Wananchi wanapoitwa wavamizi Kilosa

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,792
287,994
Na Ndimara Tegambwage

MwanaHALISI~Maslahi ya Taifa Mbele

NI vilio vitupu. Baadhi ya wananchi wenye mifugo – Wamasai, Wairaqw, Wabarbaig na Wasukuma wanawindwa kama swala. Wanaambiwa waondoke wilayani Kilosa. Eti warudi makwao.

Je, kila Mtanzania angeambiwa arudi kwao, nani angebaki alipo? Nani siyo uzao wa mzunguko wa mataifa madogo? Nani mtu wa asili Tanzania?

Lakini makabila haya yanawindwa na kufanyiwa ukatili kwa kuwa yana mifugo. Wilayani Kilosa serikali inaendesha kile wanachoita “operesheni” ya kupunguza mifugo na kufukuza wenye mifugo wasiokuwa “wenyeji” wa wilaya hiyo.

Wamasai wanasema ni “presheni ya kupilisi” – operesheni ya kufilisi.

Viongozi wa Kata, wakiandamana na polisi na mgambo, wanavamia eneo la mwenye mifugo, ndani au nje ya mipaka yake. Wanaswaga mifugo hadi wanakodai ni “zizi la serikali.” Kuwagomboa sharti ulipe Sh. 30,000 kwa kila kichwa.

“Wanatwambia tuuze mifugo yetu palepale; au tuisombe kwa malori hadi kwenye mnada, Pugu, Dar es Salaam, au tuhamie mkoani Lindi ambako wanasema wametenga ardhi kwa ajili ya wafugaji,” anaeleza mfugaji Kalaita Parkuris huku machozi yakimlengalenga machoni.

Kalaita ni mwathitika wa operesheni. Polisi wenye silaha na mgambo waliingia kwake na kukomba mazizi – ng’ombe 340 na mbuzi 120 katikati ya eneo la eka zipatazo 70 ambako ameishi tangu 1963.

“Presheni nini hii? Nini hii kama siyo taka kutupilisi,” alihoji Kalaita alipoongea wiki iliyopita na waandishi wa habari, chini ya mti, nje ya nyumba yake.

Kalaita anasema alikataa kugomboa mifugo yake na kuacha ichukuliwe chini ya ulinzi wa polisi. Anaulizwa kama angekutana na Rais Jakaya Kikwete angemwambia nini.

Anajibu, “Ningesema awachukue watoto awalishe. Watakufa hawa,” huku akionyesha watoto wapatao 30 walioketi nyuma yake.

Ndugu yake anadakia, “Kuwachukua ni kama kuwapoteza. Ni kama wamekufa, maana hawapo.”

Hapo ni kijijini Mkundi, Kata ya Dumila. Lakini ndivyo ilivyo katika maeneo mengi wilayani Kilosa. Haishangazi basi kukuta akina mama wa kitongoji cha Ngaiti wakiimba mbele ya waandishi wa habari:


Maisha bora
kwa mwekezaji
Maisha bora
kwa mafisadi
Maisha duni
Kwa mfugaji


Wanawake hawa ni sehemu ya jamii ambayo shughuli yake kuu, kwa miaka yote, ni ufugaji wa asili. Kuwaondolea njia yao ya maisha, kwa kasi ya kuwafilisi, hakika ni kuvunja haki za binadamu.

Kupora mifugo ambayo ni ajira, uchumi na egemeo la uhai wa wananchi, kuna athari nyingi na kubwa kwa maisha yao.

Watakosa chakula – nyama na maziwa.
Watakufa kiuchumi na kupoteza uhai kabla ya wakati wao. Watoto wao watashindwa kwenda shule au kubaki hai wakichunga mifugo ya kaya zao.

Unyang’anyi huu kwa njia ya “operesheni ya kupunguza mifugo na kuondoa wahamiaji Kilosa,” tayari umezaa mifarakano. Sasa utazaa vita vikubwa.

Bibi Yasoi Kadege, mwenye umri wa miaka 97, wa kitongoji cha Ndagani kijijini Mabwegere, amechoka, amekata tamaa, anatamani ujana wake umrejee mara moja. Hauji.

Hapa unasimuliwa jinsi polisi na mgambo, walivyokomba ng’ombe 385 wa kaya hii wakiacha nyuma ndama wachanga 21. Hadi wiki iliyopita ni ndama watatu waliokuwa wamebakia; wakiwa taabani. Watakufa.

Sikiliza kikongwe Yasoi akijadiliana na mmoja wa waliofika nyumbani kwake:

Yasoi: Huko kwenu peresheni hii imefika?
Mgeni: Ipo. Wamechukua mifugo mingi tu.
Yasoi: Sasa wewe kaa hapa; ungana na mwanangu ili mwende Morogoro; piganeni vita mkomboe mali zenu.
Mgeni: (Kicheko cha kugegema) Sawa bibi, ni kweli.

