Wabunge wa CCM chanzo cha sheria mbovu za madini

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,007
Date::7/12/2008
Wabunge chanzo cha sheria mbovu za madini
Na Daniel Mwaijega
Mwananchi

MOJA ya hoja zilizopewa uzito katika mijadala ya bunge wiki hii, ni ile ya nishati na madini, ambako kuna kashfa na masuala mazito yaliyoitikisa nchi siku za hivi karibuni.

Baadhi ya masuala hayo ni mikataba mibovu ya madini na uzalishaji wa umeme wa ziada, kufuatia serikali kuingia mikataba tata na kampuni mbalimbali, ukiwemo wa Richmond Develeopment Company ambao baadaye ulihamishiwa Dowans na ule wa Independent Power Tanzania Limited (IPTL), ambayo kwa pamoja inadaiwa kuchangia kuongeza gharama za umeme.

Kwa upande wa madini, kamapuni ya Meremeta na uuzwaji tata wa mgodi wa makaa ya mawe Kiwira, zilipewa uzito wa juu na wabunge ambao walionyesha kutoridhishwa na majibu yaliyotolewa na serikali kuhusu uendeshaji na mikataba ya uzwaji wa makampuni hayo.

Hata hivyo, leo sitajadili masuala hayo, bali nitazungumzia jinsi madini yasivyotumika ipasavyo kuinua uchumi wa nchi yetu na maisha ya Watanzania kutokana sheria mbaya zinazoruhusu mikataba mibovu.

Taarifa za utafiti zinaonyesha kuwa nchi hii ina utajiri mkubwa wa madini ambayo mpaka sasa hayajatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya tiafa wala kuwaondolea umaskini Watanzania.

Kinachoumiza zaidi ni kwamba, licha ya serikali kuruhusu wawekezaji katika sekta hiyo, asilimia kubwa ya pato la madini huwanufaisha wao (wawekezaji) huku serikali ikiambulia kiduchu kutokana na mikataba mibovu inayompendelea mwekezaji na kumpa muda wa msamaha (tax holiday), kwa madai kwamba anatumia gharama kubwa kuandaa mazingira ya uchimbaji, ambao wao huutumia kujinufaisha.

Naweza kusema kwamba, kuwalaumu wawekezaji katika suala hilo si sawa, kwa sababu kuingia kwao nchini na kwenye biashara hiyo, kumeruhuswa kisheria kupitia mikataba waliyoingia na serikali inayowapa mwanya wa kutolipa kwa muda wa zaidi ya miaka miwili tangu kuanza kuchimba madini, ili kufidia gharama walizotumia wa kuwekeza.

Kwa kutumia mwanya huo, wawekezaji huchimba madini kwa kasi ili kupata kiasi kikubwa katika kipindi hicho, hivyo kuifanya serikali kukosa mapato yanayotokana na rasilimali hiyo. Kibaya zaidi ni kwamba, kutokana na kasi hiyo ya uchimbaji, ni dhahiri baada ya kipindi hicho cha neema kumalizika, madini yatakuwa yamekwisha katika eneo husika na wao wataamua kufunga migodi, kisha kuondoka na kutuachia mashimo makubwa ambayo hayawezi kufukiwa.

Uharibifu huo mkubwa wa mazingira hauwezi kufidiwa kwa gharama yoyote, hivyo kuendelea kuwafanya Watanzania kuwa maskini, kwa kuwa ardhi hiyo haitafaa tena kwa kilimo wala matumizi mengine ya uzalishaji mali.

Hata hivyo, hayo yote yamesababishwa na mikataba mibovu ambayo imeshtukiwa na wabunge, nchi ikiwa tayari imeingia hasara kubwa.

Pamoja na hatua hiyo ya wabunge, kuna maswali mengi ya kujiuliza yakiwamo ya je, ni nani aliyetunga sheria hiyo na kuipitisha?

Ninanchofahamu mimi ni kwamba, sheria yoyote kabla haijawa sheria hupelekwa bungeni na serikali ambako hujadili na kupitishwa kuwa sheria baada ya kuridhika kuwa inafaa kwa maslahi ya maendeleo na ulinzi wa rasilimali na jamii ya Watanzania. Kwa nini sheria za namna hiyo zilizipitishwa au wakati wa kuamua asilimia kubwa ya wabunge hawakuwepo ukumbini (kama kawaida yao) na waliobaki asilimia kubwa walikuwa wanatwanga usingizi na hatimaye kupitisha bila kujua kinachoendelea?

