Wanafunzi UDSM, Ardhi hali ngumu

Msongoru

JF-Expert Member
Apr 16, 2008
306
24
na Sauli Giliard



WANAFUNZI wa mwaka wa kwanza katika vyuo vikuu vya Dar es Salaam na Ardhi, wanakabiliwa na maisha magumu kutokana na Bodi ya Mikopo kutoidhinisha majina yao huku wakitakiwa walipe kiasi cha fedha ili waweze kusajiliwa.

Tanzania Daima imeshuhudia wanafunzi hao ambao kati yao wametokea mikoani wakihangaika kwa lengo la kujua mustakabali wao huku wakilalamikia bodi hiyo, kwani kati yao majina bado hayajashughulikiwa na hawajui watapata mkopo kwa asilimia ngapi.

Jana asubuhi Tanzania Daima ilishuhudia wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ardhi wakiuhoji uongozi wa wanafunzi juu ya hatima ya maisha yao chuoni hapo huku wakitakiwa na utawala wa chuo hicho kutoa sh 450,000 bila kujali watapewa mkopo kwa asilimia ngapi.

Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa wanafunzi hao, Magesa Navigambo, alisema maisha yao hasa waliotoka mikoani ni magumu, jambo ambalo limechangiwa na Bodi ya Mikopo kuchelewa kuyashughulikia majina yao.

“Wengine hatujui majibu yetu ya mikopo yatakuwa vipi, maisha kwetu ni magumu hasa ukizingatia chuo nacho kinatutaka kulipa fedha,” alisema.

Naye Hans Mvungi kutoka mkoani Kilimanjaro, alisema kiwango cha fedha kinachohitajika chuoni hapo ni mzigo kwao na sasa hakai chuoni kwa sababu hana fedha ya kujikimu.

Hata hivyo, Waziri wa Taaluma wa chuo hicho, George Themistodes ameilaumu Bodi ya Mikopo kwa kutoshughulikia suala la mikopo mapema, kwani sasa ni wanafunzi 141 kati ya 678 ambao maombi yao yameshughulikiwa.

Kwa upande wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi (DARUSO), Ismael Emmanuel alisema tatizo la fedha za kujikimu kuchelewa limewaweka katika maisha magumu wanafunzi wa mwaka wa kwanza.

Alisema wanafunzi wengine bado majibu yao hawajapata kutoka Bodi ya Mikopo, jambo linalowafanya kuwa na wasiwasi kwani pamoja na kupata, suala la asilimia ngapi linawatatiza.

Hata hivyo, alibainisha uhaba wa vyumba vya kuishi chuoni hapo huenda ukachangia ugumu wa maisha, kwani chuo kina uwezo wa kuchukua wanafunzi 6,000 wakati wanafunzi waliopo ni 18,000.

Aliitaka Bodi ya Mikopo kutoa ushirikiano wake juu ya suala hilo na kutoyatupilia mbali malalamiko yao kwa kigezo kwamba ni ya uongo.

Mmoja wa wanafunzi wa mwaka wa kwanza ambaye hakutaka kutajwa jina, aliitaka bodi hiyo kuyashughulikia maombi yao mapema, kwani kuishi chuoni hapo bila kuwa na pesa kunahatarisha maisha yao.
 
Back
Top Bottom