Yasoi hana nguvu tena. Alibebwa na watu watatu kutoka ndani ya banda lake. Hata pale nje alipokaa, alihitajika mtu wa kuegemea na mwingine kuzuia asiangukie mbele.

Hana amani. Hana chakula. Chakula chake ni maziwa na “maziwa yote” yalichukuliwa na serikali. Maziwa ya kopo ambayo amepelekewa na wajukuu wake yanamletea kiungulia na sasa hataki hata kuyaona. Atakufa.

Mita 200 kutoka kwa Yasoi ni kwa Tisini Madamanya, mwenyekiti wa kitongoji cha Madagani, kijijini Mabwegere ambaye anasema askari walikomba mbuzi wake wapatao 250.

Tisini ana wake tisa na zaidi ya watoto 40 (jirani yake anasema ana watoto zaidi ya 70), watakufa njaa kama hawakupata msaada wa haraka. Mtoto mwenye umri mdogo hapa ana siku 14.


Kijiji cha Mabwegere ni cha wafugaji. Mkurugenzi wa Wilaya ya Kilosa, Ephrem W. Kalimalwendo anadai kuwa halmashauri haijawahi kufanya operesheni kijijini humo.

Anapoelezwa unyang’anyi katika sehemu mbalimbali ambako waandishi wamefika na kusimuliwa uporaji, anakana kuhusika kwa serikali yake ya wilaya. Sasa nani amefanya uhalifu huo?

Kalimalwendo anakataa pia kuwa watu wanaporwa mifugo; anadai kuwa wanauza wenyewe au wanaondoka nayo kwa kuwa hawana “vibali” vya kuishi Kilosa.

Anapoulizwa iwapo kuna wanaoweza kuwa wanafanya “operesheni” nje ya operesheni maalum ya wilaya, anajibu kuwa hajui; ghafla anasema hawapo; baadaye anasema, ninyi (waandishi) mnaadika kwa kupendelea wafugaji. Kigeugeu.

Bali Mkurugenzi Kalimalwendo anasema wenye mifugo kutoka bonde la Ihefu mkoani Mbeya ambako walifukuzwa na wengine kutoka mikoa kadhaa nchini, “wamevamia Kilosa” na kupunguza uwezo wake wa kuhimili mifugo.

Anasema wilaya ina eneo la hekta 530,000 kwa kilimo na hekta 430,000 kwa kufuga na kwamba kwa eneo hilo la wafugaji, wilaya inahitaji ufugaji wa kisasa wa ng’ombe 150,000 tu (wastani wa ng’ombe watatu kwa kila hekta).

Hadi sasa halmashauri imefanikiwa kuondoa wilayani humo zaidi ya ng’ombe 18,000, anasema mkurugenzi na kusisitiza kuwa wasiokuwa wenyeji wa Kilosa “lazima waondoke.”

Kalimalwendo siyo mwenyeji wa Kilosa lakini tayari anamiliki ardhi ipatayo eka 10 katika kijiji cha Malangali ambamo wenye mifugo wametimuliwa na inadaiwa ardhi itamilikishwa kwa wawekezaji kutoka nje ya nchi.

Kuhusu kwa nini mkurugenzi amiliki ardhi katika wilaya ambayo anadai ina ardhi haba, Kalimalwendo anang’aka, “Hilo haliwahusu. Haliwahusu kabisa. Yaani mtu kununua eka 10 tu…nasema haliwahusu.”

Hivi sasa Kilosa ni kilio na kusaga meno kwa wenye mifugo. Mifugo inakamatwa. Kama mfugaji hana fedha za kuigomboa, inauzwa kwa “bei ya bure.”

Kwa mfano, ng’ombe ameuzwa kwa Sh. 120,000 hata 80,000 badala ya Sh. 450,000 au 500,000 na wanunuzi wanakuwa tayari wameandaliwa na madalali.

“Wanatuvamia. Wanaamuru twende Lindi au tuuze mifugo papo hapo huku tumeshikiwa bunduki. Huu siyo ubinadamu,” anaeleza mkulima wa Mabwegere.

Utaratibu wa serikali wilayani umezaa ubaguzi, unyanyapaa kwa wafugaji na hasa Wamasai ambao wana mifugo mingi na umetoa mwanya kwa uporaji kwa kisingizio cha operesheni.

Kuna tatizo Kilosa. Panahitajika mpango mpana, wa kistaarabu, wa muda mrefu wa kugawa ardhi, kwa kushirikiana na mikoa mbalimbali ili wenye mifugo wapate maeneo ya kufugia na kulishia bila manyanyaso.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom