Waingereza wafuatilia utendaji wa JK

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
266
RAIS Jakaya Kikwete atalazimika kupunguza safari zake nje ya nchi na kutumia muda mwingi kushughulikia masuala ya ndani ya nchi ikiwa anataka kumaliza vizuri katika kipindi chake cha mwisho cha utawala wake Taasisi ya Utafiti wa masuala ya uchumi ya Uingereza, Economic Intelligence Unit(EIU), imeeleza.

Taarifa ya EIU imesema kuwa Rais Jakaya Kikwete yupo njia panda kutoa kipaumbele cha kufanya mageuzi ndani ya chama anachokiongoza (CCM), au kutumia muda wake kutekeleza ilani ya chama hicho, huku akikabiliwa na changamoto iliyoitaja kuwa kubwa ni kuimarisha CCM na kutekeleza ahadi zake kwa wananchi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo EIU iliyochapishwa Februari mwaka huu, Rais Kikwete anapaswa kutumia muda wake mwingi kushughulikia masuala mbalimbali yanayoendelea ndani ya nchi ikiwa pamoja na mpasuko ndani ya CCM, utekelezaji wa ahadi alizotoa na kusimamia mageuzi ya kiuchumi nchini.

“Katika kipindi cha kwanza cha utawala wa Kikwete, kulikuwa na ukosoaji mkubwa dhidi ya safari zake nje ya nchi. Watu waliamini kuwa hatumii muda mwingi kushughulikia matatizo yaliyopo nchini kwake. Sasa tunatarajia kuwa atapunguza safari za nje katika awamu yake ya mwisho ya uongozi,” inasema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo kuwa EIU inaeleza kuwa Tanzania imekuwa ikikabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwamo kupanda kwa bei za vyakula, bidhaa na huduma mbalimbali, ukosefu wa ajira, madai ya mishahara, mgawo wa umeme, mikopo ya vyuo vya elimu ya juu na vitendo vya ufisadi vilivyoligharimu taifa mabilioni ya fedha za walipa kodi na kwamba yote hayo yamedumu kwa muda mrefu.

EIU imetoa taarifa yake ndani ya miezi minne ya kwanza ya awamu ya pili ya utawala wake aliouanza mwishoni mwa mwaka 2010 baada ya kuchaguliwa Oktoba 31 katika Uchaguzi Mkuu, Rais Kikwete.

Katika kipindi cha kwanza cha utawala wake, Kikwete pia alikuwa na safari nyingi nje ya nchi, nazo zilizolalamikiwa kuwa hazina tija kwa maendeleo ya nchi.

Kwa mujibu wa vyombo mbalimbali vya habari nchini, Rais Kikwete alianza safari za nje Desemba 14 mwaka jana, mmoja tu baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa kiti cha urais kufuatia Uchaguzu Mkuu uliofanyika Oktoba 31, 2010, ambapo alikwenda Zambia kwenye mkutano wa nchi wanachama wa maziwa makuu.

Rais Kikwete alisafiri tena Januari 26, kwenda Uswis na Ethiopia na mwezi mmoja baadae alisafiri kwenda kuhudhuria mikutano ya kimataifa ambapo kati ya Februari 20 hadi 24 alikuwa nchini Mauritania.

Machi Mosi alikwenda nchini Ufaransa kutoa mada kwenye mkutano wa kimataifa na alikwenda nchini, Mauritania kuhudhuria mkutano wa kutafuta suluhisho la migogoro ya kisiasa iliyoikumba nchi ya Ivory Coast.

“Malengo makubwa kwake (Rais Kikwete) katika kipindi chake cha mwisho madarakani ni kujitoa ndani ya uzio wa kufurahisha watu ili kuendelea kuungwa mkono, au anaweza kuongeza juhudi zake katika kufanya mageuzi ndani ya chama. Hata hivyo, anapaswa kufanya maamuzi juu ya muda na nguvu anazotaka kutumia katika kushughulikia migogoro ndani ya chama na muda kiasi gani atahitaji katika masuala ya kitaifa.” Inasema sehemu ya taarifa hiyo.

Hivi karibuni, Rais Kikwete alitangaza kufanya mabadiliko makubwa ndani ya CCM, mabadiliko ambayo kwa kiasi kikubwa yametokana na ushindi mdogo ilioupata wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita.

Lakini, EIU inasema kuongezeka umaarufu wa Chadema ni changamoto kubwa kwa Serikali ya CCM na wakati huo Chadema itakuwa na changamoto ya kujipanga vizuri na kuunda umoja ili kufanikisha malengo yake ili kukabiliana na CCM ambacho bado ni kizuri kina nguvu na ushawishi wa kisiasa nchini.

“Jambo lingine la muhimu katika siasa za ndani, ni jinsi Chadema itakavyoweza kuendana na mazingira ya kuwa chama kikuu cha upinzani na inapaswa kukubaliana na ukweli kuwa CCM ni wazuri wa kutumia baadhi ya mawazo ya upinzani na kuyafanya yao,” inasema taarifa hiyo ya EIU na kuongeza:

“Hili limeweza kuthibitishwa baada ya Uchaguzi Mkuu ambapo Chadema ilianza kudai katiba mpya, wazo ambalo Rais Kikwete amelichukua na hivi sasa yuko mbioni kuunda Kamati ya Kupitia Mabadiliko ya Katiba.”

Kuhusu kesi inayowakabili viongozi wa Chadema baada ya kutokea vurugu za Arusha, zilizosababisha vifo vya watu wanakadiriwa kufkia watano, EIU inasema kuwa upo uwezekano kwa kesi hiyo kutupiliwa mbali kwa kile kinachoonekana kuwa kuendelea kwake kunaweza kuzuia machafuko zaidi nchini.

“Kama kesi hiyo itaendelea, kuna uwezekano wa kuibua machafuko mapya, hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kesi hiyo kutupiliwa mbali kimya kimya kukwepa hatari hiyo,” inadai taarifa EIU.

Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Ripoti hiyo imedai kuwa Tanzania inakwenda mwendo mdogo katika kufikia malengo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ikihofia ardhi yake kumilikiwa na wahamiaji kutoka nchi nyingine wanachama wa Jumuiya hiyo hasa Kenya na Uganda.

Hata hivyo, EIU ilisema kuwa nchi wanachama wa EAC hazina dhamira ya dhati kuingia katika matumizi ya sarafu moja, licha ya makubaliano yaliyofikiwa baina ya nchi hizo na Benki Kuu ya Jumuiya ya Ulaya (ECB).

“Tunaona kuwa hakuna matumaini yeyote ya kuanza kutumia sarafu moja katika muda uliopangwa wa 2012. Tunaona hiki ni ni kikwazo kwa nchi wanachama kuendelea na ratiba iliyopangwa, wakati nchi zote hazina dhamira ya kweli ya kufanya hivyo,” inadai taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ya EIU inasema, licha ya kutokuwepo usawa wa kiuchumi miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kuanza matumizi ya sarafu moja hakuna dhamira halisi ya kisiasa kama inavyodhaniwa na wengi.

Mwananchi Jumapili lilipowasiliana na Waziri wa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samweli Sitta, jana aliomba atafutwe kesho kwa sababu alikuwa kwennye mkutano muhimu.

source

Waingereza wafuatilia utendaji wa JK
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom