Wana Nyerere na Amin kukutana Butiama

Limbukeni

Senior Member
Feb 27, 2009
117
1
BBCSwahili.com | Habari | Wana Nyerere na Amin kukutana Butiama

Kuanzia Alhamisi ya tarehe 9 mwezi Aprili, Idhaa ya Kiswahili ya BBC inatarajiwa kukuletea taarifa za kihistoria kwa kuwakutanisha watoto wa viongozi wa nchi mbili za Afrika Mashariki ambao uhasama wao ulishuhudia vita kali mwishoni mwa miaka ya sabini - vita vya Kagera.
Katika tukio la kipekee litakalosimamiwa na Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Jaffer Remo Amin, mwana wa kiume wa Idi Amin aliyekuwa rais wa Uganda, na Madaraka Nyerere, mwana wa kiume wa Mwalimu Julius Nyerere “Baba wa Taifa”, wamekubaliana kukutana kwa mara ya kwanza kabisa.

Ifikapo tarehe 10 Aprili, itakuwa imetimia miaka 30 tangu kung’olewa madarakani kwa Idi Amin wa Uganda, kutokana na mapambano makali, majeshi ya Tanzania chini ya rais wa wakati huo Mwalimu Julius Nyerere yakikamilisha kazi hiyo.

Uhusiano baina ya viongozi hao haukuwa mzuri kwa muda, mnamo Oktoba 1978 hali ilizidi kuwa mbaya wakati Idi Amin alipoishambulia Tanzania na kujitangazia kuumega mkoa wa Kagera ulioko kaskazini-magharibi mwa Tanzania.

Hatimaye, kiongozi huyo wa Uganda alilazimika kukimbilia uhamishoni, kwanza alienda Libya na baadaye Saudi Arabia ambako aliaga dunia Agosti 2003.

Matangazo
Kuanzia Jumatatu ya tarehe 6 mwezi April, katika maandalizi ya mwaka 30, matangazo ya Amka na BBC yanayosikika saa kumi na mbili alfajiri na Dira ya Dunia kumi na mbili na nusu jioni, yatakumbushia historia ya matukio ya miongo mitatu iliyopita, kwa kuzungumza na wakongwe waliopigana na watu walioathirika kuelezea wanayoyakumbuka kuhusu vita vya mwaka 1979 kati ya Uganda na Tanzania.
Jaffar Amin atasafiri kutoka Arua kwenda Butiama kukutana na Madaraka Nyerere.



BBC itawashirikisha wachambuzi hodari wa maswala ya kisiasa kutathmini athari zilizotokana na vita hivyo kwa nchi za Afrika Mashariki na bara zima la Afrika. Mada muhimu kwa muda wote wa matangazo yetu itakuwa kukutana kwa wana wa viongozi hao wawili, waliotawala katika siasa za eneo hilo.

Katika matangazo yetu, tutaanza Jumatatu ya tarehe 6 Aprili, kwa kuambatana na Jaffer Remo Amin kwenye msafara wake kutoka nyumbani kwake Arua kaskazini-magharibi mwa Uganda kwenye Butiama kaskazini-magharibi mwa Tanzania kuzuru alikozikwa Mwalimu Julius Nyerere.

Arua mpaka Butiama
Kila hatua ya safari ya Jaffer, mwenye umri wa miaka 42, itanaswa na mwandishi Idd Seif wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC atakayesafiri naye mpaka kwenye makutano.

Na Butiama kwenyewe, waandishi wengine wa BBC, Vicky Ntetema na Charles Hilary watakuwa wakifuatilia maandalizi ya Madaraka Nyerere, mwenye umri wa miaka 48, kabla ya mkutano wake na Jaffer Remo Amin.

Kwa kipindi chote cha msafara wa Amin kuelekea Butiama, BBC itarusha taarifa kuhusu mwitikio wa wananchi wakizungumzia mkutano huo wa watoto wa viongozi wa pande zilizokuwa zikihasimiana.

Mratibu wa mpango huo, Caroline Karobia, tayari amekuwa akifanya mahojiano na watu waliokuwepo nyakati hizo za miaka ya sabini.

Anasema: "Haijawahi kutokea Afrika Mashariki, kabla au baada kuona mapambano makali kama yale kwa majeshi ya nchi mbili, na miaka 30 baadaye kumbukumbu bado ni dhahiri miongoni mwa watu walioshuhudia vita. Idhaa ya Kiswahili ya BBC itarekodi kumbu kumbu hizi na pia kualika wasikilizaji wetu kutupia macho yatakayofuata siku za usoni."

Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Solomon Mugera, anaongeza: "Idi Amin and Julius Nyerere walikuwa maadui wakubwa. Tofauti zao ziligubika siasa za eneo zima kwa kipindi chote cha miaka ya sabini. Uongozi wao ulikuwa na athari kubwa kwa raia wao, na hiba isiyosahaulika.

Katika kuchambua athari za vita kwa Tanzania, Uganda na eneo zima la Afrika Mashariki, Idhaa ya Kiswahili ya BBC imeratibu mkutano wa wana wa kiume wa mahasimu hao wawili. Tunatarajia kunasa kila lililo muhimu katika safari yao ya kihistoria."
 
Back
Top Bottom