Wakatoliki: Silaha kali, jeshi havitalinda amani

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797



na Happiness Mnale


KANISA Katoliki nchini limewataka viongozi wa serikali kutambua kuwa amani na usalama haviwezi kulindwa wala kudumishwa kwa kutumia nguvu kubwa za jeshi na matumizi ya silaha kali, bali ni kwa kila kiongozi kuwatendea haki watu wake.


Kauli hiyo imetolewa juzi jioni na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Yuda Thadeus Ruwa-Inchi, wakati wa ibada ya misa takatifu kwa ajili ya kuadhimisha miaka 50 ya uhuru iliyofanyika kitaifa katika Kanisa Kuu la Mt. Joseph.

Amesema tabia ya kuendeleza ubinafsi na usaliti wa baadhi ya viongozi katika matumizi ya rasilimali za taifa ni mambo yaliyolifikisha taifa hapa lilipo na njia pekee ya kudumisha amani na utulivu ni kutenda haki.


“Usalama wa nchi haulindwi kwa silaha kali au kuwa na jeshi kubwa,” alisema kiongozi huyo na kuongeza kuwa namna pekee ya kuleta utulivu ni kuwa karibu na Mungu katika safari ya kuivusha nchi kutoka hapa ilipo.


Ruwa-Inchi alisema malumbano ya vyama vya siasa, na tabia ya kulipiza visasi ni mambo yanavyovunja umoja na mshikamano wa wananchi na yanapaswa kuepukwa na kila mtu anayeitakia mema Tanzania. Bila kutaja mtu wala chama, rais huyo ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza, alisema kiongozi bora ni yule anayetimiza kikamilifu wajibu wake kwa kutenda kadiri ya mapenzi na mpango wa Mungu.


“Sifa ya kiongozi bora ni kuhakikisha kuwa anaachana na malumbano, ubinafsi, usaliti, kisasi na anakuwa na utendaji wa hekima iliyojaa upendo na kumtambua Mungu na kuishi atakavyo huku akizingatia kulisimamia taifa letu kwa kuishi na kushuhudia aliyoyatenda Mungu,” alisema.


Alisema ni wajibu mkubwa wa viongozi na wananchi kudumisha upendo, amani, utulivu na hekima ili uhuru uliopatika bila kutolewa jasho uendelea kuwepo nchini.


“Watu wakiishi kwa amani na kuacha malumbano, na kuwa watu wakweli wanaosimamiwa na kuongozwa na Mungu, tukiacha malumbano, ubinafsi uliokithiri nchini, huruma na wema wa Mungu vitaendelea kutawala nchi yetu,” alisema.


Alisema kuwa viongozi wa dini siku zote wamekuwa wakiwaombea watawala na taifa kwa ujumla, lakini kila mmoja anatakiwa kujiuliza ikiwa msimamo, nia na mwonekano wake unaendana na mapenzi ya Mungu ama ni kinyume.


“Tunapowaombea viongozi na kuliombea taifa kwa miaka 50 ya uhuru wa taifa letu lililobarikiwa kila mmoja anapaswa kujiuliza msimamo, nia na muonekano wake unaendana na kuongozwa na Mungu au tupo katika hali ya kuendekeza ubinafsi uliokithiri nchini kwetu, ikiwa ni pamoja na kutafuta njia zinazofaa na kuwa wasaliti katika matumizi ya rasilimali zetu?” alisema.


Msimamo wa kanisa hilo umekuja wakati hali ya taifa ikiwa katika misukosuko inayotokana na kukithiri kwa tuhuma za wizi na ubadhirifu wa mali ya umma na mapambanao baina ya watawala na viongozi wa vyama vya upinzani kulikosababisha kufunguliwa kwa kesi dhidi ya viongozi wa upinzani nchini.


Kanisa Katoliki limekuwa mstari wa mbele bila woga kusema waziwazi kile linachokiona na kuamini kuwa tatizo katika mustakabali mzima wa usalama na amani ya taifa.


Ibada hiyo ilifanyika kuhitimisha mzunguko wa maadhimisho ya sherehe za miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania (Tanganyika), ambao ulianza katika ngazi za parokia nchi nzima, lengo kuu ikiwa ni kuliombea taifa amani na utulivu na kumshukuru Mungu kwa neema na baraka nyingi ambazo kama nchi imejaliwa kupata kwa kipindi hicho chote.

 
Back
Top Bottom