Nawaombeni ndg. zangu ni vema tukafahamu kama tuko njia sahihi. Awali nilishauri tusilaumu bali tupange na tuweke mikakati. Nashauri tena twaweza kuanza na kutambuana ni nani na wa wapi (kijiji/kata/wilaya) na unaishi wapi. Baada ya hapo tuweke mikakati ya kikanda/vijiji, kata/wilaya. Hatua hii itatutoa. Ukweli tunatakiwa kuunganisha nguvu. Hakuna ubishi hapo. Mimi ninaanza hivi: Ninatokea kijiji cha IGURUGATI, kata ya BUGANDIKA, wilaya ya MISSSENYI. Katika eneo ninalotoka kuanzia kijijini hadi wilayani changamoto ni zile zile; ugonjwa wa mnyauko wa migomba, kuporomoka kwa kiwango cha elimu, kuongezeka kwa idadi ya yatima, kushuka kwa uzalishaji wa kahawa, uwekezaji mdogo unaotokana na sisi wenyewe kutokurejea mara kwa mara nyumbani n.k. Hata hivyo, wilaya hii (vijiji na kata zake) zina miundo mbinu mizuri mfano barabara, umeme, mahospitali/vituo/zahanati na baadhi ya shule. Ninaamini sisi tunaweza kupambana na umasikini pamoja na kushuka kwa elimu katika wilaya ya Missenyi kama tutakuwa tayari kujitoa na kujitolea. Lazima tuchangie maendeleo ya watu wetu kama tunavyochangia ya wengine, mahali pengine kwenye ujenzi wa mashule, barabara, makanisa, shughuli za harusi n.k. Tunao uwezo wa kuchangia kuinua elimu angalau ya msingi na sekondari, tunao uwezo wa kusomesha yatima siyo lazima wawe ndugu wa kuzaliwa nao. Ebu tuanze. Nimeona mchangiaji mmoja anaelezea kuanzisha SACCOS. Naamini hii siyo njia mbadala ya kutatua matatizo yanayotukabili. Kwetu sisi hii siyo bali tunatakiwa kuwahimiza watu wetu kule Kagera waanzishe SACCOS na VICCOBA, tuwasaidie waanzishe hizo SACCOS. Pia, wengi wetu tumeanzisha na kujiunga kwenye vyama vya kufa na kuzikana. Sawa. Ebu tuwe na agenda endelevu. Tunatakiwa tushirikiane na watu wetu kuanzisha NGOs/CBOs zenye kulenga kuchochea maendeleo ya watu wetu na zifanyie kazi huku huko Kagera. Nawaombeni wana Kagera, wana Missenyi na wana Bugandika tuungane, tujitolee na tuchangie maendeleo ya Kagera. Asanteni