Wakili Hamid Mbwezeleni Na Hali Ya Kisiasa Ya Nchi.

Junius

JF-Expert Member
Mar 11, 2009
3,181
139
Na Jabir Idrissa
HAPENDI namna Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ilivyoondoa mafuta na gesi asilia katika masuala ya Muungano; ufisadi unavyotesa chama akiaminicho; mahakama inavyoshutumiwa kwa kuachia huru akina Abdallah Zombe walioshitakiwa kuua.
Ni Hamidu Mbwezeleni, mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wakili wa kujitegemea anayeishi mjini Zanzibar.
Katika mahojiano na MwanaHALISI, Mbwezeleni anasikitika kuona mahakama inashutumiwa vikali kwa kuwaachia huru Zombe na wenzake katika kesi ya mauaji iliyokuwa ikiwakabili.
Mbwezeleni anasema anaamini Jaji Salum Massati alitoa hukumu kwa kuchambua ushahidi uliofikishwa mahakamani na upande wa mashitaka na utetezi wa washitakiwa.
Anasema mahakama si shahidi katika kesi yoyote ile; bali ni mfano wa mwamuzi kwenye mechi. Lakini anasisitiza kuwa haina maana kuwa mahakama inapoachia mshitakiwa lazima iwe kweli hakutenda kosa, isipokuwa ndivyo “mwenendo wa kesi ulivyomsaidia kuamua.”
Alikumbusha kuwa kazi ngumu ya hakimu au jaji siyo kusikiliza kesi mahakamani; ukweli ni pale anapobaki peke yake akichambua alichosikiliza. Hapo ndipo anapokabiliwa na kazi ngumu.
Mbwezeleni anasema hakuna jaji mbaya duniani kama yule anayemhukumu mtu kifo wakati ushahidi haukuthibitisha kosa hilo.
Jaji wa namna hiyo, anasema wakili, ni sawa tu na yule mtu aliyeua kweli. “Ushahidi unapokupa imani kuwa mshitakiwa hakuua, huna sababu ya kumtia hatiani mtu bali kumuachia ili ahukumiwe na Mwenyezi Mungu, maana yeye anajua huyo alihusika au la.”
Kwa Mbwezeleni, agizo la Jaji Massati kwamba uchunguzi makini haukufanywa na kutaka ufanywe ili waliohusika kuua washitakiwe, ni muhimu.
“Najua ndugu za waliouawa wana machungu makubwa. Muhimu wawe na subira kwani zipo hatua mbili kabla ya suala hilo kufikia mwisho. Ni halali kukata rufaa lakini hiyo ni hatua inayohitaji uchunguzi makini maana inawezekana rufaa ikashindwa pia katika mahakama ya juu.”
Mbwezeleni anatamani kupata hukumu na kumbukumbu za usikilizaji wa kesi ili atoe tathmini ya kitaalamu kwa kuzingatia sheria.
Kuhusu mvutano katika Nuungano, wakili anasema viongozi wa SMZ walikuwa na hoja nzuri na ya haki, lakini wametumia njia haramu kuiwasilisha na kudai haki hiyo.
Mbwezeleni, polisi mstaafu aliyefikia wadhifa wa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa (RCO), anasema lipo tatizo kubwa kwa viongozi wa Zanzibar kuamini kwamba wanaweza wakalazimisha mambo kwa kutumia hamasa na jeuri.
Anasema mtu mwema ni yule anayejua kuwa analo tatizo lakini akatumia njia nzuri kulitafutia ufumbuzi. Anasema ufumbuzi wa tatizo kwa kutumia njia ya mkato, hautoi suluhisho zuri.
Kwanza Mbwezeleni anaamini Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa 26 Aprili 1964, haukulazimishwa kwa upande wowote ule. Pili, anasema kwa kuwa ulikubaliwa na pande zote kwa vyovyote vile, kuheshimu makubaliano ni jambo la kiungwana.
Akipinga mbinu chafu, Mbwezeleni anasema kujaribu kuondoa dosari za Muungano kwa hamasa hakuna manufaa kwa upande wowote,
Anasema njia iliyotumiwa na SMZ kutaka kuondoa suala la mafuta na gesi asilia kutoka orodha ya mambo ya Muungano ni sawa na mtu kuamua kunusa kwapa na midomo ya mwenzake akijidai anatafuta ukweli wa kitu.
“Haifai kunusana kwapa na midomo. Vyote hivi vinanuka. Mtu anatarajia nini akifanya hivyo? Ndio maana unapulizia uturi kwapani; ndio maana mtu anapiga mswaki. Anataka kuondoa harufu kwa sababu sehemu hizi zinatunza uchafu unaotoa harufu mbaya,” anasema.
Anamaanisha walichokosea SMZ ni kule kuondoa dosari ya Muungano kwa kukiuka taratibu. Muungano una taratibu na kanuni zake, anasema. Sasa hakuna nafasi ya mtu kusema “tutachelewa” tukitumia utaratibu, maana “kila kizuri kina gharama yake.”
Anahimiza, “Ni haki yao kwa sababu kila kilichoingia hutoka. Ila huwezi kutaka kuondoa tatizo kwa kukwepa taratibu. Hata kama zikiwa ni ngumu, zifuatwe na pale zinapoonekana zinakwamisha utatuzi, basi zirekebishwe ili mambo yaende mbele.”
