Wahisani waikomalia serikali

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,006
Wahisani waikomalia serikali

Na Jacob Daffi - Imechapwa 06 July 2011
Mwanahalisi

WAFADHILI wa serikali wameonyesha kuwa hawatatoa fedha kwenye bajeti ya taifa hadi watakapokuwa wamepata maelezo ya kina kuhusu mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi nchini.
Katika taarifa yao ya tarehe 9 Juni, wahisani wamesema hawajaridhishwa na hatua zinazochukuliwa na serikali katika vita dhidi ya walarushwa na wezi wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) iliyoko Benki Kuu (BoT).

Wahisani hao, ambao huchangia fedha katika Bajeti ya serikali kupitia Mfuko wa kusaidia Bajeti (GBS) wanataka maelezo ya kina kabla hawajaachia "fedha zao."
Katika taarifa hiyo wamesema watakuwa tayari kuendelea kutoa misaada katika Mfuko wa Kusaidia Bajeti ya Serikali (General Budget Suport – GBS), endapo wataridhishwa na utendaji katika mikakati ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini.

Aidha, wafadhili wamesikitishwa na hatua ya serikali ya kukaa kimya kuhusu dokezo lao la kutaka kufanyika uhakiki wa hesabu katika matumizi ya fedha kwenye miradi ya barabara.
Walitaka serikali, kwa kutumia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi maalum kwa miradi ya ukandarasi iliyoko chini ya Wakala wa Barabara (Tanroads) kwa mwaka 2009/2010.
Katika kuonyesha kuishiwa uvumilivu, wahisani wamesema, hatua ya serikali ya ukimya imewaweka katika "wakati mgumu."

"Iwapo serikali haitaonyesha utayari wa kushughulikia suala hili kwa ubora zaidi, itatuwia vigumu kutetea mfuko huu," taarifa imesema.
Wahisani wanataka maelezo ya kina na mchanganuo wa fedha zilizorejeshwa katika kila kesi ya EPA; pia kueleza kwa ufasaha matokeo ya uchunguzi wa makampuni yaliyotuhumiwa kutumika kuiba fedha za EPA.
Wanataka pia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ithibitishe maeneo yote ambako fedha zimerejeshwa kisheria.

Aidha, wanataka serikali ionyeshe kwa dhati namna inavyopambana na kuzuia rushwa.
Taarifa ya wafadhili inalalamika kuwa kikao kingine cha kujadili masuala yanayohusu misaada kwa Tanzania kimeahirishwa.

"Ninaelewa kuwa hizi ni nyakati za shughuli nyingi kwenu, lakini bila ya kuwepo majadiliano, hatuwezi kuwa makini katika kufanya kazi yetu ambayo, napenda kukukumbusha, ni kuwasaidia ninyi," imeeleza taarifa.
Wakionekana kuwa na shauku ya mafanikio ya haraka, wahisani hao wametaka mpango wa kukomesha rushwa uwe endelevu na utapitiwa katika kikao cha mapitio cha GBS kitakachofanyika Novemba mwaka huu.

Kikao hicho kitakuwa cha pili baada ya kilichotangulia kufanyika Juni 9, 2011 katika Hoteli ya Dodoma ambako wahisani kutoka nchi za Jumuiya ya Ulaya (EU) walionyeshwa kukerwa na namna suala la rushwa linavyoshughulikiwa kilegevu.

Kikao hicho kiliwahusisha wahisani kutoka nchi za EU, Waziri Mkulo na mawaziri kadhaa.
Pamoja na mambo mengine yaliyojadiliwa, wahisani walihoji hatima ya kesi za EPA, inavyoshughulikiwa rushwa pamoja na misaada yao kwa nchi.
Mbali na kukutana na mawaziri wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, wahisani pia walipanga kukutana na Jaji Mkuu na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) ili kujadili mbinu za mapambano dhidi ya rushwa ambayo inalitafuna taifa.

"Tunaamini kuwa Jaji Mkuu ana mtazamo mzuri katika masuala haya na hilo litaongeza utendaji katika mfumo wa mahakama. Tutajadiliana naye kuhusu masuala haya na tutajua namna gani tutaweza kusaidia," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Katika hatua nyingine, wahisani wameahidi kusaidia sekta ya elimu kwa kutoa kiasi cha Sh. 25,000 kwa kila mwanafunzi ili kusaidia katika ununuzi wa vitabu na vifaa vingine vya masomo.
Mpango huo ulitakiwa uanze kutekelezwa kuanzia Juni mwaka huu.

Kwa upande wake, serikali imetoa Sh. 25.9 bilioni kati ya Sh. 40 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya sekta hiyo; na Benki ya Dunia (WB) imeahidi kuchangia Sh. 12 bilioni katika Mpango wa Maendeleo ya Elimu kwa Shule za Sekondari (MMESS).

Hata hivyo, wahisani wameeleza hofu yao iwapo serikali itaweza kutoa fedha zote. Kiasi cha Sh. 2.5 bilioni kilitakiwa kutolewa kabla ya Juni 30, 2011.Mpango wa kusaidia eneo la elimu umekuja kufuatia matokeo mabaya ya mitihani ya kidato cha nne kwa mwaka 2010.
 
NImeisoma hiyo kwenye MwanaHALISI. iMEKAA VIZURI. tUTAONA SASA ****** KAMA ATAENDELEA KUSAFIRI NJE.
 
NImeisoma hiyo kwenye MwanaHALISI. iMEKAA VIZURI. tUTAONA SASA ****** KAMA ATAENDELEA KUSAFIRI NJE.

Hawa wafadhili nao ni bomu sana. Nakumbuka mwaka jana pia wakati wa bajeti waligoma kutoa mapeza yao ambayo kama sikosei ilikuwa ni zaidi ya $800 million. Kwa mshangao wa Watanzania wengi tusiopenda pesa hizo zitolewe maana hayuoni maendeleo yoyote yale pamoka na misaada na mikopo chungu nzima kila mwaka, ilipofika August 2010 Wafadhili wakadai "wameridhishwa" na maelezo waliyoyapata toka Serikalini na hivyo kuamua kutoa pesa zile. Na hisi safari hii itakuwa hivyo hivyo. Ngoja tusubiri tuone kama kweli wataweka ngumu au ni tisha toto tu.
 
Back
Top Bottom