Wanafunzi TEWW waandamana hadi kwa Waziri Mkuu

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
Wanafunzi wa mwaka wa tatu wa kozi ya Elimu ya Watu Wazima na Maendeleo ya Jamii kutoka Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima nchini (TEWW) ya jijini Dar es Salaam, jana waliandamana hadi katika Ofisi ya Waziri Mkuu wakiitaka serikali kuamua hatma yao.

Wanataka serikali iamue juu ya aina ya kiwango cha elimu watakachopata baada ya kuhitimu masomo yaliyoko katika ‘semista’ ya mwisho ya mwaka wa tatu wa masomo.

Akizungumza na NIPASHE jana, msemaji wa wanafunzi hao, Abdallah Juma, alisema waliamua kuandamana kwenda kwa Waziri Mkuu baada ya jitihada walizozifanya siku zilizopita, ikiwamo kuzungumza na uongozi wa chuo mara tatu, kutokutoa ufumbuzi wa madai yao.

“Tulianza kusoma pale TEWW katika mwaka wa masomo wa 2008/2009. Tulipoingia pale tulielezwa kuwa kozi ya stashahada ya juu ya elimu ya watu wazima na maendeleo ya jamii iliyokuwa ikitolewa kabla, imeondolewa na kwamba sisi tunaanza masomo, ambayo baada ya kuhitimu tutatunukiwa shahada,” alisema.

Alisema baadaye baraza la kutoa vibali vya kuendesha kozi za shahada kwa vyuo vya elimu ya juu nchini, lilitembelea chuo chao kuangalia mitaala inayofundishwa na kubariki chuo kianze kutoa shahada katika kozi zinazofundishwa pale.

Juma alisema hadi jana, walikuwa hawajaelezwa rasmi kama wanachosomea ni shahada au la pamoja na kumwandikia barua Waziri Mkuu Februari, mwaka huu kuomba asaidie kutatua tatizo lao la kujulishwa aina ya cheti watakachotunukiwa baada ya masomo.

Alisema wanataka wajulishwe kwa kuwa wanafunzi waliokuja nyuma yao (mwaka 2009/2010), waliingizwa moja kwa moja kwenye programu ya shahada na kwamba kwa sasa kozi ya stashahada haitolewi tena na chuo hicho.

Timu ya wanafunzi wanne wakiongozwa na Winfrid Wandete, iliundwa kutoka katika kundi la takriban wanafunzi 70 walioandamana kwenda kwa Waziri Mkuu.

Walionana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi kwa kuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, hakuwapo jijini.

Kwa mujibu wa kiongozi wa timu hiyo, Wandete, baada ya mazungumzo na Lukuvi, aliwaelekeza wakaonane kwanza na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa leo.

Awali, wanafunzi hao waliandamana kwa makundi makundi hadi katika lango la kuingilia Ofisi ya Waziri Mkuu, lakini walizuiwa na walinzi kuingia ndani ya eneo la ofisi hiyo.

Baadaye, Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), waliongezwa kuimarisha ulinzi kabla ya timu hiyo ya wanafunzi wanne kuruhusiwa kuingia ndani kwenda kuonana na Waziri Lukuvi.
 
Back
Top Bottom