Nahoji hilo kwa sababu, pamoja na bunge la safari hii kuchachamaa kutaka sheria na mikataba hiyo, wengi wao walikuwepo bungeni wakati huo! Ukiondoa wapinzani ambao ni wachache na kutokana na uchache wao hoja zao au pingamizi lao huwa halipati nafasi, wabunge wengi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), walikuwemo na ndiyo waliozipitisha. Je,wabunge waliokuwepo wakati huo, walikuwa wapi siku hiyo au walizipitishaje?

Serikali inatupiwa lawama kwa kosa hilo na kweli ina haki ya kulaumiwa kwa sababu kupitia kwa wataalamu wake, ikiwamo ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ndiyo inayoandaa muswada wa sheria unaopelekwa bungeni na kuutetea. Nadhani kwamba, wabunge walioipitisha sheria hiyo wanatakiwa kuingizwa kwenye kashfa hiyo, kwa sababu kama si wao kuipisha, serikali ingekwama.

Kinachoonekana hapa ni kwamba sheria hizo zilipitishwa kisiasa zaidi badala ya kuangalia maslahi ya taifa kwa miaka mingi ijayo. Ni ukweli usiopingika kwamba, kutokana na wingi wao, wabunge wa CCM wana nguvu mfano wa kura ya turufu katika kupitisha au kukwamisha miswada na hoja zenye manufaa kwa taifa, na nyingine sizizokuwa nayo. Hivyo lazima wabebe sehemu ya lawama hizo, vinginevyo waliokuwepo watuambie kwamba hawakuwepo na kama hawakuwepo walikuwa wapi, wakati walitumwa bungeni na wananchi kufanya kazi kwa ajili hiyo?

Siamini na sitakubaliana na ushawishi wowote kwamba, labda wabunge wa wakati huo hawakuwa na uwezo (vihiyo) ndiyo maana sheria hizo zilipitishwa kwa sababu hawakuwa na uwezo wa kuzichambua kama ilivyo sasa, ila nadhani walifanya makusudi kupoteza rasilimali za taifa kutokana na wengi wao kujua kwamba kutokana na umri wao hawana matumaini ya kuishi siku nyingi, hivyo hawahusiki na Tanzania na kizazi chake cha kesho.

Nashawishika kusema waliopitisha sheria hiyo walikuwa na mawazo kwamba, "Acha mambo yaende, huko mbele sisi hatutakuwepo." Sijui Muasisi wa Taifa hili, Marehemu Julius Nyerere angekuwa na mawazo hayo, nchi hii ingekuwaje sasa!"

Wabunge wetu waliopita wametutia hasara kubwa kutokana na kutokuwa makini, kwani sasa zimetumika fedha nyingi na kamati ya Rais iliyoundwa kupitia upya sheria na mikata ya madini, kazi ambayo ilitakiwa kufanyika wakati huo. Hivyo nadiriki kusema kwamba, asilimia kubwa ya wabunge wa CCM hawaisaidii serikali yao, ila wamejaa unafiki na ushabiki wa kisiasa, hata katika masuala nyeti yanayohusu mstakabali wa kitaifa yenye manufaa kwa Watanzania.

Ni vizuri tabia hiyo ikakomeshwa na kuanza kuwaunga mkono wapinzani wanapotoa hoja zinazotetea maslahi ya taifa, badala ya kubeza, halafu baada ya mambo kubadilika, kuanza kuchachamaa na kuamua kuunda tume zinazotumia fedha nyingi za umma, wakati tayari tumepata hasara kubwa.

Inafahamika kwamba, serikali wakati mwingie huingia kwenye mikataba mibovu kutokana baadhi ya watu waliopewa madaraka kutaka kujinufaisha au kutokana na matatizo yanayolikabili taifa, ikiwamo hali ngumu ya kiuchumi kama njia moja wapo ya kuyatatua. Hivyo wabunge wanatakiwa kuwa makini katika kufanya maamuzi ili yasifanyike makosa kama ya sasa yaliyoliingiza taifa kwenye matatizo makubwa.

Baruapepe:mwaijega@yahoo.com

Simu: 0713704898
 
Back
Top Bottom