Wakili: Mbowe, Slaa, wabunge wamefunguliwa kesi ya kufikirika

Dingswayo

JF-Expert Member
May 26, 2009
4,019
2,923
Wakili wa utetezi katika kesi inayowakabili viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amewashauri polisi kwenda shuleni ili kusomea sheria kwa ajili ya kuepuka kesi za kufikirika kuzipeleka mahakamani na kusababisha kukwama kwa kazi za maendeleo kwa sababu ya kushughulikia kesi hizo.

Aidha, amesema polisi hawana mamlaka ya kuzuia maandamano au mikusanyiko, isipokuwa ni hakimu pekee ndiye mwenye mamlaka ya kuzuia maandamano au kama hakimu imethibitika hayupo anaruhusiwa Kamanda wa Jeshi la Polisi wa mkoa kuzuia maandamano hayo kwa kupewa maagizo na hakimu.


Wakili huyo, Method Kimomogolo, alidai hayo jana alipokuwa akitoa mapingamizi yake dhidi ya maelezo ya mashitaka yaliofunguliwa mahakamani hapo dhidi ya wateja wake ya kufanya maandamano bila kibali na kutoa lugha za uchochezi. Kimomogolo alisema kuwa mapingamizi yake yanahusu mashitaka nane yanayowakabili washitakiwa wake 19, wakiwemo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe; Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa; wabunge, viongozi wa ngazi mbalimbali na wafuasi wa chama hicho. Wabunge hao ni Godbless lema (Arusha Mjini), Joseph Selasini (Rombo) na Philemon Ndesamburo (Moshi Mjini).


Kimomogolo aliwasilisha taarifa yake kwa maandishi kwa ajili ya kuipatia mahakama kumbukumbu na pia alitoa maelezo ya mdomo ili mahakama iweze kuyasikiliza.


“Naanza kwa kusema kuwa hizi sheria lazima kila mmoja azipitie na kuzielewa, kesi hii imekosewa kuanzia mwanzo hadi mwisho na kwa kuwa imekosewa kuanzia mwanzo, imezaa makosa mengine yote,” alidai.


Alidai kuwa katika shitaka la kwanza, washitakiwa hao wanashitakiwa kwa kutenda makosa sita tofauti, wakati kisheria yalipaswa kuwa katika chaji sita tofauti yakiwa na maelezo ya kina, lakini hakuna kitu kama hicho.


”Mfano, hapa inasema Chadema na washitakiwa walitoa taarifa kwa OCD Arusha saa zaidi ya 100 kabla ya mandamano waliyokusudia kufanya hapo Januari 5, 2011 na iliandikwa barua ya mombi hayo Desemba 31, mwaka jana 2010,” alidai Kimomogolo.

Alidai kuwa kosa hilo halipo kisheria kwa sababu maelezo hayo yanakiri kuwa taarifa ilitolewa saa 100 ambao ni muda unaotakiwa, hivyo maelezo ya kosa yanapishana yenyewe.

”Shitaka la pili linawakabili washitakiwa 18 isipokuwa mshitakiwa wa 19, Samson Mwigamba, ambalo wanashitakiwa kutotii amri halali ya polisi. Hapo pia hakuna sababu iliyoelezwa wala haikutajwa amri hiyo ni ipi waliyokataa kuitii, wakati sheria ya polisi kifungu 42, kifungu kidogo cha kwanza kinaeleza ni lazima amri inapotolewa imtaje aliyetoa order hiyo, kwa hapo haikutaja mtu aliyetoa amri hiyo,” alidai na kuongeza:


”Hapa alitakiwa kutajwa kama ni Polisi ni yupi na mwenye cheo gani, ingawa tunafahamu sheria inamtaka hakimu ndiye atoe tangazo la kuzuia maandamano na akishindwa basi RPC, baada ya kupewa kibali maalum na hakimu, na tukio hilo lilifanyika jirani na mahakama, hivyo hakukuwa na haja maagizo ya sheria kukiukwa kwa kutolewa amri hiyo na polisi wa kawaida.”


Aliendelea kudai kuwa kutokana na amri hiyo kutolewa na polisi wa vyeo vya chini wasiojulikana kisheria, hivyo kosa hilo halipo na limekufa na limepelekwa mahakamani hapo kwa kufikirika tu. Katika kosa la tatu, ambalo wanashitakiwa kufanya mkusanyiko usio halali, alidai kuwa kosa hilo halipo kisheria kwa sababu kwa mujibu wa Sheria ya Polisi kifungu cha 74 na 75 vya Kanuni ya Adhabu, kifungu cha 45 kinataka waseme walikusanyika eneo gani, lakini haikusema wapi, na walikuwa na lengo gani na kuongeza kuwa nalo ni la kufikirika tu.


”Hapa wanadai maelezo ya kosa kuwa washitakiwa walikusanyika zaidi ya watatu katika Hoteli ya Mount Meru na hawakusema walikuwa eneo gani na amri ya kuwataka kutawanyika ilitolewa na nani? Hapa pia kosa halipo,” alidai.

Kimomogolo alidai polisi hawana mamlaka ya kuzuia maandamano wala kuzuia mkusanyiko, isipokuwa kazi yao ni kulinda amani na kuhakikisha hawasababishi madhara makubwa katika mkusanyiko.

”Hapa sheria inasema Polisi kama wataalamu, walipaswa kutumia utaalamu wao kutumia busara ya kuruhusu mandamano ili yaende yalikopangwa, lakini pale walipotumia nguvu ya kuzuia kwa mabomu ya machozi na hapo walisababisha madhara makubwa, wakati wangetumia busara madhara yasingetokea,” alidai Kimomogolo.


Shitaka la nne nalo alilipinga kuwa halina nguvu za kisheria kwa sababu linawahusu washitakiwa 18 kutotii amri halali ya Polisi ya kuwataka kutawanyika, kwa kudai kuwa polisi hawakupaswa kuzuia maandamano hayo na kama ilibidi kufanya hivyo, angeenda ofisa wa polisi na kuzuia, tena kwa kupata ruhusa ya hakimu. Baada ya Kimomogolo kudai hivyo, hakimu nayesikiliza kesi hiyo, Charles Magesa, aliingilia kati na kusema kuwa mahakimu wapo wachache ambao hawazidi 11, halafu akacheka akamruhusu Kimomogolo kuendelea.


Kuhusu shitaka la sita na la tano yanayowakabili Dk. Slaa na Ndesamburo, alidai kuwa pia limekosewa kisheria. Alidai shitaka hilo la kutoa lugha za uchochezi, sheria inataka itaje maneno hayo na kutajwa jamii iliyokwazika. “Hapo hakuna kitu kama hicho, hivyo nalo ni batili,” alidai. Alidai kuwa sheria hiyo ya mwaka 1955 ilitungwa kwa ajili ya kuzuia wakoloni wasilete chokochoko za kisiasa wakati huo, lakini siyo sahihi kuitumia katika kosa hilo ambalo kimsingi, alidai ni la kufikirika.


Katika shitaka la saba linalowakabili Ndesamburo, Dk. Slaa na Samson Mwigamba kwamba waliwachochea watu waliokusanyika eneo la viwanja vya NMC Januari 5, 2011 na kuwafanya watende kosa, alidai kuwa hapo napo hayakutajwa maneno hayo ya uchochezi hivyo kosa hilo kisheria limekosewa.


Kuhusu shitaka la nane la washitakiwa wote 19 kukataa amri ya kutawanyika, Kimomogolo alidai kuwa kosa hilo kisheria halipo pia kwa sababu penye mkusanyiko wa watu wengi usitegemee kutoa amri ya kutawanyika halafu watu wakatawanyika kama barafu, ni lazima waongozane.


Kimomogolo alisema kuna mikusanyiko miwili kisheria inaruhusiwa na kutambulika kama kusanyiko la kwanza la michezo, watu wa dini na jamii linaruhusiwa na halihitaji kibali cha polisi, lakini kusanyiko la pili la watu wa kisiasa na wengine wanahitaji kutoa taarifa polisi na hapo kama polisi hawatoridhika, pia hawaruhusiwi kusimamisha tu kienyeji, bali kwa utaratibu wa sheria ni hakimu au RPC aliyepewa kibali na hakimu.


”Mheshimiwa Hakimu, naomba uyafutilie mbali makosa haya baada ya kupitia sheria, sababu tukiendelea hivi kila kukicha kesi, kesi, kazi hazitaendelea na maendeleo hayatakuja kwa mtindo huu wa kesi za kufikirika,” alidai Kimomogolo.


Wakili wa Serikali , Edwin Kakolaki, akisaidiwa na Mwahija Ahmed, aliomba mahakama kumpatia muda wa kutosha kuyapitia mapingamizi hayo ambayo alidai ni mengi na yanahitaji muda wa kutosha ili awasilishe na akaahidi kuyawasilisha Jumatatu.


Lakini kabla ya mapingamizi hizo kuwasilishwa, kulizuka utata wa kutaka kufahamu washitakiwa watatu, akiwemo Joseph Selasini ambaye hakufika kwa sababu ya kushughulikia miili ya mapadre waliofariki katika ajali.


Wakili Kimomogolo, alidai kuwa Selasini ni kiongozi wa kanisa, hivyo analazimika kushiriki katika mipango ya kusafirisha miili ya mpadre hao.


Kuhusu washitakiwa wengine Dady Igogo na Nai Stephen, hakimu aliamuru wapatiwe taarifa kuhusu tarehe ya kesi wafike mahakamni hapo vinginevyo hatua kali za mahakama zitachukuliwa dhidi yao. Hakimu Magesa alisema hivyo kufuatia ombi la Wakili Kakolaki kutaka itolewe hati ya kukamatwa washitakiwa hao. Hakimu Magesa aliahirisha kesi hiyo hadi Jumatatu upande wa mashitaka utakapoleta majibu ya mapingamizi ya utetezi.




CHANZO: NIPASHE

 
kisheria mwenye mamlaka ya kutoa amri ya watu kutawanyika ni hakimu au askari polisi mwenye cheo kuanzia Inspekta, ambao kabla ya kufanya hivyo lazima wajiridhishe kuwa kusanyiko hilo linahatarisha amani na usalama wa watu wanaozunguka eneo husika na hati ya mashtaka haielezi iwapo majirani wa hoteli ya kitalii ya Mount Meru walilalamika kuhusu amani na usalama wao.

Hiyo statement nimeipenda!
 
Back
Top Bottom