Akizungumzia utaratibu wa Bunge wa kutumia wingi wa theluthi mbili kwa kila upande katika kupitisha jambo linalohusu masuala ya Muungano, anasema unapaswa kutumika na iwapo hautoi ufumbuzi basi urekebishwe.
“Iwapo tunaona ufumbuzi haupatikani kwa utaratibu huu, na upande mmoja unaendelea kuumia, bora utafutwe utaratibu mwingine lakini siyo kutumia njia za kusababisha mgogoro wa kikatiba,” anasema.
Anatoa maoni kwamba Muungano unatingishwa iwapo kuna upande unadhani unatawaliwa na mwingine. Anasema, “Hizi nchi ziliungana zote zikiwa sawa. Hakuna nchi ndogo; sasa inafaa kuepuka maneno ya kukerana. Kila mmoja anayajua na anaweza kuyatoa lakini watu wazima hawatatui tatizo kwa kusemana.”
Anasema majadiliano na kuheshimiana ni njia muafaka ya kutatua tatizo lolote. Anaona nafasi ya majadiliano ipo kubwa kwani kwa kuwa serikali zote ziko chini ya CCM, vikao vya juu vya chama vinaweza kutumika.
“Mtindo wa viongozi kushutumiana huku mishipa ya shingo ikichomoza, unaumiza chama. Una cabinet mbili (mabaraza ya mawaziri), una CC (Kamati Kuu), una NEC (Halmashauri Kuu ya Taifa); huwezi kufanya kazi kwa malengo tofauti bali kushirikiana na kusaidiana,” anasema.
Anasema anaona mtindo wa viongozi wa CCM kushutumiana badala ya kuelekezana ukishamiri hata ndani ya bunge.
Mbwezeleni anaiona hatari ya bunge kutumia vibaya mamlaka yake kuikandamiza serikali, ambayo anasema, inapaswa kutenda kazi kwa kuzingatia sheria na kanuni za utumishi.
Anasema mtindo wa sasa wa wabunge wa CCM ni sawa na kumfunua nguo mzee na kumwacha uchi. “Huwa hatufanyi hivyo, bali unachukua kaptula na kanzu unamvisha mzee,” anasema.
Anahofia serikali inafikishwa mahali inalazimishwa kukiuka sheria ili tu “kukidhi matamanio ya watu wanaopiga vita ufisadi.”
Kuilazimisha serikali kufukuza watumishi, wakiwemo wale walioteuliwa na rais pale wanapokosa, kuna athari kubwa kwani kunabomoa misingi ya uongozi mwema na badala yake kupandikiza utawala mbovu utakaokabwa koo na watakaoona wameonewa.
Anatoa mfano wa namna serikali inavyolazimika kulipa mamilioni ya shilingi kwa maofisa wa polisi waliokuwa wamestaafishwa kazi kwa manufaa ya umma.
“Hawa wametumia mwanya wa kukiukwa sheria na taratibu za utumishi. Mfanyakazi ana haki zake zinazolindwa na sheria na kanuni za utumishi. Unapotumia njia isiyo sahihi kuondoa tatizo, unaunda tatizo jingine hapo baadaye ambalo litakuja kukusumbua,” anasema.
Hoja hii ameiegemeza kwenye hatua ya bunge kukataa taarifa ya serikali ya utekelezaji wa maazimio ya bunge kuhusu mkataba wa kufua umeme wa dharura wa Richmond.
Anasema bunge ni zao la sheria na sheria ndizo zimeleta bunge, serikali na mahakama; vyombo ambavyo vinafanya kazi kutumia kanuni. Anaamini ni muhimu kila upande kutumia nafasi yake kiutaratibu na siyo kwa kuumiza upande mwingine.
Kwa mfumo uliopo wa uongozi wa nchi, anasema ni jambo jema kutafuta cha kufanya kila panapotokea kasoro kwa chombo kimoja kugusa kingine katika utendaji wa majukumu yake.
Wakili anasisitiza, “Nakusudia kuhimiza kwamba matumizi ya fursa kisheria yana mipaka… yanayotokea ni matokeo ya kukiuka mipaka hii. Hata hawa wabunge wanapokuwa bungeni na kumkosea mtu asiye mbunge wanavunja ustaarabu kwani wanaokosewa hawana nafasi ya kulalamika.”
Mbwezeleni anasema kampeni ya kupiga vita ufisadi lazima iende sambamba na kuheshimu haki za watu. Kwamba unataja tu utakalo dhidi ya mwingine, anasema na kuuliza, “Hivi nani fisadi.”
Anasema si sahihi kusema mtu ni fisadi kwa kuwa anatembelea gari aina ya Mercedes Benz; linaweza kuwa la mjomba wake; au mtu kumiliki majumba na viwanda ukasema ni fisadi, kumbe amepata kwa kukopa.
“Siku hizi kupata shilingi 90 milioni ni jambo dogo. Unaweza kumiliki unachotaka, hoja ni umepataje na hili lazima lifichuliwe kwa ushahidi, si kuchafuana.”
Anasema, “Uovu ufichuliwe,” lakini “Vikao vya chama ni vema vikalindwa kwani mwisho wa siku chama ndicho kinaanguka. Chama kitalipa gharama za matokeo haya.”
Mbwezeleni anasema utatuaji matatizo yoyote unahitaji kufanywa kwa kuzingatia sheria ambazo ndizo zitamlinda pia yule anayehisi anaonewa kutokana na kilichotendeka au kinachoendelea kutendeka.

SOURCE: MWANAHALISI.
 
Back
Top Bottom