makaratasi yanasambaa katika jamii kuhusu Meremeta, Deep Green, sasa jamii inayo hayo, na wanataka majibu.

Sababu usipotoa majibu juu ya haya, ndiyo hii inakuja kama aah! nadhani hapa kuna kulindana, kuna mmoja aliniambia hivi umeona aina ya watu waliopelekwa mahakamani kuhusu EPA? Akasema ukiangalia EPA waliopelekwa ni wale wezi tu, simply wezi ndiyo wamepelekwa.

Kwamba hivi kweli wamefanya hivi hapakuwa na ka-rushwa? Hivi huyu aliyepewa unamwona wapi hapa? Wanasema na zile kampuni zinazoonekana kuwa karibu na wakubwa ziko wapi hapa mahakamani? Nasema hizi kesi zipo mahakamani lakini kuna kujiuliza, hivi huyu ndiye aliyepaswa kushitakiwa pekee au kuna mwingine ambaye wamemwacha?

Kwa sababu kuna kesi nyingine kwa maelezo yale unaona ama watamfikia mtu mwingine au huyu ataachiwa, kwa hiyo ni vizuri haya tusiyadharau, siyo malumbano ya wakubwa ni yaliyomo ndani ya jamii usipoyatolea ufafanuzi ile credibility inakwisha na hakuna kitu kibaya kwa uongozi ambao wale wanaoongozwa credibility yao wanaiona ni ya wasiwasi.

Sasa tuangalie natoa hadhari tu wakati mwingine watu wanaogopa kwa kusema hatari inaweza kutokea wanaogopa kwa sababu ni kitu popular kwa wakati ule.

Nasema haya masuala lazima tuyaweke katika njia ambayo itakuwa sustainable siyo suala la muda mfupi tu kisha tunaicha. Na katika uongozi haya malumbano maana kuna baadhi wanasema wakati wote kuna mapesa yanatumiwa kutaka kutumaliza kila wakati wanapiga kelele lakini kimya, hivi ni nani hao wanatoa hizo pesa? Haya yote uongozi umekaa kimya, yanabaki ni mambo ya chini chini, haifai kabisa.”

Mitandao katika vyama vya siasa

“Katika yale niliyoeleza niliacha moja, kati ya yale yanayotugawa. Mitandao katika vyama vya vya siasa inatugawa sana. Mimi ni mwana-CCM, napenda kuamini kwamba CCM tuna ushawishi mkubwa katika nchi hii na kama tuna ushawishi mkubwa, mgawanyiko ndani yetu ni mgawanyiko wa nchi.

Sasa mgawanyiko ulioko kwa sasa hivi unaigawa nchi na inakuwa mbaya zaidi kwa sababu unatoka juu mpaka chini, siku hizi ukienda katika uchaguzi na ni vyama vyote tu yaani inakuwa kama dhambi akiwa mtu ameshika nafasi na ameipata kwa kuchaguliwa tu, akija mwingine anakuwa adui.

Yaani imekuwa ni uadui, uhasama kabisa na nilitishika kweli nilitishika niliposikia Rais siku ile alipokuwa akijibu swali la mwananchi kuhusu haya matatizo ndani ya CCM. Akasema si matatizo makubwa sana ya mpasuko ni watu tu wanauhasama wanachukiana hata hawaaminiani kuachiana glass mimi hili lilinitisha kidogo.

Maana ukisema humwamini kumwachia glass mwenzako ni kwamba unaamini labda ukitoka ukimwachia anaweza kukutilia sumu, ile ni mbaya. Na siasa hizi za uhasama na naanza kuziona zile zile za mwaka 2005 hata ninyi (waandishi wa habari) mmeanza kugawanyika, najua gazeti gani linaelekea upande gani kwa mtindo ule wa 2005.

Na hii itatufikisha mahali pabaya kwa sababu tumeanza kuiona na hatuchukui hatua za kuzuia. Hii ya ufisadi inaonekana ni kufuatia watu yaani ufisadi ni kumfuatia mtu ashitakiwe hatuchukui hatua za kuzuia. Wote hawa wanaosema wanaandama ufisadi hawapendekezi namna ya kuzuiya haya yasitokee na sasa tunakwenda kwenye uchaguzi.

Mwaka 2005, akihutubia Bunge kwa mara ya kwanza, Rais alisema katika kipindi hiki tutashughulika na tatizo la takrima. Tunakwenda kwenye uchaguzi mwaka kesho takrima ipo pale pale – ndiyo msingi wa ufisadi.

Mahakama inapotoa hukumu kupinga sheria fulani ni lazima sasa itengenezewe utaratibu mpya. Nasikia sasa hivi kuna mmoja amenunua kadi (za CCM) 10,000 kwenda kuwagawia watu waje kumteua.

Kwa sababu ni kweli kwamba kuna sehemu ambazo uchaguzi hasa uko ndani ya CCM ... ukipita hapo umeshinda, sasa unafanya hiyo...sasa tusipo-deal na hili tutapata EPA nyingine, Deep Green nyingine kwa uchaguzi unaokuja.

Hata kwenye vyama vingine vya siasa, anakuja Mrema anakuwa mwenyekiti anakuja Mtungirehi anakuwa adui fukuza, anakuja Mbowe akijitokeza Kabwe anakuwa tatizo ataleta mpasuko... sasa kwenye CCM ndiyo basi. Hii siasa, actually siasa ndiyo inayotugawa, siyo kitu kingine ni lazima tutambue hili.
 
Back
Top Bottom