Wanasheria wazidi kuponda mauaji arusha

DENYO

JF-Expert Member
Sep 14, 2010
698
57
Anderew Chale
TAMKO LAO;CHAMA CHA WANASHERIA WA TANZANIA BARA
TAMKO 9 January, 2011
Na

Chama cha Wanasheria wa Tanzania Bara (kwa kifupi ‘CHAMA’) ni Jumuiya ya Kitaifa
...ya Wanasheria wa Tanzania Bara, kilichoundwa chini ya Sheria ya Chama cha
Wanasheria wa Tanganyika, Sura 307 ya Sheria, Toleo la 2002. Kwa mujibu wa Sheria
hii, majukumu ya CHAMA ni pamoja na kuisaidia Serikali katika maswala yanayohusu
sheria, utekelezaji na utendaji wa sheria, na pia kulinda na kusaidia umma katika masuala
yote yanayoambatana na yanayohusiana na sheria- kwa kifupi, utekelezaji wa mfumo wa
sheria na wa utawala bora.
Kufuatia taarifa za vyombo vya habari na watu binafsi mintarafu ya mapambano baina ya
Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (“Jeshi la Polisi”) na wafuasi wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Manispaa ya Arusha, CHAMA
kimewasiliana na vianzo mbalimbali Arusha, pamoja na vyombo vya habari na wahanga
wa vurugu ili kupata uhakika wa taarifa hizo. Jitihada zetu kuwasiliana na maafisa
mafawidhi wa Jeshi la Polisi Arusha hazikufanikiwa.
Tulifahamishwa kwamba tarehe 5 Januari, bila silaha viongozi na wafuasi wa Chadema
walifanya maandamano ya amani katika Manispaa ya Arusha, baada ya taarifa ya
kufanya hivyo kwa Kamanda wa Polisi Wilaya wa Manispaa (OCD) iliyopelekwa tarehe
31 Desemba 2010, na kwa rejea zaidi ya barua ya tarehe 4 Januari, pamoja na mkutano
shirikishi na OCD iliyothibitisha vipengele vya usalama kwa ajili ya maandamano na
mhadhara. Tunafahamu kwamba Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) kwenye taarifa ya
habari ya taifa ya saa 2 usiku (yaani chini ya masaa 24 kabla ya maandamano
yaliyopangwa) tarehe 4 Januari alitoa onyo la mdomo kusitisha maandamano lakini
kuruhusu mhadhara. Tunafahamu pia kwamba, pamoja na onyo hilo, maandamano
yalifanyika kama ilivyopangwa.
Tumehabarishwa kwamba ndipo, Jeshi la Polisi lilitumia nguvu kusitisha maandamano
na kutawanya mkusanyiko, na hatima yake ni kwamba kulitokea vifo vya watu wawili (2)
au zaidi, na majeruhi kwa raia kadhaa wasiobeba silaha. Aidha tumehabarishwa kwamba,
wakati ghasia zikiendelea, wanahabari waliotambulikana dhahiri kwa ajili hiyo
walilengwa shabaha na Jeshi la Polisi kwa kufuatilia mambo yaliyokuwa yanaendelea, na
baada ya hapo Jeshi la Polisi mwanzoni halikuruhusu mawakili waonane na watu
waliowekwa chini ya ulinzi na Polisi.
Ibara ya 20 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 (‘Katiba’)
inamhakikishia kila raia uhuru wa kujumuika na kukutana. Kifungu cha 43(1) cha Sheria
ya Jeshi la Polisi na Vikosi vya Usalama (Sura ya 322, Toleo la 2002, kinatoa mwongozo
kwa kila anayetaka kuitisha, kukusanya, kuunda au kuratibu mhadhara au maandamano
kwa mujibu wa haki ya kikatiba ya mihadhara, ambapo inahitajika tu kutoa taarifa kwa
Polisi kuhusu mahala na muda ambapo mhadhara utafanyika, na azma ya mhadhara.
Tunavyoelewa kipengele cha kutaarifu kimewekwa na sheria ili kuhakikisha kwamba
haki ya kikatiba ya Ibara ya 20 inalindwa na kuhifadhiwa, siyo kuhujumiwa na Jeshi la
