Wameacha kanuni na kubariki mafisadi

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,006
Wameacha kanuni na kubariki mafisadi

Lula wa Ndali-Mwananzela Julai 23, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

TULIOWAAMINI na kuwapa nchi waiongoze ndio hawa ambao leo wanatugeuka. Tuliowapa ulinzi wa taifa letu ndio hawa ambao hawajui waseme nini wanapoulizwa kama Zanzibar ni nchi au si nchi!

Hawa tuliowaweka kwenye kilele cha uongozi wa taifa letu ndiyo hawa wamekunjua kucha zao zilizochongwa, na wanatuparura wapendavyo. Ndiyo! Hawa tuliowapigia makofi walipotangazwa washindi ndiyo hawa ambao wameziacha kanuni, wamebariki ufisadi, na utu wetu wameutupa.

Wameziacha kanuni. Taifa letu lilipozaliwa ukilinganisha na mataifa mengi ya kiafrika, la kwetu lilizaliwa likiwa na kanuni. Na ninapozungumzia taifa letu nazungumzia Tanganyika na Zanzibar. Ni kanuni hizo ambazo zilitufanya tuone fahari kuwa Watanzania; na ni kanuni hizo ambazo leo hii Mtanzania kijana ukimuuliza sijui wangapi wanazikumbuka tena.

Zipo kanuni nyingi tulizozikumbatia wakati wa kuzaliwa kwa jamhuri yetu. Sasa sitawatungia msije mkadai Lula ametunga kanuni hizo. Nitawakumbusha. Katika hotuba yake mwaka mmoja baada ya Uhuru (Desemba 10, 1962) na siku moja baada ya kuwa Jamhuri, Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, akizungumza kama Rais wa Kwanza wa Tanganyika pale Uwanja wa Taifa alisema hivi kuhusu kanuni ya kwanza kabisa ya ujenzi wa taifa letu:

"Kanuni ambayo tuliisimamia wakati ule (kutafuta uhuru) na ambayo tunaisimamia leo hii ni kanuni ya haki za binadamu. Tulipotafuta uhuru tulidhamiria nchi ambapo raia wake wote wako sawa; ambapo hakuna matabaka ya watawala na watawaliwa, matajiri na maskini, wasomi na wasiosoma, wenye taabu na wanaoishi kwenye anasa tupu.

Tulidhamiria kujenga taifa ambao wote watakuwa sawa katika utu wao, wote watapata heshima sawa, watapata nafasi sawa ya elimu na mahitaji ya maisha, na raia wake wote watakuwa na nafasi sawa ya kuitumikia nchi yao mpaka mwisho wa kikomo chao."

Ndugu zangu, miaka karibu hamsini baadaye, ni kwa kiasi gani tumekaribia na kuendelea kushikilia kanuni hiyo? Hivi leo hii Watanzania wanajiona wako sawa kwa utu, nafasi, au heshima?

Je leo ni kwa kiasi gani tunajiona tuna nafasi sawa ya kufanikiwa katika nchi yetu? Je wewe msomaji unafikiri una nafasi sawa ya kufanikiwa licha ya jitihada zako zote kwa kutumia njia halali au na wewe lazima ugeuke fisadi mdogo ili ufanikiwe?

Hata tulipoungana, haikuwa kuungana toka hewani tu. Tuliongozwa na kanuni. Wakati Mwalimu Nyerere anazungumza bungeni kuleta pendekezo la Muungano katika kikao maalum tarehe ile ya Aprili 25, 1964 Baba wa Taifa alisema hivi kuhusu kanuni kubwa ya Muungano wetu:

"Muungano huu hautakosa matatizo yake; kuna wale ambao wataona katika maendeleo haya ishara kuwa Afrika itaungana na wao watafanya kila njia kuvuruga muungano wetu, kupanda mbegu za mashaka, na kusababisha kutoridhika. Ni lazima tuwe macho na watu hawa. Kwani pindi muungano huu tukiingia ni jukumu letu kuulinda na kuudumisha".

Je ni kwa kiasi gani watawala wetu wamedumisha kanuni hii? Leo hii bado tunahangaika na mambo ya uchaguzi wa 1995 hadi ule wa 2005. Leo hii Muungano wetu siyo tu unatiliwa shaka, lakini sisi wenyewe yaelekea hatujui ulimaanisha nini kiasi kwamba tunalazimika kuwaita wanasheria wakuu kujadiliana maana ya neno nchi!

Wamebariki ufisadi.

