Wanaotumia ARV wataka Madabida akamatwe

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
bot_tabimg.gif

Thursday, 11 October 2012 21:51

Waandishi Wetu

SIKU moja baada ya Serikali kuwasimamisha kazi vigogo wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kwa kashfa ya dawa bandia za kufifisha makali ya Ukimwi (ARVs), Mtandao wa Watu Wanaoishi na Ukimwi (IDNEPHA), umeitaka Serikali kuwakamata na kuwahoji wamiliki wa Kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd (TPIL), kinachodaiwa kutengeneza dawa hizo, Ramadhani na Zarina Madabida.

Mbali ya mtandao wa watu wanaoishi na Ukimwi, Kamati ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi imeitaka Serikali kuwasilisha kauli yake katika Kikao cha Bunge kijacho kuhusu hatua zilizochukuliwa baada ya kugundulika kuwapo kwa dawa bandia ARV nchini.


Hata hivyo, Madabida mwenyewe jana alikanusha madai ya kiwanda chake kutengeneza dawa hizo na kuzielezea taarifa hizo kuwa ni hujuma za kisiasa dhidi yake.


Wakizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, viongozi wa mtandao huo walieleza kushangazwa na kitendo cha Serikali kukifunga kwa muda kiwanda hicho na kuwasimamisha kazi viongozi wa MSD, huku Madabida akiendelea kuachwa huru.


"Tunaipongeza Serikali kwa kuwawajibisha viongozi wa MSD, lakini huyo mmiliki wa kiwanda mbona haguswi? Tunaona yuko huru tu wakati sisi maisha yetu yako hatarini," alisema Mwenyekiti wa IDNEPHA, Mwanahamisi Mhando na kuongeza;


"Tunajisikia uchungu kuendelea kutumia dawa hizi wakati hatujui kama nazo ni feki au zinafanya kazi. Kibaya zaidi zimeshasambaa nchi nzima na watu wanaendelea kutumia."
Mhando alisema hawana haja ya kuingilia mambo ya siasa, lakini wameamua kuibuka kwa kuwa suala hilo ni nyeti kwa afya ya Watanzania.


Makamu Mwenyekiti wa Mtandao huo, Issac Benson alisema licha ya kiwanda hicho kufungwa, bado wanataka na mmiliki wake awajibishwe.


"Pamoja na Serikali kuwasimamisha viongozi wa MSD na kukifunga kiwanda hicho, bado tunaitaka iende mbele zaidi kwa kumwajibisha mmiliki wa kiwanda hicho ambaye ni Ramadhani Madabida na mkewe Zarina," alisema Benson.


Alisema tangu suala hilo lilipojitokeza wamekuwa wakiishi maisha ya wasiwasi bila kuwa na uhakika na dawa wanazoendelea kuzitumia kama zina ubora unaotakiwa.

Zarina ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum (CCM), alikaririwa hivi karibuni akisema kuwa kiwanda chake ndicho kilichogundua kuwapo kwa dawa hizo feki.


Dawa hizo zilianza kugundulika mwanzoni mwa Septemba mwaka huu wilayani Tarime baada ya Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) kufanya ukaguzi.

Kauli ya Madabida
Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Limited-TPI, Zarina Madabida jana aliwaambia waandishi wa habari kuwa dawa za ARV zilizosambazwa siyo za kiwanda hicho na kwamba ni njama za kuchafua jina lao la kibiashara.

Kauli ya mkurugenzi huyo inafuatia hatua ya Serikali juzi kutangaza kukifunga kiwanda hicho kwa kukihusisha na utengenezaji wa dawa feki za kurefusha maisha.

Alidai kuwa huo ni mchezo unaofanywa na watu wachache ambao hata hivyo hakuwataja.

Mkurugenzi huyo alisema kiwanda hicho kilitarajiwa kuzinduliwa rasmi Novemba mwaka huu na wangefanya kazi chini ya Shirika la Afya Duniani (WHO) na kwamba wangeweza kupewa leseni ya kuuza dawa hizo ndani na nje ya nchi, lakini kwa sababu kimefungiwa huenda mipango hiyo isifanikiwe.

"Hizi ni siasa zinazofanywa na watu wachache ambao wanataka kutuharibia jina la kiwanda chetu kwa kutuwekea ARV za bandia ambazo zina jina la biashara ya TT-VR30 la kiwanda chetu," alisema Madabida.

Madabida alisema dawa zao zina rangi nyeupe na upande mmoja zina alama ya T30 na upande wa pili zina alama ya TPI,lakini dawa zilizosambazwa ambazo ni bandia zina rangi mbili ambazo ni rangi nyeupe na rangi ya chungwa.