Polisi. Kwa maoni yetu lile onyo la mdomo la IGP athari yake halisi liliharamisha
maandamano ya Chadema kwa kuwa halikutoa fursa nyingine maandamano yafanywe
lini. Lakini penye haki pana tiba, na Chadema ilipaswa kutafuta haki ndani ya mfumo wa
sheria. Hata hivyo hatuna uhakika kwamba onyo la mdomo la IGP lilitoa fursa ya
kutosha ya kufuatilia haki kwa mujibu wa sheria ama kulikanusha onyo au kusitisha
maandamano. Pamoja na hayo, Jeshi la Polisi halipaswi kuwa chanzo cha ukiukaji au
kusababisha ukiukaji wa haki wa haki zinazolindwa kikatiba.
Ibara ya 18 ya Katiba inahakikisha haki ya kila mtu kutoa maoni, ambayo ni pamoja na
kujieleza mawazo na maoni yake kwa uhuru, na pia haki ya kuhabarisha na
kuhabarishwa. Haki hii inatumika kulinda matamshi, taarifa na mawasiliano, pamoja na
yale ya wanahabari. Kutokana na taarifa, haki hizi zimebezwa na Jeshi la Polisi.
Kifungu cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, Sura ya 20 Toleo la 2002,
inamwajibisha afisa wa polisi kutoa fursa stahiki kwa mtu aliye chini ya ulinzi aweze
kuwasiliana na wakili, ndugu au rafiki anayemtaka, Kwa mujibu wa taarifa, haki hii
imedhulumiwa na Jeshi la Polisi angalau mwanzoni.
Kwa kuwa tumejidhatiti kulinda na kuimarisha utawala wa sheria na utawala bora wa
Serikali, kwa uelewa kwamba ukilindwa kwa usahihi, utawala wa sheria na utawala
bora vinawalinda wananchi dhidi ya matumizi ya mamlaka ya Serikali kwa udhalimu;
kwa kuwa tunaamini kwamba dhana ya kutowajibika daima unapelekea kufanyika
maovu makubwa zaidi; na kwa kuamini kwamba haki siyo tu itendeke, bali ni lazima
ionekane kwamba inatendeka:
1. CHAMA kinatoa mwito kwa raia na Serikali pamoja na taasisi zake kuzingatia
na kufuata sheria na utawala bora; na
2. CHAMA kinalaani vikali hatua zilizochukuliwa na Jeshi la Polisi za kupora haki
za kikatiba za kujumuika, mikusanyiko na uhuru wa kujieleza; na
3. CHAMA kinalaani vikali matumizi ya nguvu kubwa mno za Jeshi la Polisi katika
kutawanya umati wa raia usio na silaha, unaoandamana na uliokusanyika kwa
amani; na
4. CHAMA kinatoa mwito kwa Serikali ya Tanzania kufanya uchunguzi wa kiini na
kupeleleza tukio hili la kusikitisha, kuwawajibisha wahusika kwa mujibu wa sheria,
na kuendelea kutumia njia za amani za kuendeleza mfumo wa sheria na utawala
bora na kulinda demokrasia kwa maslahi ya taifa.
Imewasilishwa kwa niaba ya Chama cha Wanasheria wa Tanzania Bara
RAIS

Source Facebook Mnyika -wall
 
Duh nimeipenda hiyo wamechambua na kuelezea vizuri.

Swali: Kama wako pale kama walivyoelezea nanukuu "Kwa mujibu wa Sheria
hii, majukumu ya CHAMA ni pamoja na kuisaidia Serikali katika maswala yanayohusu
sheria, utekelezaji na utendaji wa sheria, na pia kulinda na kusaidia umma katika masuala
yote yanayoambatana na yanayohusiana na sheria- kwa kifupi, utekelezaji wa mfumo wa
sheria na wa utawala bora". Mwisho wa kunukuu

Je wako tayari kuwapeleka Askari waliouwa Mahakama kusaidia familia zilizoathirika na
uongozi mbovu wa polisi kwani yawezekana familia hizi
zisiwe na uwezo wa kugharamia wanasheria?
 
Back
Top Bottom