Wananchi ndio wenye kuamua kuhusu katiba - shivji

abdulahsaf

JF-Expert Member
Aug 31, 2010
858
130




Wazanzibari watakiwa kutodharau mchakato


Na Juma Khamis


WAKATI asasi za kiraia zilizopo Zanzibar nazo zikiungana na za Tanzania Bara katika mijadala ya katiba mpya, Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Issa Shivji ameelezea hofu yake kwamba mchakato wa kupata katiba mpya ya wananchi huenda ukatekwa na wanasiasa.


Akitoa mada “Kwa nini Tunahitaji Katiba mpya Tanzania” katika mjadala wa wazi uliofanyika ukumbi wa Eacrotanal, Profesa Shivji alisema ipo haja kwa jumuiya za kiraia na wananchi wenyewe kushiriki moja kwa moja katika mijadala na kupata mwafaka wa katiba inayozingatia maslahi, utamaduni na silka zao.


Alisema dhana kwamba katiba ni mkataba kati ya viongozi (watawala) na watawaliwa (wananchi) imepitwa na wakati kwa sababu ni wananchi ndio wanaopaswa kuwa na mamlaka ya kuamua jinsi wanavyotaka nchi yao iendeshwe, aina ya mifumo ya uchumi wanaotaka au idadi ya serikali wanazohitaji.


“Katiba zote mbili zinatambua serikali mbili lakini ukiangalia kwa undani utagundua kwamba kuna serikali mbili na nusu,” alisema Profesa Shivji.


Profesa Shivji alisema katiba zote mbili ile ya Tanzania ya mwaka 1979 na ya Zanzibar ya mwaka 1984, zote zimetungwa bila ya kushirikishwa wananchi kwa njia yoyote hivyo hapana budi kwa katiba mpya ijayo kuandikwa kutokana na matakwa ya wananchi wenyewe kwa kushirikishwa moja kwa moja.


Profesa Shivji ambae kwa sasa ni Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, alisema katiba inayowaridhisha wananchi ni ile inayotokana na wananchi wenyewe na wala sio kuamuliwa na kundi la watu wachache.


Kwa upande wake, Wakili maarufu wa Mahakama Kuu Zanzibar, Awadh Ali Said alitoa wito kwa wananchi wa Zanzibar kutodharau kushiriki katika mijadala kuhusu katiba waitakayo kwa sababu wao pia ni sehemu ya katiba hiyo hasa kwa vile wakati mwengine wanakuwa waathirika wa katiba hiyo.


Alisema yapo mambo ya msingi yanayojadiliwa na wananchi kwa sasa kama kuwepo kwa mgombea binafsi, haki ya kupinga matokeo ya urais kama ilivyo kwa matokeo ya ubunge pamoja na madaraka makubwa ya kikatiba aliyonayo rais.


Aidha alisema mijadala hiyo ni muhimu kwa Zanzibar, kwani wananchi watapata fursa ya kujadili muundo wa muungano na mambo gani yapunguzwe au yaongezwe kwenye muungano huo.


Akichangia mjadala huo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU) , Mohammed Dedes pamoja na mambo mengine alisema muda umefika kwa Zanzibar kudai kupewa nafasi kushiriki katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kama mwanachama kamili ili iweze kulinda maslahi yake kwa kuwa mambo yaliyokubaliwa kwenye ushirikiano wa Jumuiya hiyo,hayamo katika orodha ya mambo ya muungano wa Tanzania.


Mjadala huo muhimu kwa Zanzibar, utaendelea tena Machi 5, ambapo Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP) Othman Masoud Othman atawasilisha mada “Kuna Migongano kati ya Mapatano ya Muungano na Katiba ya Tanzania.


Machi 19, Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Ibrahim Mzee atawasilisha mada “Katiba ya Tanzania na Zanzibar, Changamoto juu ya mianya na utata uliopo.”


Mjadala huo wa wazi umeandaliwa na Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC), Jumuiya ya Wanasheria Zanzibar (ZLS), Taasisi ya Utafiti wa Bahari ya Hindi (ZIORI) na Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo (WAHAMAZA).
 
Back
Top Bottom