Wafanyakazi tanzania kaeni macho na kauli za kampeni

Msharika

JF-Expert Member
May 15, 2009
947
69
SIKU chache baada ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), kutangaza mgomo wa wafanyakazi nchi nzima, Rais Jakaya Kikwete amesema anaamini shirikisho hilo litatumia busara na si kugoma katika kipindi hiki ambacho Serikali inatafuta utatuzi wa matatizo yao.

Hatua hiyo ya Rais Kikwete imekuja baada ya shirikisho hilo kutangaza kuwa halitamwalika katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi mwaka huu, ikiwa ni hatua ya kuelekea kwenye mgomo utakaofanyika siku nne baadaye.

Hii itakuwa mara ya kwanza Rais wa nchi kutoalikwa kwenye maadhimisho hayo ambayo mwaka huu yatafanyika Dar es Salaam. Akizungumza na gazeti hili baada ya tamko la Tucta, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salvatory Rweyemamu, alisema ni matarajio ya Rais kuwa hakutakuwa na ulazima wa mgomo, kwa sababu madai yao yanashughulikiwa na Serikali.

"Ikulu haijapokea mwaliko wa kumkaribisha siku hiyo ya Mei Mosi, ingawa bila shaka Rais kama mfanyakazi mwenzao, angependa ashiriki nao katika sherehe hiyo muhimu ya wafanyakazi,” alifafanua Rweyemamu.

Mkurugenzi huyo alisema madai ya wafanyakazi hao yapo serikalini na yanashughulikiwa na ifahamike kuwa inachukua muda mrefu kupata majibu ya matatizo, hivyo Rais anawaomba wawe na subira.

Hata hivyo, alisema Tucta ni chama huru kinachojitegemea, hivyo kina uhuru wa kuamua nani awe mgeni rasmi kwenye sherehe yao.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Katibu Mkuu wa Tucta, Nicholas Mgaya, alisema Shirikisho limefikia uamuzi huo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mgomo wao waliosisitiza kufanyika Mei 5 mwaka huu na hautakuwa na kikomo hadi madai yao yatakapotekelezwa.

“Tumechoka kila mwaka kutoa risala na hatutekelezewi … mwaka huu hatumwaliki Rais wa nchi kuwa mgeni rasmi, badala yake mgeni rasmi kitaifa atakuwa Rais wa Shirikisho, Ayoub Omar Juma na mikoani watakuwa wenyeviti wa vyama wa mikoa,” alifafanua.

Mgaya alisema sherehe za mwaka huu watazitumia kuhamasisha mgomo ambapo mabango yote yatahamasisha mgomo huo aliouita halali kwani wamefuata sheria inavyotaka.

“Tunawaomba wafanyakazi wasiwe na wasiwasi, tumefuata sheria kama inavyotaka, ikiwamo kutoa notisi ya mgomo wetu,” alisema.

Alitaja sababu za kusisitiza kugoma Mei tano, kuwa ni pamoja na kutopewa ufumbuzi wa madai ya muda mrefu yakiwamo ya mishahara duni isiyokidhi mahitaji, nyongeza duni ya mishahara na mafao madogo kutoka kwenye mifuko ya pensheni ya wastaafu.

"tunataka mifuko ya wastaafu iwe miwili; ya sekta binafsi na ya umma, si sasa unakuta mifuko yenye vigogo kama PSPF mafao yao mazuri, lakini mingine mtu anapata Sh milioni mbili,” alisema.

Malalamiko mengine ni kodi kubwa wanayokatwa wafanyakazi na kutokuwapo bodi za kushughulikia mishahara kwa sekta binafsi ambapo alifafanua: “Sheria inasema ndani ya siku 60 Waziri wa Kazi aunde bodi baada ya kupelekewa mapendekezo, lakini tangu Aprili mwaka jana, bodi zimemaliza muda hajateua nyingine”.

Wiki iliyopita, shirikisho hilo lilitangaza nia ya mgomo lakini Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo akawaeleza wafanyakazi, kuwa kuigomea Serikali ni kupoteza muda, kutokana na kutoweza kisheria kubadilisha bajeti yoyote katikati ya mwaka.

Alisema mwenye mamlaka ni Bunge na kuitaka Tucta kuwasilisha bungeni malalamiko yake kuhusu kodi na mishahara. Hata hivyo Mgaya alisema hawawezi kuwasilisha bungeni kwani walishawahi kufanya hivyo miaka ya nyuma, lakini wabunge wakajiondolea kodi wenyewe.

Shirikisho hilo la vyama vya wafanyakazi, liliwahi kutangaza mgomo kama huo mwaka juzi ukilenga pia kufanya maandamano katika wilaya na mikoa, kupinga Serikali kuwanyanyasa, kuwanyima nyongeza na malimbikizo ya mishahara. Hata hivyo waliusitisha kutokana na kilichoelezwa kwamba Rais Kikwete atashughulikia tatizo hilo.
SOURCE: HABARI LEO

MY COMMENTS: HIZI SHIDA ZA WAFANYAKAZI ZIMEKUJA LEO? MIAKA YOTE 4 KAWAFANYIA NINI ZAIDI YA KUWAONGEZEA MFUMUKO WA BEI NA HALI DUNI YA MAISHA? TAFAKARI
 
Back
Top Bottom