Wananchi wachoma kituo cha polisi, magari,

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,316
33,125
motomoto.jpg


VITENDO vya wananchi kuvamia vituo vya polisi kwa lengo la kuwaua watuhumiwa vinazidi kushika kasi nchini baada ya wananchi zaidi ya 300 kuvamia kituo cha polisi cha Hedaru na kukiteketeza kwa moto usiku wa kuamkia jana.

Mbali na wananchi hao kuchoma moto kituo hicho chenye askari wapatao 10 na kukiteketeza pamoja na majalada na vielelezo, kundi hilo pia lilichoma magari matatu ya watu binafsi yaliyokuwa yameegeshwa kituoni hapo.

Kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro, Lucas Ng’hoboko alisema jana kuwa chanzo cha tukio hilo ni wananchi hao kutaka kuwaua watu wanane waliokamatwa na polisi kwa tuhuma za kumteka mtoto aliyejulikana kwa jina la Grace Kelvin na kumtoa kafara kwenye machimbo ya madini yaliyo msitu wa Shengena.

Kamanda Ng’hoboko alisema wananchi hao wanaamini kuwa mtoto huyo anasoma shule ya chekechea ya Mt. Sovavi alitolewa kafara, lakini baadaye jana ilifahamika kuwa mtoto huyo alipatikana eneo la soko la Mbuyuni, Pasua ambako alikuwa peke yake na mama mmoja kutoa taarifa polisi.

Baada ya watu hao kuvamia kituo hicho, polisi walilazimika kuwaokoa watuhumiwa hao na wao wenyewe kutimua mbio kunusuru maisha yao kutokana na kituo hicho kutokuwa na silaha za moto kwa kuwa hakina ghala la silaha.

Kamanda Ng’hoboko alifafanua kuwa Mei 28, mtoto huyo alikwenda shuleni kama kawaida na alitarajiwa kurejea nyumbani saa 5:00 asubuhi, lakini, hakurejea na ndipo wazazi na ndugu wa mtoto huyo walipotoa taarifa polisi.

“Polisi walianzisha uchunguzi mara moja na watu wanane walikamatwa, lakini hawakuwa washukiwa hasa wa tukio hilo na waliachiwa kwa dhamana, huku polisi wakiendelea kukusanya taarifa za kiintelejensia,” alisema.

Mei 31 ilipokelewa taarifa kuwa mtoto huyo amepelekwa msitu wa Shengena kwa lengo la kutolewa kafara ili madini yatoke mengi zaidi. Habari hizo zilidai kuwa mtoto huyo alipelekwa kwenye msitu huo na watu wanane, akiwemo mwanamke mmoja.

“Sungusungu walijikusanya na kwenda kwenye machimbo na kuwakamata watu wanane na mwanamke mmoja na kuwakabidhi kituo cha polisi cha Hedaru wakiwatuhumu kuhusika katika utekaji wa mtoto huyo,” alisema Ng’hoboko.

Kamanda Ng’hoboko alifafanua kuwa baada ya taarifa kuzagaa kwamba waliomteka mtoto huyo wamekamatwa na kuhifadhiwa kituoni hapo, wananchi walianza kuhamasishana ili wavamie kituo na kuwaua watuhumiwa hao.

“Kwa hiyo kwenye usiku wa saa 4:00 hivi, kundi la zaidi ya watu 300 lilifunga barabara kuu ya Same-Dar kwa mawe na mipira ya magari na kadri hamasa ilivyozidi ndivyo watu hao walipopanda mori wa kuvamia kituo hicho na ndipo walipovamia kituo na kukichoma,” alisema.

Ng’hoboko alisema polisi inawashikilia watu wanane kuhusiana na tukio la kuchoma kituo hicho na polisi wameanzisha msako mkali kwa kutumia polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia(FFU), kuwatafuta watuhumiwa wengine wa tukio hilo.

Hata hivyo, zipo taarifa nyingine zinazodai kuwa hasira ya wananchi hao ilichangiwa na polisi wa kituo hicho kutoonyesha umakini katika kufuatilia tukio hilo, hadi wananchi wenyewe walipoamua kuwasaka watuhumiwa hao.

