Wanasiasa kuwakoromea waandishi

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,006
Wanasiasa kuwakoromea waandishi

Ndimara Tegambwage
Tanzania Daima~Sauti ya Watu

SITAKI mwanasiasa akejeli na kuwaelekeza waandishi wa habari jinsi ya kufanya kazi yao.

Sitaki mwanasiasa ajifanye mjuzi wa majukumu ya vyombo vya habari, na kujiweka katika nafasi ya kukoromea waandishi.

Wiki iliyopita, Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Stephen Wassira alinukuliwa akikejeli vyombo vya habari, tena kwa njia ya kudhalilisha; na katika mazingira alimokuwa, alionekana anavikoromea.

Wassira, ambaye ni mdau wa habari, kama mwananchi yeyote, aliwaambia wananchi kijijini kwamba vyombo vya habari hivi sasa vimejipa jukumu moja tu: kuandika habari juu ya Richmond na EPA.

Kwa kukariri maneno “Richmond, EPA, Richmond, EPA, Richmond,” Wassira alilenga kuonyesha mchoko alionao, na huenda walionao viongozi wengine – mawaziri na watendaji wengine serikalini.

Richmond ni kampuni ya kitapeli, iliyoundwa haraka na baadhi ya viongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi, ambao pia walikwenda kwa msajili na kuiba, na huenda kuharibu kabisa nyaraka za usajili, kiasi kwamba hivi sasa inaonekana Richmond haijawahi kusajiliwa nchini.

Kampuni hii ilidai ina uwezo wa kuzalisha umeme wa dharura wakati nchi inakabiliwa na tatizo la umeme kutokana na kukauka kwa mabwawa yaliyotoa maji ya kuendeshea mitambo ya kuzalisha umeme.

Hadi hali ya ugavi wa umeme inarejea kawaida, Richmond ilikuwa haijazalisha kiasi chochote cha umeme. Ni kasheshe ya Richmond iliyosababisha kuachia ngazi kwa aliyekuwa Waziri Mkuu na mawaziri wawili na kufuatiwa na kuvunjwa kwa Baraza la Mawaziri.

EPA ni Akaunti ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambako kampuni binafsi zilikwapua, kwa njia ya udanganyifu usiomithilika, jumla ya sh bilioni 133 za umma.

Richmond na EPA ni msitu mnene wa ujambazi wa kutumia kalamu na ulaghai ulioshirikisha watu wengi, wakiwemo viongozi wa serikali, CCM na baadhi ya wananchi waliotumiwa kama “vibarua wa kulegeza milango ya sefu”.

Wakati Richmond ilikuwa ikichota kutoka mfuko wa umma sh milioni 152 kila siku, wezi walichota sh bilioni 133 kupitia BoT.

Waliochota, waliokula, walionyimwa, waliokosa kutekelezewa ahadi, sasa wanavutana na habari hazivuji; zinamwagika kama mkondo wa mto mkubwa umwagavyo maji ya mafuriko katika bahari.

Habari zinamwagika Dar es Salaam, lakini nchi nzima inataka kujua. Sharti waandishi wa habari waziandike na kuwapelekea wananchi nchi nzima.

Habari zinazomwagika zinaacha ukoko ndani ya bomba; kwenye mkondo uingiao baharini. Ni ukoko huo unaohitajika kuchokonolewa na waandishi wa habari mahiri.

Habari hizo za ukwapuaji wa fedha za umma, si simulizi zisizokuwa na mashiko. Hapana. Zinatokana na vitendo maalum vya wahusika – wakiwemo watawala na wasaidizi wao.

Hivyo, unahitajika utaratibu na utaalam wa kuwaeleza wananchi, ilikuwaje fedha zao zikaibiwa, mbinu gani zilitumika, wapi, lini, nani wahusika wakuu na wahusika wadogo; nafasi ya serikali katika uoza huu na hatua zinazochukuliwa hivi sasa. Yote haya ni muhimu ili kuwezesha wananchi kujua kinachoendelea katika ofisi zao.

Wizi wa mabilioni ya fedha kutoka BoT haukuandaliwa kwa wiki au mwezi mmoja. Ni mipango ya muda mrefu. Ni njama za chinichini za miezi mingi. Ni mitandao ya wajuzi katika kuficha siri kwa muda mrefu.

Kupata taarifa kamili na sahihi; kupata washiriki katika mitandao ya kifisadi; kuandaa taarifa sahihi juu ya njia zilizotumika kuwaibia wananchi na wapi fedha hizo zimekwenda na kutangaza taarifa hizo, haiwezi kuwa kazi ya mwezi mmoja.

Haiwezi kuwa kazi ya miezi michache. Ni kazi ya muda mrefu inayostahili kufanywa kwa makini. Lakini ni kazi pia inayostahili kufanywa kwa kurudiarudia.

Kurudia kuna maana yake. Ni kusisitiza hoja. Ni kuwezesha ambaye alikuwa hajaona au kusikia taarifa hiyo, kuipata bila kiwingu. Ni kujenga marejeo yasiyo na shaka kwa kila mwananchi anayesikia taarifa hizo.

Lakini pia kurudiarudia ni kushindilia hoja ndani ya vichwa vya wakwapuaji, kwamba wamefahamika na waache wizi. Ni kuendelea kuiambia serikali kwamba haijachukua hatua zinazostahili kukabiliana na ufisadi huo.

Aidha, kwa yeyote anayefuatilia habari za ufisadi, ataona kuwa zinatokana na kiu ya wananchi kujua serikali inafanya nini kusitisha wizi; kuadhibu wahusika na kuziba mianya ya ukwapuaji.

Wassira anaona aibu hata kutamka neno “mafisadi” au “ufisadi.” Anasema waandishi wamezidi kuandika Richmond na EPA.

Kwa wananchi wa vijijini ambao hawajapata undani wa ujambazi katika EPA na Richmond, wanaweza kufikiri kuwa vyombo vya habari vinaandika habari za marais wa nchi za nje peke yake.

Na huo ndio umuhimu wa kuendelea kuandika ufisadi huu hadi wananchi wengi, kama si wote, waelewe jinsi fedha zao zinavyoibiwa na baadhi ya wale waliowaweka madarakani.

Wassira anaweza kukuta anatuhumiwa kwa ufisadi mpya; ule wa ukwapuaji wa haki ya wananchi ya kujua kinachoendelea katika ofisi zao, na hasa juu ya fedha za umma. Hakika hatapata njia ya kujitetea na hata akijitetea, hakuna atakayemwonea huruma na hatashinda. Bado wananchi wanataka kujua nani kawaibia na anachukuliwa hatua gani.

Wassira asiwafundishe waandishi wa habari jinsi ya kufanya kazi zao; lipi waandike, lini watangaze na wapi waende kukusanya habari. Anachofanya ni kupanda mbegu ya udikteta.

Mtawala wa sasa au baadaye, haweza kunawirisha mbegu hii, kuikomaza na hapo kuua uhuru wetu wa kufikiri na kutoa mawazo. Tukatae kwa nguvu zote.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com na www.ndimara.blogspot.com
 
Back
Top Bottom