Ijumaa ya wiki iliyopita makachero wa polisi walivamia ofisi za MwanaHalisi kumpekua mhariri wake na kwenda kupekua hadi nyumbani kwake kwa kusingizia kutafuta "nyaraka za kibenki" ambazo alidaiwa kuwa nazo. Hawakuwa na ushahidi isipokuwa walikuwa na tuhuma na kutokana na tuhuma hizo walienda mahakamani, kupata kibali ili waende kukagua.

Walifanya kile ambacho watu wanatarajia vyombo vya usalama kufanya kunapotokea tuhuma nzito. Hawakumuita mhariri na kukaa naye mezani kunywa naye chai na kumuuliza kirafiki juu ya akaunti hizo? Waliamua kumshtukiza ili asipate nafasi ya kuharibu ushahidi.

Cha kushangaza na kuudhi ni kuwa watu hawa hawa wa usalama wamepewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano tuhuma; kuwa kuna makampuni 22 ambayo yamekwapua siyo majina ya akaunti za watu, bali wamekwapua fedha za mabilioni ya Shilingi toka Benki Kuu.

Tena wameambiwa siyo tuhuma tu bali hadi makampuni yalitajwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Bw. Philemon Luhanjo. Na siyo hivyo tu, Rais mwenyewe alithibitisha kuwa kilichofanyika ni uhalifu na akaagiza hatua zichukuliwe mara moja na yote yafanyike ndani ya miezi sita.

Walichofanya vyombo vya usalama siyo siku ya pili kwenda kuyashtukiza hayo makampuni; Hawakwenda muda ule ule Luhanjo anatangaza kuanza kuwapekua wamiliki wa makampuni hayo na watu wanayohusiana nayo ili wasiharibu ushahidi. Hapana, walichofanya wao ni kuunda kamati, kukaa chini na mafisadi, kujadiliana nao, na kuwabembeleza waturudishie fedha zetu. Zaidi ya yote hata kutaja majina yao hawataki kutaja kwa vile ni watuhumiwa tu!

Yaani anayedaiwa kukutwa na namba za akaunti (siyo fedha zao!) anavamiwa na makachero wa polisi na aliyechota fedha mbele ya Jeshi la Polisi na Usalama wa Taifa na kuziweka kwenye akaunti yake, anaandaliwa chai na ripoti ya uchunguzi!

Yaani kwa mhariri mdogo tu wamekimbia kwenda mahakamani na kupata warranty ya kuchunguza hadi chumbani kwake, lakini kwa kina Kagoda Agriculture Limited na ‘dada zake', wanatuambia "uchunguzi unaendelea, mtajulishwa".

Kama huku siyo kubariki ufisadi ni nini basi? Hivi kati ya anayedaiwa kukutwa na namba za akaunti na ambaye amewaambia watu akaunti hizo zimeficha nini, na yule aliyechukua fedha hizo za umma na kuzificha kwenye akaunti hizo, ni nani mhalifu wa kweli? Labda IGP Mwema ana majibu ya maswali haya.

Yaelekea mafisadi wameshinda kwani baraka wamepewa hadi na mahakama! Tukubali kwamba mafisadi wameiteka nchi. Washukuru tu kwamba hii ni Tanzania ambako mafisadi wanabarikiwa na kuchangamkiwa wakati wafichua ufisadi wanalaaniwa na kupekuliwa!

Utu wetu wameutupa:

Ndiyo, tulikuwa na utu sisi. Tuliheshimiwa na kujiheshimu. Tulipoongozwa na ile kanuni ya usawa na utu wa watu tulijijua sisi ni nani. Tulipopinga utawala wa kibaguzi wa Ian Smith kule Rhodesia na ule wa Wareno kule Msumbiji, tuliongozwa na kanuni ya utu wa Mwafrika.

Tulipopinga utawala wa kibaguzi wa Makaburu wa Afrika Kusini na kuungana na watu wa ANC, tuliongozwa na kanuni kuwa na sisi ni binadamu na hatuko tayari kuona tunadharauliwa, kunyanyaswa na kubaguliwa kwa sababu ya rangi yetu au nasaba yetu.

Siku chache zilizopita, Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Umoja wa Mataifa alitangaza mashitaka kadhaa dhidi ya Rais wa Sudan, Omar Bashir. Mashitaka hayo yalihusu makosa ya kivita, makosa ya mauaji ya halaiki, na makosa dhidi ya binadamu. Ukisoma mashitaka hayo (unaweza kuyapata kwenye http://www.klhnews.com) utaona kuwa ni mashtaka mazito kabisa.