Mtendaji wa Kata ya Hedaru, Charles Karia alikanusha madai ya polisi kuzembea kushughulikia tuhuma hizo akisema kuwa wakati wananchi wanachukua uamuzi wa kuchoma kituo cha polisi na magari, tayari washukiwa saba walikuwa wameshakamatwa.

Tukio la kutekwa nyara kwa mtoto huyo ni la pili ndani ya kipindi cha mwezi mmoja baada ya mtoto mwingine wa mwenye umri wa miaka nane, Faraj Haruna kutekwa nyara na kusafirishwa hadi nchini Uganda .

Mtoto huyo alipatikana nchini Uganda baada ya wazazi wa mtoto huyo kuwalipa dola 400 za Kimarekani (sawa na Sh560,000 za Kitanzania) watu waliomteka.

Baba mzazi wa mtoto huyo, Haruna Ayoub alilitupia lawama Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro kuwa halikuonyesha kujali na kuchukua hatua madhubuti hadi wazazi na wakazi wa Moshi walipoungana kuchanga fedha hizo.

Fedha hizo ziliwekwa kwenye akaunti iliyo benki ya Stanbic la Busia mpakani mwa Kenya na Uganda kwa jina la Kaaya Sarali na ndipo walipoelekezwa mahali watakapompata mtoto huyo.

Jijini Dar es salaam, Hussein Kauli anaripoti kuwa mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Said Mwema amesema watu watano wamekamatwa wakihusishwa na uchomaji moto kituo hicho cha polisi Hedaru.

IGP Mwema alisema awali Mei 28 mwaka huu alipotea katika mazingira ya kutatanisha na kudaiwa kuwa alitolewa kafara kwenye kijiji cha Chome Mlimani yalipo machimbo.

Alisema Mei 30 baada ya mkuu wa kituo hicho kufuatilia tukio hilo, aliwakamata watuhumiwa sita kwa mahojiano zaidi, na kuongeza kuwa ilipofika Mei 31, vijana waliamua kumtafuta mtoto huyo baada ya kupata uvumi kuwa alitolewa kafara.

"Hata hivyo vijana hawa hawakufanikiwa kumpata mtoto huyo, lakini baadaye waliwakamata watu wanane waliokutwa na vifaa vya kuchimbia madini ya dhahabu kwenye mgodi usio rasmi," alisema IGP Mwema.

Alisema watu hao walifikishwa kwenye kituo kidogo cha pilisi cha Hedaru wakisubiri kupelekwa Same kwa mahojiano, na ilipofika saa 2:00 usiku wananchi wapatao 300 walivamia kituo hicho na kukichoma moto.

IGP Mwema alisema kuwa mtoto Grace aliokotwa jana sokoni eneo la Pasua na alipelekwa kuungana na familia yake.

Akizungumzia ongezeko la vitendo vya wananchi kuvamia vituo vya polisi, IGP Mwama alisema kuna haja kwa jamii kupewa elimu ya urai ili kuepusha watu kuchukua sheria mikononi kutokana na sababu mbalimbali.

"Watu wamechukua hatua ya kuchoma kituo cha polisi kwa imani za kishirikina, halafu mtoto ameonekana... ni hasara kupoteza chombo kinachotoa usalama kwa wananchi," alisema IGP Mwema.

Alisema kwa sasa jeshi hilo kwa kushirikiana na wilaya hiyo wataweka utaratibu wa kuhakikisha huduma ya kipolisi kwa wananchi inatolewa katika kipindi hiki cha kukosekana kwa kituo cha polisi katika eneo hilo.

IGP Mwema pia alitangaza kutovifunga vituo vidogo vya polisi visivyokuwa na zana na askari wa kutosha kama alivyotangaza msimamo huo siku chache zilizopita.

Wananchi wachoma kituo cha polisi, magari,

Hapo Kwetu Bongo Kuna Serikali Jamani?
 
Back
Top Bottom