Alisema dawa hizo za kwao zilitengenezwa kati ya Machi na Aprili mwaka 2011 na kusambazwa na MSD na kwamba wagonjwa hawakupata matatizo hadi taarifa za kuwapo dawa feki zilizoibuka Agosti mwaka huu.

Hata hivyo, alisema baada ya kuwapo taarifa hizo walikaa kikao na TFDA na kukubaliana kuwa dawa za ARV zilizosambazwa siyo dawa zao, hivyo waliomba dawa hizo zirudishwe MSD.

Alisema baada ya kuona hakuna hatua yoyote waliyochukua TFDA waliamua kuwaandika barua Agosti 28 mwaka huu kusisitiza kuwa dawa bandia zlizopo sokoni zirudishwe MSD ili kuokoa maisha ya wananchi.

"Kuanzia 2007 hadi leo hii tumetengeneza dawa za ARV zaidi ya dozi 2.28 milioni iweje leo hii sisi wenyewe tutengeneze dawa feki dozi 8,000 ambazo zimebainika, haingii akilini," alisema.

Pia alisema wanafanya uchunguzi kubaini ni kina nani waliofanya kitendo hicho ili waweze kuwachukulia hatua za kisheria wanaowachafulia jina la kampuni yao.

Mjadala kutua bungeni
Katika hatua nyingine, Kamati ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi imeitaka Serikali kuwasilisha kauli yake katika kikao cha Bunge kijacho kuhusu hatua zilizochukuliwa baada ya kugundulika kuwapo kwa dawa bandia za ARV.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Lediana Mng'ong'o alisema hayo jana katika ofisi ndogo za Bunge alipokutana na waandishi wa habari kuzungumzia tatizo hilo.


Mng'ong'o ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) alisema Serikali inatakiwa iendelee kufuatilia suala hilo kwa undani na kuchukua hatua kali pale vyombo vya usalama vitakapomaliza uchunguzi wao.

"Tunataka Serikali itoe kauli bungeni kuhusu hatua zilizochukuliwa baada ya kugundulika tatizo hilo," alisema.

Alisema wanalaani vikali wafanyabiashara wanaoingiza dawa bandia nchini, hivyo uchunguzi ukikamilika wachukuliwe hatua kali za kisheria ikiwamo kunyang'anywa leseni zao za biashara.


"Hatukubaliani na kitu hicho na kimetusikitisha, hatuwezi kufurahia dawa ambazo ni bandia," alisema.

Alisema baada ya kupata taarifa za kuwapo ARV walikutana
na viongozi wa Serikali akiwamo Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi pamoja na mitandao mbalimbali ya Ukimwi.


Mung'ong'o alisema baada ya kupata taarifa hizo na Serikali kuanza kuchukua hatua kamati hiyo imeridhika na hatua zilizochukuliwa tangu tatizo hilo ligundulike.


Alisema kutokana na Serikali kukusanya dawa hizo katika maeneo zilikogundulika, wanawaomba wagonjwa ambao waliacha kutumia dawa za ARV waendelee kutumia kwa kuwa zipo za kutosha.

Juzi Serikali ilimsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Joseph Mgaya, kutokana na kubainika kuwapo na kusambaa ARV bandia.


Mbali na Mkurugenzi huyo pia imesimamisha Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti Ubora, Daud Maselo na Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti Ubora wa Dawa, Sadick Materu.

Pia wamesitisha kiwanda cha TPI cha jijini Dar es Salaam kuzalisha dawa hizo.

Habari hii imeandikwa na Pamela Chilongola, Boniface Meena na Elias Msuya.

 
Wote Mr & Mrs Madabida wote wanagombea u-CCM-NEC... Kwahiyo bado Watachaguliwa na WanaCCM kwenye
Hizo Nafasi ?
 
huyu mama ni mtu wa short cut miaka mingi sana siwezi kumuaini hata kidogo..alihusika kuifilisi MADAWA enzi hizo, akatapeli wanawake wenzake kwenye scheme inayofanana na DECI. ni muongo muongo, tapeli tapeli, mtu wa mjini
 
huyu mama ni mtu wa short cut miaka mingi sana siwezi kumuaini hata kidogo..alihusika kuifilisi MADAWA enzi hizo, akatapeli wanawake wenzake kwenye scheme inayofanana na DECI. ni muongo muongo, tapeli tapeli, mtu wa mjini

eeh! Kumbe! Fafanua mkuu hii ni mpya kwangu.
 
Back
Top Bottom