Cha kushangaza ni kuwa Serikali ya Tanzania kwa haraka yake ikakimbilia kumtetea Bashir na kutaka Mahakama ya Uhalifu ya Dunia kusubiri kidogo! Tena siyo kusubiri tu; bali wasiendelee na mpango wa kumkamata Rais Bashir na kumfanya ajibu mashtaka! Hii ndugu zangu ni Tanzania ya Mwalimu Nyerere?

Yaani watu wale wale waliomlaani Mugabe na kutaka kumtenga kutoka AU ambako nchini mwake hadi sasa idadi ya waliokufa kutokana na mgogoro huo wa sasa haijafikia watu 200 na maneno makali yakatumika dhidi yake, watu hao hao wanamkumbatia mtuhumiwa uuaji na makosa ya kivita (Rais Bashiri) ambaye chini yake huko Darfur peke yake watu karibu laki tatu wamekufa kutokana na mgogoro huo!

Yaani leo hii Tanzania iliyokuwa inaheshimu utu wa Mwafrika inakubali Mwafrika mwingine amdhalilishe na kumtesa Mwafrika mwingine kwa kisingizio cha "Ni Rais aliyeko madarakani". Hivi ni nani kawaambia kuwa mtu akiwa Rais basi ana haki ya kutawala apendavyo?

Binafsi, naamini hatua ya Mwanasheria Mkuu huyo imekuja wakati muafaka ikituma ujumbe kwa viongozi wote ambao wamejifanya waamini kuwa wao ni miungu watu, kuwa haijalishi uko madarakani au la utajibu kwa vitendo vyako.

Jambo hili ni zuri hasa kwa nchi kama ya kwetu ambapo katiba inamlinda Rais kuwa akifanya vitendo vya jinai hawezi kushtakiwa. Ndio maana mtu kama Mkapa aliweza kuamuru risasi zirindime kule Pemba mwaka 2001 na kuua ndugu zetu.

Na kwa kadri siku zinavyokwenda, sitoshangaa siku moja mtawala mwingine naye atajaribu kutumia nguvu ya risasi inukayo moto kuzima mijadala huru. Masikini Tanzania, tumekubali kuchagua upande wa wenye kutesa na kuukana upande wa wenye haki. Tumepotea wapi?

Hivi kama serikali ya Sudan ingekuwa ni ya Makaburu na tungesikia kuwa mahakama hiyo imetoa waranti ya kumkamata Rais wa kikaburu anayefanya yanayotokea Darfur, tusingeshangilia? Hivi kama tungesikia wakati ule wa mauaji ya Sharpeville na Soweto kuwa wahusika wamekamatwa mara moja tusingeruka ruka sisi? Iweje leo serikali yetu inamtetea Rais Bashir na imeshindwa kusimama kuwatetea wananchi masikini wa Darfur?

Yaani tumeuza utu wetu kwa mafuta na ushirika wa kinafiki? Ndugu zangu, hatutafika mbali kwani ushirika wenye mashaka kama wa kwetu kiungo chake si kanuni nzuri bali woga. Tanzania badala ya kusimama na kina Bashir tusimame na wananchi wa Darfur.

Leo nashangazwa na wale waliokuwa wanaandamana kupinga ujio wa Rais George W. Bush kwa vile anaua watu wa Irak na Afghanistan, lakini leo hakuna hata mmoja wao anayeandamana kumpinga Bashir na mauaji yanayofanywa mbele yake huko Darfur!

Inashangaza wale waliosimama na kuchoma bendera ya Marekani wakijifanya ni watetezi wa "haki za binadamu" kumbe wao wanatetea binadamu wa Irak na Afghanistan tu, lakini wale ‘binadamu nusu' wa Darfur hakuna anayesimama kuchoma moto bendera ya Sudan au kuandamana kuunga mkono hatua ya Mahakama ya Kimataifa.

Wanafiki, watoto wa wanafiki na uzao wa wanafiki; iweje mwanadamu wa Irak na Afghanistan awe na utu zaidi wa kulazimika kuandamana, lakini wa Darfur hana?

Ndugu zangu, sisi kama taifa hatuna budi kurudi kwenye misingi yetu kama taifa. Ni lazima turudi kwenye kuukataa ufisadi, na kwa hakika ni lazima turudi kwenye kuuinua utu wetu kama Waafrika na kuwapinga viongozi wote wanaotawala bila kujali.

Niandikie: lulawanzela@yahoo.co.uk
 
Back
Top Bottom